Alhamisi kuu, siku Kristo Yesu alipoweka Sakramenti ya Ekaristi Takatifu, Daraja Takatifu ya Upadre na Huduma ya Upendo. Alhamisi kuu, siku Kristo Yesu alipoweka Sakramenti ya Ekaristi Takatifu, Daraja Takatifu ya Upadre na Huduma ya Upendo.   (Vatican Media)

Alhamisi Kuu: Ekaristi Takatifu, Daraja Takatifu na Huduma ya Upendo

Alhamisi kuu Mama Kanisa anaadhimisha mambo makuu matatu. Kwanza ni kuwekwa kwa Sakramenti ya Ekaristi Takatifu, chakula chetu cha kiroho. Pili kusimikwa kwa Sakramenti ya Daraja Takatifu la Upadre. Na tatu ni Amri Kuu ya mapendo aliyoidhihirisha Yesu kwa kuwaosha Mitume miguu. Mambo haya matatu ndiyo kiini cha maadhimisho ya Fumbo Kuu la Pasaka linaloanza kwa adhimisho la Karamu ya Mwisho, siku ya Alhamisi Kuu.

Na Padre Pascha Ighondo, - Vatican.

Tafakari ya Neno la Mungu Siku ya Alhamisi Kuu. Katika siku hii, Mama Kanisa anaadhimisha mambo makuu matatu. Kwanza ni kuwekwa kwa Sakramenti ya Ekaristi Takatifu, chakula chetu cha kiroho. Pili kusimikwa kwa Sakramenti ya Daraja Takatifu la Upadre. Na tatu ni Amri Kuu ya mapendo aliyoidhihirisha Yesu kwa kuwaosha Mitume miguu. Mambo haya matatu ndiyo kiini cha maadhimisho ya Fumbo Kuu la Pasaka linaloanza kwa adhimisho la Karamu ya Mwisho, siku ya Alhamisi Kuu. Ni katika muktadha huu mama Kanisa katika sala ya mwanzo anasali hivi; “Ee Mungu, tunaadhimisha Karamu takatifu ya Mwanao wa pekee. Yeye alilikabidhi Kanisa kwa siku zote sadaka mpya na karamu ya upendo wake. Tunakuomba utujalie, tujipatie wingi wa mapendo na uzima katika fumbo hili kubwa.” Ni katika muktadha huu masomo tunayoyasoma katika maadhimisho ya siku hii ya Alhamisi Kuu yamejikita katika kuelezea namna na maana ya maadhimisho ya karamu ya kipasaka jinsi yalivyokuwa katika Agano la Kale na utimilifu wake katika Agano Jipya na la milele kwa kifo cha Msalaba cha Bwana wetu Yesu Kristo na ufufuko wake. Ndiyo maana maneno ya wimbo wa mwanzo yanasema hivi; “Lakini sisi yatupasa kuona fahari juu ya msalaba wa Bwana wetu Yesu Kristu. Yeye ndiye wokovu, uzima, na ufufuko wetu; nasi tumeokolewa na kusalimishwa naye.

Alhamisi Kuu: Ekaristi Takatifu, Daraja na Huduma
Alhamisi Kuu: Ekaristi Takatifu, Daraja na Huduma   (Vatican Media)

Somo la kwanza ni kutoka Kitabu cha Kutoka (Kut 12:1-8, 11-14). Somo hili linasimulia jinsi Wayahudi walivyoadhimisha mlo wa kwanza wa Kipasaka, siku ile walipokombolewa kutoka utumwani Misri. Mlo huu ulikuwa ni wa kifamilia ambapo walipaswa kula nyama ya mwanakondoo aliyeokwa na damu yake kunyunyiziwa katika miimo ya milango ili Malaika wa Bwana atakapopita kuwaangamiza wazaliwa wa kwanza wa wamisri, asiwadhuru wana wa Waisraeli. Lakini pia walipaswa kula mikate isiyotiwa chachu kwa sababu ya haraka waliyokuwa nayo ya kuondoka Misri, na mboga chungu zikiwakumbusha mateso waliyopata mda wote wakiwa watumwa hapo Misri. Sikukuu hii ya kipasaka kwa Wayahudi ya maandalizi ya kukombolewa kutoka utumwani, ilikuwa ni mwangwi tu wa kukombolewa kwa wanadamu wote kutoka utumwa wa dhambi na nguvu za shetani na Kristu Yesu, Mwana kondoo wa kweli wa Pasaka, aondoaye dhambi za ulimwengu, kwa kumwaga damu yake Msalabani. Ni katika muktadha huu kiitikio cha wimbo wa katikati kinasema hivi; Kikombe kile cha baraka tukibarikicho, Je! Si ushirika wa Damu ya Kristo? (1Kor. 10:16). Naye mzaburi akiutafakari ukuu huu wa matendo ya Mungu, katika mashairi ya wimbo huu wa katikati anasema hivi; “Nimrudishie Bwana nini, kwa ukarimu wake wote alionitendea? Nitakipokea kikombe cha wokovu; na kulitangaza jina la Bwana. Ina thamani machoni pa Bwana, mauti ya wacha Mungu wake. Ee Bwana, hakika mimi ni mtumishi wako, mwana na mjakazi wako, umevifungua vifungo vyangu. Nitakutolea dhabihu ya kukushukuru, na kulitangaza jina la Bwana. Nitaziondoa nadhiri zangu kwa Bwana, naam, mbele ya watu wake wote (Zab. 116:12-13, 15-18). Nasi hatuna cha kumlipa Mungu kwa wema na ukarimu wake kwetu sisi, zaidi ya kulisifu jina lake takatifu na kuishi kadiri ya amri na maagizo yake.

Ekaristi Takatifu chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa
Ekaristi Takatifu chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa   (Vatican Media)

Somo la pili ni la Waraka wa Kwanza wa Mtume Paulo kwa Wakorintho (1Kor 11:23-26). Na Injili ni ilivyoandikwa na Yohane (Yoh. 13:1-15). Vyote kwa pamoja vinaelezea juu ya kuwekwa kwa Sakramenti ya Ekaristi Takatifu na Daraja la Upadre katika mlo wa Kipasaka, mlo wa mwisho aliokula Yesu na mitume wake. Lakini ikumbukwe kuwa mlo wa kipasaka aliokula Yesu na wanafunzi wake ni tofauti na waliokula wayahudi wengine. Kwanza, Kristo ndiye Mwanakondoo mwenyewe aondoaye dhambi za ulimwengu. Hivyo hawakuwa na haja ya kuandaa na kuchinja mwanakondoo. Ndiyo maana Mtume Paulo anapouelezea mlo huu anasisitiza kuwa sisi tunaouadhimisha unatukumbusha kifo cha Kristo Yesu. Anasema hivi; “Kwa maana mimi, nalipokea kwa Bwana niliyowapa ninyi, ya kuwa Bwana Yesu, usiku ule aliotolewa, alitwaa mkate, naye akiisha kushukuru akaumega, akasema; “Huu ndio mwili wangu ulio kwa ajili yenu; fanyeni hivi kwa ukumbusho wangu”. Na vivi hivi baada ya kula akakitwaa kikombe, akisema; “Kikombe hiki ni Agano Jipya katika damu yangu; fanyeni hivi kila mnywapo, kwa ukumbusho wangu”. Maana kila mlapo mkate huu na kukinywea kikombe hiki, mwaitangaza mauti ya Bwana hata ajapo”. Mwinjili Yohane kwa upande wake anatilia msisitizo kuwa Yesu aliingia saa ya mateso na kifo chake kwa moyo mtulivu na kwa hiari yake yeye mwenyewe baada ya kula mlo wa kipasaka na wanafunzi wake.

Ibada ya Misa Takatifu ilete mabadiliko katika utu wa ndani
Ibada ya Misa Takatifu ilete mabadiliko katika utu wa ndani   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Kisha kula aliwaosha miguu, alama ya utumishi na upendo wake uliotimizwa kikamilifu msalabani. Yeye Bwana na Mwalimu, Mfalme, Masiha, Mwokozi, na Mungu kweli, alijishusha, akajinyenyekeza, kwa upendo mkuu aliwaosha wanafunzi wake miguu. Mtume Petro hakuelewa jambo hili akakataa. Lakini baada ya Yesu kusisitiza juu ya umuhimu wake alikubali. Namna hii Yesu ametuchia mfano wa kupendana na kutumikiana sisi kwa sisi unaodumu milele yote. Tendo hilo Padre, katika nafsi yake Kristo hulifanya kwa kuwaosha miguu wanaume 12, kutukumbusha wajibu huu wa kupenda sisi kwa sisi na kutumikiana. Na zaidi sana katika mlo huu, Yesu kwa upendo aliweka Sakramenti ya Ekaristi Takatifu, akajiweka mzima, Mwili wake na Damu yake, ubinadamu na Umungu wake katika maumbo ya mkate na divai, akae nasi ili tumwone, tuongee naye, ajue hali zetu, shida, matatizo, furaha na huzuni zetu katika nafsi za Mapadre, ili atupe nguvu na moyo wa kuyashinda yote.Kumbe, tunaona kuwa katika adhimisho la Karamu ya Bwana, Alhamisi Kuu, Kristo Yesu ametuachia mambo mengi ya kujifunza katika maisha yetu ya kila siku. Kwanza ni kupendana sisi kawa sisi kama Yeye alivyotupenda hata akayatoa maisha yake kwa ajili ya wokovu wetu. Pili tunapaswa kuwahudumia wenzetu kwa upendo huo huo alivyfanye Yeye hata ambao ni adui zetu.

Alhamisi Kuu: Huduma ya upendo kwa watu wa Mungu
Alhamisi Kuu: Huduma ya upendo kwa watu wa Mungu   (ANSA)

Kama Yesu Kristo alivyopiga magoti mbele ya mitume, akawaosha miguu. Nasi tujifunze kujishusha kwa unyenyekevu katika nafasi tulizo nazo ili tuwahudumie wengine. Tukumbuke kuwa vyeo tulivyo navyo, nafasi tulizo nazo ni kwa ajili ya kuwahudumia wengine, tukifuata mfano wa Yesu mwenyewe. Zaidi sana tuushinde ubaya kwa wema, kwa kuwapenda, kuwaombea na kuwatumikia wanaotuchukia na kutudhulumu. Basi tumwombe Mungu atusaidie kuyaelewa mafumbo hayo matatu: Amri kuu ya mapendo, Ekaristi Takatifu na Daraja Takatifu ya Upadre, ili tuweze kujichotea neema na baraka tunapoyaadhimisha na kuyaishi. Ndiyo maana mama Kanisa katika sala ya kuombea dhabihu anasali hivi; “Ee Bwana, tunakuomba utujalie kuadhimisha vema mafumbo haya, kwa maana kila tunapoadhimisha ukumbusho wa sadaka hii, kazi ya ukombozi wetu inafanyika”. Nao utangulizi wa siku hii unasisitiza hivi; “Ndiye kuhani wa kweli na wa milele, aliyeanzisha sadaka hii ya daima. Ndiye wa kwanza aliyejitoa mwenyewe kwako sadaka ya wokovu, akatuamuru tuitoe kwa kumkumbuka Yeye. Tunapata nguvu tuulapo mwili wake uliotolewa sadaka kwa ajili yetu; tunatakaswa tuinywapo damu yake aliyoimwaga kwa ajili yetu sisi”. Na katika Sala baada ya komunyo anahitimisha maadhimisho haya akisali hivi; “Ee Mungu Mwenyezi, kwa vile tunavyotiwa nguvu na karamu ya Mwanao hapa duniani, utujalie tuje tushibe karamu ya milele mbinguni”. Na hili ndilo tumaini letu. Tumsifu Yesu Kristo!

Alhamis Kuu 2025
16 Aprili 2025, 15:16