Kristo amefufuka kwa wafu, kwa kifo chake alishinda dhambi na mauti na amewakirimia wafu uzima wa milele Kristo amefufuka kwa wafu, kwa kifo chake alishinda dhambi na mauti na amewakirimia wafu uzima wa milele 

Sherehe ya Pasaka ya Bwana: Kilele cha Ukweli wa Imani ya Kikristo Inayopaswa Kushuhudiwa

Ufufuko wa Kristo Yesu ni kilele cha ukweli wa imani ya Kikristo, ambayo jamii ya kwanza ya wakristo iliusadiki na kuuishi kama kiini cha ukweli; waliiendeleza kama msingi kwa njia ya Mapokeo; waliithibitisha kwa njia ya Maandiko ya Agano Jipya; na wakaihubiri kama sehemu muhimu sana ya Fumbo la Pasaka yaani: mateso na kifo cha Kristo Msalabani. Kristo amefufuka kwa wafu, kwa kifo chake alishinda dhambi na mauti na amewakirimia wafu uzima wa milele.

Na Padre Bonaventura Maro, C.PP.S., Kolleg St. Josef, Salzburg, Austria.

Utangulizi. Wapendwa Taifa la Mungu, leo ni Dominika ya Sherehe ya Pasaka. Tunamshangilia, “Kristo Mfufuka, ameshinda mauti, amefufuka kama alivyosema” Ufufuko wa Bwana wetu Yesu ni msingi wa Imani yetu, kama anavyotuambia mtume Paulo, “Kama Kristo asingalifufuka basi Imani yenu ni bure” (1 Kor 15:14). Tunamshangilia Kristo aliyetoka mzima kaburini siku ya tatu kama alivyosema, baada ya mateso na kifo chake pale Msalabani. Kwa ufufuko wake, Kristo alikata minyororo ya mauti akatoka kuzimu ameshinda (Mbiu ya Pasaka). Ufufuko wa Kristo Yesu ni kilele cha ukweli wa imani ya Kikristo, ambayo jamii ya kwanza ya wakristo iliusadiki na kuuishi kama kiini cha ukweli; waliiendeleza kama msingi kwa njia ya Mapokeo; waliithibitisha kwa njia ya Maandiko ya Agano Jipya; na wakaihubiri kama sehemu muhimu sana ya Fumbo la Pasaka yaani: mateso na kifo cha Kristo Msalabani. Kristo amefufuka kwa wafu, kwa kifo chake alishinda dhambi na mauti na amewakirimia wafu uzima wa milele. Kaburi tupu na vitambaa vilivyolala ni ushuhuda wa Kristo Mfufuka. Kristo Yesu wa kwanza katika wafu ni msingi wa ufufuko wetu, tangu sasa kwa kufanywa haki roho yetu na baadaye kwa kuhuishwa miili yetu. Rej. KKK 638-658. Tunashangilia utimilifu wa ahadi ya Mungu, ahadi ya kuwaletea taifa lake ukombozi wa milele kwa njia ya sadaka ya mwanaye mpenzi Bwana wetu Yesu Kristo, baada ya anguko la wazazi wetu wa kwanza Adamu na Eva. Nasi tunashiriki mateso kifo na ufufuko wa Kristo kwa njia ya ubatizo wetu. tunapokea zawadi kubwa ya ukombozi kutoka katika utumwa wa dhambi na kuanza safari ya mpya ya maisha ndani ya Kristo mfufuka. Herini nyote kwa sherehe ya Pasaka. Kwa njia ya Ubatizo, tunakufa na kufufuka pamoja na Kristo na tunaanza safari ya maisha yetu mapya hapa duniani kuelekea kuungana na Mungu muumba wetu mbinguni. Hivyo Ndugu zangu, ili kuwa mashuhuda wa kweli wa maisha ya Yesu Mfufuka, tunapaswa na tunaalikwa kuijua na kuiishi vyema imani yetu.

Ufufuko wa Kristo Yesu ni msingi wa imani ya Kanisa
Ufufuko wa Kristo Yesu ni msingi wa imani ya Kanisa

Somo la Injili: Ni Injili ya Yn 20:1-9: Somo la Injili kutoka kwa Mwinjili Yohane, linaeleza ukweli mkuu wa Imani yetu kwamba Kristo amefufuka. Ushahidi juu ya hili upo wazi kabisa, kwanza Kaburi tupu, Bwana hayupo tena kaburini, pili, vitambaa na sanda alivyolalia vinatupa uthibitisho kwamba amefufuka, tatu, katika Injili nyingine, Malaika anathibitsiha kwamba hayupo tena kaburini, amefufuka. Nne, zaidi ya hayo yote akajionyesha kwa wafuasi wake kwa nyakati mbalimbali akiwadhihirishia kuwa amefufuka kama alivyosema. Sisi nasi tunaadhimisha leo na tunashuhudia kwamba Kristo amefufuka. Tunaalikwa kama Maria Magdalena na Mitume walipotoka kwa haraka kwenda kueneza habari kwamba Kristo amefufuka, nasi tutoke na kueneza furaha hii ya Kristo mfufuka kwa wengine. Tuupeleke mwanga wa Kristo Mfufuka kwa mataifa yote. Katika somo la Injili Takatifu tunapata mafundisho makubwa mawili ya kujifunza. Fundisho la Kwanza: Kwa nini tunasherehekea Pasaka? Pasaka ni Sherehe kubwa na ya muhimu sana katika utume na maisha yetu sisi waamini na kanisa kwa ujumla. Maana ya kawaida ya Pasaka au kwa Kiingereza Easter ni, “Sherehe ya maua mapya.” Maua yanayochipua na kuchanua ni ishara ya matumaini mapya, ishara ya uhai. Tunasherehekea Pasaka kwa furaha na shangwe kwa sababu kuu tatu. Kwanza: Ufufuko wa Kristo ni msingi wa Imani yetu: Ufufuko wa Kristo unatuthibitishia kuwa Kristo ni Mungu. Mtume Paulo anatuambia katika waraka wa kwanza kwa Wakorinto 15:14,17,20 kwamba kama Kristo asingalifufuka Imani yetu ni bure na kwamba Kristo amefufuka kutoka wafu ni limbuko lao wote waliolala.

Waamini wanapaswa kutangaza na kushuhudia Habari NJema
Waamini wanapaswa kutangaza na kushuhudia Habari NJema   (ANSA)

Katekisimu ya Kanisa Katoliki namba 638 ina tufundisha kuwa, Ufufuko wa Kristo ni taji ya ukweli wa Imani yetu kwa Kristo, imani waliyoiishi Mitume na jumuiya ya wakristo wa kwanza, iliyorithishwa kwa vizazi vilivyofuata kwa njia ya mapokeo ya kanisa. Hivyo tunaweza kabisa kusema kuwa kama Kristo asingalifufuka basi Kanisa lisingekuwepo leo hii na Imani yetu ingekua ni bure. Pili: Ufufuko wa Kristo unatupa uhakika juu ufufuko wetu pia. Yesu katika Injili ya Yohane 11:25-26 anamhakikishia Martha dada yake na Lazaro wakiwa mbele ya kaburi la Lazaro kwamba, “Mimi ndimi ufufuo na uzima, yeye aniaminiye mimi hata akifa, atakua anaishi” Kristo atatufufua sisi siku ya mwisho na hii ni hakika kwa kuwa, kwa ubatizo tumekwisha kufa na kufufuka pamoja na Kristo. Kwa njia ya Roho Mtakatifu tunapata neema ya kushiriki katika kifo na ufufuko wa Kristo (KKK #1002-1003). Tatu: Pasaka inatupa moyo na matumaini katika ulimwengu huu uliojaa maumivu, uchungu na machozi. Pasaka inatupa uhakika wa uwepo wa Kristo Mfufuka katika roho zetu, katika Kanisa, katika Neno lake Takatifu, katika Sakramenti zake mbalimbali na katika nyakati mbalimbali za maisha ya Mkristo. Kristo anasafiri nasi katika njia yetu ya msalaba hapa duniani, njia iliyojaa kila aina ya madhila, hofu, uchungu, machozi, maumivu, kuanguka na udhaifu. Yeye aliyetembea kwa uaminifu mkubwa pasi na kuchoka katika njia yake ya msalaba anatupa nasi pia moyo wa kuendelea kuvumilia na kuchukua misalaba yetu kwa imani na matumaini ili kwayo tuweze kuupata uzima wa milele. Yapo matumaini ya uzima mpya, uzima wa milele hata licha ya mateso na maumivu ya ulimwengu huu.

Fumbo la Pasaka ni chemchemi ya wokovu, imani na matumaini
Fumbo la Pasaka ni chemchemi ya wokovu, imani na matumaini   (Vatican Media)

Fundisho la Pili: Sababu kwa nini tunaamini katika ufufuko wa Kristo. Fundisho la pili tunalotafakari leo ni sababu kwa nini tunaamini katika ufufuko wa Kristo. Ningependa tutafakari sababu sita. Kwanza: Yesu mwenyewe alitabiri juu ya Mateso, kifo na ufufuko wake. Yesu alitabiri juu ya mateso, kifo na ufufuko wake ili kuudhihirisha Umungu wake aliposema, “Livunjeni hekalu hili nami nitalijenga kwa siku tatu” (Yn 2:19). Kumbe, alipoyasema haya pale hekaluni baada ya kuwafukuza wale waliokua wanafanya biashara na mambo yasiyofaa katika hekalu, Yesu alitabiri tayari juu ya mateso, kifo na ufufuko wake.  Pili: Kaburi wazi. Kaburi wazi linatupa uhakika kuwa Kristo amefufuka kutoka wafu. Ni utimilifu wa utabiri juu ya masiya. Malaika anawaambia waliokwenda kaburini, kwa nini mwamtafuta aliye hai, amefufuka hapa hayupo (Lk 24:5-6). Hapa sio swala tu la kaburi wazi bali ni Kristo mfufuka anayeishi ndani ya mioyo ya waamini daima. Mioyo iliyokosa matumaini, iliyokuwa wazi inajazwa sasa na Roho ya Kristo mfufuka kwa matumaini mapya na uzima. Tatu: Kutokuamini kwa Mitume na Kristo kujidhihirisha kwao mara nyingi baada ya ufufuko. Mara baada ya Yesu kufa, mitume walijawa na hofu, walipoteza matumaini kwa kwa Kristo, Bwana na mwalimu wao. Baada ya ufufuko, Mitume bado walikua wazito kuamini na Kristo anawatokea mara kwa mara akiwakumbusha na kuwathibitishia kwamba ni yeye. Mitume wanapata nguvu ya kwenda kumtangaza Kristo mfufuka baada ya kupokea Roho Mtakatifu siku ya Pentekoste. Wanakwenda kutoa ushuhuda juu ya ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo kama tulivyosikia katika Masomo yote matatu yakieleza juu ya ufufuko wa Yesu Kristo.

Kristo Yesu ni Mwanga wa Matumaini
Kristo Yesu ni Mwanga wa Matumaini   (Vatican Media)

Nne: Ushuhuda wa Mitume wa Kristo, kutoka kutokuamini kwao hadi kuamini. Mitume walipoteza kabisa matumaini, wengine wakaanza kurudi tena kuendelea kufanya kazi zao waliozokua wanafanya kabla ya kuitwa na Kristo. Kristo anapowatokea, wanaondolewa hofu na wanajawa na furaha kubwa. Wanafunzi wa Emaus walisafiri na Yesu lakini hawakumtambua. Walimtambua katika kuumega mkate na mara baada ya kumtambua wanapata nguvu mpya na wanaondoka mara kurudi Yerusalemu, hofu na mashaka vikaondoka nao wakaamini tena. Imani ya mitume hawa ndio imani yetu sisi leo hii ya kwamba, Kristo ni mzima, amefufuka kutoka wafu, wajibu wetu ni kumwamini, kufurahi na kuwashirikisha wengine furaha hiyo. Tano: Utayari wa kufa kifo dini wa wanafuzi wa kwanza wa Yesu. Wanafunzi wa kwanza wa Yesu mara baada ya kushuhudia mateso na kifo cha Kristo, na zaidi ya yote wakashuhudia ufufuko wake na kupaa kwake mbinguni walipata nguvu ya kuendelea mbele katika kuhubiri Habari Njema na kuishuhudia imani yao hata katika mateso na kifo. Waling’amua kwa hakika kuwa mateso na kifo dini sio mwisho wa maisha bali ni mwanzo wa maisha mapya, maisha ya umilele. Wafia dini hawa wa kwanza wanatupa na sisi moyo kwamba kuna maisha baada ya kifo na imani kubwa katika ufufuko wa wafu inayopata msingi wake kutoka kwa Kristo mwenyewe. Sita: Kuongoka kwa Mtume Paulo (Gal 1:11-17, Mdo 9:1, 9:24-25, 26:15-18). Kuongoka kwa mtume Paulo kunaeleza kwa hakika kuwa Kristo alifufuka. Yesu anapomtokea Paulo ambaye hapo mwanzo alikua alilidhulumu na kulitesa kanisa, Paulo anathibitisha kuwa ni kutaniko lake na Kristo mfufuka. Anatokewa na Yesu mwenyewe ambaye kwa matendo ya Paulo, alimtesa na kuumiza. Paulo anaanza maisha mapya baada ya kukutana na Kristo mfufuka. Sisi leo tuanze nasi maisha mapya baada ya kukutana na Kristo Mfufuka.

Mshumaa wa Pasaka ni kielelezo cha Kristo Mfufuka
Mshumaa wa Pasaka ni kielelezo cha Kristo Mfufuka   (Vatican Media)

Somo la Kwanza: Ni kitabu cha Matendo ya Mitume 10:34, 37-43. Mitume wa Yesu mara baada ya Pentekoste, walipata nguvu na ujasiri wa kumshuhudia Kristo mfufuka na kutangaza kwa nguvu Habari ya Injili ya Kristo. Somo hili ni hotuba ya mtume Petro ambayo msingi wake ni Fumbo la Pasaka, yaani mateso, kifo na ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo. Ni Kristo yule aliyezaliwa na kuishi kati ya Wayahudi, akahukumiwa na kuuwawa ndiye aliyefufuka na ndiye aliyewapa nguvu na ujairi wa kumhubiri. Mtume Petro pamoja na Mitume wengine walifanya kazi kubwa ya kuhubiri Injili, na hapa Injili imefika mpaka kwa watu mataifa ambao hapo Mwanzo hawakumjua Kristo. Mtakatifu Petro baada ya kupata maono, alikiri ya kuwa Mwenyezi Mungu hana upendeleo. Zawadi ya Mungu ya ukombozi kwa watu wake ni bure na ipo wazi kwa watu wote wanaotafuta wokovu.  Kumbe Mtume Petro anatukumbusha kuwa, sisi sote twapaswa kupokea zawadi ya ukombozi na kuwa mashuhuda wa Kristo kwa watu wote. Wapo watu wengi ambao bado hawajamjua Kristo, bado hawajasikia Habari Njema ya Injili, bado wapo katika giza. Sisi sote tuliobatizwa na kushirikirikishwa zawadi ya ukombozi kwa njia ya Kristo tunatumwa kuwa wamisionari wa matumaini na ufufuko wake.

Fumbo la Pasaka ni chemchemi ya wokovu, imani na matumaini
Fumbo la Pasaka ni chemchemi ya wokovu, imani na matumaini   (Vatican Media)

Somo la pili: Ni waraka wa Mtume Paulo kwa Wakolosai 3:1-4. Somo la pili linatueleza namna gani sisi tunapaswa kuishi Fumbo hili la Pasaka. Mtume Paulo akiwaandikia Jumuiya ya Kolosai juu ya ufufuko, anawaambia kuwa siku ya ubatizo walizaliwa katika maisha mapya, maisha yatakayofikia ukamilifu wake si kwa mambo ya dunia hii bali kwa kuungana kabisa na Mungu. Kumbe maisha ya hapa duniani ndiyo yanayotofautisha kati ya waamini na wasioamini. Katika ubatizo wetu tulikufa na kufufuka na Kristo na tukaahidi kumfuasa daima katika nyakati zote za maisha yetu. Hayo yapaswa kuwa maisha yetu kila siku, kuuishi vyema ukristo wetu, hayo ndiyo maisha ya kipasaka. Sisi tunaalikwa kufanya nini katika sherehe hii ya Pasaka? Katika sherehe hii ya pasaka sisi sote tunaalikwa kufanya mambo yafuatayo. Tunaalikwa kuwa watu wa ufufuko. Sherehe hii ya Pasaka inatupa ujumbe wa furaha na matumaini kwamba sisi pia tunaalikwa kuwa watu wa ufufuko. Kuwa watu wa ufufuko maana yake ni nini? Hii ina maana kuwa hatupaswi kubaki wafu tena katika maisha ya dhambi. Hatupaswi kubaki tena katika makaburi yetu, kaburi la dhambi, udhaifu, uregevu, vilema, mazoea mabaya, uchoyo, ubinafsi nk. Pasaka inatupa sisi Habari Njema kwamba, hakuna kaburi tena inaweza kutufunga, kaburi ya kukata tama, kukatisha wengine tamaa, kukosa imani, na kifo chenyewe. Vyote hivi havina nguvu tena na kutufunga na kutushinda kwa maana Kristo amevishinda nasi tunapata nguvu kwamba havitatuangusha. Tunaalikwa kuishi maisha ya Upendo na Msamaha wa kweli. Pasaka inatualika sisi sote kuishi maisha ya upendo, furaha na amani sisi kwa sisi, tukidhihirisha kwa matendo yetu uwepo kweli wa Kristo mfufuka katika familia zetu, jumuiya zetu, maeneo yetu ya kazi na kila mahali tutakapokuwa panukie harufu nzuri ya maisha mapya ya ufufuko. Tupendane, tuhurumiane, tusahemeheane na kusaidiana kindugu. Tuitafute Amani na furaha yetu kwa Kristo Mfufuka. Uwepo wa kudumu wa Kristo mfufuka kati yetu unatuhakikisha furaha isiyo na mwisho, furaha ya mbinguni hata katika nyakati ngumu, nyakati za uchungu, misiba, magonjwa na changamoto nyingine mbalimbali.  Kristo anapowatokea mitume wake ambao walikua wamechanganyikiwa kwa hofu, wakiwa wamejifungia ndani anawaambia, “Amani iwe kwenu” Yn 20:19. Sisi tunapopita katika nyakati ngumu za mateso makali na mkato wa tama, tuisikie daima sauti ya Kristo inayosema nasi kwa upole, “Amani iwe kwenu”. Kumbe amani na furaha ya kweli tutaipata tu katika kuungana daima na Kristo Mfufuka.

Fumbo la Pasaka ni chemchemi ya wokovu, imani na matumaini
Fumbo la Pasaka ni chemchemi ya wokovu, imani na matumaini

Tunaalikwa kuwa kioo cha kumdhihirisha Kristo Mfufuka kwa wengine. Pasaka inatulika kuwa kioo cha kumuonesha Kristo kwa ulimwengu mzima. Kwa njia ya maisha yetu ya kila siku, kwa kupenda, kwa kusamehe, kwa kusaidiana, kwa kuguswa na shida za wengine, kwa kuhurumia na kujitoa sadaka, kwa kuvumilia katika mateso na ustahimilivu katika kubebea misalaba yetu, tunaonesha kwa ulimwengu kwamba Kristo Mfufuka anaishi ndani yetu. Tunaalikwa kukumbuka Pasaka katika kila Ijumaa kuu zetu. Pasaka inatualika kutambua kuwa katika kila Ijumaa kuu kuna furaha ya Pasaka. Kila mara tunapokutana na magumu na mateso, tunaposalitiwa na kunyanyaswa bila hatia, katikati ya nyakati ngumu za maisha yetu tuone nguvu ya ufufuko wa Kristo ili ndani mwetu, ya kwamba hayo yote tunapoyapokea na kuyaunganisha na mateso ya Kristo, Kristo mwenyewe atatuinua. Yeye aliyepitia kila aina ya mateso hata kufa msalabani, Mungu alimfufua siku ya tatu. Hakuna mateso na magumu yasiyokuwa na mwisho. Tumshirikishe naye atatuinua katika Pasaka mpya ya maisha yetu. Pasaka ni maisha, sio jambo tu la kufikirika. Baba Mtakatifu Francisko kwenye moja katika ya jumbe zake za Pasaka aliwahi kusema, inawezekana mara zote kuanza tena kila kitu upya kwa sababu daima kuna maisha mapya ambayo Mungu anayaamsha tena ndani mwetu licha ya udhaifu na kushindwa kwetu. Jambo la pili Baba Mtakatifu anatukumbusha kuwa, Imani sio mkanda wa picha za matukio ya nyuma bali ni jambo jipya kila siku. Kristo hapitwi na wakati wala imani kwake sio tu jambo la kihistoria bali ni maisha yetu ya kila siku. Mwisho Baba Mtakatifu anatuambia kuwa, Yesu anatupenda bila kikomo na yupo nasi katika nyakati zote za maisha yetu. Hitimisho: Katika Dominika hii ya Pasaka, tumshukuru Mungu ambaye ametupenda kwa mapendo makuu, ambaye amekubali kuwa sawa na sisi ili aturudishie tena uzima wa kimungu tulioupoteza kwa sababu ya dhambi kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wake. Tuombe neema ya kumshuhudia Kristo mfufuka kwa maneno na matendo yetu.

19 Aprili 2025, 16:37