Sherehe ya Pasaka ya Bwana: Kiini cha Liturujia Na Imani ya Kanisa
Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.
Tafakari ya Neno la Mungu, Sherehe ya Pasaka, Siku ya ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo. Wimbo wa mwanzo unaofungua maadhimisho ya siku hii takatifu sana unaweka wazi tunacho kisherehekea ukisema; “Nimefufuka na ningali pamoja nawe, umeniwekea mkono wako, maarifa hayo ni ya ajabu, alaluya” (Zab. 139: 18, 5-6). Ufufuko wa Kristo Yesu ni kilele cha ukweli wa imani ya Kikristo, ambayo jamii ya kwanza ya wakristo iliusadiki na kuuishi kama kiini cha ukweli; waliiendeleza kama msingi kwa njia ya Mapokeo; waliithibitisha kwa njia ya Maandiko ya Agano Jipya; na wakaihubiri kama sehemu muhimu sana ya Fumbo la Pasaka yaani: mateso na kifo cha Kristo Msalabani. Kristo amefufuka kwa wafu, kwa kifo chake alishinda dhambi na mauti na amewakirimia wafu uzima wa milele. Kaburi tupu na vitambaa vilivyolala ni ushuhuda wa Kristo Mfufuka. Kristo Yesu wa kwanza katika wafu ni msingi wa ufufuko wetu, tangu sasa kwa kufanywa haki roho yetu na baadaye kwa kuhuishwa miili yetu. Rej. KKK 638-658. Pasaka ya Bwana ni siku ya uumbaji mpya ambapo mwanadamu alirudishiwa sura na mfano wa Mungu alioupoteza kwa dhambi ya asili. Hali hii ndiyo inayoifanya Pasaka kuwa ni sikukuu ya sikukuu, sherehe ya sherehe. Mtakatifu Atanasi anaiita Dominika Kuu. Sio tena sikukuu ya wayahudi ya kukumbuka kutolewa kwao utumwani Misri. Bali ni siku ya ulimwengu wote kukombolewa kutoka utumwa wa dhambi na mauti. Ni katika tumaini hili mama Kanisa katika sala ya mwanzo anasali hivi; “Ee Mungu, umetufungulia leo mlango wa milele kwa njia ya Mwanao wa pekee aliyeshinda mauti. Tunakuomba utujalie sisi tunaodhimisha kufufuka kwake Bwana wetu, tufufuke katika nuru yako kwa kufanywa wapya na Roho wako.” Basi hatuna budi kuimba na kushangilia tukisema; “Bwana amefufuka kweli kweli, aleluya. Utukufu na ukuu una Yeye hata milele na milele” (Lk. 24:34; Ufu. 1:6).
Somo la kwanza ni la kitabu cha Matendo ya Mitume (Mdo.10:34; 37-43). Somo hili ni hotuba ya Mtume Petro nyumbani kwa Kornelio, Jemedari wa jeshi la Kirumi aliyekaa katika mji wa Kaisaria. Maandiko yanasimulia kuwa Kornelio alikuwa mtu mwadilifu na mkarimu. Hivyo alipata maono akiagizwa atume wajumbe waende katika mji wa Yafa alikokuwako Petro akisali, ili wamuite aje kuwahubiria habari za Kristo mfufuka. Petro naye kwa njia ya ndoto aliambiwa asisite kuwafuate wajumbe hao na kwenda nao nyumbani kwa Kornelio. Petro alitii agizo hili licha ya kuwa ilikuwa ni kinyume na sheria ya kiyahudi ya katazo la kuingia katika nyumba za wapagani. Petro alipofika, Kornelio alimkaribisha kwa heshima kubwa na kumwambia; “tupo hapa kusikiliza ujumbe ambao Mungu amekupa kwa ajili yetu”. Mtume Petro aliwaeleza habari za kuja kwake Yesu Kristo duniani, mahubiri yake na matendo makuu aliyoyatenda kwa miujiza mingi, ikiwa ni pamoja na kuwaponya watu magonjwa yao. Lakini alihukumiwa kifo cha msalaba pasipo na hatia (Mdo 10:39), na siku tatu Mungu alimfufua kutoka wafu (Mdo 10:40), na wao mitume ni mashahidi wa tukio hili kwa kuwa walikula na kunywa naye baada ya kufufuka kwake na kwa jina lake kila amwaminiye atapata ondoleo la dhambi na kuurithi uzima wa milele. Ni katika muktadha huu wimbo wa katikati unasema hivi; “Siku hii ndiyo aliyoifanya Bwana, tutashangilia na kuifurahia. Aleluya. Mshukuruni Bwana kwa kuwa ni mwema, kwa maana fadhili zake ni za milele. Israeli na aseme sasa, ya kwamba fadhili zake ni za milele. Mkono wa kuume wa Bwana umetukuzwa, mkono wa kuume wa Bwana hutenda makuu. Sitakufa bali nitaishi, nami nitayasimulia matendo ya Bwana. Jiwe walilolikataa waashi, limekuwa jiwe kuu la pembeni. Neno hili limetoka kwa Bwana, nalo ni ajabu machoni petu” (Zab. 118, 24, 1-2, 16-17, 22-23).
Katika Dominika ya ufufuko wa Bwana Misa ya mchana, Mama Kanisa ameweka masomo mawili ya kuchagua kwa somo la pili. Linaweza kusomwa somo la waraka wa Mtume Paulo kwa Wakolosai (Kol. 3:1-4) au somo la Waraka wa kwanza wa Mtume Paulo kwa Wakorintho (1Kor. 5:6-8). Katika somo la Waraka wa Mtume Paulo kwa Wakolosai (Kol. 3:1-4), Mtume Paulo anayaweka wazi matunda ya ufufuko kuwa ni kufanywa upya na kurudishwa katika maisha ya kweli katika Kristo. Hii inaonyesha jinsi gani Sherehe ya Pasaka ilivyo na maana kubwa katika maisha yetu! Lakini kufufuka huku katika maisha mapya katika Kristo kusipofanyika ndani ya mioyo yetu, furaha yetu ya kipasaka ni bure. Katika ubatizo tulikufa na kufufuka na Kristo, tukaahidi kumfuata daima katika taabu na raha. Hivyo yatupasa kuishi kadiri ya ahadi hiyo tukiacha mabaya na kutenda mema. Hivyo mawazo yetu yanapaswa kulenga mambo ya mbinguni, na siyo ya duniani. Kwa maana kwamba, yote tunayofanya katika maisha yetu hapa duniani, iwe ni kwa sifa na utukufu wa Mungu. Katika somo la Waraka wa Kwanza kwa Wakorintho (1Kor. 5:6-8), Mtume Paulo anatufundisha kuwa; kama ilivyokuwa kwa waisraeli kabla ya kula mwana kondoo wa Pasaka walitoa kwanza chachu yote ya zamani nyumbani mwao, yaani walijipatanisha wao kwa wao, na wao na Mungu, na hivyo kuacha maisha mabaya ya zamani na kuanza maisha mapya, maisha mema. Ndivyo tunavyopaswa kufanya nasi tunaposherehekea sikukuu ya Pasaka, kujipatanisha sisi kwa sisi na kujipatanisha na Mungu, huku ndiko kutoa chachu yote. Mtume Paulo anasisitiza hivi; “Kujisifu kwenu si kuzuri. Hamjui kwamba chachu kidogo hulichachusha donge zima? Basi, jisafisheni, mkatoe ile chachu ya kale, mpate kuwa donge jipya, kama vile mlivyo hamkutiwa chachu. Kwa maana Pasaka wetu amekwisha kutolewa kuwa sadaka, yaani, Kristo; basi na tuifanye karamu, si kwa chachu ya kale, wala kwa chachu ya uovu na ubaya, bali kwa yasiyochachika, ndio weupe wa moyo na kweli.”
Injili ni kama ilivyoandikwa na Yohane (Yn. 20:1-9). Sehemu hii ya Injili inasimulia ukweli mkuu wa imani yetu kwamba Kristo amefufuka kweli kweli, aleluya, ameshinda dhambi na mauti. Ni katika tumaini hili Mama Kanisa katika sala ya kuombea dhabihu anakiri kuwa “Kristo ametolewa sadaka awe Paska yetu. Yeye ndiye Mwana kondoo wa kweli aliyeondoa dhambi za ulimwengu, alishinda mauti yetu kwa kufa kwake, na akaturudishia uzima wetu kwa kufufuka kwake.” Kumbe basi tunaweza kusema kuwa kwetu sisi ufufuko ni mabadiliko kutoka utu wa kale kwenda utu upya, kutoka maisha ya dhambi kwenda maisha ya utakatifu kwa kuzaa matunda ya rohoni ambayo ni upendo, furaha, amani, mshikamamo, uvumilivu, unyenyekevu, utii na uchaji kwa Mungu (Gal. 5:22-23). Kwa kuwa tumefufuka pamoja na Kristo tuepuke matendo ya mwili yanayotutia unajisi kama vile; chuki, fitina, ufisadi, ibada ya sanamu, uadui, ugomvi, kijicho, hasira, ubinafsi, utengano, mafarakano, wivu, ulevi, ulafi, ushirikina, uzinzi na uasherati (Wagalatia 5:19-20). Ndiyo kusema Pasaka kwetu ni siku ya kurejesha matumaini kama tulikuwa tumekata tamaa ya maisha. Pasaka ni Habari Njema kwetu kwamba Kristo Mfufuka yuko kati yetu, yupo pamoja nasi na ndani ya kila mmoja wetu. Ni katika muktadha huu tunaweza kuuonja ukuu wa Sherehe ya Pasaka, kuwa ni siku ya kuzaliwa upya, kuumbwa upya, kurudishiwa sura na mfano wa Mungu ndani mwetu. Naye mama Kanisa akiutambua ukuu huu, katika sala kuombea dhabihu anasali hivi; “Ee Bwana, tunakutolea sadaka kwa furaha ya Sherehe ya Pasaka, Kanisa lako linazaliwa upya na kulishwa kwa sadaka hizi”. Katika utangulizi anashuhudia hivi; “Yeye ndiye Mwana kondoo wa kweli aliyeondoa dhambi za dunia. Alishinda mauti yetu kwa kufa kwake, akaturudishia uzima wetu kwa kufufuka kwake”. Na katika sala baada ya komunyo anahitimisha maadhimisho ya Sherehe hii Takatifu sana akisali hivi; “Ee Mungu, ulilinde Kanisa lako kwa wema wako wa siku zote, litiwe nguvu mpya kwa mafumbo haya ya Paska na kuifikia nuru ya ufufuko”. Na hili ndilo tumaini letu. Tumsifu Yesu Kristo!