Baba Mtakatifu Francisko katika hotuba yake amekazia kuhusu maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo, Diplomasia ya Vatican. Baba Mtakatifu Francisko katika hotuba yake amekazia kuhusu maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo, Diplomasia ya Vatican.  (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Hotuba ya Baba Mtakatifu Francisko Kwa Wanadiplomasia: Diplomasia ya Matumaini

Papa Francisko amekazia kuhusu: maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo; Diplomasia ya matumaini na ya ukweli inayosimikwa katika Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo; Diplomasia ya msamaha ili kuepuka vita, kinzani na migogoro; Mikataba ya Kimataifa inapaswa kuheshimiwa kwa uwajibikaji katika mchakato wa ujenzi wa amani; Uhuru wa kuabudu na kidini uwawezeshe wananchi kushiriki kikamilifu katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko mwanzoni kabisa mwa Mwaka 2025, tarehe 9 Januari amekutana na kuzungumza na Mabalozi pamoja na wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa mjini Vatican. Katika maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025, ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, Mwaka huu utakuwa ni mwaka wa neema, mwaka ambao umesheheni ukweli na msamaha; haki na amani na kwamba, katika kila sakafu ya moyo wa mwanadamu matumaini yabubujike na kushamiri na kwamba, walimwengu waonje tena amani, utulivu, ustawi na maendeleo, mambo ambayo yanaonesha kiu ya binadamu katika ulimwengu mambo leo. Baba Mtakatifu katika hotuba yake amekazia kuhusu maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo, Diplomasia ya Vatican, Hija za Kitume, Ukarimu wa Waroma, Ulinzi na Usalama. Yote haya yanahitaji: Diplomasia ya matumaini, Diplomasia ya ukweli inayosimikwa katika Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo; Diplomasia ya msamaha ili kuepuka vita, kinzani na migogoro; Mikataba ya Kimataifa inapaswa kuheshimiwa kwa uwajibikaji katika mchakato wa ujenzi wa amani; Uhuru wa kuabudu na kidini uwawezeshe wananchi kushiriki kikamilifu katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Huu ni mwaliko kwa Jumuiya ya Kimataifa kujikita katika diplomasia ya uhuru wa kweli inayofumbata diplomasia ya haki sanjari na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Baba Mtakatifu Francisko anasema, Kanisa Katoliki linaadhimisha Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo, kwa kukazia mambo msingi yanayowaunganisha watoto wateule wa Mungu. Ni fursa ya kugundua tena kwamba, wote ni watoto wa Mwenyezi Mungu, kumbe, ni ndugu wamoja, wanaopaswa kuheshimiana, kupendana na kusameheana; kuwakumbutia maskini na kujitahidi kutunza ardhi; kwa kutenda haki ili hatimaye, kuibua tena Injili ya matumaini, kwa kutambua kwamba, siasa kimsingi ni huduma ya upendo. Vatican katika kukuza na kudumisha diplomasia yake, katika kipindi cha Mwaka 2024, Baba Mtakatifu amebahatika kukutana na kuzungumza na wakuu wa nchi na serikali wapatao thelathini. Vatican imetia saini mikataba kati yake na Burkina Faso, Jamhuri ya Watu wa Czech.

Jubilei ya Miaka 2025 ni fursa ya kukuza matumaini
Jubilei ya Miaka 2025 ni fursa ya kukuza matumaini   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Baba Mtakatifu amegusia kuhusu: Mkataba wa Kihistoria wa Muda Mfupi kati ya Vatican na China Kuhusu Uteuzi wa Maaskofu Mahalia uliotiwa saini kwa mara ya kwanza tarehe 22 Septemba 2018; ukapyaishwa tena tarehe 22 Oktoba 2020, 22 Oktoba 2022 na hatimaye, tarehe 22 Oktoba 2024. Mkataba umeongezwa tena kwa muda wa miaka minne yaani hadi mwaka 2028. Papa anapenda kuonesha uvumilivu unaosimikwa katika matumaini, ili kuwapatia watu wa Mungu wachungaji wema na watakatifu. Hiki ni kielelezo kwamba, Vatican inapenda kuendelea kujikita katika majadiliano kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya Kanisa na watu wa Mungu nchini China katika ujumla wake. Hija za kitume Kimataifa zinapania pamoja na mambo mengine: kuwaimarisha ndugu zake katika imani, mapendo na matumaini, kwa kuendelea kujikita katika kutangaza na kushuhudia amani inayofumbatwa katika ukweli, uwazi, udugu wa kibinadamu na upatanisho wa kitaifa. Ni muda muafaka wa kujikita katika majadiliano ya kidini, kiekumene na kijamii. Ni nafasi ya kuwatia shime Waamini kuendelea kushirikiana na kufarijiana. Katika kipindi cha Mwaka 2024 Baba Mtakatifu ametembelea: Indonesia, Papua New Guinea, Timor ya Mashariki na Singapore. Akiwa nchini Italia amebahatika kutembelea Majimbo ya Verona, Venezia na Trieste. Baba Mtakatifu amewashukuru viongozi wa Serikali na watu wa Mungu Jijini Roma kwa moyo wao wa upendo na uvumilivu wakati wa utekelezaji wa miradi mbalimbali ya Jubilei ya miaka 2025 ya Ukristo. Wajiandae sasa kuwapokea na kuwakaribisha mahujaji na wageni ambao wamekwisha anza kuwasili. Baba Mtakatifu anavipongeza vyombo vya ulinzi na usalama kwa kazi kubwa wanazozitekeleza, ili kuhakikisha kwamba, kunakuwepo na ulinzi na usalama kwa raia na mali zao.

Hija ya Kitume ya Papa Francisko zinapania kujenga imani, matumaini na mapendo
Hija ya Kitume ya Papa Francisko zinapania kujenga imani, matumaini na mapendo   (Vatican Media)

“Roho wa Bwana yu juu yangu, Kwa maana amenitia mafuta kuwahubiri maskini habari njema. Amenituma kuwatangazia wafungwa kufunguliwa kwao, Na vipofu kupata kuona tena, Kuwaacha huru waliosetwa, Na kutangaza mwaka wa Bwana uliokubaliwa.” Lk 4:18-19. Huu ni muhtasari wa Fumbo la Umwilisho na Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo. Pamoja na ukweli huu, bado dunia inaendelea kushuhudia vitendo vya kigaidi kama vile vilivyoshuhudiwa huko Magdeburg, nchini Ujerumani na New Orleans nchini Marekani. Bado habari za kughushi zinaendelea kusababisha kinzani na misigano; nyanyaso na dhuluma, kiasi cha kuhatarisha amani na mafungamano ya Kitaifa na Kimataifa. Baba Mtakatifu amewakumbuka na kuwaombea viongozi wa Slovakia na Rais mteule wa Marekani, walionusurika kuuwawa hivi karibuni Baba Mtakatifu emegusia mgawanyiko uliopo kwenye Kisiwa cha Cyprus, hali ambayo imesababisha mpasuko wa mafungamano ya kijamii kwa zaidi ya miaka hamsini, kumbe, bado kunahitajika kukutana, kufahamiana na kujadiliana. Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025 iwe ni fursa ya kujenga na kudumisha utamaduni wa watu kukutana katika umoja, kwa kutambua kwamba, wao ni mahujaji wa faraja. Diplomasia isaidie kunogesha majadiliano katika ukweli na uwazi; ili hatimaye, kuweza kuvunjilia mbali mnyororo wa chuki na uhasama; ubinafsi, kiburi na majigambo chanzo cha uharibifu na vita. Huu ni mwaliko kwa Jumuiya ya Kimataifa kujikita katika diplomasia ya matumaini kwa kuzama katika ujenzi wa amani, viongozi wa kisiasa wahakikishe kwamba, wanatekeleza dhamana na wajibu wao barabara, kwa kujikita katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Diplomasia ya matumaini
Diplomasia ya matumaini   (AFP or licensors)

Huu ni muda muafaka wa kuwatangazia maskini Habari Njema ya Wokovu na kwamba, kila mtu anaweza kuwa ni chombo cha matumaini na ukweli. Vyombo vya mawasiliano ya jamii pamoja na teknolojia ya akili mnemba visitumiwe vibaya kwa ajili ya malengo ya kiuchumi, kisiasa na kiitikadi, bali visaidie kuboresha ujuzi na ufahamu wa binadamu. Lakini pia vyombo hivi vinaweza kuwa ni hatari sana ikiwa kama mitandao ya kijamii haitajikita katika maadili na utu wema na matokeo yake ni ongezeko la michezo ya kamari mitandaoni na uraibu kwa vijana. Kumbe, viongozi wa Serikali wanapaswa kuhakikisha kwamba, njia hizi za mawasiliano zinatumika barabara kama chanzo cha ujuzi na maarifa; ukuaji wa mtu binafsi pamoja na ushiriki mkamilifu wa vijana katika ujenzi wa jamii yao. Baba Mtakatifu Francisko anasema, diplomasia ya ukweli ijenge na kudumisha mawasiliano jamii, majadiliano katika ukweli na uwazi; kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, kwa kuhakikisha kwamba, lugha inayotumika ni nyepesi na inaweza kueleweka kwa wengi; ni wazi na inachochea maridhiano. Diplomasia ya ukweli ilinde Injili ya uhai tangu pale mtoto anapotungwa mimba tumboni mwa mama yake hadi mauti inapomfika kadiri ya mpango wa Mungu. Kamwe hasiwepo mtoto au mzee anayenyimwa matumaini ya kuendelea kuishi! Uvamizi wa Urusi dhidi ya Ukraine umetia doa diplomasia na mahusiano ya Kimataifa. Urusi ilidai kwamba, uvamizi huu ulikuwa na lengo la kujiimarisha kimkakati upande wa Jeshi na pili ilikuwa ni kuondoa hatari za siasa za kibaguzi nchini Ukraine.

MIkataba ya Kimataifa inapaswa kuheshimiwa
MIkataba ya Kimataifa inapaswa kuheshimiwa

Kimsingi vita hii imevunja makubaliano ya kuundwa kwa Jumuiya ya Nchi Huru, Mkataba wa nchi mbili kati ya Urusi na Ukraine, Mkataba wa mpaka unaotambulika kimataifa wa Urusi na Ukraine, Mkataba wa Umoja wa Mataifa, Sheria ya Helsinki ya 1975 pamoja na Mkataba wa Budapest. Kumbe kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kujikita katika ujenzi wa mikataba ya amani duniani, kwa kukazia Sheria ya Kimataifa sanjari na kukuza ushirikiano na mshikamano kati ya pande zinazohusika, lengo ni kujenga na kudumisha amani na usalama duniani.Baba Mtakatifu anasema, diplomasia ya matumaini inakita mizizi yake kwenye diplomasia ya msamaha, kwa kusitisha vita, kinzani na misigano, ili kujenga mazingira ya amani ya kudumu, tayari kuganga na kuponya madonda ya vita, kinzani na misigano, kwa kuhakikisha kwamba, Israeli na Palestina zinasitisha vita; kwa kujenga daraja la majadiliano; kwa kuheshimiana na kuaminiana na kwamba, Yerusalemu uwe ni mji unaowakutanisha watu katika medani mbalimbali za maisha. Kuwepo majadiliano ya kidini na kiekumene. Itakumbukwa kwamba, tarehe 8 Juni 2014, Baba Mtakatifu Francisko aliungana na Hayati Simon Peres, Rais wa Israeli na Bwana Mahmoud Abbas -Abu Mazen, Rais wa Mamlaka ya Palestina pamoja na Patriaki Bartolomeo wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox la Costantinopoli kupanda miti ya kumbukumbu ya kuombea amani duniani.

Diplomasia ya haki na amani
Diplomasia ya haki na amani

Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kuwaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuungana pamoja naye kwa ajili ya kusali na kuombea amani katika Nchi Takatifu. Hili ni tukio ambalo linaonesha kwamba, majadiliano na ujenzi wa urafiki ni mambo yanayowezekana na kwamba, Jumuiya ya Kimataifa ishinde kishawishi cha kutumbukia katika mitazamo ya chuki na uhasama. Vita inaendelea kukuzwa na biashara haramu ya silaha sehemu mbalimbali dunia. Fedha inayotumika kwa ajili ya vita isaidie kuanzisha Mfuko wa Maendeleo, ili kuokoa maisha ya watoto wengi wanao teseka kwa vita, njaa na maradhi kwa utu na heshima yao kuendelea kusiginwa. Utakatifu wa maisha, utu, heshima na haki msingi za binadamu vilindwe kwa nguvu zote. Utekelezaji wa Sheria ya Kimataifa uwe ni jambo la lazima. Mkataba wa Kimataifa wa Geneva wa mwaka 1949 pamoja na itifaki zilizoongezwa baadaye ni chombo cha sheria kimataifa kinachoratibu hali tete wakati wa vita vya nchi kavu kwa kuwalinda raia, kuwahudumia askari waliojeruhiwa pamoja na kuwalinda mateka wa vita. Hii ni sheria inayozingatia utu, heshima na haki msingi za binadamu kimataifa. Mtakataba wa kwanza ulijihusisha na mchakato wa kuwalinda askari waliojeruhiwa vitani. Mkataba wa pili, ukaongezwa ili kuwasaidia askari wa majini waliojeruhiwa vitani na meli zao kuharibiwa. Mkataba wa tatu ulikusudiwa kwa ajili ya kuwalinda mateka wa vita, kwa kuzingatia athari zilizojitokeza wakati wa Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia pamoja na Vita Kuu ya Pili ya Dunia. Kwamba, mateka wa vita watapaswa kuachiwa huru mara tu vita inapokoma. Mkataba wa Nnne unahusu umuhimu wa kuwalinda na kuwasaidia raia wakati wa mapambano ya silaha; kwa kutenga maeneo maalum ambapo raia wanaweza kupata huduma bila upendeleo wowote ule. Kumbe, Mkataba wa Kimataifa wa Geneva wa mwaka 1949 umeridhiwa na Nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa na kwamba nchi zote zinawajibika kutekeleza yote yaliyobainishwa kwenye Mkataba huu.

Wakimbizi na wahamiaji ni amana na utajiri wa Kanisa na Jamii.
Wakimbizi na wahamiaji ni amana na utajiri wa Kanisa na Jamii.   (2023 Getty Images)

Huu ni Mkataba unaopaswa kuheshimiwa ili kukomesha vita nchini Sudan, Katika Ukanda wa Sahel, Kwenye Nchi zilizoko kwenye Pembe ya Afrika pamoja na DRC. Haya ni maeneo ambayo pia yameharibiwa kwa vitendo vya kigaidi, changamoto ya idadi kubwa ya wakimbizi na wahamiaji bila kusahau athari za mabadiliko ya tabianchi. Huu ni mwaliko kwa Jumuiya ya Kimataifa kuwa ni chombo cha amani na kwamba, tofauti zao msingi ni amana na utajiri na wala zisiwe ni chanzo chuki, uhasama kinzani na migawanyiko. Baba Mtakatifu amewakumbuka watu wa Mungu Myanmar, ambako watu wa Mungu wanaendelea kuteseka kutokana na vita ya wenyewe kwa wenywe na kwamba, kuna idadi kubwa ya wanachi imeyakimbia makazi yao. Haiti kwa sasa hali ni tete! Venezuela inapaswa kukita maisha yake katika tunu msingi zinazoheshimu: maisha, utu, haki na uhuru, ili kuanza tena mchakato wa majadiliano. Baba Mtakatifu amezikumbuka nchi kama Bolivia, Colombia, Nicaragua zinazopitia hali nguvu ya kisiasa, kijamii na kiuchumi na kwamba, Vatican iko tayari wakati wowote kuanzisha majadiliano na kwamba, uhuru wa kuabudu na uhuru wa kidini vitaheshimiwa. Amewataka watu wa Mungu nchini Lebanon wajibidiishe kuijenga nchi yao baada ya vita, ili kweli iweze kuwa ni mjumbe wa mariadhiano na amani. Baba Mtakatifu Francisko anasema biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo ni mambo ambayo yanafumbatwa kwa namna ya pekee kabisa katika: Kazi za suluba, ukahaba, biashara haramu ya binadamu pamoja na viungo vyake, biashara na matumizi haramu ya dawa za kulevya pamoja na uhalifu wa magenge; matendo yote haya ni uhalifu dhidi ya ubinadamu na yanapaswa kutambulika hivi na viongozi wa kidini, kisiasa na kijamii kama yanavyobainishwa na sheria za kitaifa na kimataifa bila kupindishwa pindishwa au kufumbiwa macho! Na kwamba, diplomasia ya matumaini inakita mizizi yake katika uhuru kamili, changamoto na mwaliko kwa Jumuiya ya Kimataifa, kukomesha janga hili.

Jubilei ni mwaka wa matumaini
Jubilei ni mwaka wa matumaini   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kusema, sera na mbinu mkakati wa Kanisa Katoliki katika huduma kwa wakimbizi na wahamiaji inajikita katika mambo makuu manne yaani: “Kuwapokea, kuwalinda, kuwaendeleza na kuwahusisha wakimbizi na wahamiaji” katika maisha ya jamii inayowapokea na kuwapatia hifadhi, usalama na matumaini ya maisha. Kumbe, kuna haja ya kuwasaidia wakimbizi na wahamiaji, lakini kwa kuendelea kutafuta ufumbuzi wa kudumu wa vyanzo vinavyopelekea watu kuzikimbia nchi na makazi yao. Diplomasia ya haki isaidie kufuta deni kwa nchi maskini duniani, sanjari na kutokomeza adhabu ya kifo ambayo kimsingi imepitwa na wakati. Baba Mtakatifu amewakumbuka watu wa Mungu walioathirika kutokana na mabadiliko ya tabianchi hasa katika: Nchi zilizoko kati kati ya Bara la Ulaya, Hispania, Madagascar, Moyotte na Msumbiji. Hii ni changamoto ya kuhakikisha kwamba, Jumuiya ya Kimataifa inasimama kidete kulinda, kutunza na kudumisha mazingira bora nyumba ya wote. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, Mkutano wa 29 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu mabadiliko ya tabianchi (COP-29) uliofanyika katika mji wa Baku nchini Azerbaijan, utasaidia kukoleza ushirikiano na mshikamano katika matumizi ya rasilimali, ili kupambana na athari za mabadiliko ya tabianchi pamoja na ufutwaji wa mzigo wa deni kubwa kwa nchi changa zaidi duniani. Baba Mtakatifu ametoa angalisho kwa Jumuiya ya Kimataifa kuhusu kuongezeka kwa deni la kiikolojia kati ya Nchi zilizko Kaskazini na Kusini. Vatican iko tayari kusindikiza mchakato wa ufutwaji wa deni la nje. Katika maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025, ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, Mwaka huu utakuwa ni mwaka wa neema, mwaka ambao umesheheni ukweli na msamaha; haki na amani na kwamba, katika kila sakafu ya moyo wa mwanadamu matumaini yabubujike na kushamiri na kwamba, walimwengu waonje tena amani, utulivu, ustawi na maendeleo, mambo ambayo yanaonesha kiu ya binadamu katika ulimwengu mambo leo.

Papa Diplomasia ya Matumaini

 

09 Januari 2025, 14:59