Ilikuwa ni tarehe 13 Machi 2013, Baraza la Makardinali lilipomchagua Kardinali Jorge Mario Bergoglio kuwa Khalifa wa Matakatifu Petro. Ilikuwa ni tarehe 13 Machi 2013, Baraza la Makardinali lilipomchagua Kardinali Jorge Mario Bergoglio kuwa Khalifa wa Matakatifu Petro. 

Kumbukizi ya Miaka 12 ya Maisha na Utume wa Papa Francisko!

Ilikuwa ni tarehe 13 Machi 2013, Baraza la Makardinali lilipomchagua Kardinali Jorge Mario Bergoglio kuwa Khalifa wa Matakatifu Petro na katika maadhimisho ya Sherehe ya Mtakatifu Yosefu, tarehe 19 Machi 2013, Papa akasimikwa rasmi na kuwa ni Khalifa wa Mtakatifu Petro wa 266 kwa kuchagua jina la Mtakatifu Francisko wa Assisi. Baba Mtakatifu anaadhimisha kumbukumbu hii akiwa bado amelazwa kwenye Hospitali ya Chuo Kikuu cha Agostino Gemelli iliyoko mjini Roma.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Ilikuwa ni tarehe 13 Machi 2013, Baraza la Makardinali lilipomchagua Kardinali Jorge Mario Bergoglio kuwa Khalifa wa Matakatifu Petro na katika maadhimisho ya Sherehe ya Mtakatifu Yosefu, Mume wake Bikira Maria, tarehe 19 Machi 2013, Baba Mtakatifu Francisko akasimikwa rasmi na kuwa ni Khalifa wa Mtakatifu Petro wa 266 kwa kuchagua jina la Mtakatifu Francisko wa Assisi. Baba Mtakatifu anaadhimisha kumbukumbu hii akiwa bado amelazwa kwenye Hospitali ya Chuo Kikuu cha Agostino Gemelli iliyoko mjini Roma tangu Ijumaa tarehe 14 Februari 2025; kwa hakika Baba Mtakatifu anasema: anaonja: umakini wa huduma na huruma kutoka kwa madaktari na wafanyakazi katika sekta ya afya. Baba Mtakatifu anawashukuru kutoka katika sakafu ya moyo wake wote na anawakumbuka wote wanaowahudumia wagonjwa sehemu mbalimbali za dunia, kama ishara ya uwepo na ukaribu wa Mungu kwa waja wake na kwamba, binadamu katika udhaifu wake anahitaji kuonjeshwa “Muujiza wa huruma ya Mungu” unaowaambata na kuwashindikiza wale wote walioko kwenye majaribu na kuwakirimia mwanga mdogo katika usiku mnene wa maumivu. Baba Mtakatifu anawashukuru kwa dhati kabisa waamini na watu wote wenye mapenzi mema, wanaoendelea kumwonesha uwepo wao wa karibu kwa njia ya Sala na Sadaka zao na kwamba, yeye pia anawakumbuka na kuwaombea. Hali ya afya ya Baba Mtakatifu inaendelea kuimarika zaidi na zaidi. Anaendelea kupata tiba, kusali na kufuatilia mafungo ya kiroho yanayotolewa kwa Sekretarieti kuu ya Vatican; kufanya mazoezi pamoja na kuendelea kupumzika zaidi na kwamba, usiku wa kuamkia Alhamisi tarehe 13 Machi 2025 Baba Mtakatifu amepana usingizi mnono!

Kumbukizi ya Miaka 12 tangu Papa  achaguliwe kuwa Khalifa wa Mt. Petro
Kumbukizi ya Miaka 12 tangu Papa achaguliwe kuwa Khalifa wa Mt. Petro   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi tarehe 13 Machi 2025 ameendelea kupokea salam na matashi mema kutoka sehemu mbalimbali za dunia, wakati huu anapofanya Kumbukizi ya Miaka 12 tangu alipochaguliwa kuwa ni Khalifa wa Mtakatifu Petro.Watu wa Mungu Jimbo kuu la Roma, wanamtakia heri na baraka, wakati huu anapoendelea kukabiliana na changamoto ya afya na kwamba, watu wa Mungu sehemu mbalimbali za dunia wanaendelea kusali na kumwombea afya njema! Wanamshukuru Baba Mtakatifu kwa Mafundisho yake; Unabii, sadaka na majitoleo yake katika kipindi cha miaka kumi na miwili. Hata katika hali yake ya ugonjwa, bado anaendelea kuwaenzi watu wa Mungu Jimbo kuu la Roma, mwaliko ni kuendelea kusonga mbele kwa matumaini na nguvu na kwamba, waamini wanaendelea kumsubiri ili kukutana naye tena, mara atakapokuwa ameruhusia kutoka hospitalini. Baraza la Maaskofu Katoliki Poland, katika mkutano wake wa 400 linamwombea Baba Mtakatifu na kuendelea kuwakumbusha waamini umuhimu wa kujikita katika upendo kwa Mungu na jirani. Anapoendelea kuubeba Msalaba Msalaba wa mateso pamoja na Kristo Yesu, Baba Mtakatifu anahitaji kutiwa shime kwa sala na sadaka ya waamini. Maaskofu wa Poland wanamtakia heri, neema na baraka, huku wakiendelea kushikamana katika hija ya maisha yao ya huduma kwa watu wa Mungu, huku wakielekea tumaini ambalo kimsingi ni Kristo Yesu. Salama na matashi mema yanatoka pia kwa Vahagn Khachaturyan, Rais wa Jamhuri ya Watu wa Albania. Bila kuwasahau Maaaskofu Katoliki kutoka Argentina.

Watu wa Mungu kutoka nchini Argentina wanasali na kumwombea Papa.
Watu wa Mungu kutoka nchini Argentina wanasali na kumwombea Papa.   (AFP or licensors)

Tangu Baba Mtakatifu Francisko achaguliwe kuliongoza Kanisa vipaumbele katika maisha na utume wake vimekuwa ni: Maskini, Amani, Mazingira na sasa ni ujenzi wa Udugu wa kibinadamu unaofumbatwa katika huruma na upendo wa Mungu usiokuwa na mipaka kwa waja wake wote. Maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii ni amana na utajiri wa Kanisa; wao ndio walengwa wakuu wa Habari Njema ya Wokovu. Hawa ni maskini wa hali na mali; wanaotumbukizwa katika biashara ya binadamu na viungo vyake; wanaodhalilishwa na kunyanyaswa utu, heshima na haki zao msingi kama watu walioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Hawa pia ni wakimbizi, wahamiaji na watu wanaotafuta hifadhi ya kisiasa. Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu kuanzia tarehe 8 Desemba 2015 hadi tarehe 20 Novemba 2016 katika Maadhimisho ya Sherehe ya Kristo Yesu, Mfalme wa Ulimwengu. Hii ilikuwa ni fursa adhimu kwa huruma ya Mungu kuwa ni kiini cha tafakari ya maisha na utume wa Kanisa; tafakari ambayo inapaswa kumwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu kwa njia ya matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Hii inatokana na ukweli kwamba, huruma ya Mungu ni kiini cha Injili na njia muafaka ya uinjilishaji mpya unaojikita katika mchakato wa ushuhuda wenye mvuto na mashiko, kielelezo cha imani tendaji! Imekuwa ni nafasi kwa waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuchunguza dhamiri zao, ili kuangalia ikiwa kama maisha yao yanaendana na kweli za Kiinjili zinazotangazwa na kushuhudiwa na Mama Kanisa.

Siku ya Maskini Duniani ni matunda ya Jubilei ya Huruma ya Mungu
Siku ya Maskini Duniani ni matunda ya Jubilei ya Huruma ya Mungu   (Vatican Media)

Kanisa linapaswa kuwa ni kielelezo cha utandawazi wa mshikamano wa maisha ya kiroho na kimwili, dhidi ya sera na mikakati ya kiuchumi inayotenga, nyanyasa na kuwabagua maskini. Kwa sasa tofauti msingi kati ya watu, kimekuwa ni chanzo cha kinzani, migogoro na uhasama. Lakini, ikumbukwe kwamba, dunia inahitaji wajenzi wa madaraja yanayowakutanisha watu, kwa kujikita katika majadiliano yanayofumbatwa katika ukweli na uwazi, kwa kuthamini, utu, heshima na haki msingi za binadamu. Huu ni mwaliko wa toba na wongofu wa ndani, ili kuwa na Uso wa huruma kama ulivyofunuliwa na Kristo Yesu. Waamini na watu wote wenye mapenzi mema, wawe ni wajenzi na vyombo vya amani duniani; manabii wa huruma na wasamaria wema, wanaothubutu kuwahudumia maskini kwa: unyenyekevu, ari na moyo mkuu, kwa kutambua kwamba, Kanisa ni Sakramenti ya wokovu, umoja na mshikamano wa binadamu.Siku ya Maskini Duniani ni matunda ya maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, na kwa mara ya kwanza imeadhimishwa kunako mwaka 2017. Baba Mtakatifu Francisko anasema, hii ni kumbukumbu endelevu ya huruma ya Mungu inayopaswa kuwa ni sehemu ya vinasaba na utambulisho wa waamini katika ujumla wao. Siku hii ni fursa ya kushikamana kwa kujenga na kudumisha utamaduni wa watu kukutana na kusaidiana, kama alama ya: urafiki, umoja na udugu wa kibinadamu unaovunjilia mbali kuta za utengano kwa sababu mbali mbali. Baba Mtakatifu anasema, Kanisa daima limekuwa likisikiliza na kujibu kilio cha maskini na wahitaji kama inavyoshuhudiwa kwenye Kitabu cha Matendo ya Mitume, kwa kuwachagua Mashemasi saba walioshuhudiwa kuwa wema, wenye kujawa na Roho na hekima, ili waweze kutoa huduma kwa maskini. Rej. Mdo 6:1-7.

Utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote ni wajibu wa wote
Utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote ni wajibu wa wote   (AFP or licensors)

Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko, “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote”, anazungumzia kwa muhtasari mambo yanayotokea katika mazingira; Injili ya Uumbaji; Vyanzo vya mgogoro wa ikolojia vinavyohusiana na watu; Ikolojia msingi; Njia za kupanga na kutenda na mwishoni ni elimu ya ikolojia na maisha ya kiroho. Baba Mtakatifu mintarafu utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote anakazia mambo makuu matatu: Umuhimu wa kujikita katika wongofu wa kiikolojia; Unafishaji wa tunu msingi za Kiinjili za haki, amani na udugu wa kibinadamu pamoja na mwaliko kwa watu wa Mungu kusimama kidete kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote kwa sababu madhara yake ni makubwa kwa maisha ya binadamu na ni kikwazo kikuu cha ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Diplomasia inayotekelezwa na Vatican sehemu mbali mbali za dunia inajikita kwa namna ya pekee, katika msingi wa haki, amani na maridhiano kati ya watu! Ni diplomasia inayojipambanua kwa kusimama kidete: kulinda, kutetea na kudumisha utu, heshima, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi! Tangu mwanzo wa utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro, Baba Mtakatifu Francisko, amekazia kuhusu umuhimu wa diplomasia ya Vatican kufumbatwa katika amani, kwa kusimama kidete kupambana na baa la njaa na umaskini duniani; kwa kulinda na kutunza mazingira bora nyumba ya wote kwani kuna mamilioni ya watu wanaoathirika kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi na ukosefu wa fursa za ajira na maendeleo fungamani ya binadamu! Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wa Kitume: "Fratelli tutti": Yaani “Wote ni Ndugu”: Kuhusu Udugu na Urafiki wa Kijamii” anapembua utamaduni wa udugu wa kibinadamu kama chombo cha ujenzi wa ushirikiano na mafungamano ya Jumuiya ya Kimataifa kwa kubainisha njia itakayotumika na malengo yake katika uhalisia wa maisha ya watu.

Mchakato wa ujenzi wa udugu wa kibinadamu
Mchakato wa ujenzi wa udugu wa kibinadamu   (Vatican Media)

Baba Mtakatifu anakazia umuhimu wa ujenzi wa ushirikiano na mafungamano yanayokita mizizi yake katika maendeleo na ushirikiano katika masuala ya kiuchumi kwa kuzingatia majadiliano ili kufikia malengo yaliyokusudiwa yaani amani. Kwa sababu vita inasababisha maafa kwa watu na mali zao; vita ina sababisha vifo, inaharibu mazingira pamoja na kufisha matumaini ya watu. Majadiliano katika ukweli na uwazi yanavunjilia mbali kuta za utengano: kiroho na kiakili; yanafungua nafasi ya msamaha na kukoleza upatanisho. Majadiliano ni chombo cha haki kinachochochea na kuimarisha mahusiano na mafungamano ya Jumuiya ya Kimataifa kwa kukazia amani. Majadiliano ya kidini, kiekumene na kitamaduni yanapaswa kufumbata uvumilivu, yanajielekeza katika mchakato wa ushuhuda kama chombo cha ujenzi wa udugu wa kibinadamu, upendo na mafao ya wengi. Malengo ya Waraka wa Kitume:"Fratelli tutti" ni kuhamasisha ujenzi wa mshikamano wa kidugu unaoratibiwa na kanuni auni, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa utu, heshima na haki msingi za binadamu. Hii ni dhana inayokumbatia maisha ya kifamilia, kijamii, kitaifa na kimataifa. Ili kufikia lengo hili, kuna haja ya kujenga na kudumisha tasaufi ya udugu wa kibinadamu kama chombo cha kufanyia kazi katika medani za kimataifa, ili kusaidia kupata suluhu ya matatizo yanayoikumba Jumuiya ya Kimataifa. Huu ni msaada mkubwa katika kupambana na changamoto mamboleo kama vile: Vita na kinzani mbali mbali; baa la njaa na umaskini duniani pamoja na athari za uharibifu wa mazingira nyumba ya wote.

Papa Francisko: Vipaumbele: Haki na Amani Duniani
Papa Francisko: Vipaumbele: Haki na Amani Duniani

Kipaumbele cha kwanza ni ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Mshikamano wa kidugu usaidie ujenzi wa mahusiano na mafungamano ya Jumuiya ya Kimataifa kama ilivyo pia miongoni mwa wananchi wenyewe. Ujasiri na ukarimu ni mambo yanayohitajika ili kufikia malengo ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Baba Mtakatifu Francisko anakazia utawala bora kama sehemu muhimu sana ya Mafundisho Jamii ya Kanisa. Utawala bora unaozingatia: sheria, kanuni na taratibu zinazopaswa kutekelezwa na wengi. Hapa, dhana ya “Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa” ni mfano bora wa kuigwa! Kumbe, utawala bora unapaswa kuakisi matakwa ya jamii na wala si hisia za mtu binafsi. Pamoja na vipaumbele hivi vyote, Injili ya uhai na maisha ya ndoa na familia yanapaswa kupewa uzito wa pekee katika maisha na utume wa Kanisa ili kutangaza na kushuhudia ukuu, uzuri na utakatifu wa maisha ya ndoa na familia ndani ya Kanisa na katika ulimwengu mamboleo.

Papa Kumbukizi 2025
13 Machi 2025, 15:14