Katika maadhimisho ya Kumbukizi ya Miaka 61 ya Muungano wa Tanzania, Hayati Baba Mtakatifu Francisko alimwandikia Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania kwa niaba ya watanzania wote, ujumbe wa heri na matashi mema. Katika maadhimisho ya Kumbukizi ya Miaka 61 ya Muungano wa Tanzania, Hayati Baba Mtakatifu Francisko alimwandikia Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania kwa niaba ya watanzania wote, ujumbe wa heri na matashi mema. 

Hayati Papa Francisko: Salam za Kumbukizi ya Miaka 61 ya Muungano wa Tanzania

Ni katika muktadha wa kukuza na kudumisha mahusiano ya kidiplomasia kati ya Vatican na Tanzania, katika maadhimisho ya Kumbukizi ya Miaka 61 ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati Baba Mtakatifu Francisko alimwandikia Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania kwa niaba ya watanzania wote, ujumbe wa heri na matashi mema katika maadhimisho ya Miaka 61 ya Muungano kati ya Tanganyika na Zanzibar. Uhusiano wa kidiplomasia ulianzishwa tarehe 19.4.1968.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Uhusiano wa kidiplomasia kati ya Tanzania na Vatican ulianzishwa kunako tarehe 19 Aprili 1968 na Askofu mkuu Pierluigi Sartorelli akateuliwa kuwa ni Balozi wa kwanza wa Vatican nchini Tanzania, utume alioutekeleza hadi tarehe 22 Desemba 1970. Uhusiano huu kama alivyobainisha Baba Mtakatifu Benedikto XVI wakati akipokea hati za utambulisho kutoka kwa Balozi Ali Abeid Aman Karume wa Tanzania mjini Vatican unasimikwa katika tunu msingi za: Amani, haki, mshikamano na uhuru, kwani haya ni mambo yanayopata asili yake kutoka katika utu, heshima na haki msingi za binadamu, daima ustawi, maendeleo na mafao ya wengi yakipewa msukumo wa pekee. Tangu mwanzo wa mchakato wa uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji msingi ya binadamu kiroho na kimwili nchini Tanzania, Kanisa limekuwa mstari wa mbele katika kuchangia ustawi, maendeleo na mafao ya wengi hususan katika nyanja za elimu, afya, maendeleo na ustawi wa jamii, bila kusahau huduma ya maisha ya kiroho kwa watu wa Mungu nchini Tanzania na katika mchakato wa kudumisha misingi ya haki, amani, ustawi na maendeleo ya wengi.

Mazishi ya Papa Francisko, Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican
Mazishi ya Papa Francisko, Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican   (ANSA)

Itakumbukwa kwamba, wakati wa mkesha wa uhuru wa Tanganyika kunako mwaka 1961, Baba Mtakatifu Yohane XXIII alitunga sala maalum kwa ajili ya kuiombea Tanganyika ili uhuru wake uwawezeshe watanzania kuishi maisha mema zaidi kadiri iwastahilivyo watoto wa Mungu. Papa Yohane wa XXIII aliwaombea viongozi wa Serikali na watunga sera na sheria: ziwe ni kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Aliwaombea Watanganyika paji la imani, hekima, ukweli na uaminifu kwa Amri za Mungu. Aliwaombea upendo wa Kimungu ili kujenga na kudumisha umoja na mshikamano wa Kitaifa ili kushinda: utengano, ushindani, ukabila, utaifa ili watanganyika wote waweze kuwa ndugu wamoja na katika Fumbo la Utatu Mtakatifu. Mtakatifu Yohane XXIII aliombea amani na maridhiano kati ya Tanganyika na majirani zake; viongozi wa Serikali ili waweze kutimiza wajibu wao kama inavyostahili; raia kujipatia maisha bora zaidi na hatimaye, waweze kuwa ni raia katika Ufalme wa mbinguni milele na milele. Rej. Misale ya Waamini Ukurasa 1510.

Makamu wa Rais wa Tanzania alihudhuria mazishi ya Papa Francisko
Makamu wa Rais wa Tanzania alihudhuria mazishi ya Papa Francisko

Kumbe, kuna historia ya mahusiano ya kidiplomasia kati ya Tanzania na Vatican na jinsi ambavyo Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alivyokuwa akitenda shughuli zake kwa ajili ya kutafuta haki, amani na maridhiano kati ya watu wa Mataifa. Jumuiya ya Mtakatifu Egidio, yenye makao yake makuu mjini Roma, ilianzishwa rasmi tarehe 7 Februari 1968 kwa kujikita katika Sala, Maskini na Amani duniani; mambo msingi yaliyopewa kipaumbele cha kwanza na Hayati Baba Mtakatifu Francisko katika maisha na utume wa Kanisa katika ulimwengu mamboleo. Jumuiya hii pia ina historia ndefu ya mahusiano na mafungamano ya kidiplomasia katika kutafuta na kukoleza haki, amani na maridhiano kati ya watu wa Mataifa. Kumbe, Jumuiya ya Mtakatifu Egidio, Serikali ya Italia na Vatican wana mahusiano ya pekee sana na Tanzania katika kuleta haki, amani, utu na ubinadamu anasema Mahmoud Thabit Kombo, Mbunge na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki. Ni katika muktadha wa kukuza na kudumisha mahusiano ya kidiplomasia kati ya Vatican na Tanzania, katika maadhimisho ya Kumbukizi ya Miaka 61 ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati Baba Mtakatifu Francisko alimwandikia Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania kwa niaba ya watanzania wote, ujumbe wa heri na matashi mema katika maadhimisho ya Miaka 61 ya Muungano. Baba Mtakatifu Francisko alimtakia wingi wa hekima na busara kwake binafsi na kwa watanzania wote. Ujumbe huu wa Baba Mtakatifu umetolewa rasmi tarehe 23 Aprili 2025 na Askofu mkuu Angelo Accattino, Balozi wa Vatican nchini Tanzania.

Makamu wa Rais, Waziri na Balozi wa Tanzania mjini Vatican wakati wa mazishi
Makamu wa Rais, Waziri na Balozi wa Tanzania mjini Vatican wakati wa mazishi

Wakati huo huo, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango amesema, namna bora ya kumuenzi Hayati Baba Mtakatifu Francisko ni kudumisha amani, kuwajali maskini, kutunza mazingira na kujenga udugu wa kibinadamu. Makamu wa Rais amesema hayo wakati wa mazungumzo mara baada ya kumalizika kwa Ibada ya Misa Takatifu, iliyoadhimishwa Kardinali Giovanni Battista Re, Dekano wa Baraza la Makardinali, Jumamosi tarehe 26 Aprili 2025, ili kumwombea Hayati Baba Mtakatifu Francisko pumziko la amani, furaha na maisha ya uzima wa milele, nyumbani kwa Baba wa milele, ambako furaha yake haina mwisho. Kardinali Giovanni Battista Re, katika mahubiri yake, alitambua uwepo wa wawakilishi kutoka sehemu mbalimbali za dunia waliofika mjini Vatican ili kutoa heshima zao kwa Hayati Baba Mtakatifu Francisko, bila kuwasahau wale wote ambao wameguswa na kutikiswa na msiba huu mzito.

Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania alipokutana na Papa Francisko.
Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania alipokutana na Papa Francisko.   (Vatican Media)

Makamu wa Rais amesema kati ya nyaraka za mwisho alizosaini Hayati Baba Mtakatifu Francisko ni pamoja na barua aliyomwandikia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kumtakia heri na baraka katika maadhimisho ya Miaka 61 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar. Katika Ibada Misa hiyo ya mazishi, Makamu wa Rais aliongozana na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo, Balozi wa Tanzania mjini Vatican Mhe. Balozi Hassan Mwameta pamoja na Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Amerika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Swahiba Mndeme. Hayati Baba Mtakatifu Francisko amezikwa kwenye Kanisa kuu la Bikira Mkuu Jimbo kuu la Roma. Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango tarehe 27 Aprili 2025 alipata fursa ya kutembelea na kusali mbele ya Kaburi la Mtakatifu Rita wa Cascia kabla ya kushiriki Ibada ya Misa Takatifu ya Dominika ya Pili ya Pasaka, maarufu kama Dominika ya Huruma ya Mungu kwenye Kanisa Kuu la Mtakatifu Rita wa Cascia, lililopo katika Mji wa Cascia nchini Italia.

Papa Tanzania Muungano
29 Aprili 2025, 16:45