Nia za Baba Mtakatifu Francisko Kwa Mwezi Aprili 2025: Teknolojia Mpya Ziwe Ni Kiungo!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko katika nia zake za jumla kwa Mwezi Aprili 2025 zinazosambazwa na Utume wa Sala Kimataifa, anasali kwa ajili ya teknolojia mpya ili kwamba, matumizi ya teknolojia mpya kamwe yasichukue nafasi ya mahusiano na mafungamano ya kibinadamu; yaheshimu na kuthamini utu, heshima na haki msingi za binadamu; na yasaidie kushughulikia matatizo na changamoto katika ulimwengu mamboleo. Baba Mtakatifu anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuhakikisha kwamba, wanajenga utamaduni wa matumizi sahihi ya teknolojia mpya, ili kujenga na kudumisha mahusiano na mafungamano ya kijamii kwa kutambua kwamba, nyuma ya luninga kuna watu wanaopumua, wanaocheka na kuhuzunika. Baba Mtakatifu anasema, teknolojia ni matunda ya akili ambayo mwanadamu amepewa na Mwenyezi Mungu na yanapaswa kutumiwa vyema, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi; kwa kujenga umoja na mafungamano ya kijamii. Teknolojia itumike kwa ajili ya kuboresha maisha ya maskini na “akina yakhe pangu pakavu tia mchuzi” itumike kuboresha afya ya wagonjwa na kuwainua watu wenye kipato cha chini. Maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia yasaidie kulinda, kutunza na kudumisha mazingira bora nyumba ya wote na kwamba, teknolojia kiwe ni kiungo muhimu katika ujenzi wa mshikamano na udugu wa kibinadamu, kwa kutambua kwamba, binadamu wote ni ndugu wa Baba mmoja.
Kwa upande wake, Kardinali Michael Czerny, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo Fungamani ya Binadamu, anasema maendeleo makubwa ya teknolojia ni rasilimali na nyenzo muhimu sana kwa ajili ya huduma kwa familia ya binadamu. Matumizi yake yanapaswa kuratibiwa na kuongozwa na utu, heshima na haki msingi za binadamu, ili kukuza na kudumisha haki, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Padre Frèdèric Fornos, SJ., Mkurugenzi wa Utume wa Sala Kimataifa anasema, kumekuwepo na mafanikio makubwa ya maendeleo ya sayansi na teknolojia katika: Elimu, huduma ya afya: uchunguzi wa magonjwa na tiba na kwamba, maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia yanaweza kuwa ni nyenzo muhimu kwa Jumuiya ya Kimataifa kupambana na umaskini, magonjwa na uharibifu wa mazingira nyumba ya wote. Jambo la msingi ni kuhakikisha kwamba, kanuni maadili na utu wema vinawaongoza wanasayansi, ili kulinda na kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu na kwamba, matumizi ya sayansi na teknolojia yalete ustawi, mafao na maendeleo ya wengi.
Itakumbukwa kwamba, tangu kuanza na hatimaye kugundulika kwa teknolojia mbalimbali, dunia imeendelea kukua kwa kasi sana katika medani mbalimbali za maisha ya mwanadamu. Lakini pia kumekuwepo na madhara makubwa yaliyosababishwa na maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia kupitia ulimwengu wa utandawazi. Wataalam wanasema, sayansi ni maarifa yanayopatikana kwa vitendo, kutazama na kujaribu kweli ambazo zimebainishwa na hazijathibitishwa na kwamba, teknolojia ni elimu inayohusu: uhandisi, ufundi, ujenzi, vifaa na mbinu za uzalishaji wa vifaa na huduma katika jamii hali ambayo imechangia ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia yamepelekea pia kuporomoka kwa kanuni maadili, utu wema na haki msingi za binadamu; uchafuzi na uharibifu wa mazingira nyumba ya wote; pamoja mfumuko wa magonjwa makubwa. Kumekuwepo na maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia na hasa katika mawasiliano ya jamii. Dhamana na utume wa wana tasnia ya mawasiliano ya jamii watambue kuwa wao ni sehemu ya mchakato wa kujenga na kudumisha jumuiya inayofumbatwa katika mawasiliano, kwa kukazia ukweli na mafungamano ya kijamii; kwa kujenga na kudumisha utamaduni wa majadiliano na kusikilizana; kwa kuunganisha na kamwe mawasiliano yasiwe ni kwa ajili ya kuwatenganisha na kuwasambaratisha watu. Mitandao ya kijamii iwe ni madaraja ya kuwakutanisha watu!
Kwa ufupi, hiki ndicho kilichokuwa kiini cha ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Siku ya 53 ya Upashanaji Habari Ulimwenguni kwa mwaka 2019. Baba Mtakatifu anawaalika na kuwahamasisha wadau katika tasnia ya mawasiliano ya jamii kuuvua uongo na kusema ukweli kwa maana wao ni viungo, kila mmoja kiungo cha mwenzake. (Rej. Ef. 4:25). Ikiwa kama mitandao ya kijamii itatumika kama daraja na matumaini ya kuwakutanisha watu, basi hapo itakuwa imetekeleza dhamana na wajibu wa kujenga jumuiya inayoheshimiana na kuthaminiana. Maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia ya mawasiliano ni muhimu sana, ikiwa kama yatasaidia mchakato wa kukuza na kudumisha umoja na mafungamano ya kijamii; kanuni maadili na utu wema; siasa shirikishi pamoja na haki. Katika ulimwengu huu ambamo watu wanathamini sana takwimu, kuna haja ya kuhakikisha kwamba, utu, heshima na haki msingi za binadamu zinaheshimiwa na kuthaminiwa na wote. Baba Mtakatifu Francisko anasema, kuna umuhimu wa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa utu, heshima na kanuni maadili ili kujibu changamoto za kijamii zinazoendelea kuibuliwa na maendeleo ya teknolojia ya unde “akili mnemba” kiasi cha kuathiri utu wa binadamu. Teknolojia huzaliwa kwa kusudi na, katika athari zake kwa jamii ya wanadamu, daima huwakilisha aina ya utaratibu katika mahusiano ya kijamii na mpangilio wa mamlaka, hivyo kuwawezesha watu fulani kufanya vitendo maalum huku wakiwazuia wengine kufanya tofauti. Kwa njia iliyo wazi zaidi au kidogo, mwelekeo huu wa nguvu wa teknolojia daima unajumuisha mtazamo wa ulimwengu wa wale walioivumbua tekenolojia hii na kuiendeleza.
Teknolojia ya akili unde isaidie kujenga leo na kesho iliyo njema na bora zaidi, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Kumbe, msukumo wa kimaadili ni muhimu sana katika maendeleo ya teknolojia ya akili unde. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba watu wote wenye mapenzi mema wataendelea kushirikiana kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi; kwa kusimama kidete kuwalinda na kuwatetea wanyonge na kwamba, maendeleo ni kwa ajili ya wengi. Teknolojia ya akili unde inaendelea kushika kasi ya ajabu katika maendeleo ya binadamu. Viongozi wa dini mbalimbali duniani wanahimizwa kushikamana kama ndugu wamoja, ili kutoa msukumo wa pekee katika ujenzi wa haki, amani na udugu wa kibinadamu. Ni dhamana na wajibu wa viongozi wa kidini kuhakikisha kwamba, wanashikamana kwa dhati ili kukabiliana na changamoto za maendeleo makubwa ya teknolojia ya akili mnemba; kwa kuzingatia kanuni maadili na utu wema na kwamba, kuna haja ya kuwa na uongozi utakaosimamia kanuni maadili ya teknolojia ya akili mnemba. Teknolojia ya akili unde inatumia hali ya binadamu, changamoto kwa binadamu wenyewe ni kuwa wazi kwa Mwenyezi Mungu pamoja na binadamu wenzake na kwamba, teknolojia hii inawaelekeza binadamu kwa maendeleo ya siku zijazo. Dhamiri ndicho kiini cha siri zaidi cha binadamu na hekalu la Mungu, ambamo sauti yake inasikika na utimilifu wa sheria hii ni upendo kwa Mungu na jirani. Baba Mtakatifu anataka kuona kwamba: Utu, heshima, haki msingi, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi yanaheshimiwa katika kipindi hiki cha maendeleo makubwa ya teknolojia ya akili mnemba. Ni hatari sana ikiwa kama teknolojia ya akili mnemba itatumika katika vita, kumbe, haki na amani vinapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza.
Matumizi ya teknolojia ya akili unde “Artificial Intelligence” yanaendelea kuleta mageuzi makubwa katika ulimwengu wa kazi na mahali wanapoishi watu! Mabadiliko haya ni makubwa, kumbe, yanapaswa kuongozwa na kusimamiwa na sheria mpya, kanuni maadili na utu wema. Katika mchakato wa tasnia ya mawasiliano, kuna haja ya kujikita katika: huruma na upendo, udugu wa kibinadamu na mshikamano. Maendeleo ya sayansi na teknolojia yanachangia kwa kiasi kikubwa ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, lakini hayana budi kufumbatwa katika utu na heshima ya binadamu. Compyuta ni chombo cha huduma ambacho kimetumiwa na watu wengi kwa ajili ya maendeleo, lakini pia, kuna baadhi ya watu wamekitumia vibaya kwa malengo yao binafsi kiasi cha kuleta tafrani ulimwenguni.Sayansi na teknolojia haina budi kujikita katika misingi ya maadili na utu wema; malezi na majiundo kwa ajili ya matumizi sahihi ya nyenzo za mawasiliano ya jamii; ili kujenga uelewa na uwajibikaji wa pamoja. Matumizi ya akili unde yataendelea kusababisha mabadiliko makubwa katika maisha ya watu, kumbe, malezi na majiundo makini ni muhimu sana hasa kwa vijana wa kizazi kipya. Hili ni jukumu la viongozi wa Serikali, wanasiasa, watunga sera na sheria; wafanyabiashara, wasomi na wanazuoni pamoja na viongozi wa dini kushirikiana na kushikamana, ili kuhakikisha kwamba, utu, heshima na haki msingi za binadamu zinalindwa na kudumishwa. Kwa njia hii, wataweza kugundua mapungufu yanayoweza kujitokeza na hivyo kuyafanyia kazi kwa kuangalia mambo msingi yanayopaswa kupewa kipaumbele cha kwanza. Maendeleo ya sayansi na teknolojia yalenge ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Uwajibikaji wa wote, kanuni maadili na utu wema; utawala wa sheria na haki ni mambo msingi katika kukuza matumizi halali ya sayansi na teknolojia ya mawasiliano ya jamii.