Papa Francisko: Alihimiza: Utu, Heshima, Haki Msingi Na Wanawake
Na Mama Evaline Malisa Ntenga, - Dar es Salaam, Tanzania
Radio Vatican inakuletea Ujumbe kutoka kwa Mama Evaline Malisa Ntenga, Rais wa Shirikisho la Umoja wa Wanawake Wakatoliki Kanda ya Afrika ambaye pia ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanawake Wakatoliki Tanzania kama sehemu ya maombolezo ya kifo cha Hayati Baba Mtakatifu Francisko, kilichotokea tarehe 21 Aprili 2025. Anasema, kwa mioyo mizito lakini iliyojawa na shukrani kuu, tunasimama kama wanawake Wakatoliki wa Afrika kumuenzi Hayati Baba Mtakatifu Francisko. Tunamwomboleza si tu kama kiongozi wa Kanisa la ulimwengu, bali kama Baba wa kiroho, aliyeishi maisha ya unyenyekevu wa kina, mshikamano, na utume wa amani. Safari yake ya maisha ni simulizi ya huduma isiyokoma, ya kupenda bila mipaka, na ya kuwa karibu na waliokuwa pembezoni – maskini, wagonjwa, na waliotengwa. Tumejifunza kutoka kwake kwamba ukuu wa kiroho haulazimishi, bali huvutia; haulazimishi kwa nguvu, bali huchochea kwa upole. Hayati Baba Mtakatifu Francisko alikuwa mtu wa imani ya kina na mwenye ibada kwa Mama Bikira Maria. Katika kila hatua ya maisha yake ya Kipadre na Kiaskofu, alitamka mara nyingi kwamba ameyaweka maisha na huduma yake chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, Mama wa Bwana wetu Yesu Kristo, Bikira Maria Mtakatifu. Maisha yake ya sala kupitia kwa Mama Bikira Maria yalimfanya kuwa kiongozi wa sala ya ndani na uaminifu wa kiroho, hasa kwa sala ya Rozari na tumeshuhudia mara nyingi akisali Rozari katika Kanisa kuu la Bikira Maria Mkuu lililoko Jimbo kuu la Roma.
Kifo chake kilitokea siku ya Jumatatu ya Pasaka, tarehe 21 Aprili 2025 siku moja baada ya kutoa Salam na Baraka kwa mji wa Roma na Ulimwengu katika ujumla wake, maarufu kama “Urbi et Orbi” wakati wa Sherehe ya Pasaka ya Bwana. Tumemwona akihitimisha utume wake akiwa amesimama, akiwa bado anawabariki watu wa Mungu. Ni fumbo la maisha ya kiroho lililobeba alama ya mwaliko kwa kila mmoja wetu: kuwa mwaminifu hadi mwisho, kama yeye. Nawaalika watu wote wa mungu kuendelea kuomboleza kifo chake kwa bubujiko la furaha na matumaini. Yapo mengi ya kuendelea kutafakari na kuyaenzi, na hapa nitasema machache tu! Alikuwa Kiongozi wa Rehema na Tumaini: Baba Mtakatifu Francisko alikuwa kiongozi wa aina ya pekee – si tu kwa hadhi ya upapa, bali kwa jinsi alivyoishi ufukara na unyenyekevu wa kweli wa Injili. Alihubiri kwa matendo kuliko kwa maneno. Alitembea pamoja na watu wa kawaida, akakumbatia maskini, wagonjwa, wafungwa na wakimbizi na wale wote waliosukumizwa pembezoni mwa vipaumbele vya jamii. Alifanya Kanisa lionekane kuwa kweli ni hospitali ya uwanja wa vita, mahali pa uponyaji, si hukumu. Kwa maisha yake, tuliona sura ya Kristo Yesu anayependa na kuwahurumia wote bila ubaguzi. Kama wanawake, tulimwona Baba Mtakatifu Francisko akisimama imara katika nyakati za changamoto wakati wa janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19, katika migogoro ya kivita, na pale ambapo dunia ilihitaji sauti ya matumaini. Yeye alikuwa sauti hiyo. Kwa kweli, alikuwa ni kiongozi wa rehema, matumaini na huruma ya Kristo Yesu duniani.
Baba Mtakatifu Francisko alikuwa ni shuhuda na chombo cha Matumaini: Tuendelee kumwombea: Katika mafundisho yake, Baba Mtakatifu Francisko alitufundisha kuwa kifo si mwisho, bali ni mwanzo mpya wa kukutana na Mungu. Katika Moja ya Homilia yake alisema, “Kifo ni kumbatio na Bwana, linalopaswa kuishiwa kwa tumaini.” “He himself said in a homily "Death is an embrace with the Lord, to be lived with hope" Pope Francis at Casa Santa Marta. Kauli hii ni mwanga wa kiimani unaotufundisha kwamba hata katika huzuni, tunapaswa kubaki na tumaini. Hakukimbia udhaifu wa mwili wala hofu ya mwisho wa maisha; aliendelea kuhudumu, kusali, na kubariki hadi pumzi yake ya mwisho. Kwa sala zetu, tunamkabidhi mikononi mwa Mungu, tukimwombea kupokelewa katika makao ya milele, pale ambapo machozi hayapo tena na furaha ya kweli inatawala. Pumzika kwa amani Baba Mtakatifu, mtumishi mwaminifu, uliyeitikia wito wako hadi mwisho. Baba Mtakatifu Francisko alionesha nguvu ya sala katika maisha na utume wake: Umuhimu wa Sala katika maisha ya mwamini. Ibada ya Rozari Takatifu ni muhtasari wa historia nzima ya kazi ya ukombozi; maisha na utume wa Kristo Yesu. Baba Mtakatifu Francisko alikuwa na mapenzi ya dhati kwa Mama Bikira Maria, akimwona kama Mama wa huruma, wa matumaini na wa faraja kwa waamini wote. Mojawapo ya tabia yake ya kipekee ilikuwa ni kwenda kila mara kusali katika Kanisa la Bikira Maria Mkuu, Jimbo kuu la Roma hasa kabla na baada ya safari za kitume. Hili halikuwa tendo la ibada tu, bali ni ushuhuda wa maisha ya mtu anayemtegemea maombezi na tunza ya Mama Bikira Maria kama mlinzi na mwongozi wake wa kila siku. Katika mafundisho yake alisema: "Rozari ni sala ya watu wa kawaida na sala ya watakatifu – ni fumbo la tumaini."
Kwa mfano huu, tunahimizwa kuwa na sehemu maalum ya sala katika maisha yetu iwe nyumbani, kwenye parokia zetu au hata pembezoni mwa bustani, panapoweza kuweka "makao ya sala". Rozari si ibada ya kawaida, bali ni kutafakari maisha ya Kristo Yesu kupitia macho na moyo wa Bikira Maria. Tuwe wanawake wa kusali Rozari – tusali kwa ajili ya familia zetu, kwa ajili ya amani Barani Afrika na duniani, na kwa ajili ya roho ya Baba Mtakatifu Francisko. Hebu tusali Rozari si kwa mazoea bali kwa moyo uliojaa imani, matumaini na mapendo tukimwomba Mama Bikira Maria atusindikize, kama alivyomsindikiza Papa hadi safari ya mwisho ya maisha yake hapa duniani Heshima kwa Bikira Maria na Wanawake: Wanawake Wakatoliki Barani Afrika wanapenda kumpongeza Baba Mtakatifu Francisko kwa kuwashirikisha kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa. Baba Mtakatifu ameonesha kuguswa sana na matatizo na changamoto zinazowakabili wanawake sehemu mbali mbali za dunia hasa kulinda na kudumisha Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo. Kumbe, ni wajibu wa wanawake pia kusimama kidete kulinda na kudumisha utu na heshima ya binadamu; kusaidiana na kukamilishana katika maisha na utume wa Kanisa. Wanawawake wanapaswa kuhusishwa kikamilifu katika mchakato wa majadiliano, ili waweze kuchangia ustawi na mafao ya wengi, kwa kuwapatia wanawake nafasi ya kutumia vyema karama na mapaji yao. Wanawake Wakatoliki wanasema, umefika wakati wa kumwilishwa mawazo katika uhalisia wa maisha ya watu badala ya watu kuendelea “kuning’inia kwenye ombwe.
Wanawake washirikishwe kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa. Wanampongeza Baba Mtakatifu ambaye katika Wosia wake wa kitume, “Amoris laetitia” yaani “Furaha ya upendo ndani ya familia” ambako anakazia umuhimu wa majadiliano katika maisha ya ndoa na familia ili kukuza na kudumisha upendo ndani ya familia. Majadiliano yajikite katika ukweli na uwazi; kwa kusali na kutafakari; kwa kukazia mambo msingi katika maisha, ili kukuza na kudumisha Injili ya familia. Wanawake Wakatoliki wanahamasishwa kushiriki kikamilifu katika mchakato wa majadiliano, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya familia ya Mungu. Baba Mtakatifu Francisko alimtambua mwanamke si tu kwa nafasi yake ya kuzaa, bali kwa zawadi yake ya pekee ya kuumba, kutunza, kusamehe, na kuponya. Mwanamke kwa mujibu wa Baba Mtakatifu ni zawadi ya Mungu kwa dunia, na ndani yake kuna sura ya Bikira Maria – mtii, jasiri, mpole na mama. Alipendekeza tujitazame sisi sote kwa jicho la Maria, aliyeweza kulia na kufurahi, kusimama na kuvumilia, kusikiliza na kushikilia ahadi ya Mungu. Katika hotuba yake ya tarehe 13 Mei 2023, kwenye Sikukuu ya Bikira Maria wa Fatima, Baba Mtakatifu Francisko alituambia tuelekeze macho yetu kwa Bikira Maria wa Fatima. Alisema kwa msisitizo: "Dunia bila mwanamke ni ukiwa na utupu." Hili halikuwa tamko la kishairi tu, bali ni tamko la kinabii. Kwetu sisi wanawake, huu ni mwaliko wa kutambua kuwa heshima kwa mwanamke ni heshima kwa maisha, kwa familia, na kwa wokovu wenyewe. Ni wito wa kujivunia kuwa wanawake wa imani, wanawake wa huduma, wanawake wa maombi na wanawake wa matumaini. Tunapomuenzi Baba Mtakatifu Francisko, tunamshukuru kwa kutufungua macho kuona kwamba sauti ya mwanamke ndani ya Kanisa ni sauti halali, ya Roho Mtakatifu mwenyewe.
Usawa na Ushirikishwaji wa Wanawake Katika Uongozi wa Kanisa. Baba Mtakatifu Francisko alifanya maamuzi makubwa ya kihistoria kwa kuvunja baadhi ya vikwazo vya kimfumo vilivyowazuia wanawake kushika nafasi za uongozi ndani ya Kanisa. Aliwateua wanawake kushika nyadhifa katika Baraza la Kipapa, kuwa washauri wa maskofu, na kushiriki katika maamuzi ya kiutawala ya kiwango cha juu. Alisisitiza mara kwa mara kwamba: "Kanisa haliwezi kuendelea bila sauti ya mwanamke." Kwa mtazamo wake, mwanamke hachangii tu uzuri wa Kanisa, bali hubeba mantiki ya kiroho, ya kichungaji, na ya kiutawala. Kwetu wanawake, heshima hii ni wito wa kuchukua nafasi zetu kwa ujasiri, kwa utakatifu na kwa utume. Tunapoona wanawake wakiongoza mashirika ya Kipapa, wakifundisha taalimungu sanjari na kusimamia miradi ya huruma na kutetea haki, tunajua kwamba Papa Francisko aliona ndani yetu uwezo wa kipekee ambao kwa muda mrefu haukuthaminiwa vya kutosha. Leo tunamuenzi si kwa maneno tu, bali kwa matendo ya uwajibikaji wa kina ndani ya Kanisa na jamii katika ujumla wake.
Majadiliano ya kidini na kiekumene ili kujenga na kudumisha haki, amani, ustawi na maendeleo ya wengi. Baba Mtakatifu Francisko alitambua kwa kina kuwa uinjilishaji wa kweli hauwezi kufungwa ndani ya mipaka ya dhehebu moja au tamaduni chache. Alijihusisha na mazungumzo ya kidini na viongozi wa madhehebu mbalimbali, wakiwemo Waprotestanti, Waislamu, Wayahudi, Wahindu na wasiokuwa wa dini yoyote. Katika safari zake za kitume, alijitahidi kuwa daraja, si ukuta. Alikumbusha mara nyingi kwamba: "Maendeleo ya kweli hayawezekani bila mazungumzo kati ya watu wa imani tofauti." Uekumene kwake haukuwa nadharia bali vitendo, alishiriki sala za pamoja, alitembelea makanisa na misikiti, na akakemea kwa nguvu chuki inayojificha chini ya kivuli cha dini. Kwetu wanawake, mafundisho haya yanatufundisha kuwa wajenzi stadi wa udugu wa kibinadamu, kuwa mabalozi wa maelewano na amani – kuishi pamoja na wengine kwa heshima, kusikilizana na kushirikiana katika matendo ya huruma ya kijamii bila kujali tofauti zetu. Kwa mfano wake, tunatambua kuwa undugu wa kweli haumaanishi kufanana, bali kuheshimiana katika tofauti zetu – huku tukisongesha mbele wema wa pamoja. Utunzaji bora wa Mazingira na kutetea uhai kama wajibu wa kimaadili na kiutu! Katika waraka wake "Laudato si'", Baba Mtakatifu Francisko alifungua ukurasa mpya wa kiroho katika suala la mazingira. Alitufundisha kuwa dunia si mali yetu binafsi, bali ni zawadi kutoka kwa Mungu – tuliyoitiwa kuilinda kwa vizazi vya sasa na vijavyo. Alisema kwa maneno yenye nguvu: "Sisi si wamiliki wa dunia, bali ni wasimamizi wake."Alitufundisha kuwa dunia ni nyumba yetu sote, na tunalo jukumu la kuilinda. Alisema: "Uharibifu wa mazingira ni dhambi dhidi ya uumbaji, na dhambi dhidi ya maskini." Alihusisha kwa karibu hali ya mazingira na hali ya kiuchumi ya maskini, akisisitiza kwamba ni wale walio katika pembezoni ndio wanaoumia zaidi.
Baba Mtakatifu pia alikemea vikali vitendo vya uaviaji mimba, akivitambua kuwa ni sehemu ya utamaduni wa kutupa unaodhihirisha kupotea kwa heshima ya maisha ya binadamu. Alisisitiza kwamba haiwezekani kutetea mazingira wakati huo huo tunapuuza maisha ya binadamu alieko tumboni mwa mama. Baba Mtakatifu Francisko alitukumbusha kuwa mazingira bora huanza na heshima kwa maisha tangu kutungwa mimba hadi kifo cha asili. Huu ni wito kwetu sote lakini zaidi kwa wanawake ambao athari za uharibifu wa mazingira zinatuumiza zaidi kuwa walinzi wa uumbaji: kupanda miti, kuelimisha watoto kuhusu mazingira, kupinga uharibifu wa rasilimali na kutetea maisha ya kila mtoto aliye tumboni. Hii si kazi ya serikali peke yake, bali ni wito wa kiroho kwa kila mmoja wetu. Laudato Si’ ni wito kwetu kuishi maisha yenye uwiano – tukitambua kuwa kila tendo la uchafuzi wa mazingira ama kutishia uhai ni tendo la uasi dhidi ya Mungu Muumba wetu.
Mjumbe wa Amani na Msamaha Katika Familia na Jamii: Katika mafundisho yake ya kila mara, Baba Mtakatifu Francisko aliweka familia katikati ya mpango wa Mungu wa upendo. Aliifananisha familia na "Kanisa dogo la nyumbani” ambapo tunajifunza kusamehe, kupendana na kuombeana. Alisisitiza kuwa hakuna amani ya kweli katika jamii kama familia hazijajengwa juu ya msamaha. Alisema: "Familia inayosamehe huishi, familia isiyosamehe hufa." Alitufundisha kwamba kila mgogoro, uwe wa ndoa, jamii au taifa, unaweza kutatuliwa kupitia moyo wa msamaha na huruma. Kama wanawake, tuna nafasi muhimu ya kukuza amani ndani ya familia zetu, kuwa walimu wa maadili kwa watoto wetu, na kuwa madaraja ya upatanisho. Tunamshukuru Baba Mtakatifu Francisko kwa kutuonesha njia ya upendo unaosamehe, na tunamuombea tulioachiwa urithi huu tuweze kuuendeleza kwa vitendo vya kila siku. Kupitia Waraka wake wa Kitume: "Fratelli tutti": Yaani “Wote ni Ndugu”: Kuhusu Udugu na Urafiki wa Kijamii” Baba Mtakatifu Francisko alitutaka tujione kuwa ni familia moja ya kibinadamu – bila kujali mipaka ya nchi, lugha, dini au tamaduni. Aliandika: “Tumeumbwa kwa sura ya Mungu; si kwa migawanyiko, bali kwa mshikamano.” Tumeitwa kuwa kina Maria mashuhuda na watangazaji wa amani, kina Veronica: wafuta machozi, na kina Martha – watenda kazi ya upendo, udugu na mshikamano. Pumzika kwa amani, Baba Mtakatifu Francisko. Tutakukumbuka daima, kwa unyenyekevu wako wa kweli, kwa sauti yako ya matumaini, na kwa moyo wako uliojaa huruma kwa wote.