Baraza la Makardinali linawaalika watu wa Mungu, kukiishi kipindi hiki cha neema na utambuzi wa maisha ya kiroho na hatimaye, kusikiliza mapenzi ya Mungu. Baraza la Makardinali linawaalika watu wa Mungu, kukiishi kipindi hiki cha neema na utambuzi wa maisha ya kiroho na hatimaye, kusikiliza mapenzi ya Mungu.   (@Vatican Media)

Uchaguzi wa Papa Mpya Ni Tukio la Kikanisa, Kipindi Cha Neema na Utambuzi wa Kiroho

Baraza la Makardinali kama sehemu ya maandalizi ya uchaguzi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro “Conclave” linawaalika watu wa Mungu, kukiishi kipindi hiki cha neema, utambuzi wa kiroho na kusikiliza mapenzi ya Mungu. Makardinali wakitambua ukubwa na unyeti wa kazi na dhamana iliyoko mbele yao, wanatambua kwamba, kuna haja ya kuungwa mkono na kusindikizwa na sala za waamini. Hii ndiyo nguvu ya kweli ambayo inakuza ndani ya Kanisa umoja wa kweli!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baraza la Makardinali katika mikutano yake elekezi kama sehemu ya maandalizi ya uchaguzi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro “Conclave” linawaalika watu wa Mungu, kukiishi kipindi hiki cha neema na utambuzi wa maisha ya kiroho sanjari na kusikiliza mapenzi ya Mungu. Makardinali wakitambua ukubwa na unyeti wa kazi na dhamana iliyoko mbele yao, wanatambua kwamba, kuna haja ya kuungwa mkono na kusindikizwa na sala za waamini. Hii ndiyo nguvu ya kweli ambayo inakuza ndani ya Kanisa umoja wa viungo vyote vya Fumbo la Mwili wa Kristo yaani Kanisa. Rej. 1Kor 12: 12. Baraza la Makardinali linatambua uzito wa kazi kubwa iliyoko mbele yao kwa wakati huu, kwanza kabisa Makardinali wenyewe wanapenda kujinyenyekesha, ili waweze kuwa ni vyombo vya hekima isiyokuwa na kikomo na kwa maongozi ya Baba yao wa milele na kwa unyenyekevu wa utendaji wa Roho Mtakatifu. Makardinali wanakaza kusema, kwa hakika Roho Mtakatifu ndiye Mhusika mkuu wa maisha ya watu wa Mungu, changamoto na mwaliko wa kumsikiliza na kuitikia kile anacho sema kwa Mama Kanisa. Rej. Ufu 3:6. Bikira Maria Mama wa Kanisa awasindikize kwa sala na kwa ulinzi na tunza yake ya Kimama.

Hiki ni kipindi cha Kanisa, Neema na Utambuzi wa kiroho
Hiki ni kipindi cha Kanisa, Neema na Utambuzi wa kiroho   (@Vatican Media)

Baraza la Makardinali katika kikao chake cha Jumatano tarehe 30 Aprili 2025, pamoja na mambo mengine, wamejadili kuhusu: hali ya uchumi ilivyo mjini Vatican pamoja na changamoto zake, ili kuendelea kuimarisha mfumo wa uchumi utakaoenzi utume wa Khalifa wa Mtakatifu Petro sehemu mbalimbali za dunia. Sera na mikakati ya vitega uchumi vya Vatican; hali ya kifedha ya Benki Kuu ya Vatican, IOR, iliyoanzishwa kunako mwaka 1942 na Papa Pio XII, inajihusisha na huduma kwa mashirika ya kitawa, kazi za kitume na shughuli za uinjilishaji unaofanywa na Kanisa la Kiulimwengu. Makardinali wamesikiliza pia taarifa ya ukarabati mkubwa unaoendelea kufanyika kwenye Sekretarieti kuu ya Vatican. Baraza la Huduma ya Upendo limeonesha kwa kina na mapana shughuli zake mbele ya Makardinali.

Waamini wanaalikwa kufunga na kusali kwa ajili ya uchaguzi wa Papa
Waamini wanaalikwa kufunga na kusali kwa ajili ya uchaguzi wa Papa   (@Vatican Media)

Mambo mengine yaliyojadiliwa ni pamoja na: taalimungu ya watu wa Mungu; mateso na mahangaiko ya watu wa Mungu; tunu msingi za ujenzi wa Kanisa la Kisinodi na Kimisionari; Urika wa Maaskofu pamoja na marejeo ya umuhimu wa Nyaraka za Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, lakini zaidi: Mwanga wa Matafa, Lumen gentium; pamoja na Furaha na Matumaini, Gaudium et spes. Makardinali wamekazia umuhimu wa kutangaza na kushuhudia tunu msingi za Kiinjili kama sehemu muhimu sana ya mchakato wa uinjilishaji mpya. Baada ya maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya uchaguzi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro, tarehe 7 Mei 2025, Makardinali watatakiwa kuhamia kwenye Hosteli ya Santa Martha. Chumba kilichokuwa kinatumiwa na Hayati Baba Mtakatifu Francisko kitafunguliwa tu, mara baada ya uchaguzi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro. Mchakato wa upigaji kura utakuwa ni mara mbili kwa siku; asubuhi na jioni.

Uchaguzi wa Papa ni kipindi cha Kikanisa, Neema na Utambuzi
Uchaguzi wa Papa ni kipindi cha Kikanisa, Neema na Utambuzi   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Wakati huo huo, Kardinali Giovanni Battista Re, Dekano wa Baraza la Makardinali kwa niaba ya Baraza la Makardinali amemtumia barua ya shukrani Mstahiki Meya wa Jiji la Roma, Mheshimiwa Roberto Gualtieri, kwa jinsi ambavyo watu wa Mungu Jijini Roma walivyoshiriki kwa wingi kutoa heshima zao za mwisho na hatimaye, maziko ya Hayati Baba Mtakatifu Francisko. Jiji la Roma liliwawezesha mahujaji wa matumaini kutoka sehemu mbalimbali za dunia kuweza kushiriki katika mazishi ya Baba Mtakatifu Francisko. Amewashukuru watu wote wa Mungu Jijini Roma kwa utayari na ushiriki wao uliowezesha kufanikisha mazishi ya Baba Mtakatifu Francisko.

Baraza la Makardinali
01 Mei 2025, 15:05