Kardinali Tagle: Jubilei ya Miaka 100 ya Jimbo Kuu la Danzica Poland: Yaliyojiri
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko anasema kwamba, kadiri ya Maandiko Matakatifu, Jubilei ni kipindi cha kumbukumbu, toba na wongofu wa ndani; muda muafaka wa mapumziko; muda wa kujichotea nguvu pamoja na kufurahia matunda ya kazi ya uumbaji. Ni muda wa kuyatafakari yaliyopita kwa moyo wa shukrani, kuyaishi ya sasa kwa moyo wa hamasa na kuyakumbatia ya mbeleni kwa moyo wa matumaini. Ni katika muktadha huu, Jimbo kuu la Danzica, lililoko nchini Poland, kwa Mwaka 2025 linaadhimisha Jubilei ya Miaka 100 tangu kuanzishwa kwake kwa uwepo na ushiriki wa Kardinali Luis Antonio Gokim Tagle, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu kuanzia tarehe 6 hadi tarehe 9 Machi 2025. Katika hija hii, Kardinali Tagle alikutana na kuzungumza na Mapadre; Aliadhimisha Ibada ya Misa Takatifu pamoja na kukutana na Watu wa kujitolea kama sehemu ya Maadhimisho ya Jubilei yao, Dominika tarehe 9 Machi 2025. Kardinali Luis Antonio Gokim Tagle amekazia kuhusu: Majiundo ya awali na endelevu kwa ajili ya Makleri ili kuwawezesha kuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa upendo na huruma ya Mungu kati ya watu wanaowahudumia. Anakazia umuhimu wa maisha ya sala tangu mwanzo ili hatimaye, Mapadre waweze kuchota nguvu ya kutekeleza dhamana na wajibu wao barabara, katika maisha na utume wa Kanisa. Wawe ni viongozi wanaojitaabisha kulisoma Neno la Mungu, kulitafakari na hatimaye, kulimwilisha katika uhalisia wa maisha, vipaumbele na utume wao. Maandiko Matakatifu yasomwe na kueleweka kwa msaada wa Roho Mtakatifu na chini ya uongozi wa Ualimu wa Kanisa, kwa kuzingatia yaliyomo katika Maandiko yote katika umoja wake; kwa kuheshimu Mapokeo hai ya Kanisa na mwishoni kwa kujali ulinganifu wa imani, yaani mshikamano wa kweli zote za imani!
Kardinali Tagle amekazia kuhusu ukuhani wao, ili kweli waweze kuwa ni vyombo na mashuhuda wa matumaini yanayosimikwa katika huduma, tayari kushiriki katika mchakato wa ujenzi wa Kanisa la Kimisionari na Kisinodi. Katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni kumekuwepo na mabadiliko makubwa katika maendeleo ya sayansi na teknolojia ya mawasiliano. Kutokana na changamoto zote hizi, Kanisa limeona kwamba, kuna busara ya kuanzisha, kupyaisha na kutoa kipaumbele cha kwanza kwa malezi na majiundo ya Kipadre katika maisha na utume wa Kanisa. Lengo kuu ni kuliwezesha Kanisa kuwapata Mapadre: wema, watakatifu na wachapakazi wanaoweza kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya Kristo Yesu na Kanisa lake. Kardinali Tagle amewakumbusha watu wa Mungu kwamba, Kipindi cha Kwaresima ni fursa kwa watu wa Mungu kujenga na kudumisha utamaduni wa kusikilizana, kwa kutembea na kufanya kazi kwa pamoja kwa ajili ya ujenzi wa Ufalme wa Mungu; kwa kuonesha upendo na ukarimu kwa wahitaji zaidi, kwa njia ya toba na wongofu wa ndani mintarafu ujenzi wa Kanisa la Kisinodi. Watu wa Mungu wanaalikwa kutembea katika mwanga wa matumaini kwani “tumaini halitahayarishi.” Rum 5:5, kiini cha ujumbe wa Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo na kwamba, hatima ya Kipindi cha Kwaresima ni maadhimisho ya ushindi wa Pasaka, kielelezo cha upendo mkamilifu, kwa hiyo; waamini wanapaswa kuwa ni mahujaji wa matumaini. Kumbe, Kwaresima ni kipindi cha toba, wongofu wa ndani, sala na tafakari tayari kujenga mahusiano na mafungamano na Kristo Yesu katika hija ya maisha na utume wao kwa watu wa Mungu.
Waamini walei ndani ya Kanisa wanapaswa kutambua dhamana na wajibu wao kama wabatizwa, yaani watu waliozaliwa upya kwa maji na Roho Mtakatifu; wanao wajibu na haki zao msingi zinazopaswa kumwilishwa katika maisha na utume wa Kanisa. Kimsingi waamini walei wanaitwa na kutumwa kutangaza na kushuhudia Injili ya Kristo Mfufuka mintarafu uhalisia wa maisha yao. Waamini walei daima wajibidiishe kuchota utajiri na amana ya maisha yao ya Kikristo kutoka katika: Neno la Mungu, Sala, Sakramenti za Kanisa pamoja na Mafundisho Jamii ya Kanisa, dira na mwongozo wa jinsi ya kuyatakatifuza malimwengu. Waamini walei watambue kwamba, amana na utajiri huu wanapaswa kuwashirikisha pia jirani zao kama sehemu ya mchakato wa majadiliano ya kidini, kiekumene na kitamaduni; katika kuyatakatifuza maeneo ya kazi pamoja na utume wa familia. Waamini walei wakiwa wamepyaishwa kutoka katika undani wa maisha yao, wanaweza sasa kuwa ni vyombo na mashuhuda wa huruma, upendo na msamaha wa Mungu; watu wenye wenye uwezo wa kusikiliza kwa makini na kujibu kilio cha Dunia Mama kuhusu utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote pamoja na kilio cha maskini wanaowazunguka; watu wanaoweza kuendeleza majadiliano katika ukweli na uwazi; ukarimu na upendo kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.
Baba Mtakatifu katika maadhimisho ya Jubilei ya Watu wa Kujitolea ametumia fursa hii, kuwatakia heri na baraka watu wa kujitolea katika maadhimisho ya Jubilei yao, kwani kwa hakika, wao ni mfano bora wa kuigwa kama ilivyokuwa kwa Kristo Yesu kwa ajili ya huduma ya upendo kwa jirani zao. Hawa ni watu ambao wameendelea kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma kwa wasafiri, faraja kwa wagonjwa na maskini; huduma kwa wafungwa, vijana na wazee. Kwa hakika, anasema Baba Mtakatifu Francisko watu wa kujitolea ni mahujaji wa Injili ya Matumaini kwa watu waliovunjika na kupondeka moyo. Ni faraja kwa watu wanaotembea katika jangwa la umaskini na upweke hasi na kwa njia matendo na huduma zao, wanaweza kuanzisha Bustani ya ubinadamu mpya, ndoto ambayo Mwenyezi Mungu anaendelea kumwotea mwanadamu. Kardinali Tagle amewataka watu wa Mungu kuwa ni mashuhuda na vyombo vya matumaini kwa watu waliovunjika na kupondeka moyo. Waendelee kujibidiisha katika ujenzi wa Kanisa: Moja, Takatifu, Katoliki na la Mitume, hata katika tofauti zao msingi, kwani wote wanaunganishwa na tumaini moja linalobubujika kutoka kwa Kristo Yesu.