Alhamis Kuu Jioni 2025: Tangazeni Na Kushuhudia Injili Ya Upendo
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Alhamisi Kuu, Mama Kanisa anakumbuka Siku ile iliyotangulia kuteswa kwake, Kristo Yesu, alipoweka Sakramenti ya Ekaristi Takatifu, yaani Mwili na Damu yake Azizi, chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa. Hii ni Sakramenti ya Sadaka: Shukrani, sifa na utukufu kwa Baba wa milele. Ni Kumbukumbu ya mateso yaletayo wokovu na ni sadaka ya uwepo wa Kristo kwa Neno na Roho wake Mtakatifu. Mama Kanisa anakumbuka pia Siku ile Kristo Yesu alipoweka Sakramenti ya Daraja Takatifu kwa kuwateuwa baadhi ya waamini na kuwaweka wakfu kwa ajili ya maadhimisho ya Mafumbo ya Kanisa. Hawa ni Makuhani waoliopewa dhamana ya kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu, katika Nafsi ya Kristo ambaye ni kichwa cha Kanisa lake! Hii ni Siku ambayo Kristo alikazia huduma ya upendo kwa kuwaosha mitume wake miguu, kielelezo cha upendo unaonafsishwa katika huduma makini kwa watu wa Mungu! Kardinali Mauro Gambetti, O.F.M. Conv., Makamu Askofu kwa mji wa Vatican, Alhamisi kuu jioni tarehe 17 Aprili 2025 kwa niaba ya Baba Mtakatifu Francisko ameongoza Ibada ya Misa Takatifu, jioni ya Alhamisi kuu na katika mahubiri yake amejikita zaidi katika kufafanua maana ya Pasaka, Usaliti wa Yuda Iskarioti, Mateso na Kifo cha Kristo Yesu Msalabani na kwamba, Mapadre wanaitwa kushiriki katika kutangaza na kuishi Injili ya upendo, kiasi hata cha kusadaka maisha yao kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya Kanisa la Kristo Yesu. Itakumbukwa kwamba, Pasaka ya kwanza ya Kiyahudi iliadhimishwa katika mazingira ya utumwa, unyonyaji na ukandamizaji pamoja na mateso. Ilikuwa ni alama ya shukrani kwa Mwenyezi Mungu kuwakomboa kutoka utumwani Misri. Akawasikiliza wanyenyekevu na maskini wanaomtumainia. Kristo Yesu aliadhimisha Pasaka ya Agano Jipya na la milele katika mazingira ya: Udhalimu, unyanyasaji, kashfa, umaskini, magonjwa, vurugu na upweke hasi. Lakini Kristo Yesu, anatamani sana kuratibisha mahusiano na mafungamano na waja wake; kujenga na kudumisha urafiki; anataka kula na kunywa na familia yako, ili kusheherekea Pasaka yake.
Pasaka ilisherehekewa na mkusanyiko mkubwa wa watu, wote wakiwa na kiu ya kuuona utakatifu na utukufu; unyenyekevu na ukweli, ili kushiriki karamu ya mwisho pamoja na wafuasi wake, ambao Baba wa milele amempatia. Hii ni fursa ambayo inatolewa kwa watu wote, lakini kwa bahati mbaya, binadamu katika maisha yake, hajaweza kuwashirikisha wengine. Kati ya Mitume wa Yesu alikuwepo Yuda Iskarioti aliyemsalati Kristo Yesu kwa vipande thelathini vya fedha. Hata leo hii kuna usaliti mkubwa wa kimaadili na utu wema; akili, dhamiri na utu wema; kunakosekana upendo wa kibinadamu na matokeo yake ni usaliti na kuuzwa kwa misingi ya gharama, mafao ya kiuchumi na hatimaye wawe kupata madaraka na nguvu za kiuchumi. Hakuna tena watunzaji bora wa mahusiano na mafungamano ya kijamii; wala huruma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii; na hawa ndiyo maskini na wahamiaji pamoja na uharibifu wa mazingira nyumba ya wote. Hivi ndivyo Yuda Iskariote alivyo fanya kwa Kristo Yesu. Watu wanatafuta faida na mafao yao binafsi na matokeo yake ni kuzuka kwa vita, migogoro na machafuko pamoja na kuzorota kwa uchumi na kuna mamilioni ya watu wanaosulubishwa kutokana na hali hii. Kundi la wanafunzi wa Kristo Yesu lilionesha udhaifu mkubwa. Lakini pia walikuwa imara na hivyo kujikita katika uhuru, haki na amani. Hata leo hii, Kristo Yesu anajali upendo na anataka kupendwa na kuhudimia, kama alivyofanya Siku ile ya Alhamisi kuu, ili kuleta mabadiliko katika maisha; mabadiliko yanayosimikwa katika huduma ya upendo.
Mapadre kwa namna ya pekee kabisa wanaitwa na kutumwa kutangaza na kushuhudia Injili ya upendo unaomwilishwa katika huduma, kiasi hata cha kuwa tayari kuyamimina maisha yao, tayari kutoa nafasi kwa watu wengine waweze kuishi.Huu ni wakati kwa Mama Kanisa kujifunua na kudhirisha asili yake kama watu wa Kikuhani, asili ambayo inapata chimbuko lake katika Ekaristi Takatifu, ili hatimaye, waweze kuwa ni Ekaristi nyingine, kwa kutangaza na kushuhudia Umungu wa Kristo Yes una Ubinadamu wake, mambo ambayo Kristo Yesu amewashirikisha kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo aliyowakabidhi. Kristo Yesu anashuka kila wakati kutoka kifuani mwa Baba yake wa mbinguni na kuingia mikononi mwa Padre mhudum wa Ekaristi Takatifu ili kuwaonesha ile Sura ya unyenyekevu unaowaonesha Mwili na Damu yake Azizi, iliyo hai na ya kweli; Mwili unaotolewa kwa ajili ya wokovu wa wengi. Mama Kanisa anamshukuru Kristo Yesu kwa zawadi ya Ekaristi Takatifu, Daraja Takatifu pamoja na upendo unaomwilishwa katika huduma kwa watu wa Mungu.