Vatican yafuta Harakati ya Maisha ya Kikristo(Sodalicio)wanachama waomba msamaha!
Vatican News.
Kuanzia Jumatatu Aprili 14 Jumuiya ya Harakati ya Maisha ya Kikristo (S.C.V.), ijulikanayo pia kama 'Sodalicio,' haipo tena. Ni Jumuiya ya Harakati ya walei, iliyoanzishwa katika miaka ya 1970 na kuenea katika Bara la Amerika ya Kusini, ambako iliwakilisha mojawapo ya mitume walio hai na ambayo sasa imefutwa kwa Hati iliyotiwa saini tarehe 14 Aprili 2025, kufuatia na kashfa za unyanyasaji na rushwa ziliyodaiwa dhidi ya baadhi ya viongozi wake. Hati ya kufutwa kwa Harakati hiyo ya kitume ilitangazwa na Harakati yenyewe katika taarifa kwenye tovuti yake rasmi ambayo ilibainisha kuwa ilitiwa saini na mkuu wake, José David Correa, katika makao makuu ya Baraza la Kipapa la Maisha ya Kitawa na Vyama vya Kitume, mbele ya Mwenyekiti wa Baraza hilo Sr Simona Brambilla.
Kufukuzwa kwa Mwanzilishi
Wakati huo huo, Monsinyo Jordi Bertomeu Farnós , alikuwa ameteuliwa kuwa Kamishna wa Kitume kwa ajili ya shughuli zinazohusiana na kufutwa kwa Harakati hiyo ya kitume, ambapo Afisa wa Baraza Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa hapo awali aliteuliwa na Baba Mtakatifu Francisko kuchunguza, pamoja na Askofu Mkuu Charles Scicluna, Askofu Mkuu wa Malta na Rais wa Baraza kwa ajili ya uchunguzi (katika masuala nyeti) katika Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa) kuhusu kesi za unyanyasaji nchini Chile na maeneo mengine ya Amerika ya Kusini, pamoja na nchini Peru, mahali alikozaliwa Luis Fernando Figari, mwanzilishi wa Harakati hiyo(Sodalicio). Figari alifukuzwa mnamo Agosti 2024, kutoka katika Harakati ya Jumuiya hiyo ambayo yeye mwenyewe alianzisha kwa sababu ya tuhuma za unyanyasaji wa kimwili, kisaikolojia na kingono, ikiwa ni pamoja na watoto wadogo.
Na kesi hiyo inatazama nyuma, kama miaka 20 iliyopita, hadi mwanzoni mwa miaka ya 2000, wakati malalamiko kutoka kwa wanachama wa zamani yaliposababisha uchunguzi na ripoti za vyombo vya habari kuhusu unyanyasaji,na udhalilishaji, wa wanachama vijana zaidi wa Harakati hiyo ya kitume. Mnamo 2015, waandishi wa habari Pedro Salinas na Paola Ugaz walichapisha kitabu cha ushuhuda wa waathirika wa nyanyaso. Hatua kadhaa za Ofisi ya Mwendesha Mashtaka wa Umma wa Peru na uchunguzi wa ndani ndani ya Harakati hiyo ya kitume (Sodalicio) yenyewe zilifuata, na kusababisha kuingilia kati kwa Papa Francisko, ambaye amekuwa akifuatilia kwa makini kesi hiyo. Katika hafla hiyo, kulingana na taarifa za uchunguzi kwenye Mtandao wa Crux, Papa alikuwa ametangaza hitimisho linalokuja la kesi dhidi ya Harakati hiyo ya kitume
Huzuni na utii
Tangazo rasmi la kuvunjwa kwa Sodalitium siku ya Jumatatu lilipokelewa kwa huzuni na utii na wanachama, wa Harakati hiyo kwa mujibu wa taarifa kutoka Harakatii hiyo ya kitume. Taarifa hiyo pia ilihusu hatua za ulipaji fidia zilizofanywa na Harakati hiyo kuanzia Mei 2016 hadi sasa, ikiwa ni pamoja na usaidizi wa kimasomo, tiba na fidia ya kifedha. Wanachama wa jumuiya hiyo walisema wanamshukuru Mungu kwa kuruhusu "watu wengi kutoka nchi mbalimbali kuishi nasi uzoefu wa pamoja wa imani ya kweli, udugu, na bidii ya kitume, ambayo imezaa matunda mengi." Wakati huohuo, mawazo yao tanakwenda kwa waathirika ambao tunaomba msamaha kwa sababu ya unyanyasaji uliofanywa katika jamii yao.” Taarifa hiyo pia inaomba msamaha wa Kanisa zima na jamii “kwa maumivu yaliyosababishwa, na tunaamini kwamba jitihada zilizofanywa katika mchakato wa ukarabati zitazaa matunda, na tutaendelea kutoa maombi yetu ili Bwana aponye majeraha ya dhuluma.”
Wakati wa uongofu
Taarifa ya Harakati hiyo ya (Sodalicio) pia inatoa shukrani kwa wale ambao wamekuwa sehemu ya jumuiya na ambao wamejitolea kwa ukarimu miaka ya maisha yao kwa utume wa Kanisa. Pia inawashukuru wachungaji ambao wamejali jumuiya katika majimbo, “wajumbe wa kipapa ambao wametuongoza na kutusindikiza kwa ari kubwa, upendo, na hekima katika mchakato wetu wa kufanywa upya, na familia na marafiki ambao wameonyesha ukaribu na msaada. Bwana Mwema ana njia za ajabu, ambazo kupitia hizo anaweza kufanya mambo yote kuwa mapya siku zote,” inahitimisha barua hiyo, ikionesha tumaini kwamba kinachofungua sasa kinaweza kuwa “wakati wa pendeleo wa kuongoka na kufanywa upya kwa sauti ya Mungu, daima katika ushirika na Baba Mtakatifu na pamoja na Mama yetu, Kanisa.”