Baraza la Kipapa kwa ajili ya Wakleri katika maadhimisho ya Dominika ya Matawi, tarehe 13 Aprili 2025 limechapisha Waraka Kuhusu Nidhamu ya Nia za Misa Takatif.u Baraza la Kipapa kwa ajili ya Wakleri katika maadhimisho ya Dominika ya Matawi, tarehe 13 Aprili 2025 limechapisha Waraka Kuhusu Nidhamu ya Nia za Misa Takatif.u  (Vatican Media)

Waraka Kuhusu Nidhamu ya Nia za Misa Takatifu 2025

Baraza la Kipapa kwa ajili ya Wakleri katika maadhimisho ya Dominika ya Matawi, tarehe 13 Aprili 2025 limechapisha Waraka Kuhusu Nidhamu ya Nia za Misa Takatifu na Waraka huu utaanza kutumika rasmi wakati wa Sherehe ya Pasaka ya Bwana tarehe 20 Aprili 2025. Waraka huu umeridhiwa na Baba Mtakatifu Francisko na kwamba, haya ni Mapokeo na desturi inayopaswa kuheshimiwa na kulindwa. Waamini wajenge utamaduni wa kuchangia ustawi na maendeleo ya Kanisa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baraza la Kipapa kwa ajili ya Wakleri katika maadhimisho ya Dominika ya Matawi, tarehe 13 Aprili 2025 limechapisha Waraka Kuhusu Nidhamu ya Nia za Misa Takatifu na Waraka huu utaanza kutumika rasmi wakati wa Sherehe ya Pasaka ya Bwana tarehe 20 Aprili 2025. Waraka huu umeridhiwa na Baba Mtakatifu Francisko na kwamba, haya ni Mapokeo na desturi inayopaswa kuheshimiwa na kulindwa. Kufuatana na Mapokeo na mazoea yaliyoidhinishwa na Kanisa, Padre anayeadhimisha Ibada ya Misa Takatifu, hata akiwa pamoja na Mapadre wengine anaweza kupokea fedha ili kuitolea Misa kwa nia maalum. Mapadre wakumbuke kwamba, wao ni vyombo vya Sakramenti ya Ekaristi Takatifu na wala si wamiliki wa Sakramenti hii. Waamini wanatambua ushiriki wao, kwa njia ya sadaka na hivyo wanajiunga na Sadaka ya Misa Takatifu, kwa kutoa fedha kwa ajili ya kuchangia ustawi, maendeleo na mafao ya Kanisa pamoja na Mapadre wao. Kwa njia hii, waamini wanaungana na Kristo Yesu anayejisadaka Altareni, kielelezo cha ushirika na Kristo Yesu. Haya ni Mapokeo ambayo yameidhinishwa na yanaendelezwa na Mama Kanisa. Wahudumu wa Altare wana haki pia ya kupata ujira wao kutoka Altareni. Sheria, taratibu na kanuni zinazoratibu fedha inayotolewa kwa ajili ya Nia za Misa, sehemu ya fedha hii inapaswa kutolewa kwa ajili ya huduma kwa maskini, kwa Askofu mahalia na sehemu ya fedha hii wanapewa Mapadre wanaoadhimisha mafumbo haya ya Kanisa. Ikumbuke kwamba, waamini Wakristo wanaotoa fedha kwa ajili ya Nia ya Misa wanachangia katika mema ya Kanisa na kwa fedha hiyo wanashiriki katika wajibu wa Kanisa wa kuwategemeza wahudumu wake na kazi zake. Kusiwepo na “harufu ya biashara katika fedha ya Nia ya Misa.”

Waraka Kuhusu Nidhamu ya Nia za Misa Takatifu 2025
Waraka Kuhusu Nidhamu ya Nia za Misa Takatifu 2025   (Vatican Media)

Fedha ya Nia ya Misa ni zawadi na wala si gharama ya Ibada ya Misa Takatifu. Kumbe, Padre mhadhimishaji wa Ibada ya Misa Takatifu anatakiwa kisheria kupokea fedha ya Nia moja ya Misa. Kutokuadhimisha Ibada ya Misa kwa nia iliyotolewa ni ukosefu wa haki. Kutokana na upungufu wa Mapadre kuweza kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa nia zilizotolewa kumepelekea maadhimisho ya Ibada ya Misa kwa kupokea fedha kutoka kwa waamini wengi, lakini Ibada ya Misa Takatifu inayoadhimishwa ni moja tu. Waraka huu unaounganisha na maudhui yaliyomo kwenye Waraka wa “Mos iugiter wa Mwaka 1991” ulipania kuratibu masuala msingi yaliyojitokeza lakini zaidi kuhusu umati wa waamini unaokusanyika kwa “nia moja” au maadhimisho ya Sherehe zenye nia nyingi katika Ibada ya Misa Takatifu. Kwa sasa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Wakleri, linasema ikiwa itaamriwa na Mabaraza ya Maaskofu mahalia au Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Kikanda “Mapadre wanaweza kupokea matoleo mengi kutoka kwa watoaji watofauti, wakiyakusanya pamoja na wengine na kuwatosheleza kwa Ibada ya Misa Takatifu moja inayoadhimishwa kulingana na nia moja ya pamoja. Watoa fedha wanapaswa kujulishwa kwa hiari tu. Jambo la msingi ni kwa Jumuiya ya waamini kuhakikisha kwamba, walau kila siku kunaadhimishwa Ibada ya Misa Takatifu kwa nia moja, lakini Padre kama inavyoelekezwa katika Waraka huu anaweza kusherehekea Misa mbalimbali hata kulingana na “nia ya pamoja” huku akibaki imara kwamba anaruhusiwa kubaki, kila siku na sadaka moja kwa nia moja. Waamini waendelee kujenga utamaduni na uelewa wa kuchangia mafao ya Kanisa kwa kuwasaidia maskini sanjari na kuchangia utume wa Kanisa.

Kwa nia za Misa waamini wanashiriki kikamilifu katika Sadaka ya Yesu
Kwa nia za Misa waamini wanashiriki kikamilifu katika Sadaka ya Yesu   (Vatican Media)

Mhudumu wa Sakramenti ya Ekaristi Takatifu hapaswi kuomba fedha ya ziada kwa ajili ya usimamizi wa Sakramenti na wala maskini wasinyimwe Sakramenti kutokana na umaskini wao. Jimbo lipange vyema juu ya ugawaji wa matoleo ya Ibada ya Misa Takatifu, kwa kuzingatia mazingira na hali halisi ya Jimbo husika. Lengo kuu ni kudhibiti shughuli haramu. Kila Nia na Matoleo kwa ajili ya Ibada ya Misa Takatifu yaorodheshwe kwenye Daftari maalum, huku wakionesha tofauti kati ya Nia maalum pamoja na nia tofauti hata kama ni za pamoja. Misa tofauti zinapaswa kuadhimishwa kwa nia za kila mmoja aliyetoa fedha yake hata kama ni kidogo, nayo imepokelewa. Anayelazimika kuadhimisha na kutolea Misa takatifu kwa wale waliotoa fedha, anafungwa na faradhi hata kama fedha iliyotolewa imepotea kwa kosa lisilo la kwake. Waamini wahamasishwe kuchagia ustawi, maendeleo na mafao ya Makanisa ya Kimisionari kwa nia za Ibada ya Misa Takatifu, kwa kujikita katika katekesi makini pamoja na ushirika kwa mambo matakatifu “Communio sanctorum” yaani: umoja wa imani na mapendo yanayopata chimbuko lake katika Fumbo la Ekaristi Takatifu. Pale ambapo hakuna tamko la Askofu mahalia, Baraza la Maaskofu Kitaifa na Kikanda, Sheria, Kanuni na Taratibu zinazotumika ni zile zilizomo kwenye Waraka wa “Mos iugiter wa tarehe 22 Februari 1991. Waraka huu, utatumika kwa kipindi cha miaka kumi na baadaye utafanyiwa upembuzi yakinifu kuhusu matumizi yake na hatimaye, utaboreshwa zaidi.

Nia ya Misa
15 Aprili 2025, 14:41