Balozi Gertrude Mongella,miaka 30 baada ya Mkutano wa Beijing kunako 1995!
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Mwaka huu, imetimia miaka thelathini tangu ulipofanyika Mkutano wa Beijing jijini Beijing,China na kupitisha kile kinacoendelea kufahamika kama Azimio la Beijing,lengo likiwa kuleta usawa wa kijinsia kwa kuwainua wanawake katika nyanja mbalimbali baada ya kundi hilo kuwa limekandamizwa kwa miaka mingi duniani kote. Kwa majuma mawili mfululizo hadi tarehe 21 Machi 2025 ulimwengu uliwaona washiriki wa Mkutano katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani wa 69 wa Hali ya Kamisheni ya Hali ya Wanawake duniani, CSW69 ili kujadili ni kwa kiasi gani Azimio la Beijing limefikiwa. Miongoni mwa waliohudhuria mkutano huo aliyekuwa ni Katibu Mkuu wa wa zamani wa Mkutano huo wa 4 wa Beijing, kanoko mwaka 1995, Balozi Gertrude Mongella mzaliwa wa Tanzania. Anold Kayanda wa Idhaa ya Kiswahili ya Radio ya Umoja wa Mataifa alipata fursa ya kuzungumza naye. Yafuatayo ni mazungumzo yao:
Ni ujumbe gani Gertrude Mongella anauacha kwa msichana au mwanamke wa miaka 30 ijayo?
Balozi Mongella analijibu swali hili kwa namna tofauti kabisa – anasema, “ujumbe ninaouacha sio kwa mtoto wa kike tu, mimi nawaachia wote, mtoto wa kike na mtoto wa kiume. Kwasababu taabu iliyotupata huko nyuma ni kutokana na kutenganisha binadamu mwanaume, binadamu mwanamke ndio imetupa matatizo wanaume wakaanza kuwanyanyasa wanawake hata mahali ambako hawapaswi kunyanyasika.”
Bi Mongela kwa kutoa ujumbe:tubadilishe mtazamo
“Kwa hiyo mimi ujumbe nilionao ni kubadilisha mtazamo wa binadamu, wanaume kwa wanawake. Kwa hiyo sasa ndio mwanzo mzuri watoto wa kiume na wa kike wote wajifunze haki za binadamu na wazione kwamba haki ya mwanamke pia ni haki ya binadamu ili tufike mahali suala lisiwe ni mwanamke au mwanaume, tuseme ana uwezo? Ndilo liwe suala.” Alisisitiza Bi. Mongella.
Kwa upande wa Matumaini:wanawake wafanye shughuli kwa usawa
Pamoja na changamoto zilizopo, Balozi Gertrude Mongella anayo matumaini na anatia ushuhuda akisema katika maisha yake kabla hawajaenda kwenye Mkutano wa Beijing, “kuzungumzia mwanamke kwenda kuwinda ilikuwa mwiko, kuzungumzia mwanamke kwenda kuvua samaki ilikuwa mwiko, kuzungumzia suala la kuchimba madini hiyo ndio mwiko zaidi mwanamke kwenda shimoni.” Lakini sasa anasema, “tunaanza kubadilika kuna vikundi vya akina mama wavuvi, wakina mama wachimba madini, wakina mama ambao wanafanya kazi na shughuli mbalimbali.”