Tafuta

Dominika ya IV ya Kipindi cha Kwaresima inabeba ujumbe wa furaha ya Baba mwenye huruma anayewapenda, kuwajali na kuwasubiri watoto wake ili awafanyie sherehe kubwa baada ya toba na wongofu wa ndani. Dominika ya IV ya Kipindi cha Kwaresima inabeba ujumbe wa furaha ya Baba mwenye huruma anayewapenda, kuwajali na kuwasubiri watoto wake ili awafanyie sherehe kubwa baada ya toba na wongofu wa ndani.  (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Tafakari Dominika IV Kwaresima Mwaka C: Baba Mwenye Huruma na Wanawe Wapotevu!

Dominika ya IV ya Kipindi cha Kwaresima pia huitwa "Domenica Laetare" hii ni furaha ya toba na wongofu wa ndani tayari kumrudia Mwenyezi Mungu. Ni furaha, utulivu na amani ya ndani, baada ya mwamini kujipatanisha na nafsi yake, Mwenyezi Mungu, jirani na mazingira nyumba ya wote. Rej. Lk 15:1-3, 11-32. Sehemu hii ya Injili kwa wengi inajulikana kama Injili ya Mwana Mpotevu. Lakini inapaswa kuitwa Injili ya Baba Mwenye Huruma kwani ndiye mhusika mkuu!

Na Padre Pascha Ighondo, - Vatican.

Tafakari ya Neno la Mungu, katika Dominika ya nne ya Kipindi cha Kwaresima, Mwaka C wa Kiliturujia katika Kanisa, siku ya ishirini na sita ya kujitakatifuza. Dominika ya IV ya Kipindi cha Kwaresima inabeba ujumbe wa furaha ya Baba mwenye huruma anayewapenda, kuwajali na kuwasubiri watoto wake ili waweze kutubu na kumwongokea. Dominika ya IV ya Kipindi cha Kwaresima pia huitwa "Domenica Laetare" au “dominika ya furaha” hii ni furaha ya toba na wongofu wa ndani tayari kumrudia Mwenyezi Mungu. Ni furaha, utulivu na amani ya ndani, baada ya mwamini kujipatanisha na nafsi yake, Mwenyezi Mungu, jirani na mazingira nyumba ya wote. Rej. Lk 15:1-3, 11-32. Sehemu hii ya Injili kwa wengi inajulikana kama Injili ya Mwana Mpotevu. Lakini inapaswa kuitwa Injili ya Baba Mwenye Huruma kwani ndiye mhusika mkuu anayewangojea watoto wake wawili, waweze kutubu na kurejea tena nyumbani, ili aweze kuwafanyia sherehe. Baba Mwenye huruma ni kielelezo cha Mungu Baba Mwenyezi anayesamehe daima, yuko tayari kuwapokea na kuwafanyia watoto wake sherehe, hata kama wametenda dhambi kubwa kiasi gani. Jambo la msingi ni kutubu na kumwongokea Mungu. Hii ni Dominika ya Furaha “Domenica Laetare” kama maneno ya wimbo wa mwanzo yanavyosema; “Furahi, Ee Yerusalemu, mshangilieni ninyi nyote mmpendao; furahini, ninyi nyote mliao kwa ajili yake, mpate kunyonya, na kushibishwa kwa maziwa ya faraja zake” (Isa. 66:10-11). Tunaalikwa kufurahi kwa sababu Pasaka i karibu. Ndiyo maana liturujia ya dominika hii inaruhusu altare kupambwa kwa maua, rangi ya mavazi ya Misa kuwa ya pinki badala ya zambarau, na ala za muziki zinaruhusiwa kupigwa. Ni katika tumaini hili mama Kanisa katika sala ya mwanzo anasali hivi; “Ee Mungu, umeleta kwa namna ya ajabu upatanisho wa wanadamu kwa njia ya Neno wako. Tunakuomba utujalie wakristu bidii ya kujiweka tayari kwa ibada na imani kuadhimisha sikukuu ijayo.”

Maelezo ya jinsi ya kuadhimisha Sherehe ya Pasaka: Uhuru wa watoto wa Mungu
Maelezo ya jinsi ya kuadhimisha Sherehe ya Pasaka: Uhuru wa watoto wa Mungu

Somo la kwanza ni la Kitabu cha Yoshua (Yos. 5:9a, 10-12). Nalo linahusu maagizo ya Mungu kwa wana wa Israeli namna ya kuadhimisha sikukuu ya Pasaka, wakikumbuka jinsi alivyowatoa utumwani Misri na kuwafikisha katika nchi ya ahadi. Ni siku ya kukumbuka siku ambayo aliwaondolea aibu ya kuwa watumwa, akawawezesha kupigana vita wakaichukua, kuimiliki na kuikalia nchi ya ahadi, wakaanza maisha mapya huko Kanaani maeneo ya Gilgali. Hivyo wakala sikukuu ya Pasaka, siku ya 14 ya mwezi, jioni, katika nchi tambarare za Yeriko. Nao wakala katika mazao ya nchi siku ya pili ya kuiandaa hiyo sikukuu ya Pasaka kwa mikate isiyotiwa chachu, na bisi, siku hiyo hiyo. Ndipo ile manna ikakoma siku ya pili yake, hapo ndipo walipoanza kula mazao ya nchi ya Kaanani kuanzia mwaka huo. Mzaburi alipotafakari ukuu na wema huu wa Mungu aliimba maneno haya ya wimbo wa katikati akisema; “Onjeni mwone ya kuwa Bwana yu mwema. Nitamhimidi Bwana kila wakati, sifa zake zi kinywani mwangu daima. Katika Bwana nafsi yangu itajisifu, wanyenyekevu wasikie wakafurahi. Mtukuzeni Bwana pamoja nami, na tuliadhimishe jina lake pamoja. Nalimtafuta Bwana akanijibu, akaniponya na hofu zangu zote. Wakamwelekea macho wakatiwa nuru, wala nyuso zao hazitaona haya. Maskini huyu aliita, Bwana akasikia, akamwokoa na taabu zake zote” (Zab. 34:8, 1-6).

Kielelezo cha Injili ya Baba Mwenye Huruma Kwa Watoto Wake Wote
Kielelezo cha Injili ya Baba Mwenye Huruma Kwa Watoto Wake Wote   (Vatican Media)

Somo la pili ni la Waraka wa Pili Mtume Paulo kwa Wakorintho (2 Kor. 5:17-21). Katika somo hili Mtume Paulo anatufundisha jinsi dhambi ilivyotutenganisha na Mungu na jinsi Kristo alivyotupatanisha na Mungu kwa kifo chake na huo upatanisho unaendelezwa na wajumbe waliotumwa na Kristo nasi tunapaswa kufanya jitihadi za kujipatanisha na Mungu kwa njia yake Kristo. Yeye ambaye hakujua dhambi, Mungu alimfanya kuwa dhambi kwa ajili yetu, ili sisi tupate kuwa haki ya Mungu katika Yeye. Ni upendeleo wa hali ya juu sana tunaopewa na Mungu, hivyo hatuna budi kuupokea kwa moyo wa shukrani na furaha. Injili ni kama ilivyoandikwa na Luka (Lk. 15:1-3, 11-32).  Sehemu hii inahusu simulizi la mwana mpotevu na Baba mwenye huruma. Lengo ni kutufundisha kuwa wakosefu wanaweza kuingia katika Ufalme wa Mungu kama wakitubu dhambi zao.  Lakini kinyume chake wema wanaweza kuingia katika moto wa milele kama watakengeuka na kuziacha amri za Mungu. Yesu anatoa fundisho hili baada ya mafarisayo na waandishi kumnung¢unikia kwa kuwakaribisha watoza ushuru na wenye dhambi, akala na kunywa nao. Msisitizo hapa upo katika ukuu wa huruma ya Mungu kwa wenye dhambi wanaotubu, kuwa Mungu anampokea mara moja, anamkumbatia, anambusu, anamvika mavazi mapya, anamfanyia sherehe, anamuweka huru na kumpa hadhi ya kushiriki karamu ya Kristo, Ekaristi Takatifu ambayo ni kiini cha maisha yetu ya kikristo, na hivyo anapata nafasi ya kuanza maisha mapya. Hii ndiyo furaha anayokuwa nayo mtu akifanya toba ya kweli na kuungama vyema dhambi zake, akizitaja waziwazi kwa ujasiri bila kuzimumunya wala kuficha chochote. Ni furaha ya ajabu isiyoelezeka, furaha inayotuondolea mawazo ya kukata tamaa na inayotupa matumaini na nguvu ya kusonga mbele katika maisha yetu. Sakramenti hii ya kitubio inatuondolea aibu itokanayo na dhambi na kutuweka huru tukiwa wenye furaha.

Injili ya Baba Mwenye huruma na Mwana Mpotevu
Injili ya Baba Mwenye huruma na Mwana Mpotevu   (Vatican Media)

Waisraeli walipelekwa utumwani Misri kwa sababu ya dhambi na mwana mpotevu alipelekwa kwenye banda la nguruwe kwa sababu ya dhambi baada ya kula mali ya baba yake na makahaba. Ndivyo tunavyokuwa nasi tunapotenda dhambi, tunakuwa watumwa wa shetani, tunachakaa na kuwa wachafu. Mwaliko ni huu, kama mwana mpotevu, tunapaswa kutafakari na kuzingatia mioyoni mwetu na kujiuliza; “Misri yangu ni wapi?” na “banda langu la nguruwe ni lipi?” Je, ni kitu gani kimenipeleka huko? Je, ni dhambi ipi imenipeleka huko - ukahaba, uasherati, ulevi, uchawi, ushirikina, uzembe, ubinafsi, maseng’enyo, umbea, uongo, ulafi, kiburi, marafiki wabaya, dawa za kulevya, wizi, ujambazi, rushwa, ukaidi, au ni nini? Ni wakati wa kutafakari na kuzingatia moyoni na kuamua na kusema; inatosha, ninaondoka na kurudi kwa Baba yangu na kwamwambia, Baba nimekosa naomba unisamehe. Mama Kanisa anatufundisha kuwa dhambi inaondolewa kwa njia ya Sakaramenti ya ungamo la Dhambi. Sakramenti hii inaitwa pia Sakramenti ya toba, Sakramenti ya kitubio, Sakramenti ya maungamo, Sakramenti ya msamaha, Sakramenti ya Upatanisho. Kuungama ni ile hali ya mdhambi aliyetayari kutubu kwa kujishutumu mwenyewe kutokana na dhambi alizozitenda mbele ya mhudumu halali wa Kanisa ili kujipatanisha na Mungu. Mungu tuliyemkosea ndiye aliyeanzisha upatanisho nasi kwa kutuwekea sakramenti hii kwa njia ya mwanae wa pekee Bwana Yesu Kristo. Mwaliko tunaoupewa wa kufurahi kwa sababu Pasaka i karibu, unatudai tuondoke, twende kwa Baba, tukaungame, tukamwambie tumekosa na kuomba msamaha.

Kimbilieni Mahakama ya Huruma ya Mungu kujichotea msamaha
Kimbilieni Mahakama ya Huruma ya Mungu kujichotea msamaha

Lakini kuondoka na kwenda si rahisi. Inahitaji ujasiri na neema ya Mungu. Hivyo kila mmoja katika hali yake anahitaji ujasiri na kusema sasa imetosha, nitaondoka na nitakwenda. Kamwe tusikubali ukubwa wa dhambi utukatishe tamaa ya kupata msamaha, kwani jinsi dhambi ilivyo kubwa ndivyo nguvu ya huruma ya Mungu ilivyo kuu zaidi. Bwana ni mwema na mwenye huruma, hapendi wadhambi wapotee na si mwepesi wa hasira ni mwingi wa huruma kwa kila anayetubu na kuomba msamaha. Lakini tujue wazi kuwa wapo watakaochukiza na maamuzi yetu hasa wale tuliozoea kuishi nao katika dhambi, kama mafarisayo na waandishi walivyomnung’unikia Yesu au kama kaka wa mwana mpotevu. Tusiogope kwani furaha tutakayoipata ni kubwa zaidi kuliko kuendelea kubaki katika dhambi. Tukumbuke kuwa dhambi ikiingia moyoni haimuachi mtu salama mpaka atakapoamua kutubu na kuungama. Madhara ya dhambi ni makubwa mno. Kila dhambi inaadhiri akili, inadhoofisha utashi, inaua dhamiri na kupoteza dira na mizani ya maadili. Dhambi isipoungamwa inampumbaza mtu, ikimwambia usiogope, hakuna shida. Baada ya mda dhamiri inakufa, mshipa wa aibu unakatika, unaanza kutenda dhambi hadharani bila kuogopa. Zaidi sana dhambi inadhuru afya ya mwili, kwani humfanya mtu kuwa na hasira na chuki ndani mwake hivyo yaweza kusababisha magonjwa mengine kama vile vidonda vya tumbo, au shinikizo la damu. Dhambi inaharibu lengo la jumuiya na jamii ya walio katika safari ya kumfikia Mungu pia inaharibu mwili wa fumbo wa Kristo (1Wakor. 12:26).

Baba Mwenye huruma: Kufanya Sherehe iliwapasa!
Baba Mwenye huruma: Kufanya Sherehe iliwapasa!   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Dhambi inafanya roho ya mkosaji kukosa amani na zaidi sana Neema ya Utakaso. Mtu akikosa thamani ya Mungu lengo na thamani ya maisha yake inapotea na hivyo anaanza kuwayawaya na kuhangaika, haoni cha maana na hivyo linalobaki kwake ni dhamiri iliyojaa mawazo maovu tu kwani upendo, amani, furaha, msamaha kwake ni mwiko. Kumbe ni vyema sana kufanya maamuzi ya mwana mpotevu ya kujinasua na dhambi. Tuweke nia ya kujikosoa kwa unyofu, na kufanya toba ya kweli, tuondoke, tuenda kwa Baba na kumwambia nimekosa.  Dhambi hii ninaiacha! Baada ya kufanya hayo maamuzi basi tuijongee Sakramenti ya kitubio kwani ndimo tunapozoeshwa kunyenyekea na kujikubali kuwa tu wanyonge mbele ya Mungu na kinatustahilisha kupokea Ekaristi Takatifu, chakula cha kiroho kinachoimarisha katika maisha ya kifadhila. Tuepukane na Komunyo za mashaka na kufuru kwani huko ni kuila hukumu yetu wenyewe. Basi kujibidisha kila mara tuangukapo dhambini kuisogelea Sakramenti kitubio. Kuungama mara nyingi kunatupa fadhila ya unyenyekevu hivyo inatupa nafasi ya kujijua na kujikubali kuwa tu dhaifu. Tusikate tamaa tunapoungama mara nyingi maana ndiyo njia pekee ya kuipokea huruma ya Mungu. Lakini tusifanye hivyo kwa mazoea bali kwa moyo wa majuto. Tukifanya hivyo Mungu ni mwenye huruma atatupokea na kutuandalia karamu ya Pasaka ya sas ana ile ijayo Mbinguni. Ni katika tumaini hili mama Kanisa katika sala ya kuombea dhabihu anasali hivi; “Ee Bwana, tunakutolea kwa furaha dhabihu ziletazo wokovu wa milele. Tunakuomba sana utusaidie kuziheshimu kwa moyo wote na kuzitoa vema dhabihu hizi kwa ajili ya wokovu wa ulimwengu”. Na katika sala baada ya Komunio anahitimisha maadhimisho ya dominika hii akisali hivi; “Ee Mungu, unayemtia nuru kila ajaye ulimwenguni humu, tunakuomba uitie mioyo yetu nuru ya neema yako, tuweze kuwaza daima yakupendezayo wewe Mwenyezi na kukupenda kweli.” Na hili ndilo tumaini letu. Tumsifu Yesu Kristo.

Tafakari D4 Kwaresima
27 Machi 2025, 11:12