Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko anasema, huruma ya Mungu ndiyo mahangaiko ya upendo wake kwa binadamu dhaifu na mdhambi. Baba Mtakatifu Francisko anasema, huruma ya Mungu ndiyo mahangaiko ya upendo wake kwa binadamu dhaifu na mdhambi.   (Vatican Media)

Tafakari Dominika ya IV Kwaresima Mwaka C: Injili ya Baba Mwenye Huruma

Baba Mtakatifu Francisko anasema, huruma ya Mungu ndiyo mahangaiko ya upendo wake kwa binadamu dhaifu na mdhambi. Mwenyezi Mungu anajisikia kuwajibika, kwa maana ya kwamba, anatamani kuwaona watu wake wakiwa na afya njema, furaha na amani tele nyoyoni mwao. Hii ni njia ambayo upendo wa huruma ya Wakristo unaopaswa pia kujimwilisha. Huruma ndiyo msingi thabiti wa uhai wa Kanisa kama inavyojionesha katika Injili ya Baba mwenye huruma kuu!

Na Padre Joseph Herman Luwela, - Vatican.

UTANGULIZI: Mpendwa msikilizaji na msomaji wetu, Karibu katika tafakari ya Neno la Mungu kutoka hapa Radio Vatican. Tafakari ya Dominika ya Nne ya Kwaresima (Laetare) furahini kwani tumesonga sana katika maadhimisho ya Kipindi cha Kwaresima, matumaini na furaha ni kubwa kwa mwaka C. Baba Mtakatifu Francisko anasema, huruma ya Mungu ndiyo mahangaiko ya upendo wake kwa binadamu dhaifu na mdhambi. Mwenyezi Mungu anajisikia kuwajibika, kwa maana ya kwamba, anatamani kuwaona watu wake wakiwa na afya njema, furaha na amani tele nyoyoni mwao. Hii ni njia ambayo upendo wa huruma ya Wakristo unaopaswa pia kujimwilisha. Huruma ndiyo msingi thabiti wa uhai wa Kanisa. Kazi zake zote za kichungaji zinapaswa kufungamanishwa katika upole linalouonesha kwa waamini; hakuna chochote katika mahubiri na ushuhuda wake kwa ulimwengu kinachoweza kukosa huruma. Umahiri wa Kanisa unaonekana kwa namna linavyoonesha huruma na upendo. Huruma ya Mungu inafungua malango ya moyo ili kuonesha upendo na ukarimu kwa watu wanaoishi katika upweke na kusukumizwa pembezoni mwa jamii, ili kweli waweze kujisikia ndugu na watoto wapendwa wa Baba wa milele kama ilivyokuwa kwa Mwana mpotevu, shilingi na kondoo aliyepotea. Huruma ya Mungu inawawezesha watu kutambua na kuguswa na mahitaji msingi ya jirani zao hasa wale wanaohitaji kuonjeshwa faraja na upendo. Kimsingi, huruma ya Mungu inawawezesha waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kuwa ni vyombo na mashuhuda wa haki, amani na upatanisho.

Sherehe ya Huruma na Upendo wa Mungu kwa waja wake
Sherehe ya Huruma na Upendo wa Mungu kwa waja wake   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Ikumbukwe kwamba, huruma ya Mungu ni kiini cha imani, maisha na utume wa Kanisa; ushuhuda makini wa Ufufuko wa Kristo Yesu. Bikira Maria, Mama wa huruma ya Mungu awasaidie waamini: kuamini na kuyaishi yote haya kama mashuhuda wa Injili ya huruma, furaha na mapendo. Katika Injili ya Luka 15:1-3, 11-32 Yesu anatoa mfano wa Baba mwenye huruma na Mwana mpotevu ili kuonesha huruma na upendo wa Mungu kwa wale waliopotoka na kurudi kwa toba. Katika mfano huu, Yesu anafundisha kuhusu huruma ya Mungu, ambaye anapokea kwa furaha yule aliyepotea na kurudi kwake kwa toba. Huu ni mfano wa upendo wa Baba kwa watoto wake, na umuhimu wa kutubu na kurejea kwa Mungu. Tunaendelea na vita vyetu vya kiroho na mazoezi ya kupendana, kufunga na kusali. Ni kipindi cha toba, msamaha na maondoleo ya dhambi ndio maana Injili leo inatupatia simulizi la mwana mpotevu na huruma ya Baba, karibuni tuutafakari upendo huu wa Baba tukiongozwa na wazo hili “Upendo wa Baba umetukomboa.” Mfano wa mwana mpotevu ni hitimisho la mifano 2 ya Yesu kuhusu huzuni ya kupotea na furaha ya kupatikana. Kuna aina 2 za kupotea: kupotelea nje - Mfano 1 ulikuwa ni kupotea kwa kondoo porini na kupotelea ndani - wa 2 ni kupotea kwa shilingi na mama anafagia nyumba kuitafuta… Mwana mpotevu ni muhtasari/hitimisho sababu unahusisha aina zote 2, yupo mwana mpotevu aliyepotelea nje na anaonekana wazi na tulio wengi tunamlaumu na yupo pia kaka yake aliyepotea akiwa ndani na wengi hatumuoni wala hatumlaumu.

Sakramenti ya Upatanisho ni kielelezo cha huruma na upendo wa Mungu
Sakramenti ya Upatanisho ni kielelezo cha huruma na upendo wa Mungu   (Vatican Media)

UFAFANUZI: Kristo anatupatia wahusika 3: mwana mpotevu, kaka mkubwa na Baba yao. Tuanze na mwana mpotevu. Kadiri ya mila na desturi za kiyahudi baba hakuwa huru na mali zake, mwana mkubwa alipaswa kupata 2/3 ya mali zote (ili awasaidie na ndugu zake) na mdogo alipata theluthi tu. Urithi uligawiwa baada ya mzazi kufariki. Hivi mwana mpotevu kwa kuomba urithi kwa baba yake ilhali bado ni mzima lilikuwa ni pigo kwa mzazi yule, ni kama vile alimtangazia wazi kuwa wewe umekwisha kufa, haumo tena moyoni mwangu. Baba hasemi lolote, wala hamkatazi, dakika kama zile watoto hawasikilizagi hivi ni bure kujadili, anatambua kuwa ili mwana akomae anapaswa kujifunza kwa kupita njia ngumu, anampa na mtoto anaondoka kwa jeuri. Anapoishiwa kila kitu njaa inaingia, anajikuta kwenye hali ngumu akilisha na kula chakula cha nguruwe, mnyama aliyekatazwa kuliwa (Kumb 14:8). Katika mazingira yale magumu na hali ya kukata tamaa ndipo anapopata akili, mmoja anapokuwa mbali na baba hawi mwenyewe. Hakuipata furaha aliyotazamia sababu furaha ya kweli haimo katika starehe au raha za mwili, dawa za kulevya, vinywaji na mahusiano ya kijinsia. Katika muktadha wa Maadhimisho ya Jubilei ya Matumaini, tafakari hii inatufundisha kuwa Mungu daima anaturuhusu kurudi kwake, hata pale tunapoharibu na kupotea. Jubilei ya Matumaini inatufundisha kuwa, hata kama tumepotea katika dhambi, huruma ya Mungu inatufanya tuwe na matumaini. Mwana mpotevu ni mfano wa wote wanaotafuta na kupokea huruma ya Mungu kwa toba, na tunalewa na furaha ya kupata msamaha na ukarimu wa Baba yetu wa mbinguni.

Msamaha na maondoleo ya dhambi ni chemchemi ya furaha ya kweli.
Msamaha na maondoleo ya dhambi ni chemchemi ya furaha ya kweli.   (Vatican Media)

Furaha ya kweli ipo kwa Baba mwenye huruma (nyumbani mwa baba mna makao mengi…Yn 14:2) anaamua kurudi ili kuomba fadhili za baba lakini kama mtumishi na si kama mwana mpendwa. Wa pili ni baba, daima alitazama nje, labda kutoka dirishani, akitaraji kumuona mwanae, anasukumwa na upendo wa kibaba, ndio maana alimuona akingali mbali bado, akamkimbilia na kumbusu, hakumsikiliza porojo zake badala yake akamvalisha vazi zuri (heshima), pete (mamlaka), viatu (uhuru vs watumwa), na halafu sherehe kubwa. Mwishoni kabisa anafika muhusika wa 3, kaka mkubwa, hafurahii kurejea kwa mdogo wake, anabaki nje, naye ni mpotevu aliyepotelea ndani (shilingi) na baba analazimika kutoka nje mara ya 2, kama alivyotoka mara ya 1 kumkimbilia mwana mdogo, ili kumtafuta huyu naye. Mosi, mfano huu labda tusingeuita mwana mpotevu sababu mdogo yule sio shujaa hata abebe kichwa cha habari, wala kaka mtiifu sababu naye alikuwa mpotevu kama mdogo wake, jina zuri lingekuwa Baba mwenye huruma sababu anawatafuta, anawasamehe na kuwaingiza nyumbani wanawe wote wawili. Pili, ni mfano unaozungumzia huruma ya Mungu anayetusubiri turudi na anatuona tukiwa mbali bado na kutukimbilia, zaidi sana anatusamehe bila masharti. Binafsi sioni kama Mwana mpotevu alirudi nyumbani sababu alitubu, tafakari yake haioneshi toba… ‘ni watumishi wangapi wa baba yangu wanaokula chakula na kusaza, na mimi hapa ninakufa kwa njaa…’ Njaa ndio iliyomrudisha nyumbani… Angewaza hivi ‘Tazama nilipoishia sababu ya dhambi na ujinga wangu. Nimepotea mimi, nami nitakufa hapa kama mnyama, ngoja niende kwanza kwa baba nimwombe msamaha, nimkumbatie mara ya mwisho halafu niondoke zangu nikafe kwa amani, hata akinipa kitu sitapokea, hata kikombe cha maji tu, sababu sistahili...’ Hii ingekuwa ni toba ya kiukweli, "dogo" alirudi nyumbani sababu ya njaa na laiti asingepata matatizo asingerudi hata kwa "bull dozer."

Waamini wajenge utamaduni wa kukimbilia huruma na upendo wa Mungu
Waamini wajenge utamaduni wa kukimbilia huruma na upendo wa Mungu   (Vatican Media)

Hivi ni mfano unaoonesha huruma tu ya Mungu. Tatu, kaka mkubwa anasimama badala ya mafarisayo na anatuwakilisha sisi ambao tunatamani kuona mkosefu anaadhibiwa kuliko kuokolewa. Ni kaka anayeonesha kuwa miaka yote aliyobaki nyumbani ilikuwa ni kazi ya ajira, kuwekeza, na matarajio ya faida na sio huduma ya upendo kwa baba… ‘hujanipa hata mbuzi…’ ndio sababu anamuita mdogo wake ‘huyu mwana wako…’  na sio ‘huyu mdogo wangu’.Katika ujumbe wa Kwaresima 2025, tunahamasishwa kutubu na kumwongokea Mungu kwa moyo mnyenyekevu. Kama ilivyo kwa mwana mpotevu, sisi pia tunaitwa kutambua dhambi zetu, kutubu, na kurudi kwa Baba yetu wa mbinguni. Huu ni muda wa kutafakari na kufanya mabadiliko ya kiroho, ili tuweze kushiriki katika furaha ya wokovu. Kwaresima ni kipindi cha toba, lakini pia ni kipindi cha furaha, kwa sababu tunajua kwamba huruma ya Mungu haikuwa na mipaka kwa wale wanaotubu. Baba mara moja anamrekebisha akisema … ‘kwani huyu ndugu yako alikuwa amekufa…’ zaidi sana, haoni kama yule ni baba yake na hivi hajamwita  BABA hata mara 1 katika mfano huu wakati mdogo wake ametaja jina la BABA mara 5, kwake yeye ni kweli BABA yake sababu amempokea katika hali mbaya, hana la kujivunia mbele ya baba yake kumbe kaka mkubwa anaanza kwa kulaumu, kujisifu na anaishia kuorodhesha dhambi za mdogo wake… kula mali na makahaba…  na hata jina hili ‘makahaba’  linatajwa na yeye tu katika simulizi lote. Jiulize mdogo asingemkuta baba nyumbani badala yake akamkuta kaka yake, kingetokea nini? hata glasi ya maji tu asingepata, angeishia nje. Hii inatuhusu, mara nyingi tunaojihesabia haki na kuwa vikwazo kwa wanaorudi kundini. Tunawatazama wanaokuja kusali na kuwashangaa ‘hata wewe umekuja, mvua itanyesha’ tunasahau kwamba ‘wenye afya hawahitaji tabibu…’ (Mk 2:17.)

Huruma na upendo wa Mungu umetundikwa Msalabani.
Huruma na upendo wa Mungu umetundikwa Msalabani.   (ANSA)

Tumalizeje hadithi hii? Bila shaka kaka mkubwa aliingia ndani shingo upande na kukaa kimya akitazamana na mdogo wake. Bila shaka sherehe iliendelea na baba akaendelea kuzungumza nao akimuonesha kaka mkubwa umuhimu wa msamaha kwani wao ni ndugu, na tuseme basi kuwa mwishoni baba, kaka na mwana mpotevu walikumbatiana na kwa pamoja wakalia machozi ya furaha. Tuombe neema ya kuwasamehe na kuridhiana na wanaotukosea. Msamaha haupimwi (7x70), hauchagui, haubagui, unaleta furaha, amani na unaimarisha umoja. Mungu anatusamehe katika Kristo (Somo II 1Kor 5:17-21), basi baba msamehe mama, mama msamehe baba, wazazi mumsamehe mtoto wenu, mtoto msamehe mzazi wako, kijana msamehe rafiki yako, na sisi sote tusameheane ili tuile vema Pasaka ya Bwana na yetu (Somo I Yos 5:9a, 10-12). Dominika ya Nne ya Kwaresima (Laetare) inatufundisha kuhusu furaha ya wokovu kupitia huruma na upendo wa Mungu kwa wale waliopotoka na kurudi kwake kwa toba. Jubilei ya Matumaini ni mwaliko wa kufurahi kwa sababu huruma ya Mungu inatufanya tuwe na matumaini, hata tunapokosea. Katika kipindi cha Kwaresima, tunaitwa kujiunga na Mungu kwa toba, huku tukisherehekea furaha ya wokovu na matumaini ya maisha ya milele. Amina.

Liturujia Kwaresima D 4

 

28 Machi 2025, 11:21