Tanzania-Dodoma,Ask.Mkuu Kinyaiya:sikilizeni na ulizeni maswali kama Maria!
Na Patrick Tibanga - Radio Mbiu na Angella Rwezaula – Vatican.
Vijana wametakiwa kusoma kwa bidii ili kufikia malengo yao na kuuliza maswali kama Bikira Maria na kuacha tabia ya kuendekeza uvivu na kuwa wabunifu katika maisha ya kila siku pamoja na kuishauri Serikali ya Tanzania kutoa wanafunzi wenye uwezo mkubwa wa kufikiri. Rai hiyo ilitolewa na Askofu Mkuu Beatus Kinyaiya (O.F.M Cap,) wa Jimbo Kuu Katoliki la Dodoma nchini Tanzania, wakati wa adhimisho la Misa Takatifu ya Sherehe ya Kupashwa Habari kwa Bikira Maria, tukio lililoambatana na uzinduzi wa Bweni la wanafunzi katika Shule ya Wavulana ya Mtakatifu Maria, Jimbo Kuu Katoliki la Dodoma Tanzania tarehe 25 Machi 2025.
Katika homilia yake Askofu Mkuu Kinyaiya amesema kuwa wanafunzi wanaposoma wanatakiwa wasome kwa bidii na kuelewa, na kamwe wasisome kwa kukariri ili akili zao zipanuke na kuwa wabunifu baadae na kukumbuka watakayo elekezwa na kufundishwa darasani. “Ulizeni Maswali kwa walimu wenu kwa mambo ambayo hamuelewi kama Maria, sikilizeni kwa makini mnachofundishwa na mpambane kufikia malengo yenu. Naomba nitoe wito kwa wanafunzi mliopo hapa na wanafunzi wote Tanzania, ukitaka kufanikiwa kwenye maisha, maisha hayana shortcut na mnaposoma, someni kwa kuelewa msisome kwa kukariri ili muelewe mnachosoma maana akili yako itapanuka na utakuwa mbunifu baadae.” Alisisitiza Askofu Mkuu Kinyaiya katika homilia yake.
“Binti Maria anasikia maelezo ya Malaika aliyempelekea habari njema lakini haelewi anauliza Malaika swali itakuaje? Naye anapewa maelezo anakubali na anapata mimba na hapo historia ya wokovu inajifunua. Najiuliza swali huyu binti angekataa ingekuaje? Ni wazi Mungu angetafuta njia nyingine hasingeshindwa. Kila mmoja wetu anaalikwa kujenga ufalme wa Mungu hapa duniani na leo tunaalikwa upya kuitikia wito wake na kumuiga mama Maria”. Alisema Askofu Mkuu Beatus Kinyaiya.
Katika tafakari yake hata hivyo, kwa kutazama hata uwepo wa viongozi wa Serikali Askofu Mkuu Kinyaiya aliishauri Serikali kupitia kwa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Bi Rosemary Senyamule ambaye alihudhuria uzinduzi huo na kuiomba Serikali “kuzingatia sera mpya ya mtaala wa Elimu ya amali ili na mtaala huo mpya uweze kuwasaidia kuwa na fikra tunduizi, kwa kuwa wabunifu ili kulenga katika kufikiria, kuwa wabunifu katika maisha yao ya kila siku itakayowainua kimaisha.” Katika hilo alitumia mifano kadhaa ya maisha yake ambayo ilimjenga kimaisha katika kujifunza mambo mengi wakati yuko shuleni.
“Pamoja na mafundisho ya darasani katika sera hii mpya ya Amali ambayo tunaanza kuitekeleza hata nje ya darasa, tahadhari yangu ni kwamba huu mfumo wa amali naomba usije ukaongeza mafundi wengi mtaani kipindi watakapohitimu,hata hao mafundi waliosoma mafunzo hayo ya amali wakakosa kazi na kujikuta tunao mafundi wengi mtaani ambao hawana kazi tena,” alitoa onyo Mkuu wa Kanisa Kuu la Dodoma.
Askofu Mkuu Kinyaiya kwa njia hiyo aliwataka walimu watakaofundisha wanafunzi katika sera ya amali kuwaandaa wanafunzi kuwa wa bunifu pamoja na kutoa shahada kwa wahitimu wenye uwezo wa kubuni kitu kipya na kuwa na msukumo mzuri wa maisha na kuondokana na mfumo wa kunakili na kuchapisha (copy & paste). Askofu Kinyaiya aidha alitumia fursa hiyo kuwapongeza Masista wa Shirika la Maria kwamba” Kupashwa habari kwa Bikira Maria ni tunda la kumsikiliza Malaika aliyekuja kwao kupitia nafsi ya ya Balozi wa Vatican, Askofu Mkuu Novatus Rugambwa kuja nao Tanzania na kwa upendo mkubwa walikubali kuja kuinjilisha Tanzania. Askofu Mkuu Kinyaiya alisema “Mlipata changamoto nyingi mwanzoni na kuja kuleta habari njema hapa Tanzania na sasa tumshukuru Mungu kwa kuendelea kuinjiisha tunaomba muendelee kuwahamasisha na kuufanya utume huu kwa umoja.”
Tukio hilo liliudhuriwa na Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Tabora Tanzania, Kardinali Protase Rugambwa, pamoja na mapadre, wata wa mashirika mengine na wageni kutoka ndani na nje ya nchi, pamoja na viongozi wa vyama na serikali.