Tafuta

Hayati Baba Mtakatifu Francisko anasema, huruma ya Mungu ni chemchemi ya furaha ya kweli; msamaha unaowawezesha wafuasi wa Kristo kuwa ni vyombo na mashuhuda wa huruma ya Mungu Hayati Baba Mtakatifu Francisko anasema, huruma ya Mungu ni chemchemi ya furaha ya kweli; msamaha unaowawezesha wafuasi wa Kristo kuwa ni vyombo na mashuhuda wa huruma ya Mungu   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Huruma ya Mungu ni Chemchemi ya Furaha, Faraja na Msamaha!

Hayati Papa Francisko anasema, huruma ya Mungu ni chemchemi ya furaha ya kweli; msamaha unaowawezesha wafuasi wa Kristo kuwa ni vyombo na mashuhuda wa huruma ya Mungu na hatimaye, huruma ya Mungu ni faraja kubwa kwa wasioamini, wanaotaka kugusa Madonda Matakatifu, ili waweze kuamini kama ilivyokuwa kwa Mtume Toma! Lakini wawe tayari kugusa na kuganga madonda ya jirani zao kwa mafuta ya faraja na divai ya matumaini, tunda la Pasaka!

Na Padre Bonaventura Maro, C.PP.S., - Kolleg St. Josef, Salzburg, Austria.

Utangulizi: Wapendwa Taifa la Mungu, leo ni Jumapili ya 2 ya Pasaka mwaka B wa Kanisa. Kwa namna ya pekee leo ni, “Dominika ya Huruma Mungu” ambayo hujulikana pia kama Dominika nyeupe. Mwenyezi Mungu amedhihirisha kwetu Huruma yake kuu isiyo na mipaka kwanza kabisa kwa kumtuma kwetu Mwanaye wa pekee Bwana wetu Yesu Kristo, kwa fumbo la umwilisho, utume wake hapa duniani, na hatimaye kwa njia ya fumbo Takatifu la Pasaka, yaani mateso, kifo na ufufuko wake. Hata baada ya ufufuko na kupaa kwake Mbinguni, ameendelea bado kutuonesha huruma yake kuu kwa njia ya Roho Mtakatifu anayefanya kazi ndani yetu sisi tulio wafuasi wake. Hayati Baba Mtakatifu Francisko anasema, huruma ya Mungu ni chemchemi ya furaha ya kweli; msamaha unaowawezesha wafuasi wa Kristo kuwa ni vyombo na mashuhuda wa huruma ya Mungu na hatimaye, huruma ya Mungu ni faraja kubwa kwa wasioamini, wanaotaka kugusa Madonda Matakatifu, ili waweze kuamini kama ilivyokuwa kwa Mtume Toma! Lakini wawe tayari kugusa na kuganga madonda ya jirani zao kwa mafuta ya faraja na divai ya matumaini. Baba Mtakatifu anasema, kimsingi huruma ya Mungu ni chemchemi ya furaha inayobubujika kutoka kwa Kristo Yesu Mfufuka. Huruma hii kuu ya Mungu inatuletea: Upendo, amani, furaha, faraja, matumaini mapya, wema, haki, upatanisho, utakaso na msamaha ndani ya mioyo yetu. Ni mwaliko kwetu sote kwa Imani thabiti na matumaini hai, kuipokea huruma hii kubwa ya Mwenyezi Mungu iliyo wazi kwa watu wote, kwa njia ya Mama Kanisa Mtakatifu. Tunapopokea huruma ya Mungu tunaalikwa nasi kuwa na huruma kama Baba yetu wa mbinguni alivyo na huruma, kwa kupenda bila mipaka, kwa kuhurumia, kwa kusamehe, kwa kufariji, kwa kuguswa na shida na mahaingaiko ya wenzetu, na kwa kujitoa sadaka bila kujibakiza.

Huruma ya Mungu ni matunda ya Pasaka ya Bwana
Huruma ya Mungu ni matunda ya Pasaka ya Bwana   (ANSA)

Dominika ya Huruma ya Mungu: Dominika ya pili ya Pasaka iliwekwa rasmi kuwa Dominika ya Huruma ya Mungu na Baba Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili katika maadhimisho ya Jubilei Kuu mwaka 2000, siku tano tu baada ya kutangazwa kuwa Mtakatifu kwa Sister Maria Faustina Kowalska. Ikumbukwe kuwa, kuanzia mwaka 1930-1937, Bwana wetu Yesu Kristo alijidhihirisha kwa Sister Maria Faustina Kowalska aliyekuwa Sista wa Shirika la Mama wa Huruma huko Poland.  Alimtokea katika maono, akiwa na vazi refu, mkono wake wa kuume akiwa ameunyanyua kubariki, na mkono wake wa kushoto akiwa ameshikilia vazi lake juu kidogo ya moyo wake Mtakatifu. Miale myekundu na myeupe ilitoka moyoni mwa Yesu, ikiwa ni ishara ya Damu na maji vilivyomwagika msalabani kwa ajili ya utakaso wetu, maji ishara ya sakramenti ya Ubatizo na Damu ishara ya Ekaristi Takatifu. Yesu alimwomba Sr. Maria Faustina kwamba, “Yesu ninakutumainia” iandikwe chini ya picha yake na iheshimiwe katika dunia yote. Alitoa pia ahadi kwamba, yeyote atakayeheshimu picha hiyo inayowakilisha huruma kubwa ya Mungu iliyotoka katika Moyo Mtakatifu wa Yesu hatapotea kamwe. Ni Kristo kwa Huruma yake kuu anaguswa na hitaji la ukombozi wa roho zetu. Hivyo katika Dominika hii tunasukumwa nasi kwa furaha hii ya Pasaka kutambua na kuguswa na shida na mahitaji ya ndugu na jirani zetu ambao wanahitaji kuonjeshwa faraja na upendo ambao tumeupokea kutoka kwa Kristo. Pia kuwa mashuhuda wa huruma hii ya Mungu wetu kwa kuwa watu haki, msamaha, upatanisho na upendo wa kweli.

Papa Francisko alikuwa chombo na ushuhuda wa huruma ya Mungu
Papa Francisko alikuwa chombo na ushuhuda wa huruma ya Mungu

Somo la Injili: Ni Injili ya Yn 20:19-31: Somo la Injili Takatifu katika Dominika hii ya Pili ya Pasaka, limegawanyika katika sehemu kuu mbili. Sehemu ya kwanza (Yn 20:19-23) yatueleza tokeo la Yesu kwa wanafunzi wake ambao walikua wamejifungia ndani kwa hofu ya Wayahudi. Yesu anapowatokea hawa Mitume waliokuwa wamejawa hofu, mashaka, na mkato wa tamaa, Neno lake la kwanza kwao ni, “Amani iwe kwenu” na kisha anawaonesha mikono yake na miguu yake ya kwamba ni yeye. Wanafunzi wanafurahi wanapomwona Bwana. Kisha kuwaondolea hofu na mashaka, Yesu anawavuvia Roho Mtakatifu na kuwapa uwezo wa kuwaondolea watu dhambi zao. Kristo anamimina kwetu huruma yake kwa njia ya Sakramenti hii ya upatanisho ambayo kila mara inatupatanisha sisi na Mungu na kutupatanisha sisi na wenzetu, ikituondolea dhambi na kutufanya kuwa safi na watakatifu. Sakramenti ya upatanisho inatuondolea hofu na mashaka, inaturudishia amani na furaha ya kweli mioyoni mwetu na na inatibu tena mahusiano mema kati yetu sisi kwa sisi na kati yetu sisi na Mungu wetu. Sehemu ya pili ya Injili hii (Yn 20:24-29), twapata habari ya Mtume Thomaso ambaye hakuwepo pamoja na wenzake wakati Bwana wetu Yesu Kristo alipowatokea Mitume wake 10. Na hivyo hakuamini ya kuwa Bwana amefufuka na amewatokea Mitume wake hata alipoambiwa na Mitume wenzake. Baada ya siku nne Yesu anawatokea tena Mitume wake kama alivyofanya mwanzo na sasa Tomaso akiwemo pamoja nao. Kristo mfufuka anamwimarisha Tomaso Imani yake, kutoka kutokuamini, hadi kukiri Imani kwa Kristo mfufuka. Kristo mfufuka anajidhihirisha kwetu katika Neno lake, na tunampokea katika sakramenti ya Ekaristi Takatifu, tuombe neema ya kumtambua anapojidhihirisha kwetu. Tufurahi tunapokutana na Bwana.

éaèa Francisko alikuwa ni chombo na shuhuda wa huruma na upendo wa Mungu
éaèa Francisko alikuwa ni chombo na shuhuda wa huruma na upendo wa Mungu   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Katika somo hili la Injili Dominika ya leo tuna mafundisho matano ya kujifunza. Kwanza: Kristo Mfufuka anatuondolea hofu na mashaka yetu, Anatupa Amani. Mitume wa Yesu mara baada ya Yesu kukamatwa, kuteswa na kufa msalabani, wengi walikimbia na walijawa na hofu na mashaka wakajifungia ndani kwa hofu ya Wayahudi. Kristo mfufuka alipowatokea aliwaambia, “Amani iwe kwenu” Alitambua ya kuwa walikua na hofu na mashaka, na hivyo anawapa habari njema ya furaha kwamba, amefufuka kwa hivyo hawakupaswa kuwa na hofu tena. Nao wanafurahi walipomwona Bwana. Ndugu mpendwa sana, katika maisha yetu kuna nyakati tunakua na hofu na mashaka, juu ya maisha, juu ya familia zetu, juu ya biashara na kazi zetu za kila siku, mashaka juu ya Imani yetu hasa tunapopitia katika mtikisiko kiimani. Katika hali zote hizi Kristo mfufuka anakuja kwetu na neno lake la kwanza kama ilivyokuwa kwa Mitume wake, anatuambia, “Amani iwe kwako” Kristo kwa huruma yake kuu anakuja kwetu katika Neno lake kila siku, Neno linalotupa faraja na kitulizo katika nyakati mbalimbali tunazopitia, neno linaloinua tena matumaini yetu, neno linaloimarisha tena Imani yetu, Neno linalotutia nguvu rohoni ya kuendelea tena mbele. Tufurahi tunapokutana na Bwana, tufurahi anaposema nasi. Pili: Kristo mfufuka anawatuma mitume wake kuwa mabalozi wa Huruma ya Mungu. Kristo alipowatokea Mitume na kisha kuwaondolea hofu na mashaka, anawaambia, “Kama vile Baba alivyonituma mimi, mimi nami nawapelekea ninyi” Mitume baada ya kumpokea Roho Mtakatifu walitumwa kwenda kutangaza huruma ya Mungu. Walitumwa kwenda kuyaishi na kuyafundisha yote ambayo Yesu aliwaamuru, na kuwabatiza watu kwa jina la Baba na la mwana na la Roho Mtakatifu, kuponya magonjwa na udhaifu kati ya watu. Sisi sote tuliobatizwa tumepokea tunda la huruma kubwa ya Mungu na hapo kila mmoja wetu anatumwa kuwa mmisionari wa huruma yake. Tunakuwa mabalozi wa huruma ya Mungu kwanza kabisa kwa kuiishi na kuishuhudia Imani yetu kwa maneno na kwa matendo yetu. Kristo aliwaonesha Mitume wake mfano, namna kwa uaminifu mkubwa alivyotekeleza kazi aliyotumwa na Baba, ya kutuletea sisi ukombozi wa milele, kazi ambao ilimpasa kuteseka na kufa, kisha akafufuka katika utukufu.

Huruma ya Mungu ni chemchemi ya imani, matumaini na faraja
Huruma ya Mungu ni chemchemi ya imani, matumaini na faraja   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Kila aliyebatizwa basi anatumwa kuwa shuhuda wa Kristo. Katika miito mbalimbali ambayo tumeitwa, Kristo anatushirikisha kazi yake ya kuwa mabalozi wa huruma yake. Kila mmoja apaswa kuwa shuhuda wa Imani yake katika hali hali zote, kuifundisha, kuiishi na kuishuhudia, katika familia zetu, katika kanisa, katika jumuiya zetu za kitawa, katika shughuli zetu za kila siku, Kristo ajulikane na kupendwa. Tupeane moyo pale yajapo mateso na misukosuko katika maisha, tuinuane pale tunapoangushwa na kupata mitikisiko kiimani, tushikane mikono na kutembea pamoja ili sote tufike mbinguni. Hakuna utukufu bila msalaba na mateso. Tatu: Kristo anaweka rasmi Sakramenti ya Kitubio, kielelezo cha huruma yake kwa wakosefu. Kristo anawavuvia mitume wake, akiwaambia, “Pokeeni Roho Mtakatifu, wowote mtakaowaondolea dhambi wameondolewa na wowote mtakaowafungia dhambi wamefungiwa” Kitendo cha kuvuvia ni ishara ya uumbaji, tukirejea katika kitabu cha Mwanzo 2:7, Mwenyezi Mungu alipomwumba mtu kwa mavumbi ya ardhi, akampulizia puani pumzi ya uhai, na mtu akawa nafsi hai. Kumbe Yesu anawavuvia Mitume wake, anawapa nguvu ya kusamehe watu dhambi kwa njia ya Kanisa, ambao tunakuwa wapya kila tunaposamehewa dhambi zetu. Ile furaha ninayopata moyoni kwa kuambiwa, “Mwenyezi Mungu amekusamehe dhambi zako, nenda na amani” Ni furaha ya namna gani! Nakua mpya kabisa rohoni. Ndugu wapendwa, ni Bwana wetu Yesu Kristo kwa huruma yake kubwa aliweka sakramenti hii ya muhimu kabisa katika kanisa, sakramenti ya upatanisho ili kutuondolea dhambi, kutusafisha na kutufanya wapya tena machoni Mungu. Sakramenti ya Kitubio inatuondolea dhambi zetu, inatupatanisha sisi na Mungu inatupatanisha sisi na wenzetu na kisha tunapata amani na furaha ya kweli ndani ya mioyo yetu. Ni Yesu mwenyewe aliwapa Mitume wake uwezo huu wa kuwaondolea watu dhambi zao. Nasi mapadre, kwa njia ya sakramenti ya Daraja Takatifu, tunapokea uwezo huu, kwa mamlaka ya Kanisa na kwa niaba ya Kristo wa kuwaondolea watu dhambi zao. Tunaalikwa kuikimbilia huruma ya Mungu ambaye hafurahii tufe katika dhambi bali anatupa nafasi ya kujipatanisha naye na kujipatanisha sisi na wenzetu. Usione aibu, kwenda kuungama mara nyingi iwezekanavyo, hakuna kikomo cha huruma ya Mungu. Kila mara tunapoanguka dhambini tukumbuke kuwa Yesu anatuita kwake katika sakramenti hii ya huruma yake.

Huruma ya Mungu inabubujika kutoka katika Fumbo la Pasaka
Huruma ya Mungu inabubujika kutoka katika Fumbo la Pasaka

Nne: Kwa njia ya maisha yetu, watu wapaswa kuona na kumwamini Kristo mfufuka. Mtume Tomaso hakuwepo pamoja na Mitume wengine wakati Bwana wetu Yesu Kristo alipowatokea Mitume. Hakusaidiki maneno ya Mitume wengine kwamba ni kweli Kristo amefufuka. Anasema, “Mimi nisipoziona mikononi mwake kovu za misumari na kutia kidole chake katika ubavu wake, mimi sisadiki hata kidogo” Baada ya siku nne Yesu anawatokea tena, kisha Tomaso anamkiri Yesu, Bwana na Mungu. Anatoka katika hali ya kutokuamini na kisha anaamini ya kwamba kweli Kristo amefufuka. Ndugu wapendwa, katika maisha yetu, katika familia zetu, katika jumuiya zetu, tunao bado watu wengi wenye mashaka katika Imani yao. Pengine wanashindwa kufanya maamuzi sahihi katika maisha yao ya kiimani. Kila mbatizwa anapaswa kuwa kioo cha kumwonesha na kumtambulisha Kristo kwa watu wengine. Namna yetu ya maisha yapaswa kumdhihirisha Kristo, maneno yetu, matendo yetu, mahusiano yetu kwa wengine, Imani yetu, matumaini yetu, mapendo yetu kwa Mungu na kwa wengine, haya yote yanawasaidia wengine kumwona Kristo mfufuka ndani mwetu na matokeo yake wanaimarika katika imani. Kuna mmoja huenda amepata nguvu na matumaini mapya pale alipotuona tunavumilia na kustahimili katika changamoto mbalimbali tunazopitia. Mara zote ambapo haturudi nyuma kiimani, hatukukata tamaa, hatukupoteza matumani. Hivyo tunawapa wengine sababu ya kuendelea kuamini. Huenda katika miito yetu, tumekuwa waaminifu, changamoto zetu tumeishi nazo na kumpa Yesu nafasi atuongoze na awe mwanga na taa yetu, tumewainua wengi ambapo walikwishakata tamaa na kuona maisha hayana thamani tena.

Kristo Yesu anakutana na waja wake katika Neno na Ekaristi
Kristo Yesu anakutana na waja wake katika Neno na Ekaristi   (Vatican Media)

Tano: Katika Ekaristi Takatifu, Yesu anatualika tumguse, anatuongezea Imani. Yesua alipowatokea mitume wake mara ya pili, anawambia Tomaso, “Lete hapa kidole chako, uitazame mikono yangu; ulete hapa na mkono wako uutie ubavuni mwangu, wala usiwe asiyeamini, bali aaminiye” Ni baada ya tukio hilo Tomaso anaamini na anakiri, “Bwana wangu na Mungu wangu” Kristo amemwongezea na kumwimarisha imani yake. Ndugu wapendwa, tunakutana na Kristo mfufuka kila siku katika Neno lake na katika Ekaristi Takatifu. Fumbo la Pasaka ambalo tunaliadhimisha kila tunapoadhimisha Ibada ya Misa Takatifu latukumbusha kila wakati thamani ya ukombozi wetu kwamba, hatukukombolewa kwa fedha wala dhahabu bali na kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wa Kristo. Kristo anatualika tumguse, amejiota kwetu kwa huruma kubwa, kama chakula kwa ajili ya uzima wetu. Kila mara ananialika kumgusa, ninapompokea. Tomaso alikiri, Bwana wangu na Mungu wangu. Sisi pia tunapompokea Yesu anatupa nguvu ya kumkiri kama Bwana na Mungu wetu. Katika mateso na changamoto zetu, tuwe na ujasiri wa kusema, “Bwana wangu na Mungu wangu” Katika furaha, “Bwana wangu na Mungu wangu” katika huzuni, katika kukataliwa kwako, katika kudhulumiwa, katika kuanguka na kuinuka kwako, katika kustahimili uzito wa msalaba wako, Yesu mfufuka anakupa nguvu ya kukiri kila mara, “Bwana wangu na Mungu wangu.” 

Dominika ya Huruma ni chemchemi ya msamaha wa kweli
Dominika ya Huruma ni chemchemi ya msamaha wa kweli   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Somo la 1: Ni kitabu cha Matendo ya Mitume Mdo 5:12-16: Mwinjili Luka, Mwandishi wa Kitabu cha Matendo ya mitume anatupa picha ya maisha na kazi za Mitume baada ya Yesu kufufuka na kupaa kwake mbinguni. Wakiisha kupokea Roho mtakatifu, Bwana wetu Yesu Kristo anaendelea kudhihirisha huruma yake kwa njia ya kazi mbalimbali walizozitenda hawa Mitume wake. Kwa nguvu hiyo ya Roho Mtakatifu, Kanisa liliendelea kustawi na mitume waliweza kutenda kazi na maajabu mbalimbali.  Ni picha halisi ya uzuri wa kanisa la kwanza, jumuiya ya kwanza ya Wakristo jinsi walivyoishi kwa pamoja, kwa upendo, furaha, ushirika na umoja, vyote hivi walivipata kutoka kwa Kristo Mfufuka. Hivyo, tunaambiwa wakawa na moyo mmoja na roho moja. Kwa upendo waliweka mali zao pamoja, na wakagawana kadiri kila mmoja alivyokuwa anahitaji, wala hapana aliyesema chochote alicho nacho ni mali yake. Hawakuwa na uchoyo, hawakuwa wabinafsi, hawakuwa fisadi wala wabadhirifu wa mali za jumuiya. Kupendana kati yao kulikua ndio msingi wa kuhubiri kwao furaha ya Kristo Mfufuka. Ndugu zangu katika somo hili la kwanza tuna mambo matatu ya kujifunza. Kwanza: Mitume wanaendeleza kazi na utume wa Bwana wetu Yesu Kristo, kazi ya huruma na uponyaji (continuity with Jesus’ Ministry). Mara baada ya Pentekoste, Mitume walikusanyika kwa nia moja katika ukumbi wa Sulemani na humo mwinjili Luka anatuambia kuwa walikuwako kwa nia moja na zilifanyika ishara na maajabu Mengi. Walihubiri Neno la Mungu, waliadhimisha Ekaristi Takatifu na waliponya magonjwa na wale wote walioudhiwa na pepo wachafu. Kristo kwa njia ya Roho Mtakatifu anaendelea kutenda kazi kati ya Mitume wake katika kanisa. Anaendelea kudhihirisha huruma yake katika utendaji kazi wa Mitume wake. Ndugu wapendwa, Bwana wetu Yesu Kristo, kwa njia ya Huruma yake kubwa, ametupatia zawadi ya Roho Mtakatifu ambaye anatenda kazi ndani yetu kwa namna mbalimbali. Kwa njia ya mapaji yake, sisi sote tumepata karama mbalimbali ambazo kwa umoja wetu zinapaswa kumdhihirisha Kristo anayeendelea kila siku kufanya kazi kupitia sisi. Pasaka inatukumbusha wajibu wetu wa kutumia vyema karama za Roho Mtakatifu katika kuleta uponyaji katika familia zetu, uponyaji katika jumuiya zetu.

Huruma ya Mungu ni chemchemi ya furaha, imani, matumaini na mapendo
Huruma ya Mungu ni chemchemi ya furaha, imani, matumaini na mapendo

Roho Mtakatifu analeta Upatanisho katika familia na jumuiya zilizo na mafarakano. Analeta upatanisho katika nchi na mataifa yaliyo na migogoro ya kisiasa, chuki na uhasama. Roho Mtakatifu anatusaidia katika kutegemezana sisi kwa sisi katika changamoto mbalimbali ambazo tunapitia katika maisha yetu ya kila siku. Huo ndio uponyaji wenyewe. Wapo wenzetu wengi ambao wamekata tamaa kabisa kwa sababu mbalimbali, wapo watu walio katika depression, msongo wa Mawazo, wanahitaji maneno ya faraja, wapo watu waliovunjika moyo, waliokata tamaa, waliojeruhiwa katika familia nk. Hawa wote wanahitaji uponyaji, na ni Roho Mtakatifu anayetutumia sisi kama alivyowatumia Mitume kuwa chanel ya huruma ya Mungu kwa wengine. Je, ninatumia karama ya Roho mtakatifu kuleta uponyaji au ninaleta maanguko, vilio na huzuni kwa wengine? Pili: Mitume wanatoa ushuhuda wa maisha, wanagusa watu mioyo (community and public witness). Mitume walikutanika kila mara kusali, walishirikiana kwa kila jambo, hawakua na uchoyo na ubinafsi kati yao, kila mmoja alimwona mwenzake ni bora kuliko nafsi yake, walishirikiana katika kila jambo. Jambo hili liliwagusa watu mioyo, waamini walizidi kuongezeka kwa Bwana, wengi waume kwa wake. Ndugu wapendwa, maisha ya mitume yalikua maisha ya ushuhuda. Waliishi upendo, waliishi umoja, waliishi maisha ya sala, waliadhimisha Ekaristi Takatifu, waliponya wagonjwa kwa kuwawekea mikono, walihubiri Neno la Mungu na baadaye wengi watakufa kifo dini kwa sababu ya Kristo. Maisha haya yaligusa mioyo ya watu, watu wakawastaajabia. Kila mmoja wetu ajiulize katika familia yangu, katika ndoa, katika utume wangu mimi kama padre, katika kazi zetu za kila siku, ninaishi maisha ya ushuhuda? Je, ninashirikiana na wengine kwa karama na vipaji ambayo Mungu amenijalia, kuleta furaha na matumaini kwa wengine? Ni mara ngapi maneno na matendo yangu yameleta uponyaji kwa wengine? Huenda kwa kunena au kwa katenda kwangu nimewakatisha tamaa wengine, nimewavunja moyo na kuwarudisha nyuma. Kristo mfufuka ametumiminia wingi wa huruma na neema zake, vitusaidie katika kuishi kweli maisha ya ushuhuda. Maisha yangu yaguse mioyo ya wengine, yaache alama njema na nzuri katika maisha ya watu wengine, nilete uponyaji, kwa kusamehe wale walionikosea na kuwa tayari pia kuomba msamaha pale ninapowakwaza na kuwaumiza wengine. Kwa kufanya hivi, familia zetu zitakua za mfano, ndoa zetu zitakua za mfano, jumuiya zetu za kitawa zitakua za mfano, jumuiya zetu ndogondogo zitakua za mfano. Watu watastaajabia maisha yetu na kutamani kumjua, kumpenda na kumfuata Kristo Mfufuka.

Bikira Maria Mama wa Huruma ya Mungu
Bikira Maria Mama wa Huruma ya Mungu   (AFP or licensors)

Tatu: Maisha baada ya ufufuko wa Yesu ni Maisha mapya. Mitume kabla ya ufufuko wa Yesu walikua na hofu na mashaka mengi. Walijifungia ndani wakiwa na hofu na mashaka ya Wayahudi. Hawakua na matumaini tena baada ya Bwana na Mwalimu wao kuteswa na kufa Msalabani. Baada ya ufufuko, Yesu anawatokea, na neno lake la kwanza kwao ni, “Amani iwe kwenu” Baada ya Pentekoste wanapata nguvu mpya ya kumtangaza Kristo. Maisha yao yanakuwa tofauti kabisa. Hawana hofu tena, hawana mashaka tena, wamepata nguvu mpya ya kumtangaza Kristo mfufuka hata katikati ya mateso na madhulumu. Ndugu wapendwa, maisha baada ya pasaka ni maisha mapya kabisa. Kuna nyakati Fulani katika maisha tunaingiwa na hofu na mashaka. Huenda mipango yetu haikwenda vile tulitamani na tulitegema iende, huenda watoto watu hawakufanikiwa katika Masomo au katika ajira, huenda magonjwa ya muda mrefu yameniweka katika hofu, huenda ni misiba, hasara, kila mtu anafahamu nyakati zake za hofu na mashaka. Tuzikabidhi nyakati na hali zetu zote kwa Kristo mfufuka. Yeye atatuinua tena pale ambapo tumekuwa dhaifu na kukata tamaa kabisa. Kama alivyowasha moto ndani ya Mitume wake hawa na wakawa watu wapya kabisa, ninawaombea ndugu wapendwa, Kristo ambaye leo tunaadhimisha na kukiri huruma yake kuu katika maisha yetu, akawatie nguvu pale mnapokata tamaa kwa sababu mbalimbali. Akawainue tena pale mnapoona hakuna tumaini. Kristo atafanya yote kuwa mapya tena.

Kristo Yesu ni ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu
Kristo Yesu ni ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Somo la Pili: Ni kitabu cha Ufunuo wa Yohane 1:9-11a, 12-13, 17-19. Mwandishi wa Kitabu hiki, Mtume Yohane, aliwaandikia Wakristo waliokuwa wakiteseka katika kisiwa cha Patmos katika Asia ndogo, ili kuwapa moyo na kuwaimarisha Imani yao katika nyakati ngumu utumwa na mateso kutoka kwa watawala wa Kirumi. Anatueleza kuwa, ni Kristo aliyemwamuru kuandika kitabu hiki, ili kuwahakikishia wakristo hawa waliokuwa katika mateso uwepo wa Kristo Mfufuka kati yao hata katika nyakati ngumu waliozokuwa wanapitia. Tunachojifunza katika kitabu hiki ambacho kinaelezwa kwa lugha ya picha, ni ile Faraja tunayoipata kutoka kwa Kristo, na wakati huo huo, Faraja tunayoitoa kwa wenzetu wanaoteseka na kupitia katika hali ngumu. Neno hili la Kristo kupitia mwinjili Yohane limewapa moyo wakristo waliokuwa katika mateso na madhulumu. Je, ninapopokea Neno la Faraja kila siku na kwa namna ya pekee zaidi ziku ya Bwana kama alivyopokea Yohane, ninaguswa ili nami nikawape Faraja wengine ambao wapo katika nyakati ngumu?  Huruma ya Mungu inatusukuma kuona mateso na mahangaiko wanayopita ndugu, jamaa na marafiki zetu. Tumwombe Yesu ambaye ndani ya moyo wake ndimo ilimotoka chemchemi ya huruma yake kuu, afanye mioyo yetu iwe sawa na moyo wake Mtakatifu. Ndani mwetu itoke huruma, Faraja, wema, msamaha, upatanisho na kwa njia hiyo tutawagusa pia na wengine. Mtakatifu Sr. Faustina, utuombee. Hitimisho: Dominika ya leo ni mwaliko kwetu sote kwa Imani thabiti na matumaini hai, kuipokea huruma hii kubwa ya Mwenyezi Mungu iliyo wazi kwa watu wote, kwa njia ya Mama Kanisa Mtakatifu. Tunapopokea huruma ya Mungu tunaalikwa nasi kuwa na huruma kama Baba yetu wa mbinguni alivyo na huruma, kwa kupenda bila mipaka, kwa kuhurumia, kwa kusamehe, kwa kuguswa na shida na mahaingaiko ya wenzetu, na kwa kujitoa sadaka bila kujibakiza.

Huruma ya Mungu
26 Aprili 2025, 16:24