Tafuta

2025.04.07 Watawa wawili wa Shirika la Dada Wadogo wa Mtakatifu Teresa wa Mtoto Yesu waliuawa huko Haiti tarehe 1 Aprili 2025. 2025.04.07 Watawa wawili wa Shirika la Dada Wadogo wa Mtakatifu Teresa wa Mtoto Yesu waliuawa huko Haiti tarehe 1 Aprili 2025. 

Haiti:Watawa 2 wa Shirika la Dada wadogo wa Mtakatifu Teresa wauwa huko Mirebalais

Watawa wawili waliuawa na magenge yenye silaha huko Mirebalais,Port-au-Prince nchini Haiti,tarehe Mosi Aprili 2024.Kulingana na vyombo vya habari vya ndani,watawa hao wawili walifanya kazi katika shule huko Mirebalais na walikuwa wamejificha katika nyumba na msichana mmoja wakati wa mashambulizi.Hata hivyo,magenge yenye silaha yaliingia ndani ya nyumba hiyo na kuwaua watawa hao na watu wengine wote waliokuwapo.

Na Angella Rwezaula – Vatican.

Katika ujumbe wa Papa Francisko baada ya sala ya Malaika wa Bwana  Dominika ya V ya Kwaresima, tarehe 6 Aprili 2025, kati ya mambo mengine mengi  alitoa wito wake: “Silaha zinyamaze na mazungumzo yaanze tena; mateka wote lazima waachiliwe na watu lazima wasaidiwe. Tuombe amani katika eneo lote la Mashariki ya Kati; katika Sudan na Sudan Kusini; katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo; huko Myanmar, pia ilikumbwa sana na tetemeko la ardhi; na huko Haiti, ambako vurugu zinaendelea, ambazo ziliua watawa wawili siku chache zilizopita. Bikira Maria atulinde na kutuombea.”

Watawa wa Shirika la Dada Wadogo wa Mtakatifu Teresa wa Mtoto Yesu

Katika muktadha wa kuuawa watawa,  hawa ni watawa wawili wa Shirika la Dada wadogo wa Mtakatifu Teresa wa Mtoto Yesu ambao waliuawa huko Mirebalais, katikati ya Haiti  na wanachama wa magenge yenye silaha ambao walivamia eneo hilo tangu Jumatatu Mosi, Aprili 2025. Askofu Mkuu wa Port-au-Prince, Max Leroy Mésidor, alithibitisha hili kwa vyombo vya habari vya ndani, na kuongeza: "Ni hasara kubwa kwa jumuiya."  Sr Evanette Onezaire na Sr Jeanne Voltaire waliuawa siku ya Jumatatu tarehe ! Aprili 2025 huku jiji la Mirebalais likikabiliwa na mashambulizi ya silaha na muungano wa wahalifu Viv Ansanm. Ghasia hizo pia zilichukua sura ya mashambulizi dhidi ya wafanyabiashara, vituo vya polisi na hata gereza, ambapo zaidi ya wafungwa 500 waliripotiwa kutoroka. Kulingana na vyombo vya habari vya eneo hilo, watawa hao wawili walifanya kazi katika shule hiyo huko Mirebalais na walikuwa wamejificha katika nyumba na msichana mmoja wakati wa mashambulizi. Hata hivyo, magenge yenye silaha yaliingia ndani ya nyumba hiyo na kuwaua watawa wawili na watu wengine wote waliokuwapo.

Hali ngumu ya magenge ya silaha Haiti

Hadi leo, hali ya Mirebalais inaonekana ya kusikitisha. Mjumbe wa idara ya serikali katika eneo hilo, Frédérique Occéan, alisema maiti zinazooza zilikuwa zikitanda katika mitaa ya jiji hilo, na kueneza harufu ya kichefuchefu. Mamlaka za manispaa hazikuwapo na wakazi wengi walikimbia. Vyombo vya habari vya Haiti pia viliripoti kwamba magenge yenye silaha pia yalilenga Hospitali ya Chuo Kikuu cha Mirebalais katika wakati huo. Hapo tarehe 2 Aprili 2025, maelfu ya watu waliingia katika mitaa ya mji mkuu kuandamana dhidi ya hali inayozidi kuwa mbaya na ongezeko la mashambulizi ya magenge. Maandamano hayo pia yalijumuisha watu waliokimbia makazi yao wanaoishi katika kambi zilizo karibu na Port-au-Prince baada ya kulazimishwa kuacha nyumba zao, pamoja na wakaazi wa vitongoji vya Canapé-Vert (ambapo idadi ya watu wanapinga vitisho kutokana na vikundi vyenye silaha vinavyojaribu kuvamia eneo hilo), Turgeau, Carrefour-Feuilles, Pacot, Debussy, Delmas na maeneo ya karibu.

Ripoti ya Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Binadamu

Polisi wa Kitaifa wa Haiti walitumia gesi ya kutoa machozi kutawanya umati wa watu ulipofika Ville d'Accueil, nyumbani kwa Baraza la Rais wa Mpito (CPT) na serikali. Mwaka 2024,  pekee, kulingana na data iliyotolewa na Umoja wa Mataifa, ghasia nchini Haiti zilisababisha angalau vifo 5,600 (elfu zaidi ya mwaka 2023), zaidi ya majeruhi 2,000 na takriban utekaji nyara 1,500. Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Kibinadamu, Volker Türk, aliripoti baada ya kuzuka kwa ghasia huko Mirebalais kwamba watu wasiopungua 4,239 waliuawa na 1,356 walijeruhiwa nchini Haiti kati ya Julai na Februari kwa silaha zilizoingizwa kutoka nje ya nchi, licha ya vikwazo vilivyowekwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

07 Aprili 2025, 10:49