Maadhimisho ya Alhamisi Kuu: Ekaristi Takatifu, Daraja Na Huduma
Na Padre Bonaventura Maro, C.PP.S., Kolleg St. Josef, Salzburg, Austria.
Utangulizi: Wapendwa Taifa la Mungu, leo ni Alhamisi Kuu ambapo Kanisa linaanza rasmi Siku tatu kuu za Pasaka yaani, Alhamisi Kuu, Ijumaa Kuu na Kesha la Pasaka. Sherehe ya Pasaka huanza kwa Adhimisho la Karamu ya Mwisho, ambapo Yesu pamoja na wanafunzi wake alifanya Karamu, ilikua ni adhimisho la Pasaka ya Wayahudi na ndani yake mambo makubwa matatu yalitokea. Kwanza, Yesu aliweka rasmi Sakramenti ya Ekaristi Takatifu (1 Kor 11:23-26). Kwa mapendo makubwa anajitoa mwenyewe kama Mwanakondoo asiye na doa, kama sadaka kwa ajili ya uzima wa ulimwengu. Anatoa mwili wake kama chakula, anatoa damu yake kama kinywaji kwa ajili ya ukombozi wetu sio kutoka tena utumwani Misri, bali kutoka katika utumwa wa dhambi. Alichokiadhimisha siku ya Alhamisi Kuu kinatimia pale msalabani siku ya Ijumaa Kuu. Pili, anaweka Sakramenti ya Daraja Takatifu. Anawapa Mitume uwezo wa kuadhimisha karamu ile ambapo yeye mwenyewe alijitoa sadaka kila mara wakutanapo, wakitangaza fumbo la Pasaka, yaani mateso, kifo na ufufuko wa Yesu mpaka atakapokuja tena. Ndio uwezo waliopewa mapadre wa kuadhimisha ibada ya Misa Takatifu kwa ukumbusho wa karamu ya mwisho, karamu ya shukrani kwa zawadi ya ukombozi, karamu ya umoja na kifungo cha mapendo. Tatu, Yesu anaweka Amri kuu ya Mapendo (Yn 13:34). Katika siku hii Yesu ingawa yeye ni Bwana na Mwalimu alijifanya kuwa Mtumishi wa wote, akawaosha Mitume wake miguu. Kwa tendo hilo aliwapa mitume na ametupa sisi sote kilelezo cha mapendo yasiyo na mipaka katika kuwatumikia wenzetu. Kujishusha, kutwaa hali ya mtumwa na mtumishi kwa ajili ya huduma ya upendo usio na mipaka kwa wengine. Katika siku hii ya Alhamisi kuu, tumshukuru Kristo aliyetupenda kwa mapendo makuu, akajitoa sadaka kwa ajili ya ukombozi wa ulimwengu mzima na tuombe neema nasi ya kujitoa sadaka kwa ajili ya wengine. Tumshukuru Kristo kwa zawadi ya Ekaristi Tatakatifu katika Kanisa, uwepo wake halisi katika maumbo ya mkate na divai. Tuwaombee Mapadre wote ili waendelee kuwa kielelezo cha uwepo wa Kristo katika kanisa lake kwa njia ya maadhimisho ya Neno lake na Sakramenti mbalimbali katika Kanisa.
Somo la Kwanza: Ni kutoka katika Kitabu Kut 12:1-8, 11-14: Somo la kwanza kutoka kitabu cha Kutoka, latueleza juu ya Pasaka ya Wayahudi. Sikukuu ya Pasaka ya Wayahudi ilikua ni ukumbusho wa kukombolewa kwao kutoka utumwani Misri. Somo hili la kwanza ni maelekezo ya Mungu kwa Musa na Haruni namna Wayahudi walipaswa kujiandaa kwa adhimisho la Pasaka yao ya kwanza, katika usiku ule ambapo Mwenyezi Mungu aliwakumbuka, akawatoa katika utumwa na kuanzisha safari yao mpya kuelekea katika nchi ya Ahadi. Katika karamu hii walimchinja Mwanakondoo asiye na doa na wakapaka damu yake katika miimo ya mlango na kwa damu hiyo hawakuangamizwa. Pasaka hii ya Wayahudi ni mfano (Typology) wa Pasaka Mpya ambapo Kristo Yesu anajitoa kama Mwanakondoo asiye na doa na kwa sadaka hiyo anatutoa sisi sio tena katika utumwa wa Misri bali kutoka katika utumwa wa dhambi na mauti na anaanzisha safari mpya ya kuelekea katika nchi yetu ya Ahadi yaani Mbinguni. Kwa Damu hiyo ya thamani na majeraha yake sisi sote tumepona kutoka katika hasira ya Mungu kwa sababu ya anguko la dhambi ya wazazi wetu wa kwanza, Adamu na Eva. Ndugu zangu katika somo hili la kwanza tuna mambo sita ya la kujifunza. Kwanza: Mungu anaguswa na shida na mahangaiko ya watu wake, anaanzisha mpango wa ukombozi (Salvation as a Divine Iniative). Taifa la Israeli walikua utumwani Misri kwa muda mrefu, takribani miaka 430. Katika kipindi chote hicho waliteseka sana, walikua mbali na nchi ya Ahadi, mbali na ardhi nzuri ambayo Mwenyezi Mungu aliwapa Baba zao. Walimlilia Mungu na Mungu akasikia kilio chao. Mwenyezi Mungu anawakumbuka na anaahidi kuwakomboa aliposema na Musa katika mlima Sinai“ “Nimeyaona mateso ya watu wangu huko Misri nami nimesikia kilio chao, maana nimeyajua maumivu yao nami nimeshuka ili niwaokoe…” Mungu anaguswa na mateso na maumivu ya taifa lake teule, anaguswa na kilio chao. Mwenyezi Mungu hafumbii macho shida na mahangaiko yetu, anatukumbuka. Ndugu wapendwa, kila siku tunakutana na Mungu, anashuka kati na kukaa kati yetu. Tunakutana naye katika Neno lake na katika sakramenti, anashuka na kukaa nasi. Anatuambia kwa sauti yake ya upole, “Nimeona mateso na mahangaiko yako mwanangu mpendwa, nimesikia kilio chako, nimeyajua maumivu yako, nami nimeshuka ili nikuokoe” Ni maneno ya faraja, ni maneno yanayoamsha matumaini na kutupa nguvu mpya ya kusimama tena tukiwa na Imani na matumaini thabiti, kwamba Mungu atafanya kitu katika hali zetu mbalimbali ambazo kila mmoja wetu anapitia kwa wakati wake.
Ninakuombea ndugu mpendwa, Mungu mwenye huruma na neema akafanye kitu kwa ajili ya maombi yako mbalimbali, kwa ajili yako, kwa ajili ya familia yako, kwa ajili ya wito wako, kwa ajili ya kazi yako, kwa ajili ya watoto wako, masomo yako, kwa ajili ya utume wako wa kila siku, kwa ajili ya biashara yako nk. Tumwombe pia Mungu atusaidie tufungue macho na kuguswa na shida na mahangaiko ya wengine, tushuke kuleta furaha kwa watu wanaoteseka, tushuke, kuleta amani kulipo na ugomvi, tushuke, kuleta upatanisho wa kweli kati yetu sisi kwa sisi, tushuke na kuwasamehe wale wote waliotukosea, tushuke na kushirikisha wengine tone la Upendo. Pili: Kristo ni Mwanakondoo wa kweli asiye na doa (Redemption through substitutionary sacrifice). Katika Pasaka ya wayahudi, walimchinja Mwanakondoo asiye na doa na wakamuoka na kumla. Mwanakondoo huyu ni mfano (Typos/Typology) wa Kristo, Paska wetu (1 Kor 5:7), Mwanakondoo wa Mungu asiye na doa ambaye kwa sadaka ya kifo chake msalabani amekua Mwanakondoo wa Pasaka mpya ambayo kwayo sisi tumeokolewa kutoka katika kifo na utumwa wa dhambi na mauti. Katika pasaka mpya, Sasa si Mwanakondoo tena anayetolewa sadaka bali ni Yesu mwenyewe anayejitoa sadaka kwa ajili ya ukombozi wa taifa lake. Ndugu wapendwa, tunaposherehekea Pasaka, tunasherehekea Utayari, utii na unyenyekevu wa Kristo katika kutimiza mapenzi ya Baba. Alikubali kujitoa sadaka, Mwanakondoo wa Mungu asiye na doa kwa ajili ya uhai na uzima wa ulimwengu. Kwa sadaka yake msalabani amemnunulia Mungu watu wa kila kabila, lugha jamaa na taifa. Siku ya Alhamisi Kuu alijitoa mwili wake na damu yake kama chakula cha uzima wa roho zetu. Kumbe tunaposhiriki karamu ya Bwana, sasa tunashiriki mwili wake kweli na damu yake kweli, ndiyo Ekaristi Takatifu, sadaka ya shukrani kwa zawadi ya ukombozi wetu.
Tatu: Damu kama Ishara ya Agano na ulinzi (Blood as a sign of Covenant and Protection). Mwenyezi Mungu aliwaamuru Musa na Aroni na mkutano wote wa Israeli kwamba, watwae baadhi ya damu ya Mwanakondoo aliyechinjwa kwa ajili ya Pasaka na kuitia katika miimo miwili na katika kizingiti cha juu katika zile nyumba walizokuwamo (Kut 12:7-8) ili wasiangamizwe na wakati Mwenyezi Mungu alipopita kuwaangamiza Wamisri usiku. Damu ilikua ni ishara ya lake ya maagano kati ya pande mbili, hapa ni kati ya Mungu na watu wake. Ndugu wapendwa, Damu hii ya Mwanakondoo ambayo ilipakwa katika miimo ya milango ili kuwalinda na kuwaponya waisraeli wasiangamizwe wakati malaika akipita kuwaua wazaliwa wa kwanza misri, katika Agano jipya, ni Damu ya thamani ya Kristo Mwanakondoo asiye na doa ndiyo ilitukomboa sisi kutoka katika hasira ya Mungu, na kutupatanisha tena naye. Ni damu inayotulinda dhidi ya nguvu za mwovu shetani. Damu ya Kristo inatutakasa, inatufariji, inatuosha kabisa dhambi na udhaifu wetu, inatulinda, inatubariki, inatupa matumaini, inatuinua, inatupatanisha na Mungu na kutupatanisha sisi kwa sisi na nafsi zetu. Damu ni ishara ya uhai, kumbe sisi sote tunapata uhai na uzima rohoni mwetu kwa njia ya damu ya Kristo. Inatukumbusha juu ya agano jipya na la milele kati ya Mungu na sisi taifa lake jipya, watu wa kila kabila, lugha jamaa na taifa.
Nne: Kwa kumla mwanakondoo, wayahudi walishiriki katika tendo kubwa la ukombozi wao (Sacramental participation in the act of Salvation). Katika Pasaka yao, Wayahudi hawakusimama tu, bali walimla nyama yule Mwanakondoo usiku ule ule, pamoja na mboga zenye uchungu (ishara ya mateso makali waliyopitia kule misri), mkate usiotiwa chachu (ishara ya uharaka wao kutoka utumwani misri, hawakua na muda wa kupoteza). Ndugu wapendwa, nasi katika adhimisho la Ekaristi Takatifu, sisi sote tunaalikwa kushiriki katika tendo kubwa ambalo kwalo Mungu alilileta ukombozi wa milele kwa taifa lake, yaani karamu ya mwili na damu ya Bwana wetu Yesu Kristo, Paska wetu. Hatuishii tu kukumbuka bali tunashiriki sasa na kwa wakati huu katika tukio la ukombozi wetu, kila mara tunaposhiriki katika Ekaristi. Yesu anatualika kwamba aulaye mwili wake na kuinywa Damu yake huyo anao uzima wa milele (Yn 6:54). Hivyo katika Ekaristi Takatifu tunashiriki katika ukombozi wetu.
Tano: Pasaka ya Wayahudi iliwajumuisha watu wote, Ekaristi Takatifu inatujumuisha sisi sote (Communal inclusion). Maelekezo juu ya namna taifa la Israeli walipaswa kuadhimisha pasaka yao ya kwanza yanatolewa kwa watu wote (edah) ikijumuisha watu wa nyumba nzima pamoja na majirani waliokuwa karibu. Pasaka hii ilijumuisha taifa lote la Mungu, hakuna aliyeachwa na mpango huu wa Mungu wa ukombozi. Hii yatuonesha ndugu wapendwa namna Kanisa lilivyo wazi kwa watu wote, mpango wa ukombozi ni wazi kwa kila mmoja wetu. Yesu katika karamu ya mwisho anawakusanya Mitume wake wote 12, wakiwemo pia waliomkimbia, waliomsaliti, na kumkana. Hakuna hata mmoja anayeachwa katika mpango wa Mungu wa ukombozi, sote tunaalikwa. Sote tuna nafasi katika kuupata ukombozi. Yesu kwa mapendo makubwa, aliweka pia sakramenti ya Daraja Takatifu siku hii ya Alhamisi kuu, ambapo kwa njia ya Sakramenti hii, kanisa kila mara linajipatia watoto wapya kwa njia ya sakramenti ya ubatizo na sakaramenti nyingine mbalimbali za kanisa. Tunapata nafasi ya kuadhimisha na kushiriki kila siku Ekaristi Takatifu, tukikumbuka fumbo kubwa la ukombozi wetu. Sita: Pasaka, Mlo ulioashiria Safari mpya, nasi tuanze safari mpya (A meal that marks a new Journey). Wayahudi walikula karamu ya pasaka wakiwa katika maandalizi ya safari. Ni safari mpya kutoka utumwani kwenda katika nchi ya Ahadi. Walipaswa kula nyama usiku ule ule, wakiwa wamefunga viuno, wamevaa viatu miguuni na fimbo zao mikononi, nao walipaswa kumla kwa haraka maana ilikua ni Pasaka ya Bwana (Kut 12:11). Ukombozi tu haikuna mwisho, bali Mwanzo wa safari yao mpya kuelekea katika nchi ya Ahadi. Ndugu wapendwa, kwetu sisi pia, ukombozi wetu sio mwisho wa safari. Tumebatizwa na kwa njia ya ubatizo wetu tumeondolewa katika utumwa wa dhambi na kifo. Hii yaonesha Mwanzo wa safari yetu mpya kuelekea katika nchi yetu ya ahadi mbinguni. Tunaposhiriki Ekaristi Takatifu sio mwisho, bali tunatumwa tena kwenda kuwa mashuhuda wa kule kupokea kwetu Ekaristi kwa watu wengine, upendo, huruma, sadaka, msamaha wa dhambi, upatanisho, wema, matumaini mapya nk. Tunashibishwa na kuimarishwa ili tuanze maisha na utume mpya ndani ya Kristo.
Somo la Injili: Ni Injili ya Yohane 13:1-15: Somo la Injili Takatifu ni Mwanzo wa sehemu ya pili ya kitabu cha Injili ya Yohane (sura ya 13-21), kitabu cha utukufu (Book of Glory). Sehemu hii hii ya pili ya Injili ya Yohane in katika karamu ya mwisho ambapoYesu anatoa mafundisho marefu ya mwisho kwa takribani sura nne kabla ya kuingia katika mateso na kifo na ufufuko wake. Injili zote tatu zaeleza tukio la Karamu ya Mwisho lakini Mwinjili Yohane anatupa tukio la Bwana wetu Yesu Kristo kuwaosha miguu wanafunzi wake, ishara ya mapendo makubwa na unyenyekevu wa Yesu. Katika somo hili la Injili Takatifu, tuna mafundisho matatu ya kujifunza. Kwanza: Karamu ya mwisho ni kielelezo cha utimilifu wa upendo wa Kimungu (Culmination of divine love). Mwinjili Yohane anatumbia, “Kabla ya sikukuu ya Pasaka, hali Yesu akijua kuwa saa yake imefika atakayotoka katika ulimwengu huu kwenda kwa Baba, naye hali amewapenda watu wake katika ulimwengu huu, aliwapenda upeo” Yn 13:1. Pasaka ya Wayahudi ilikuwa tukio kubwa ambapo walikumbuka namna Mwenyezi Mungu kwa upendo alivyowapatia ukombozi kutoka utumwani Misri kama walivyosherekea mara ya kwanza kabla hawajatoka utumwani misri (Kut 12). Ni katika tukio hilo hilo Yesu yupo pamoja na wanafunzi wake. Saa yake, ni saa ya mateso, ambapo kama Mwanakondoo wa kweli, kwa mapendo ya Mungu yasiyo na mipaka kwa watu wake, anatolewa sadaka kwa ajili ya ukombozi wa taifa jipya la Mungu. Ndugu wapendwa, Yesu anatufundisha nini maana ya kupenda. Na anatuambia hakuna mwenye upendo mkubwa kuliko huu wa mtu kuutoa uhai wake kwa ajili ya rafiki zake (Yn 15:13). Mimi na wewe tunakumbushwa juu ya upendo na kujitoa sadaka kwa ajili ya wengine. Ni siku kila mmoja wetu anaulizwa, je ninapenda kiasi gani? Yesu ametupenda kwa mapendo yake yote. Katika ndoa, katika familia zetu, katika jumuiya zetu, katika sehemu zetu za kazi, tudumishe upendo. Tupendane kwa mapendo ya kweli, kamwe tusifanye jambo lolote kwa wengine ambalo sisi hatupendi kutendewa kama anavyotufundisha Yesu. Vile kama tunavyotamani kupendwa na kuhurumiwa na Mungu, nasi tufungue mioyo yetu katika kuwapenda na kuwahurumia wengine, kama tunayopenda kusamehewa na Mungu nasi pia tuwe tayari kuwasamehe wengine vivyo hivyo. Kwa kufanya hivyo tunaishi amri hii ya mapendo ya Yesu.
Pili: Yesu anawaosha miguu wanafunzi wake, ishara ya utakaso, upendo na unyenyekevu. Mwinjili Yohane haelezi kwa kina juu ya karamu ya mwisho kama ilivyo katika injili pacha bali anaweka mbele yetu tukio la Yesu kuwaosha miguu wanafunzi wake. Yesu hali akijua ya kuwa Baba amempa vyote mikononi mwake na ya kuwa alitoka kwa Mungu naye anakwenda kwa Mungu, aliondoka chakulani akaweka kando mavazi yake, akatwaa kitambaa, akajifunga kiuoni, kisha akatia maji katika bakuli akaanza kuwatawadha miguu” Yn 13:4-5. Ndugu wapendwa, tendo hili la Yesu ni tendo la unyenyekevu, kujishusha mpaka chini kabisa (Kenosis/self empting). Kuwaosha wanafunzi wake miguu ni ishara ya utakaso tuupatao kwa njia ya maji yaliyomwagika kutoka katika ubavu wa Kristo alipochomwa kwa mkuki, nasi tunatakaswa kwa njia ya ubatizo na kuwa wapya tena. Unyenyekevu, kutwaa hali ya mtumwa, ni ishara ya Ekaristi Takatifu, Yesu ambaye kwa mapendo makubwa anatoa mwili wake na damu yake, anapohudumia na kisha atatoa vyote pia pale msalabani kwa ajili ya ukombozi wetu siku ya Ijumaa Kuu. Kwa kuwaosha miguu Yesu anawapa pia amri ya mapendo, kwamba kama yeye alivyofanya, mitume nao walipaswa kufanya vivyo hivyo. Kazi ya kuosha miguu ilikua ni kazi ya mtumwa, yule wa mwisho kabisa katika nyumba ya Bwana wake. Yesu anachukua nafasi ya huyu mtumwa, ambaye kwa mapendo anakubali kuwa wa mwisho kwa ajili ya kutoa huduma kwa wengine. Ni mara ngapi tunakubali kushuka ili wengine wapande? Mara ngapi tunakubali kunyenyekea na kutoa huduma ya upendo kwa wangine?
Tatu: Ekaristi Takatifu na Daraja Takatifu haviwezi kutenganishwa kamwe. Bwana wetu Yesu Kristo katika siku hii ya Alhamisi Kuu aliweka Sakramenti ya Daraja Takatifu ya Upadre. Aliwapa mitume wake uwezo wa kuadhimisha fumbo lile kuu la ukombozi wetu kwa ukumbusho wa mateso, kifo na ufufuko wake. Ndio uwezo waliopewa mapadre wa kuadhimisha Ekaristi Takatifu. Hivyo Ekaristi inaunda kanisa na kanisa linaunda Ekaristi na ndimo linamochota nguvu ya kiroho. Hakuna jumuiya ya Kikristo inayoweza kujengwa pasi na Ekaristi Takatifu. Ndugu zangu, Ekaristi Takatifu na Daraja Takatifu ya Upadre haviwezi kutenganishwa kamwe. Bila Ekaristi Takatifu hakuna padre na bila Upadre na padre, hakuna Ekaristi Takatifu, na kama hakuna Ekaristi Takatifu, hakuna Kanisa. Padre ni mwanadamu aliyetwaliwa kati ya watu, akatengwa na watu kwa mambo yamhusuyo Mungu kwa ajili ya watu (Ebr 5:1-4). Padre ni Kuhani, ni Kristo mwingine. Ni mwadhimishi wa mafumbo matakatifu. Yupo na taifa la Mungu katika nyakati zote, mwanzo mpaka mwisho wa maisha ya Mkristo.
Somo la pili: Ni Waraka wa Kwanza wa Mtume Paulo 1 Kor 11:23-26. Katika Somo la pili, Mtume Paulo anatueleza ni nini maana ya Ekaristi Takatifu. Mtume Paulo anatufundisha; Kwanza, Anawafundisha wakorintho nasi sote pia kuwa, Ekaristi Takatifu inatuunganisha na kutufanya kuwa ndugu (Communion), sisi na Kristo na kuwa ndugu kati yetu sisi kwa sisi. Pili, kila tunapoadhimisha Ekaristi, tunakumbuka fumbo la Pasaka yaani, mateso kifo na ufufuko wa Bwana na hivyo ni sadaka ya shukrani. Tatu, Ekaristi takatifu ni sadaka ya shukrani kwa Mungu (Eucharistein/Thanksgiving) kwa zawadi ya ukombozi wetu. Kristo anatwaa mkate, anaumega, ishara ya kujisadaka, akitukumbusha nasi pia kukubali kuvunjwa, kujimega kama sadaka kwa ajili ya wengine. Divai ni tunda la mzabibu uliopondwa pondwa ili kuleta furaha, Kristo kwa kupigwa kwake amekua chanzo na kilele cha furaha yetu. Nasi tukubali kupondwa pondwa, kutumika kwa ajili ya kuwa chanzo cha furaha kwa wengine. Inakuwaje mkate kuwa mwili wa Yesu na divai kuwa damu ya Yesu kila mara tunapoadhimisha Ekaristi Takatifu kwa ukumbusho wake? Ndugu wapendwa, mababa wa mtaguso wa Trento wanasema hivi, “Kwa sababu Kristo Mkombozi wetu ndiye alisema mwenyewe kwamba huu ndio mwili wangu, akautoa mwenyewe kwa namna ya mkate na damu kwa namna ya divai. Hivyo kwa kutakatifuza mkate na divai hutokea mabadiliko ya kiini chote cha mkate kuwa katika kiini cha mwili wa Kristo Bwana wetu na kiini chote cha divai kuwa katika kiini cha damu yake”. Uwepo huu halisi na kweli katika maumbo haya ya mkate na divai huanza katika mageuzo na hudumu muda wote maumbo haya yanapokuwapo.
Hivyo, Kristo yupo mzima na mkamilifu katika kila mojawapo ya maumbo ya mkate na divai na ni mzima na mkamilifu katika kila sehemu yao. Kwa jinsi hii, kuimega Ekaristi Takatifu hakumgawanyi Kristo hata kidogo. Uwepo wa Yesu unabaki kwenye kila kipande kidogo kilichovunjika hata katika kila tone la damu yake, uwepo wa Yesu umo kamili kabisa kama katika Ekaristi Takatifu nzima (KKK 1376-1377). Mwisho tunaalikwa kupokea Ekaristi Takatifu katika hali ya neema. Ekaristi Takatifu ni Yesu kweli na mzima katika maumbo ya mkate na divai. Mungu aliye Mtakatifu sana anakubali kubaki nasi katika Ekaristi Takatifu. Kila mara tupokeapo Ekaristi tunampokea Yesu mzima. Tunaalikwa kujitakasa kwa njia ya sakramenti ya Kitubio ili kila mara tumpokee Yesu katika hali ya neema na tustahili kupokea matunda yatokanayo na kule kuupokea kwetu Mwili na Damu Takatifu sana ya Yesu. Hitimisho: Katika siku hii ya Alhamisi kuu, tumshukuru Kristo aliyetupenda kwa mapendo makuu, akajitoa sadaka kwa ajili ya ukombozi wa ulimwengu mzima na tuombe neema nasi ya kujitoa sadaka kwa ajili ya wengine. Tumshukuru Kristo kwa zawadi ya Ekaristi Tatakatifu katika Kanisa, uwepo wake halisi katika maumbo ya mkate na divai. Tuwaombee Mapadre wote ili waendelee kuwa kielelezo cha uwepo wa Kristo katika kanisa lake kwa njia ya maadhimisho ya Neno lake na Sakramenti mbalimbali katika Kanisa.