Sudan Kusini,Maaskofu:tekelezeni mazungumzo ya Mkataba wa kutatua mzozo!
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Sudan Kusini iko katika hatari ya kuwa uwanja wa vita kwa vikosi vya kigeni. Hili ni onyo la dharurua lililotolewa Maaskofu wa Baraza la Maaskofu wa Sudan na Sudan Kusini (SSCBC) kwa hali ambayo imetokea katika nchi ya mwisho baada ya kukamatwa kwa Makamu wa kwanza wa Rais Riek Machar. "Kukamatwa kwa viongozi wa upinzani na kuhusika kwa vikosi vya kijeshi vya kigeni, hasa kutumwa kwa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Uganda (UPDF), kumeongeza hofu na kutoaminiana. Vitendo kama hivyo vinahatarisha kugeuza nchi yetu kuwa uwanja wa vita kwa ajili ya maslahi ya nje na kinzani za kisiasa," taarifa hiyo ya Baraza la Maaskofu imethibitisha "juu ya kuongezeka kwa ghasia na mvutano wa kisiasa nchini Sudan Kusini iliyochapishwa mnamo tarehe 28 Machi 2025.
Maaskofu wanazitaka Jumuiya za kiraia, vijana na mashirika yote kuungana
Katika hati iliyotomwa katika Shirika la Kipapa la habari za Kimisionari FIDEs, inabainisha kuwa "Kupoteza maisha, kuporomoka kwa umoja wa kitaifa na kuporomoka kwa taasisi ambazo tayari ni dhaifu kutakuwa mbaya kwa vizazi vijavyo." Maaskofu wanazitaka jumuiya za kiraia, vijana, mashirika ya wanawake na jumuiya ya kimataifa kuungana dhidi ya vita na kufanya kazi kwa ajili ya amani. Kwa hivyo wanawataka watu wa Sudan Kusini kupinga matamshi ya chuki, uchochezi wa migogoro ya kikabila na habari potofu, hasa kwenye mitandao ya kijamii. "Tunasalia tayari kufanya makubaliano, kuwa sauti kwa wasio na sauti na kufanya kazi bega kwa bega na wale wote wanaotafuta amani ya kweli,” unahitimisha ujumbe uliotiwa saini na Kardinali Stephen Ameyu Martin Mulla, Askofu Mkuu wa Juba na Rais wa Baraza la Maaskofu wa Sudan na Sudan Kusini(SSCBC.)
Ziara ya Odinga huko Juba,Sudan na Uganda
Mnamo tarehe 28 Machi 2025, Waziri Mkuu wa zamani wa Kenya Raila Odinga alisafiri hadi Juba kukutana na Rais wa Sudan Kusini Salva Kiir. Odinga, ambaye aliteuliwa na IGAD (Mamlaka ya Kiserikali ya Maendeleo, jumuiya ya kiuchumi ya kikanda ya Umoja wa Afrika) kupatanisha kati ya Kiir na Machar, hata hivyo, hakuweza kukutana na viongozi hao. Waziri Mkuu huyo wa zamani wa Kenya alisafiri hadi Uganda kwa mkutano na Rais Yoweri Museveni.
Wito wa Papa kwa viongozi wa Sudan Kusini
Ikumbukwe hata hivyo mwishoni mwa tafakari kabla ya Sala ya Malaika wa Bwana Dominika tarehe 30 Machi 2025, Papa Francisko alitoa wito wa dhati "kwa viongozi wote (wa Sudan Kusini), kufanya jitihada za juu zaidi kupunguza mvutano nchini humo." "Lazima tuweke kando tofauti zetu na, kwa ujasiri na uwajibikaji, kuketi karibu na meza na kuanza mazungumzo ya kujenga. Ni kwa njia hiyo tu itawezekana kupunguza mateso ya watu wapendwa wa Sudan Kusini na kujenga mustakabali wa amani na utulivu," alihitimisha Papa.
Caritas Sudan Kusini waunga Mkono Maaskofu
Caritas ya Sudan Kusini inaunga mkono kikamilifu Baraza la Maaskofu Katoliki nchini Sudan na Sudan Kusini kwa kuibua hofu kubwa kuhusiana na kushamiri kwa ghasia, mapigano na mivutano ya kisiasa nchini humo kufuatia kukamatwa kwa viongozi wa kisiasa akiwemo Makamu wa Rais Riek Machar. "Kuhamishwa kwa raia wasio na hatia hasa wanawake na watoto, kunawakilisha kurudi nyuma kwa juhudi za amani," inasema Caritas Sudan Kusini, huku ikikumbuka kwamba maaskofu wanatoa wito thabiti wa kuwa na wastani, mazungumzo na kujitolea upya kwa utekelezaji wa Mkataba Uliohuishwa wa utatuzi wa mzozo nchini Sudan Kusini. Caritas Sudan Kusini inarejea dhamira yake ya kuunga mkono amani na maridhiano nchini humo, na kuwaalika raia na mamlaka zote kufanya kazi pamoja kwa mustakabali ulio imara na wa amani zaidi.