Marekani-Kansas:Padre Arul Carasala auawa kwa risasi nyumbani kwake
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Padre Arul Carasala, Paroko wa Parokia ya Watakatifu Petro na Paulo huko Seneca, jiji lililoko kaskazini-mashariki mwa Kansas, aliuawa siku ya Alhamisi, tarehe 3 Aprili 2025, kwa kupigwa risasi na mwanamume mmoja alipokuwa kwenye nyumba yake. Kwa mujibu wa taarifa za awali, aliyefyatua risasi alikuwa ni mzee, asiyejulikana kwa waamini wa kanisa hilo, ambaye sasa anashikiliwa. Sababu za kitendo hicho bado hazijajulikana na zinachunguzwa na vyombo vya sheria. Milio ya risasi tatu zilifyatuliwa kwa padre huyo, ambaye alifariki muda mfupi baada ya kuwasili hospitalini.
Askofu Mkuu Naumann: Padre Carasala alikuwa mchungaji mwaminifu
Askofu Mkuu Joseph Naumann, wa Jiji la Kansas, katika chapisho kwenye chaneli zake za mitandao ya kijamii, aliyataja mauaji hayo kama "kitendo kisicho na maana cha unyanyasaji ambacho kiliacha jamii ikihuzunika kwa kumpoteza kasisi mpendwa ambaye pia alikuwa rafiki. Katika wadhifa huo, Askofu Mkuu alifafanua kuwa hakuna tishio kwa jamii ya wamini huku aelezea uchungu na mshtuko uliosababishwa na kifo cha Padre: "Padre Carasala alikuwa mchungaji mwaminifu na mwenye bidii ambaye alitumikia kwa uaminifu Jimbo kuu letu kwa zaidi ya miaka ishirini, ikiwa ni pamoja na kuwa mkuu wa Kanda ya Nemaha-Marshall. Upendo wake kwa Kristo na Kanisa ulionekana wazi kwa jinsi alivyowajali watu wake kwa ukarimu na kujitolea sana. Washiriki wake, marafiki na washirika watamkosa sana."
Padre Carasala aliepwa daraja la Upadre 1994
Padre Arlu Carasala alipewa daraja la Upadre, kunako mwaka 1994 nchini India, nchi yake ya asili, na amekuwa akitekeleza huduma yake ya kichungaji huko Kansas tangu 2004. Alipata kuwa raia wa Marekani mnamo mwaka 2011, mwaka ambao alipata kuwa Paroko wa Kanisa la Parokia ya Petro na Paulo eneo moja linalohesabu wakazi wachache.