Tafuta

2025.04.20 Papa baada ya misa ya Pasaka alitoa baraka ya Urbi et orbi na kuzungukia uwanja wa Mtakatifu Petro. 2025.04.20 Papa baada ya misa ya Pasaka alitoa baraka ya Urbi et orbi na kuzungukia uwanja wa Mtakatifu Petro.  (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Pasaka na utunzaji wa mazingira:Tunaomboleza mtetezi wa nyumba ya pamoja!

Kanisa Katoliki ulimwenguni liko kwenye msiba mkubwa kwa kifo cha Papa Francisko,aliyeaga dunia tarehe 21 April,Jumatatu ya Pasaka,baada ya kuugua kwa mda mrefu. Tunapoomboleza kifo chake,tunafurahi pia katika tumaini la uzima wa milele kwa Mchungaji wa Kanisa ambaye amelihudumia kama Papa kwa miaka kumi na miwili.Papa Francisko ni Mchungaji ambaye alibadilisha ufahamu wetu juu ya uhusiano wetu na Mungu na kila mmoja wetu na viumbe vyote alivyoviumba Mungu.

Na Padre Felix Mushobozi,C.PP.S – Dodoma - Tanzania.

Katika Jumapili ya Pasaka,mioyo yetu imejaa matumaini na furaha. Ufufuko wa Kristo unatukumbusha kwamba, baada ya giza, nuru huja daima na kwamba kila mwisho unaweza kuwa mwanzo wa kitu cha ajabu na kipya. Kwa msukumo wa waraka wa Papa Francisko Laudato Si', tunakualika kutafakari juu ya uhusiano wa kina kati ya imani yetu na utunzaji wa nyumba yetu ya pamoja, katika latitudo zote za sayari yetu. Injili ya Jumapili ya Pasaka inatuonesha Maria Magdalene, Petro na Yohana mbele ya kaburi tupu, wakikabiliana na fumbo la Ufufuko. Mkutano huu na fumbo unatuita kuwa mawakala wa mabadiliko na matumaini duniani. Katika Laudato Si', tunahimizwa kutafakari jinsi "kila kitu kimehusianishwa": hali yetu ya kiroho, matendo yetu ya kila siku, na hali njema ya sayari yetu na hali za ndugu na dada zetu wote katika Kristo.

Bwana amefufuka, kaburi liko wazi ameshinda mauti
Bwana amefufuka, kaburi liko wazi ameshinda mauti

Ufufuko wa Kristo wenyewe ni kilio cha uzima kinachotuongoza kuondokana na mantiki ya ufujaji na tabia za uuaji ili kujifunza mantiki ya kukutana, kuhusiana kushikamana na kufufuka. Katika muktadha huu, kila jitihada za kutunza mazingira na maisha ya mwanadamu ni kielelezo cha imani katika ufufuko, katika ushindi wa uhai juu ya kifo. Katika Pasaka hii, tunapoadhimisha ufufuko, tukumbuke maneno ya Baba Mtakatifu Francisko aliyosema katika mahubiri yake mwaka 2019 akisema: "Pasaka ni sikukuu ya mawe yaliyoondolewa juu ya makaburi yetu, miamba iliyovingirishwa kando ya majumba yetu. Mungu huondoa hata mawe magumu zaidi ambayo hukandamiza matumaini na matarajio yetu; kifo, dhambi, hofu, malimwengu nk.

Tunaomboleza mtetezi wa mazingira

Kanisa Katoliki ulimwenguni liko kwenye msiba mkubwa kwa kifo cha Papa Francisko, aliyeaga dunia tarehe 21 April – Jumatatu ya Pasaka, baada ya kuugua kwa mda mrefu. Tunapoomboleza kifo cha Baba Mtakatifu Francisko kwa kuondoka duniani, tunafurahi pia katika tumaini la uzima wa milele kwa Mchungaji wa Kanisa amabaye amelihudumia kama Papa kwa miaka kumi na miwili. Papa Francisko ni Mchungaji ambaye alibadilisha ufahamu wetu juu ya uhusiano wetu na Mungu, na kila mmoja wetu, na viumbe vyote alivyoviumba Mungu. Kwetu sisi Wakereketwa wa utunzaji wa mazingira, mtazamo wa Papa Francisko wa utunzaji wa uumbaji umeunda sera, umehamasisha mamilioni ya watu wa mataifa na dini zote kuchukua hatua madhubuti, na kutuimarisha sisi katika Kanisa Katoliki katika utume wetu.

Umati unaendelea kuaga mwili wa Papa Francisko
Umati unaendelea kuaga mwili wa Papa Francisko   (Vatican Media)

Papa Francisko alipochapisha Waraka wake juu ya Utunzaji wa Mazingira mnamo mwaka 2015, tulipewa framework au mtazamo mpya wa jinsi tunavyoliangalia swala zima la uharibifu wa Mazingira. Tulialikwa kulitazama sio kama suala ambalo limejitenga na maisha ya jamii bali kama sehemu ya shida kubwa ya maadili ya Kikatoliki. Katika Laudato Si’,  Papa Francisko alitualika kuwa na mtazamo wa “Ikolojia fungamanishi” – “Integral Ecology”, ambayo inaunganisha ulinzi na utunzaji wa mazingira na utu wa binadamu, uhusiano wake na umaskini uliokithiri na mageuzi ya kiuchumi. Maono haya ya kijasiri yaliwapa Wakatoliki na watu wote wenye mapenzi mema changamoto na wito wa kusonga mbele zaidi kwa kuweka kando wasiwasi wa kufikirika na kukumbatia hatua madhubuti za kulinda sayari hii, ambayo ndiyo makao yetu ya Pamoja, kwa lugha yake - ndiyo nyumba yetu tunayoishiriki na wote.

Kardinali Rugambwa alitoa heshima na kumwombea Papa
Kardinali Rugambwa alitoa heshima na kumwombea Papa   (Vatican Media)

Urithi aliotuachia Papa Francisko

Papa Francisko anatuachia urithi mkubwa hasa kwa kuhakikisha kwamba Laudato inakwenda kutafsiriwa kwa vitendo vinavyoonekana ndani ya Kanisa. “Laudato Si Action Platform” yaani  “Jukwaa la kuchukuwa hatua kivitendo la Laudato Si’,” lililozinduliwa mnmamo mwaka  2021, ambalo limekuwa mpango muhimu wa kuhamasisha taasisi za Kikatoliki, Taasisi za kidini na watu binafsi kutekeleza hatua endelevu kulingana na maono ya Laudato Si. Kufikia sasa, mpango huu umeshirikisha zaidi ya watu milioni ishirini ulimwenguni, na kukuza uwongofu mkubwa wa kiikolojia na ahadi za vitendo kama vile kutokuwa sehemu ya ongezeko la hewa chafu, matumizi ya nishati safi kwa njia ya kuwajibika, na utetezi wa wale wanaoathirika na uharibifu wa mazingira katika kijamii.

Waamini wanatoa salamu za mwisho
Waamini wanatoa salamu za mwisho   (Vatican Media)

Utetezi wa Maskini

Katika kipindi chote cha Upapa wake, Papa Francisko alitoa kipaumbele kwa sauti za wale walioathiriwa zaidi na majanga ya kiikolojia na kijamii. Katika Laudato Si’ alisisitiza na kutoa wito juu ya kuguswa na mahangaiko ya le wahanga wa mabadiliko ya tabianchi, hasa maskini, jamii za kiasili, na watu waliotengwa. Dhamira yake hii hii imeonekana katika mipango mikuu ya Kanisa na ya kimataifa kama vile Sinodi ya Amazonia na Sinodi ya hivi karibuni, ambayo imezipa jumuiya hizi jukwaa la kuzungumza juu ya changamoto zinazowakabili na kutetea mabadiliko ya kimfumo.

Waamini wakitoa heshima zao
Waamini wakitoa heshima zao   (Vatican Media)

Uongozi wa Papa umethibitisha tena kwamba mgogoro wa mazingira hauwezi kutenganishwa na masuala ya usawa wa kiuchumi, uhamiaji, na haki za binadamu. Kwa njia hiyo Papa Francisko ameacha urithi mkubwa katika swala zima la ufahamu wa kiikolojia. Maono yake sio tu yamebadilisha mafundisho ya Kikatoliki kuhusu jamii lakini pia yametoa mchango mkubwa katika sera za kimataifa, majadiliano kati ya dini mbalimbali, na kutia moyo Wanaharakati wa mazingira na haki za wanyonge kwenye ngazi za chini. Msisitizo wake kwamba kutunza uumbaji ni sehemu muhimu ya ufuasi wa Kikristo umehakikisha kwamba wajibu wa kiikolojia sasa ni kiini cha utambulisho na utume wa Kikatoliki.

Umati wa watu wakenda kutoa heshima zao
Umati wa watu wakenda kutoa heshima zao   (Vatican Media)

Utunzaji wa mazingira umeingizwa katika mafundisho ya Kikatoliki kwa karne nyingi na kuzungumzwa na mapapa kwa miongo kadhaa, lakini Papa Francisko ameweka msisitizo mpya juu ya mwelekeo huu wa imani, hasa katika kukabiliana na mgogoro wa sasa wa kiikolojia kwa ngazi ya kimataifa. Amesisitiza kwamba kutunza uumbaji si jambo la hiari bali ni kipengele cha msingi cha wito wa Kikristo, wajibu wa pamoja kwa maskini, na wajibu kwa vizazi vijavyo. Kumtukuza Mungu Muumba sasa, zaidi ya hapo awali, ni sehemu ya msingi ya imani ya Kikatoliki na kutaendelea kuwa kipengele kinachobainisha utume wa Kanisa katika miaka ijayo.

Papa na mazingira nyumba yetu ya Pamoja
24 Aprili 2025, 10:47