Tafuta

Mama Maria wa Kibeho Rwanda. Mama Maria wa Kibeho Rwanda. 

Rwanda:Maaskofu wa Rwanda na Burundi wakutana kuombe amani katika Kanda ya maziwa makuu!

Maaskofu wa ACOREB wanaunga mkono ujumbe wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu wa Afrika ya Kati(ACEAC),lilitoa wito wa mazungumzo kusuluhisha mizozo kwa amani.Kuanzia Februari 24 -26,ACEAC lilifanya mkutano jijini Dar-es-Salaam ili kutafuta amani katika eneo la Maziwa Makuu,hasa mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.Haya yalikumbushwa mwishoni mwa Mkutano wa Maaskofu wa Burundi na Rwanda Machi 30-Mosi Aprili.

Na Angella Rwezaula – Vatican.

Kufungwa kwa mipaka kunazuia kukua kwa uchumi, mshikamano wa kijamii na kubadilishana kiutamaduni, ndivyo wamethibitishwa Maaskofu Katoliki wa Rwanda na Burundi mwishoni mwa Mkutano wao mkuu wa kawaida wa Shirikisho la Maaskofu wa (ACOREB), uliofanyika kuanzia tarehe 30 Machi hadi Mosi Aprili 2025 katika Kituo cha Mtakatifu Yosefu, huko Kibungo, Rwanda. Serikali ya Burundi, ilifunga mpaka wake wa barabara na Rwanda, ikiishutumu kuwaunga mkono waasi wa Burundi walioko mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo(DRC). Hata hivyo ni shutuma zilizokataliwa na serikali ya Kigali. Burundi pia inaamini kuwa Rwanda ni mwenyeji wa wahusika wa mapinduzi yaliyofeli ya na inataka wakabidhiwe kwa haki yake yenyewe. Lakini Rwanda inasema haiwezi, kwa mujibu wa sheria za kimataifa, kuwarejesha wanaotafuta hifadhi. Katika taharifa yao, waliyoituma katika Shirika la Kipapa la Habari za Kimisionari FIDES, maaskofu wanabainisha kuwa "Tunawaomba viongozi wetu wafanye kazi kwa hekima na huruma ili kurejesha hali ya kawaida na kukuza umoja kati ya mataifa yetu," Maaskofu wa nchi hizo mbili waliomba katika taarifa hiyo iliyosomwa kwenye mkutano na waandishi wa habari.

Mgogoro kati ya Rwanda na Burundi

Mgogoro kati ya Rwanda na Burundi unahusishwa na ule unaoshuhudiwa mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, ambako maeneo makubwa ya majimbo ya Kivu Kaskazini na Kusini yameishia chini ya udhibiti wa M23, vuguvugu la msituni linaloungwa mkono na Rwanda. Burundi, ambayo ilikuwa imetuma vikundi vyake vya kijeshi huko Kivu Kusini, iliviondoa muda mfupi kabla ya kutekwa kwa mji mkuu wa jimbo hilo, Bukavu, na M23 na wanajeshi wa Rwanda. Serikali ya Bujumbura sasa inahofia uwezekano wa kuvamiwa na M23 na Wanyarwanda katika eneo lake, na kuenea kwa mzozo wa Congo katika eneo lote la Maziwa Makuu. Kwa sababu hiyo, Maaskofu wa ACOREB wanaunga mkono ujumbe wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu wa Afrika ya Kati (ACEAC), ambao ulitoa wito wa mazungumzo kusuluhisha mizozo kwa amani.

Maaskofu:Jenga madaraja, shuhudia umoja na udugu ulimwenguni pote

"Kuanzia tarehe 24 hadi 26 Februari 2025, Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu wa Afrika ya Kati(ACEAC), lilifanya mkutano jijini Dar-es-Salaam ili kutafuta amani katika eneo la Maziwa Makuu, hasa mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, wanakumbusha Maaskofu wa Burundi na Rwanda. "Wajumbe wa ACOREB wanakaribisha na kuunga mkono ujumbe wa ACEAC, ambao unatoa wito kwa pande zote zinazohusika katika vita hivi hatari kurejea kwenye meza ya mazungumzo ili kutatua migogoro yao kwa njia za amani, kwa njia ya mazungumzo ya dhati na jumuishi.” Baraza la Maaskofu wa Burundi (CECAB) na lile la Rwanda(CEPR) walitafsiri ujumbe huo kwa lugha ya wenyeji na kuusambaza katika parokia zao zote ili kuwahamasisha waamini kuombea amani katika kanda yao na kuwa mashahidi wa udugu. "Katika ulimwengu ambapo watu wengi hupanda mifarakano na kujenga kuta za migawanyiko kwa ajili ya masilahi yao ya kibinafsi na uchoyo, Maaskofu wanawahimiza waamini wa Kikatoliki kuwekeza katika kujenga madaraja, kushuhudia umoja, udugu wa ulimwenguni pote na ukweli," walibainisha.

03 Aprili 2025, 11:09