Sherehe ya Pasaka ya Bwana: Ufufuko wa Kristo Kiini cha Imani
Na Padre Joseph Herman Luwela, - Vatican.
UTANGULIZI: Karibu mpenzi msikilizaji na msomaji wa tafakari ya Neno la Mungu kutoka hapa Radio Vatican leo Sherehe ya Pasaka mwaka 2025, tafakari inaongozwa na maneno ya Mtume Paulo: "Basi jisafisheni, mkatoe ile chachu ya kale, mpate kuwa donge jipya" (1 Wakorintho 5:7). Huu ni mwaliko wa kujitakasa na kuanza upya katika maisha ya kiroho, tukisherehekea Ufufuko wa Kristo Yesu kutoka wafu; kilele cha ukweli wa imani katika Kristo aliyeteswa, akafa na hatimaye kufufuka kutoka wafu kadiri ya Maandiko Matakatifu. Ni ufunuo wa Uungu wa Kristo Yesu unaowapatia waamini maisha ya uzima mpya na hivyo kuhesabiwa haki pamoja na kufanywa wana wateule wa Mungu. Ufufuko wa Kristo ni msingi wa ufufuko wa miili na uzima wa milele ijayo! Ndiyo maana Pasaka ni Sherehe kubwa katika Kanisa. Hii ni Sherehe ya upendo, huruma na msamaha wa Baba wa milele unaofumbatwa katika Fumbo la Msalaba. Imba ulimi wangu, piga kelele ewe Mkristo, utangaze ushindi wa Mfalme mkuu... imba fumbo hili la ukombozi, nyimbo nzuri na tenzi, uisifu damu ya Yesu iliyomwagika msalabani... Wamebarikiwa wale wote ambao kwa imani na unyofu wa mioyo yao wanalisadiki fumbo hili kubwa ya kwamba siku ya tatu baada ya kuteswa, kufa na kuzikwa, Kristo Yesu amefufuka mzima, alleluia… Pole shetani, enzi yako imeisha... kwa sababu yako tulifungwa kuzimuni, shimoni mwa uharibifu, ewe ‘kifo ku wapi kushinda kwako? u wapi ewe mauti uchungu wako?’ (1Kor15:55) ni nini kilichokubakia? Tutazame wakristo, tunao muhuri kwa damu ya Kristo mzima, shetani huna la kujivunia, mauti huna nguvu tena, dhambi nayo imenyenyekeshwa.
UFAFANUZI: Masomo ya Pasaka yanahimiza waamini kuacha maisha ya dhambi na kuingia katika maisha mapya ndani ya Kristo Mfufuka. Katika Injili, tunasikia juu ya wanawake waliokwenda kaburini na kugundua kuwa Yesu amefufuka, tukio linaloleta matumaini mapya kwa ulimwengu. Siku hii ni takatifu, Kristo Yesu amekata minyonyoro ya mauti, ametulipia deni la Adamu kwa Baba wa milele, amefuta mashtaka ya dhambi ya kale. Ni Pasaka ya Bwana, ambapo wenye kumsadiki Kristo, wanatengwa na maovu ya dunia na giza la dhambi, wanarudishiwa tena neema na kushikirikishwa utakatifu (Mbiu ya Pasaka). Kristo Yesu Pasaka wetu ameturudishia hadhi yetu, amekupa maana kuzaliwa kwetu, ameziunganisha mbingu na nchi, Mungu na wanadamu… Kristo amefufuka limbuko lao waliolala mauti, tumaini la marehemu toharani, utukufu wa watakatifu mbinguni, amani ya dunia na wokovu wa wote wenye mwili. Katika Ujumbe wa Kwaresima wa mwaka 2025, Papa Francisko alisisitiza kauli mbiu ya "Tutembee pamoja kwa matumaini," akiwahimiza waamini kuwa mahujaji wa matumaini, wakisafiri pamoja kuelekea ukamilifu wa maisha ya Kikristo. Alisema "katika kipindi hiki cha Kwaresima, ninapenda kushiriki nanyi tafakari kuhusu maana ya ‘kutembea pamoja kwa matumaini’ na wito wa uongofu ambao huruma ya Mungu inatualika kuuishi, si tu kama watu binafsi bali pia kama jamii. Pasaka ni adhimisho la imani yetu, kiini cha Ukristo wetu, “kama Kristo asingefufuka imani yetu ingekuwa bure (1Kor 15:17), kusali kusingekuwa na maana na dini ingekuwa batili.”
Pokeeni baraka na neema za Pasaka, msamaha wa dhambi, utu mpya, roho mpya, ng’aeni katika utukufu, ng’aeni katika matendo, mawazo na mipango yenu, ng’aeni katika kutafuta na kuombea amani, ng’aeni katika utauwa na uchamungu, naam, msifuni katika patakatifu pake, ndio… kila mwenye pumzi na amsifu Bwana, alleluia. Mtakatifu Paulo anasema Pasaka ihuishe na kufanya upya mwendo wetu mzima wa maisha kiroho na kimwili (somo II 1Kor 5:6-8). Kufufuka ni kutoka hali ya upotevu na kuingia uzima wa kimungu. Sisi tuliokufa katika dhambi tunafufuka kwa njia ya Kristo, na pamoja naye na ndani yake. Basi maisha yetu yampe Mungu Baba heshima yake, yampe Mungu Mwana shukrani zake, yampe Mungu Roho Mtakatifu nafasi yake, tena maisha yetu yamtangaze huyo Kristo Mfufuka kwa alleluia ya milele. Ufufuko wa Kristo unatuonesha ushindi dhidi ya dhambi na kifo, ukitualika kujitakasa kwa kuondoa "chachu ya kale" ya dhambi na kuishi kama "donge jipya" katika Kristo. Hii inaendana na wito wa Papa Francisko wa kutembea pamoja kwa matumaini, tukisaidiana kama jumuiya ya waamini katika safari ya imani: “Basi jisafisheni, mkatoe ile chachu ya kale, mpate kuwa donge jipya” (1Kor 5:7), chachu ya kale ni uzamani wetu katika maisha, kuna mengi ya kizamani ndani ya mioyo yetu, bado tumeyakumbatia na kuyathamini… kama vile nguo tuvaazo huchakaa na kuachwa mambo hayo pia yamechakazwa na Pasaka ya Kristo… ni yepi hayo? Kila mmoja afanye tathmini binafsi ya ndani ya nafsi yake, ayaone na kuyajutia, hilo ni kaburi lako, utoke humo uangazwe na nuru ya Kristo, “jisafisheni mkatoe chachu ya kale mpate kuwa donge jipya” donge hilo jipya ni “kuifanya karamu, si kwa chachu ya kale, wala kwa chachu ya uovu na ubaya, bali kwa yasiyochachika, ndio weupe wa moyo na kweli.”
Wasafi wa moyo ni utakatifu, mioyo yetu inapaswa kuwa myeupe sababu imeoshwa na kutakaswa katika damu ya Mwanakondoo. Lakini bila bahati tumeruhusu weupe wa mioyo yetu ufubae na nyakati nyingine kuigeuza myeusi… tumekuwa binadamu mno, tumeshuka chini kuliko kuinua nafsi zetu juu uliko ukamilifu wetu, katika nafasi nyingi tumekubali kupoteza ladha halisi ya uumbaji wetu, tumemuhuzunisha Mungu, mioyo yetu imepoteza weupe wake. Tunapozungumzia vita vinavyopiganwa kwa silaha kali duniani, sisi pia tunauana kwa maneno yetu na kauli zetu. Tumeipaka mioyo yetu wino mweusi na kuzipiga nafsi zetu chapa zisizoeleweka, tumeongeza maadui na kupunguza marafiki, tumejificha nyuma ya wengine nyakati za changamoto, hatutaki kuonekana wabaya, hatujafaulu kutatua migogoro yetu kwa amani, hatujasoma na kutafakari Neno la Kristo ipasavyo, tumewakwaza wenzetu, hatujakomunika Ekaristi katika hali njema. “Basi jisafisheni, mkatoe ile chachu ya kale, mpate kuwa donge jipya…” tutafaulu kwa kuongozwa na hekima ya Roho wa Bwana kutenda na Mt. Yohane kaburini pa Yesu, “aliona na kuamini” (Somo la Injili, Yn 20:1-9) nasi tuone na tuamini... kishapo tuyaishi mausia ya Mt. Petro katika somo I (Mdo 10:34, 37-43) katika ushuhuda kamili. Pasaka ni alleluia ya wote... baba na kijana, mama na mtoto… alleluia sebuleni, chumbani… ofisini, dukani, shambani… kichwani, kifuani, tumboni, miguuni… alleluia ya maisha! Sherehe ya Pasaka kwa Mwaka 2025 inatualika kusherehekea maisha mapya katika Kristo Mfufuka, tukijitakasa na kuondoa dhambi, na kuishi kwa matumaini kama mahujaji waaminifu. Tukumbuke maneno ya Mtume Paulo na mwaliko wa Papa Francisko wa kutembea pamoja kwa matumaini, tukisaidiana katika safari ya kiroho kuelekea ukamilifu wa maisha ya Kikristo.