Tafakari Dominika ya Huruma ya Mungu: Toba Na Wongofu wa Ndani
Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.
Tafakari ya Neno la Mungu, dominika ya 2 ya Pasaka mwaka C wa Kiliturujia katika Kanisa. Dominika hii ilipewa jina la “Dominika ya huruma ya Mungu” katika maadhimisho ya Jubilei Kuu ya mwaka 2000 na Baba Mtakatifu Yohane Paulo II. Mtakatifu Maria Faustina Kowalska wa Huruma ya Mungu, mtawa ndiye aliyepata maono na kuidhihirisha kwetu huruma ya Mungu. Katika maono hayo aliona miali ya mwanga iliyotoka kifuani pa Bwana wetu Yesu Kristo – mwali wa rangi nyekundu ukiwakilisha damu yake na rangi ya bluu hafifu ikiwakilisha maji ya ubatizo. Dominika ya Huruma ya Mungu kimsingi inakazia zaidi: Saa ya Huruma Kuu; Umuhimu wa toba na wongofu wa ndani, ili kulipyaisha Kanisa la Kristo Yesu kwa chachu ya utakatifu wa maisha. Waamini wajitahidi kushiriki Ibada ya Misa Takatifu kwa uchaji na ibada; wakimbilie daima huruma ya Mungu kwa Sakramenti ya Upatanisho; wajenge utamaduni wa kuabudu Ekaristi Takatifu na maisha ya sala sanjari na kudumisha Ibada ya Njia ya Msalaba katika uhalisia wa maisha yao. Jumapili ya Huruma ya Mungu ilianzishwa na Mtakatifu Yohane Paulo II kunako mwaka 2000. Mtakatifu Maria Faustina Kowalska ni kati ya watakatifu waliotangaza, wakashuhudia na hatimaye, kueneza Ibada ya huruma ya Mungu. Hii ni kutokana na ukweli kwamba, huruma ya Mungu ni kinga na kimbilio la maskini na wadhambi. Waamini wanaalikwa kwa namna ya pekee, kutubu na kumwongokea Mwenyezi Mungu katika maisha yao, ili waweze kupata msamaha na maondoleo ya dhambi. Huruma ya Mungu inazidi uelewa, maarifa na ufahamu wa akili ya binadamu. Katika mafunuo yake kwa Mtakatifu Sista Faustina, Bwana wetu Yesu Kristo alimwomba asali na kutafakari kuhusu Mateso yake kila alasiri saa tisa kamili saa itukumbushayo Kifo cha Bwana Msalabani. “Saa tisa kamili omba Huruma yangu, hasa kwa ajili ya wakosefu; na walau kwa muda mfupi tu jizamishe kwenye Mateso yangu, hasa pale nilipoachwa peke yangu bustanini katika saa ya masikitiko makuu, nikatoka jasho la Damu... Hii ni saa ya Huruma Kuu... Katika saa hii sitakataa ombi lolote litakaloombwa na roho yoyote kwa ajili ya Mateso yangu.” (1320). “Kila mara usikiapo saa tisa inagonga, jizamishe kabisa katika Huruma yangu; uiabudu na kuitukuza; usifu uweza wake mkuu kwa ajili ya dunia nzima, na hasa kwa ajili ya wakosefu; kwa kuwa katika saa hiyo Huruma ilifunguliwa wazi kwa ajili ya kila roho.
Ni katika muktadha huu Mama Kanisa katika sala ya mwanzo anasali hivi: “Ee Mungu mwenye huruma ya milele, unawasha imani ya taifa lako katika sikukuu hii ya Paska. Uwazidishie hiyo neema uliyowajalia, wapate wote kuelewa vyema kwamba wametakaswa kwa maji, wamepata uzima mpya kwa Roho, na kukombolewa kwa damu.” Ni katika hili tumefanywa watoto wateule wa Mungu ndivyo wimbo wa mwanzo unasema hivi; “Kama watoto wachanga waliozaliwa sasa yatamanini maziwa ya akili yasiyoghoshiwa, ili kwa hayo mpate kuukulia wokovu, aleluya” (1 Pet. 2:2). Katika ujumla wake, masomo ya dominika hii yamesheheni mafundisho msingi ya Kanisa ikiwa ni pamoja na jinsi nguvu ya imani ilivyojidhihirisha katika jumuiya ya kwanza ya wakristo, kiri kuu ya imani ya Mtume Thomaso kuwa Yesu ni mtu kweli na Mungu kweli, kuwekwa kwa sakramenti ya kitubio, vyanzo vya mafundisho ya Kanisa, na njia zinazodhihirisha uwepo wa Kristo katika maisha yetu ya kila siku. Somo la kwanza ni la Kitabu cha Matendo ya Mitume (Mdo 5:12-16). Somo hili linasimulia jinsi Kristo mfufuka alivyojidhihisha kwa ishara na maajabu aliyoyafanya kwa njia ya mitume wakiongozwa na Roho Mtakatifu na hivyo kulifanya Kanisa la kwanza kukua na kustawi kwa waamini kuishi kwa upendo wakishirikiani kwa pamoja, hata wakawa mfano wa kuigwa katika maisha ya kijumuiya. Imani yao iliwawezesha watu kumwona Kristo Mfufuka hata katika vivuli vya mitume. Ndiyo maana waliwaweka wagonjwa njiani ili kivuli cha mitume kikiwapitia waweze kupona. Ni katika imani mama Kanisa anatufundisha kuwa Kristo Yesu baada ya kufufuka, ameendelea kuwepo katika maisha yetu kwa njia ya Sakramenti zake na anaendelea kufanya kazi ya ukombozi katika nafsi ya mapadre. Imani tu yaelewa mambo haya. Waamini wenye imani juu ya uwepo wa Kristo katika nafsi ya Padre na kuwa ndiye anayeadhimisha Sakramenti katika nafsi ya Kristo, ndio wanaonufaika na kupata baraka zake.
Ni katika muktadha huu wimbo wa katikati unasema hivi; “Mshukuruni Bwana kwa kuwa ni mwema, kwa maana fadhili zake ni za milele. Israeli na aseme sasa, ya kwamba fadhili zake ni za milele. Mlango wa Haruni na waseme sasa, ya kwamba fadhili zake ni za milele. Wamchao Bwana waseme sasa, ya kwamba fadhili zake ni za milele. Walinisukuma ili nianguke, lakini Bwana akanisaidia. Bwana ni nguvu zangu na wimbo wangu, naye amekuwa wokovu wangu. Sauti ya furaha na wokovu imo hemani mwao wenye haki. Ee Bwana, utuokoe, twakusihi; Ee Bwana, utufanikishe, twakusihi. Na abarikiwe yeye ajaye kwa jina la Bwana, tumewabariki toka nyumbani mwa Bwana. Bwana ndiye aliye Mungu, naye ndiye aliyetupa nuru” (Zab. 117: 1-4, 22-27). Somo la pili ni la Kitabu cha Ufunuo (Uf 1:9-13,17-19). Somo hili linasimulia maono ya Mtume Yohane akiwa uhamishoni katika kisiwa cha Patmo siku ya Bwana – Jumapili/Dominika, siku ya ufufuko (Ufu 1:13). Yesu anajifunua kwa Yohane akisema; Usiogope, Mimi ni wa kwanza na wa mwisho na aliye hai; nami nalikuwa nimekufa, na tazama, ni hai hata milele na milele. Nami ninazo funguo za mauti na za kuzimu. Yesu anajidhihirisha kuwa ni Kuhani kwa ishara ya kanzu aliyovaa, Mfalme kwa mshipi wa dhahabu aliojifunga na hakimu kwa ishara ya vinara 7 vya moto. Kristo ni kweli Kuhani, mfalme na hakimu mwenye haki. Ufunuo huu wa Yohane ni wa kuwaimarisha wakristo waliokuwa wanateswa na utawala wa warumi na kutokana na mafundisho ya walimu wa uongo. Yohani alipata ufunuo huu kutoka kwa Yesu mwenyewe mfufuka akimwamuru aandike kitabu hiki cha ufunuo, ili kuwapa matumaini mapya na kuwatia moyo waamini ili waweze kuvumilia mateso kwa ajili ya imani yao kwake. Kumbe mapambano katika maisha ya Imani ni muhimu hatupaswi kukata tamaa kwani Kristo yuko pamoja nasi akitutegemeza.
Injili ni kama ilivyoandikwa na Yohane (Yn 20:19-31). Sehemu hii ya Injili imegawanyika katika sehemu kuu tatu. Sehemu ya kwanza Yn 20:19-25 inahusu Yesu mfufuka kuwatokea wanafunzi wake bila Tomaso na kuweka sakramenti ya kitubio. Ujumbe mkuu katika sehemu hii ni kuwekwa kwa Sakramenti ya Kitubio kwa Yesu kuwatuma na kuwaambia hivi mitume wake; “Kama Baba alivyonituma mimi, mimi nami nawapeleka ninyi…Pokeeni Roho Mtakatifu. Wowote mtakaowaondolea dhambi, wameondolewa; na wowote mtakaowafungia dhambi, wamefungiwa” (Yn.20:22-23). Namna hii Yesu aliiweka sakramenti ya upatanisho, sakramenti ya ondoleo la dhambi akiwapa Mitume na baadaye Mapadre mamlaka ya kuwaondolea dhambi wanaofanya toba ya kweli na kuomba msamaha. Naye mwenye mashaka na asiyeamini atahukumiwa, bali aaminiye ataokolewa (Mk. 16:15-16). Sehemu ya pili Yn 20:26-29 inahusu Yesu Mfufuka kuwatokea wanafunzi wake na Tomaso aitwaye Pacha akiwepo. Itakumbukwa kuwa aliposimuliwa na mitume wengine kuwa Kristo amefufuka na amewatokea hakuamini, akaapa akisema; “Mimi nisipoziona mikononi mwake kovu za misumari, na kutia kidole changu katika mahali pa misumari, na kutia mkono wangu katika ubavu wake, mimi sisadiki hata kidogo” (Yn.20:25). Yesu alipowatokea mara ya pili naye akiwapo alimwambia; “Tomaso, Lete hapa kidole chako, uitazama mikono yangu; ulete na mkono wako uutie ubavuni mwangu; wala usiwe asiyeamini, bali aaminiye” (Yn.20:27). Tomaso alikiri kiri kuu ya imani akisema; “Bwana wangu na Mungu wangu” (Yn. 20:28). Ndiyo kusema alishuhudia kuwa Kristo mfufuka ni mtu kweli na ni Mungu kweli. Naye Yesu alimwambia, “Wewe, kwa kuwa umeniona, umesadiki; wa heri wale wasioona, wakasadiki” (Yn. 20:29). Fundisho kuu tunalolipata hapa ni hili; Imani haipatikani katika kile anachoona mtu kwa macho yake. Mtu anayetaka kuona kugusa, kuonja na kuhisi katika maisha ya kihoro, mtu huyu imani yake ni ya mashaka. Ndiyo maana Yesu anasema, wamebarikiwa wale wasioona, wakaamini kwa maana imani yao ni ya kweli na haina mashaka.
Fundisho lingine tunalolipata katika sehemu hii ni kuwa tunahitaji Jumuiya, tunalihitaji Kanisa ili tuweze kukutana na kumuona Yesu Mfufuka. Ni katika maadhimisho ya kiliturujia ndipo tunapokutana na Yesu kwa njia ya sakramenti na neno la Mungu. Sakramenti na Neno la Mungu ni mali ya Kanisa – mwili wa Kristo. Ndiyo maana Tomaso alipokuwa nje ya jumuiya hakumuona wala kukutana na Yesu, na aliporudi ndani ya jumuiya alimuona na kukiri Umungu na Ubinadamu wake. Mtume Paulo anauliza: “Wataliitiaje jina lake yeye ambaye hawamwamini? Na watamwaminije yeye ambaye hawajawahi kumsikia? Na watasikiaje kama hakuna mhubiri?” (Rom 10:14). Tunaihitaji jumuiya ili kusikiliza habari za imani kwa Kristo mfufuka. Ni katika jumuiya tunaombeana, tunapata mifano kutoka kwa wengine jinsi ya kuishi imani yetu katika matendo, tunapata faida ya kuonywa na kurekebisha pale tunapokosea. Ni katika jumuiya tunapata nafasi ya kupendwa na kupenda, tunakutana na upendo wa Mungu kupitia wenzetu na sisi wenyewe tunakuwa vyombo vya Mungu kupitishia upendo wake uwafikie wengine. Kumbe wajibu wetu ni kuzifanya jumuiya zetu ziwe kweli ishara ya uwepo wa Kristo ulimwenguni ili watu wamtambue Kristo. Kama kuna shida yoyote katika jumuiya, suluhisho sio kujitenga na jumuiya, bali ni kutatua matatizo hayo. Basi kama umejitenga na Jumuiya rudi upesi, shiriki vyama vya kitume, shiriki katika shughuli za Kanisa ili ukutane na Yesu Mfufuka upate neema na baraka tele. Sehemu ya mwisho ya Injili ya dominika hii (Yn. 20:30-31) inatujulisha kuwa kuna vyanzo vingine vya Mafundisho ya Kanisa nje na Bibilia Takatifu kwa maana sio yote aliyoyafanya Kristo yameandikwa katika Biblia.
Tunasoma hivi; “Basi kuna ishara nyingine nyingi alizozifanya Yesu mbele ya wanafunzi wake, zisizoandikwa katika kitabu hiki. Lakini hizi zimeandikwa, ili mpate kuamini ya kwamba Yesu ndiye Kristo, Mwana wa Mungu; na kwa kuamini muwe na uzima kwa jina lake” (Yn. 20:30-31). Kumbe kuna mafundisho mengine ya Kanisa ambayo hayajaandikwa katika Bibilia. Haya tunayapata katika mapokeo ya mitume, mababa wa Imani na mitakuso ya Kanisa. Hivyo hatupaswi kuwa na mashaka juu ya mafundisho msingi ya Kanisa ambayo hayajaandikwa katika Bibilia Takatifu kwani hayo tunayapata katika vyanzo hivyo vingine.Basi tutambue kuwa Yesu mfufuka sasa anaishi katika maisha yetu kwa namna ambayo mifumo yetu ya fahamu haiwezi kuidhihirisha, haiwezi kuguswa kwa mikono au kuonekana kwa macho yetu ya kawaida. Imani pekee ndiyo yaweza kuelewa mambo haya, haonekani kwa macho lakini nguvu na neema zake zipo nasi daima nazo zinajidhihisha katika sakramenti zake, katika Neno lake na katika makasisi wake, katika wahitaji na wenye shida – maskini, wenye njaa, wanye kiu, wafungwa, walio uchi, wagonjwa, wenye mashaka, hofu, wasiwasi, huzuni na matatizo mbalimbali ya kimaisha. Ndiyo maana Yeye mwenyewe alisema kuwa lolote mliowatendea miongoni mwa wadogo hawa mlinitendea mimi. Basi tuombe neema na Baraka za Mungu ili tuweze kweli kumtambua Kristo Mfufuka katika maisha yetu ili tupate kustahilishwa kuurithi uzima wa milele. Ni katika tumaini hili Mama Kanisa katika sala ya kuombea dhabihu anasali hivi; “Ee Bwana, tunakuomba uzipokee sadaka za taifa lako, ili wote wanaoliungama jina lako na kubatizwa waifikie heri ya milele”. Hili litawezekana kama Kristo atakaa nasi katika mioyo yetu. Ndicho anatuombea mama Kanisa katika sala baada ya komunyo akisali hivi; “Ee Mungu Mwenyezi, tunakuomba utujalie sakramenti hii ya Paska tuliyopokea idumu katika mioyo yetu”. Na hili ndilo tumaini letu. Tumsifu Yesu Kristo.