Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko alikuwa ni shuhuda wa huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake! Apumzike kwa Amani. Baba Mtakatifu Francisko alikuwa ni shuhuda wa huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake! Apumzike kwa Amani. 

Tafakari Dominika ya Huruma ya Mungu! Ungamo la Imani

Huruma ndiyo msingi thabiti wa uhai wa Kanisa. Kazi zake zote za kichungaji zinapaswa kufungamanishwa katika upole linalouonesha kwa waamini; hakuna chochote katika mahubiri na ushuhuda wake kwa ulimwengu kinachoweza kukosa huruma. Umahiri wa Kanisa unaonekana kwa namna linavyoonesha huruma na upendo. Huruma ya Mungu inafungua malango ya moyo ili kuonesha upendo na ukarimu kwa watu wanaoishi katika upweke na pembezoni mwa jamii!

Na Padre Joseph Herman Luwela, - Vatican.

UTANGULIZI: Karibu mpenzi msikilizaji na msomaji wa tafakari ya neno la Mungu kutoka hapa radio vatican leo ikiwa ni Dominika ya Pili ya Pasaka mwaka 2025, inayojulikana pia kama Dominika ya Huruma ya Mungu, waamini wanahimizwa kutafakari juu ya huruma isiyo na kikomo ya Mungu kwa wanadamu. ‘Enyi viumbe vyote vya Bwana muhimidini Bwana msifuni na kumwadhimisha milele’ (Dan 3:57) ndio kau limbiu yetu nyakati hizi… anga linang’aa, bendera zingali zapepea, alleluia yasikika, amefufuka mzima! Huyo amwambia Mt. Yohane katika somo II (Ufu 1:9-11a, 12-13, 17-19) kuwa ndiye wa kwanza na wa mwisho, yu hai hata milele na milele, naam, astahili kuabudiwa na kutukuzwa milele, amina. Baada ya maadhimisho ya Jubilei kuu ya Miaka 2000 ya Ukristo, Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili, aliitangaza kuwa Dominika ya Pili ya Pasaka ni Dominika ya Huruma ya Mungu. Kumbe waamini waliosali Novena ya huruma tangu Ijumaa Kuu wanahitimisha leo, wanapokea rehema na kufanya matendo ya huruma. Kristo Yesu alimuahidi Mtakatifu Sr. Maria Faustina Kolowaska amani kwa ajili ya wakosefu wenye kujizamisha ndani ya bahari kuu ya huruma ya Moyo wake kwa ajili ya mateso ya Yesu huruma kwa dunia nzima.

Baba Mtakatifu Francisko alikuwa ni chombo na shuhuda wa huruma ya Mungu
Baba Mtakatifu Francisko alikuwa ni chombo na shuhuda wa huruma ya Mungu   (ANSA)

Ikumbukwe kwamba, huruma ya Mungu ni kiini cha imani, maisha na utume wa Kanisa; ushuhuda makini wa Ufufuko wa Kristo Yesu. Bikira Maria, Mama wa huruma ya Mungu awasaidie waamini: kuamini na kuyaishi yote haya kama mashuhuda wa Injili ya huruma, furaha na mapendo. Huruma ya Mungu ndiyo mahangaiko ya upendo wake kwa binadamu dhaifu na mdhambi. Mwenyezi Mungu anajisikia kuwajibika, kwa maana ya kwamba, anatamani kuwaona watu wake wakiwa na afya njema, furaha na amani tele nyoyoni mwao. Hii ni njia ambayo upendo wa huruma ya Wakristo unaopaswa pia kujimwilisha. Huruma ndiyo msingi thabiti wa uhai wa Kanisa. Kazi zake zote za kichungaji zinapaswa kufungamanishwa katika upole linalouonesha kwa waamini; hakuna chochote katika mahubiri na ushuhuda wake kwa ulimwengu kinachoweza kukosa huruma. Umahiri wa Kanisa unaonekana kwa namna linavyoonesha huruma na upendo. Huruma ya Mungu inafungua malango ya moyo ili kuonesha upendo na ukarimu kwa watu wanaoishi katika upweke na kusukumizwa pembezoni mwa jamii, ili kweli waweze kujisikia ndugu na watoto wapendwa wa Baba wa milele kama ilivyokuwa kwa Mwana mpotevu, shilingi na kondoo aliyepotea. Huruma ya Mungu inawawezesha watu kutambua na kuguswa na mahitaji msingi ya jirani zao hasa wale wanaohitaji kuonjeshwa faraja na upendo. Kimsingi, huruma ya Mungu inawawezesha waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kuwa ni vyombo na mashuhuda wa haki, amani na upatanisho.

Dominika ya Huruma ya Mungu ni chemchemi ya huruma na upendo wa Mungu
Dominika ya Huruma ya Mungu ni chemchemi ya huruma na upendo wa Mungu   (ANSA)

Kabla ya mateso, kifo na ufufuko wa Bwana ni Mtume Bartolomayo (Natanaeli) aliyeanza kumkiri Kristo kipekee akisema “Rabi, Wewe u Mwana wa Mungu, ndiwe Mfalme wa Israeli” (Yn 1:49), akafuata Mt. Petro kule Kaisaria Filipi “Wewe ndiye Kristo Mwana wa Mungu aliye hai” (Mt 16:16)… baada ya ufufuko Mt. Tomaso anaungama miguuni pa Kristo “Bwana wangu na Mungu wangu”… hivi hatupaswi kuwa na mashaka juu ya umungu wa Kristo, Mitume katika Roho Mtakatifu wamefundisha yote, muhimu ni usikivu na utendaji wa yale tuliyoambiwa na kuyasikia. “Bwana wangu na Mungu wangu…” ndio wimbo wetu leo, Kristo Mfufuka ametunyeshea mvua ya amani… ‘Amani iwe kwenu’ (Yn 20:19)… ni siku ya 8 tangu ianze Alleluia Kuu, twajionaje na hali? maisha yamebadilika? tunatembea katika upya wa ufufuko, weupe wa moyo na kweli au tungali tumejifungia ndani kwa hofu ya wayahudi? Mkristo jikusanye, inuka, jikung’ute, Bwana wako ni mzima ukaipokee amani yake… Amani hiyo i ndani ya wote waliompokea, wamefanyika watoto wa Mungu, wamezaliwa si kwa mapenzi ya mwili, wala ya mtu, bali kwa Mungu, ndio wale waliaminio Jina lake (Yn 1:12-13).

Huruma ya Mungu ni tunda la Kipasaka!
Huruma ya Mungu ni tunda la Kipasaka!

UFAFANUZI: Katika ujumbe wake wa Kwaresima 2025, Papa Francisko alisisitiza kauli mbiu "Tutembee pamoja kwa matumaini," akiwahimiza waamini kuwa mahujaji wa matumaini na kushirikiana katika safari ya imani. Alisema: "Katika kipindi hiki cha Kwaresima, ninapenda kushiriki nanyi tafakari kuhusu maana ya ‘kutembea pamoja kwa matumaini’ na wito wa uongofu ambao huruma ya Mungu inatualika kuuishi, si tu kama watu binafsi bali pia kama jamii." Masomo ya siku hii yanajikita katika huruma ya Mungu na wito wa waamini kuishi maisha yanayoakisi huruma hiyo. Katika Injili, Yesu anawatokea wanafunzi wake baada ya kufufuka na kuwapa zawadi ya amani na Roho Mtakatifu, akiwaagiza kusamehe dhambi za wengine (Yn 20:19-23). Hii inaonyesha umuhimu wa huruma na msamaha katika maisha ya Kikristo Kama vile Tomaso, akiisha kuondolewa mashaka yake haishii tu kumwona Kristo kama “Bwana” ila anaenda mbali Zaidi na kumwona kuwa ni “Mungu wake” nasi tuinue nyuso zetu, tufungue macho ya mioyo yetu na kumtambua “Seremala” huyu wa Nazareti kama Bwana na Mungu wetu, tumuabudu fudifudi, tumpokee na kuifikisha amani yake kwa wote… si busara kusema ‘Bwana wangu na Mungu wangu’ na kuendelea na maisha kama jana na juzi… Mtakatifu Tomaso alikihubiri hicho alichokiungama hadi nchi za Mashariki ya mbali kwa Waajemi hadi Uhindini (hatujui hata alifikaje kote huko) na kumwaga damu yake kwa kuchomwa mikuki na mishale kwa ajili ya ungamo lake hilo la “Bwana wangu na Mungu wangu”, sisi pengine hatuwezi kufikia kiwango hicho katika mazingira yetu ya kawaida ila tunaweza kumuungama Kristo kama Bwana na Mungu wetu katika wajibu za kawaida za kila siku tuzikitenda kwa nia njema katika jina la upendo.

Jengeni na kudumisha Ibada ya huruma ya Mungu
Jengeni na kudumisha Ibada ya huruma ya Mungu

Mtakatifu Tomaso aliona na kuamini, wanasifiwa zaidi wasioona na kuamini (Yn 20:29), imani ifungue macho ya akili zetu… Mt. Anselmo anatuhamasisha akisema ‘credo ut intelligam’ yaani naamini ili nielewe… badala ya kutanguliza akili nyingi, ubishi na kiburi kisicho na lazima kwenye mafumbo yanayozidi mno ufahamu wa kibinadamu (Intelligo ut credam yaani naelewa ili niamini) ni muhimu tuamini, naye Roho atatuongoza kuyajua hayo tuliyoyaamini... ni kwa njia ya imani akili hufunuliwa na kuelewa… Mkristo uyashike akilini mwako, yaeleze kwa midomo yako na uyatunze moyoni mwako hayo uliyoyapokea na uliyoyaamini, itakuwa heri kwako… Dominika ya Huruma ya Mungu inatualika kutafakari juu ya upendo na huruma ya Mungu kwetu, na jinsi tunavyoweza kuiga huruma hiyo kwa wengine. Katika muktadha wa Jubilei ya Matumaini 2025, tunahimizwa kutembea pamoja kwa matumaini, tukionesha huruma na msamaha kwa wale tunaokutana nao katika safari ya imani. Huruma ya Mungu inatufundisha kuwa hakuna dhambi isiyoweza kusamehewa, na kwamba tunapaswa kuwa tayari kusamehe wengine kama Mungu anavyotusamehe sisi.

Mtakatifu Faustina alipewa dhamana ya kueneza Ibada ya huruma ya Mungu.
Mtakatifu Faustina alipewa dhamana ya kueneza Ibada ya huruma ya Mungu.

“Bwana wangu na Mungu wangu…” ni ungamo muhimu katika Dominika hii ya huruma ya Mungu, tuidhihirishe huruma hiyo kwa kuhurumiana sisi kwa sisi kwa njia ya misaada ya kiutu na zaidi sana kwa kusameheana kindugu kama Mungu katika Kristo anavyotusamehe sisi kwa njia ya Upatanisho au Kitubio, ndio uwezo aliowapa Mitume leo, kuondolea au kufungia dhambi katika Roho Mtakatifu tunahitaji sana huruma yake, yale aliyoyatenda kwa mikono ya Mitume  kadiri ya somo I (Mdo 5:12-16) yaliweka msingi mwema wa Kanisa, tukiyatafakari na kuyapokea kwa mioyo mitulivu na minyenyekevu yatakuwa yetu pia nao wasioamini, wanaotaka kuona kwanza wataliamini Jina tukufu la Kristo na kumkiri pamoja na Tomaso kama Bwana na Mungu wetu. Tulio wengi tuna mengi, labda yanayotuuma zaidi kuliko yanayotufurahisha, hata hivyo hatuyasemi yaijazayo mioyo yetu na hivi tunazidi kudhoofu, tunatembea tumejeruhika… Kristo pia aliyapitia hayo na leo, tena katika kilele cha utukufu wa ushindi wake anajifunua Mitume waone na waguse alivyojeruhika ubavu, mikono na miguu yake wapate kuamini… ni fundisho kuwa ili tufahamiane, tuaminiane na tusaidiane ni lazima kuwa tayari kusaidika kwa kunyenyekea na hili linawezekana kwa kufunua ubavu, mikono na miguu yetu kama Kristo alivyofanya… tunapofunguka na kujadiliana hapo imani hujengwa, matumaini huamka, furaha hutamalaki na amani hustawai kwa kila mmoja wetu. Huruma ya Mungu ni zawadi kubwa inayotuita kuishi maisha ya: huruma, msamaha, upendo, upatanisho na matumaini, tukitembea pamoja kama jumuiya ya waamini kuelekea ukamilifu wa maisha ya Kikristo. Bwana wangu na Mungu wangu; Mungu mtu na Mkombozi wangu! Alleluia!

Dominika ya Huruma ya Mungu
26 Aprili 2025, 15:26