Tafakari Dominika ya Matawi: Mwanzo wa Maadhimisho ya Mafumbo ya Kanisa
Na Padre Pascha Ighondo, - Vatican.
Tafakari ya Neno la Mungu Dominika ya Matawi mwaka C wa Kiliturujia katika Kanisa. Dominika hii ina sura mbili - furaha na huzuni. Sura ya furaha tunaionja katika sehemu ya kwanza ya ibada ya siku hii tunapoadhimisha namna Yesu alivyoingia Yerusalemu kwa shangwe, siku sita kabla ya Pasaka. Katika kuingia kwake Yerusalemu kwa shangwe, Yesu alipanda mwanapunda, ishara ya mfalme wa amani na utakatifu wake. Nao watu walimlaki kwa shangwe wakiwa na matawi ya mitende, huku wakiimba nyimbo za furaha na ushindi wakisema: “Hosana, mwana wa Daudi; ndiye mbarikiwa, yeye ajaye kwa jina la Bwana, Mfalme wa Israeli: Hosana juu mbinguni (Mt. 21:9). Kristo Yesu ni Mfalme wa utukufu anayeingia Yerusalemu; ndiye Mbarikiwa ajaye kwa jina la Bwana. Kuingia kwa Kristo Yesu mjini Yerusalemu kunaonesha ujio wa Ufalme wa Mungu: Wa kweli na uzima, ufalme wa utakatifu na neema; ufalme wa haki, mapendo na amani. Mama Kanisa anakumbusha kwamba, maisha ya kila kiumbe yanaelekea kwenye hatima yake, yaani ufunuo wa Kristo. Sisi nasi tunafanya maandamano ya kuingia kanisani kwa shangwe tukiwa na matawi mikononi yaliyobarikiwa kama ishara ya kuingia Yerusalemu mpya, mbinguni. Ndivyo sala inayotumika kubariki matawi inavyosema: “Ee Mungu Mwenyezi wa milele, uyatakase matawi haya kwa baraka yako. Nasi tunaomfuata Kristo Mfalme kwa shangwe, utujalie tufike Yerusalemu ya milele kwa jina lake”. Maandamano haya sio ya kuiga au kurudia mambo ya kihistoria yaliyopita tu, bali ni ishara ya nje ya sisi kukiri na kuungama waziwazi kuwa Kristo aliyeteseka, akafa na kufufuka kwa ajili yetu ni Mfalme wetu.
Baada ya matawi kubarikiwa kwa kunyunyiziwa maji ya baraka, wakati huo watu wakiwa kimya wakitafakari, inasomwa Injili inayosimulia kuingia kwa Yesu Yerusalemu kwa shangwe la Kimasiha. Katika mwaka huu C wa kiliturujia tunasoma Injili ilivyoandikwa na Luka 19:28-40. Baada ya kusikiliza tafakari fupi, yanaanza maandamano kuelekea na kuingia kanisani kwa shangwe. Maandamano haya yanapaswa kupambwa kwa nyimbo za furaha na kumsifu Mungu kwa sauti kuu, kwa matendo makuu aliyotundea, tukimshangilia Yesu mbarikiwa Mfalme ajaye kwa jina la Bwana; Amani duniani na utukufu huko juu mbinguni. Katika maandamano haya mtumishi wa chetezo chenye kufuka moshi, hutangulia mbele, na nyuma yake anafuata mtumishi mwenye kuchukua msalaba uliopambwa, kati ya watumishi wawili wenye mishumaa inayowaka. Kisha anafuata Padre na watumishi wengine, na mwisho ni waamini wote wakiwa na matawi wakiimba kwa shangwe. Yesu anatuonya kuwa tusipoimba kwa shangwe na kushangilia kwa furaha au tukinyamaza, “mawe yatapiga kelele.”
Sehemu ya pili ya Ibada ya Dominika ya Matawi ni kukumbuka mateso ya Yesu Kristo yanayotuingiza katika Jumaa Kuu la kuadhimisha fumbo la ukombozi wetu, mateso, kifo na ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo, yaani Pasaka. Katika sehemu hii Kanisa linaweka mbele yetu mateso makali aliyoyapata Kristo Yesu na kutueleza mapato yake – ushindi dhidi ya dhambi na mauti unaodhihirishwa na utukufu wa ufufuko wake. Ni katika tumaini hili Mama Kanisa katika sala ya mwanzo anasali hivi; “Ee Mungu Mwenyezi wa milele, ulitaka Mwokozi wetu atwae mwili na kuteswa msalabani ili wanadamu wapate kufuata mfano wa unyenyekevu wake. Utujalie kwa wema wako tuweze kuwa na uvumilivu kama yeye, na kustahili kuishi mateso ya Yesu Kristo ambayo tunaweza kuyafahamu vizuri tu, tukiyatazama pamoja na ufufuko wake”. Kwa hiyo liturujia ya adhimisho hili imejaa mwanga wa Pasaka. Nasi tukiweka matumaini Yetu kwa Kristo Yesu, tukayaishi mafundisho yake, tutashinda na kustahilishwa kuurithi uzima wa milele. Somo la kwanza ni la Kitabu cha Nabii Isaya (Isa. 50:4-7). Somo hili linahusu utabiri wa Mtumishi wa Mungu aliye mwaminifu katika kazi yake, ambaye haogopi magumu wala mateso. Mtumishi huyu ndiye Yesu aliyevumilia mateso yote, hakuficha uso wake asipate fedheha na kutemewa mate, hakukata tamaa, bali aliwatolea watesi wake mgongo wake walipomchapa mijeledi na walipomng’oa ndevu mashavuni mwake, hakuficha uso wake. Daima alikuwa mwaminifu na msikivu kwa sauti ya Mungu wakati wote wa maisha yake. Kwa usikivu wake, alipewa nguvu na uvumilivu dhidi ya watesi wake, akapewa na uwezo wa kuwafundisha na kuwapa matumaini wanyofu, wanyonge, maskini na waliovunjika moyo. Kwa mateso yake sisi tumekombolewa kutoka utumwa wa dhambi na mauti.
Ni katika muktadha huu Zaburi ya wimbo wa katikati inasema hivi; “Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha? Wote wanionao hunicheka sana, hunifyonya wakitikisa vichwa vyao. Husema: Alimtegemea Bwana naye amponye; na amwokoe sasa, maana apendezwa naye. Kwa maana mbwa wamenizunguka, kusanyiko la waovu wamenisonga; yamenizua mikono na miguu, naweza kuihesabu mifupa yangu yote. Wanagawanya nguo zangu, na vazi langu wanapigia kura. Nawe, Bwana, usiwe mbali, Ee Mungu wangu, fanya haraka kunisaidia. Nitalihubiri jina lako kwa ndugu zangu, katikati ya kusanyiko nitakusifu. Ninyi mnaomcha Bwana, msifuni. Enyi nyote mlio wazao wa Yakobo, mtukuzeni” (Zab. 22:1, 7-8; 16-17a; 18-19; 22-23). Nasi tukimtumaini Mungu, tukalisikiliza Neno lake, tukalitii na kuliishi, hakika tutakapomlilia, atasikia kilio chetu na kutuokoa. Somo la Pili ni la Waraka wa Mtume Paulo kwa Wafilipi (Flp 2:6-11). Somo hili linaweka wazi matunda ya utii, unyenyekevu na uvumilivu wa Yesu Kristo, mtumishi mwaminifu wa Mungu – wokovu wa mwanadamu naye Yesu kuwekwa mfalme wa Mbingu na dunia. Maandiko matakatifu yanasema kuwa, dhambi na mauti viliingia katika historia ya mwanadamu kwa kosa la wazazi wetu wa kwanza, Admu na Eva, kukosa utii kwa Mungu. Lakini kwa utii wa Kristo Yesu, dhambi na mauti vimeangamizwa. Kwa kutotii kwa Adamu na Eva tulitengwa na Mungu, kwa kutii kwake Kristo tumeunganishwa na Mungu. Nasi tunapaswa kutii amri za Mungu na za Kanisa, kutii mafundisho ya Kanisa, kuwatii na kuwasikiliza viongozi wa Kanisa, ili tupate kustahilishwa kuurithi uzima wa milele. Hata waswahili hutuonya wakisema; “Asiyesikia la mkuu huvunjika guu”. Basi tujikubali kuwa sisi kwa asili tu binadamu. Lakini tusiung’ang’anie kwa nguvu ubinadamu wetu bali tuuachilie, tujitwalie hali ya kimungu kwa kuwa wana wake Mungu ili tukaishi naye milele yote mbinguni.
Injili ni kama ilivyoandikwa na Luka (Lk. 22:14; 23:56). Sehemu hii ya Injili ndiyo kiini cha maadhimisho ya dominika hii nayo inasimulia mateso ya Bwana wetu Yesu Kristo. Ikumbukwe kuwa siku ya Dominika ya Matawi Injili inasomwa pasipo mishumaa wala chetezo na bila utangulizi wala ishara ya msalaba. Nayo husomwa na shemasi baada ya kuomba na kupokea baraka ya Padre. Na kama hakuna shemasi husomwa na Padre. Lakini ili kuipamba liturujia hii, Injili husomwa na walei kwa kuimba, ili kuweze kuwa na uwakilishi wa wahusika katika simulizi hili. Lakini sehemu ya Kristo lazima isomwe au kuimbwa na Padre. Simulizi hili linatuambia kuwa Yesu alikamatwa akiwa bustanini Gethsemane akisali. Naye bila ubishi alikubali kukamatwa, akahukumiwa, na kuanza safari ya ukombozi kuelekea Golgota kusulubiwa. Safari hii ilikuwa na mateso makali sana: alibebeshwa msalaba mzito, alifanyiwa dhihaka, alipigwa mijeledi, akavuliwa nguo, akatemewa mate, akatukanwa, akasulubiwa msalabani, na hatimaye akafa, kwa sababu ya dhambi zetu na kuonekana kuwa mtu aliyelaaniwa na Mungu (Kum. 21:22-23). Lakini kwa kifo chake kilivyokuwa cha pekee, dunia ilitetemeka, jua lilififia, kukawa giza juu ya nchi, pazia la hekalu likapasuka mara mbili. Naye alipochomwa ubavu kwa mkuki, vilitoka damu na maji, ndizo chemichemi za Sakramenti za Kanisa. Nao walioshuhudia walisadiki uaguzi wa manabii na kusema, “hakika huyu alikuwa mwana wa Mungu.”
Katika simulizi hili sauti za umati wa watu husikika wakipiga makelele wakisema: Asulubishwe! Asulubishwe! Nasi kwa mawazo, maneno na matendo yetu maovu, na kwa dhambi zetu tunatoa mlio na makelele hayo hayo tukisema: Msulubishe! Msulubishe! Petro alijaribu kupambana na nguvu za giza kwa upanga. Je, sisi hatuna fikra kama za Petro za kupambana na nguvu za shetani na ibilisi kwa upanga wa giza, maseng’enyo, malumbano, mapigano, visasi na fitina? Je, hatusemi kila siku katika makundi ya watu; Msulubishe! Msulubishe! Mwondoshe! Mwondoshe! Tukumbuke kuwa hatupaswi kumpigania Kristo kwa upanga bali kwa ushuhuda wa maneno na matendo mema. Tuige mfano wa Kristo Yesu, Bwana, Mwalimu na Mkombozi wetu aliyepambana na kumshinda shetani si kwa upanga na vitisho bali kwa uvumilivu, unyenyekevu, upole na utii wake kwa Mungu Baba. Yuda alimsaliti Yesu kwa busu, alama na ishara ya upendo, Petro naye alimkana mara tatu, nao Mitume wengine, walimkimbia. Sisi nasi tunafanya mambo haya haya, tunamsaliti, tunamkana na kumkimbia Yesu Kristo, kila tunapoionea aibu Injili, tunaporudi nyuma kiimani na kukosa matumaini kwake kwa sababu ya magonjwa na matatizo ya kimaisha hata kutafuta suluhu katika dhambi. Jogoo amekwisha kuwika mara ya tatu, tunaalikwa kujirudi, tujiweke chini ya Msalaba wa Kristo, kwani hatuna tumaini lingine, japo kwao wanaopotea Msalaba ni kikwazo na upuuzi, kwetu sisi ni nguvu ya Mungu, alama na bendera ya ushindi, kama tukiutazama kwa imani na moyo wa toba.
Basi katika Juma Kuu linalofunguliwa na Dominika ya Matawi, tuombe neema ya kuwa wasikivu na watii, tujipatanishe na Mungu ili tuweze kuifurahia Pasaka, ufufuko wa Bwana, na baada ya maisha ya hapa duniani, tukastahilishwe kufurahi naye Mbinguni. Ni katika tumaini hili mama Kanisa katika sala ya kuombea dhabihu anasali hivi; “Ee Bwana, utujalie rehema yako kwa ajili ya mateso ya Mwanao wa Pekee. Basi ingawa hatustahili kitu kwa matendo yetu, tuipate rehema yako kwa ajili ya sadaka hii kubwa”. Nao utanguliza wa Dominika hii unaliweka wazi tumaini hili ukisema; “Yeye, ingawa hakuwa na kosa, alikubali kuteswa na kuhukumiwa pasipo haki kwa ajili ya wakosefu. Amefuta dhambi zetu kwa kifo chake na kutufanya wenye haki kwa ufufuko wake”. Na katika sala baada ya Komunio mama Kanisa anahitimisha maadhimisho ya dominika hii akisali: “Ee Bwana, sisi tulioshiba mapaji yako matakatifu umetupa tumaini la kupata hayo tunayoamini kwa ajili ya kifo cha Mwanao. Tunakusihi, hapo atakapofufuka utufikishe huko tuendako”. Na hili ndilo tumaini letu. Tumsifu Yesu Kristo!