Tafuta

Dominika ya Matawi, Mama Kanisa anakumbuka siku ile Kristo Yesu, alipoingia mjini Yerusalemu kwa shangwe kama Mfalme na Masiha na kushangiliwa kama Mwana wa Daudi anayeleta wokovu. Hii ndiyo maana ya wimbo wa Hosana. Dominika ya Matawi, Mama Kanisa anakumbuka siku ile Kristo Yesu, alipoingia mjini Yerusalemu kwa shangwe kama Mfalme na Masiha na kushangiliwa kama Mwana wa Daudi anayeleta wokovu. Hii ndiyo maana ya wimbo wa Hosana.   (Vatican Media)

Tafakari Dominika Matawi: Mwanzo wa Maadhimisho ya Juma Kuu!

Dominika ya Matawi, Mama Kanisa anakumbuka siku ile Kristo Yesu, alipoingia mjini Yerusalemu kwa shangwe kama Mfalme na Masiha na kushangiliwa kama Mwana wa Daudi anayeleta wokovu. Hii ndiyo maana ya wimbo wa Hosana. Ni Mfalme wa utukufu anayeingia Yerusalemu akiwa amepanda Mwana punda na kushangiliwa na Wayahudi kama kielelezo cha amani na unyenyekevu wake. Kristo Yesu ndiye Mbarikiwa ajaye kwa jina la Bwana. Mateso, Kifo na Ufufuko!

Na Padre Joseph Herman Luwela, - Vatican.

UTANGULIZI: Karibu mpenzi msikilizaji na msomaji wa tafakari ya Neno la Mungu kutoka hapa Radio Vatican leo ikiwa ni Dominika ya Matawi, mwanzo wa maadhimisho ya Juma Kuu, Mama Kanisa anapoadhimisha Mafumbo ya Wokovu wa binadamu yanayofumbatwa katika mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu; ufufuko uletao wokovu na maisha ya uzima wa milele. Hiki ni kiini cha maadhimisho ya Mwaka wa Liturujia wa Kanisa. Waamini wanaliishi Fumbo hili kila wakati wanapoadhimisha Fumbo la Ekaristi Takatifu, chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa. Ibada ya Misa Takatifu inapyaisha Fumbo la Pasaka yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu. Hii ni Njia ya Msalaba kuelekea Mlimani Kalvari. Dominika ya Matawi, Mama Kanisa anakumbuka siku ile Kristo Yesu, alipoingia mjini Yerusalemu kwa shangwe kama Mfalme na Masiha na kushangiliwa kama Mwana wa Daudi anayeleta wokovu. Hii ndiyo maana ya wimbo wa Hosana. Ni Mfalme wa utukufu anayeingia Yerusalemu akiwa amepanda Mwana punda na kushangiliwa na Watoto wa Wayahudi kama kielelezo cha amani na unyenyekevu wake. Kristo Yesu ndiye Mbarikiwa ajaye kwa jina la Bwana. Liturujia ya leo inaeleza yote, kila tendo katika maadhimisho haya linahubiri kwa sauti kuu... matawi tuliyoshika, maandamano tuliyofanya, hossana tuliyoiimba na historia ya mateso ya Kristo Yesu tuliyosomewa vinatosha kutuweka sawa... tuseme nini basi? Tunaalikwa kushangaa, halafu kumakinika, kusikia na kutenda kadiri ya mapenzi yake sababu pamoja tutafakari pamoja neno hili kwa matumaini hasa  “Bwana ana haja nasi.” Katika muktadha wa Jubilei ya Matumaini, tafakari hii inatufundisha kuwa, ingawa watu walimlaki Yesu kwa furaha, walikuwa bado hawajamfahamu kikamilifu na hivyo walikuwa wanategemea wokovu wa kisiasa. Hata hivyo, Jubilei ya Matumaini inatufundisha kuwa wokovu wa kweli unapatikana kwa njia ya Fumbo la Pasaka yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kwa wafu. Furaha ya wokovu inaanza kwa kutambua kuwa Kristo alikubali mateso kwa ajili ya ulimwengu, na kwa njia hii, tunaweza kuwa na matumaini ya uzima wa milele.

Dominika ya Matawi: Kristo Yesu Mfalme na Masiha wa Bwana
Dominika ya Matawi: Kristo Yesu Mfalme na Masiha wa Bwana   (Vatican Media)

UFAFANUZI: Kristo Yesu alipokaribia Yerusalemu aliagiza aletewe punda, akasema mkiulizwa mbona mnamfungua jibuni “Bwana ana haja naye.” Punda ni mpole, wayahudi walimtumia kwa uchukuzi na kilimo, alitunzwa na kunawiri, nyumba ya punda ilikuwa safi na hata mtu aliweza kulala humo bila shida... Viongozi na watu mashuhuri walipanda farasi, mnyama wa fahari mwenye mbio na nguvu za kutosha, apitapo wote hupisha, farasi anavutia, analeta raha... Kristo hakuwa na haja na huyo bali mwanapunda atufunze unyenyekevu... Somo I (Isa 50:4-7) linaonesha “BWANA alivyo na haja na mtumishi wake”.. mtumishi huyo si mkaidi, anawatolea mgongo wampige, anang’olewa ndevu kwa dhihaka, anatemewa mate na kufedheheshwa, lakini amekaza uso kama gumegume, misheni lazima itimizwe, anaamini Mungu atamsaidia. Nalo somo II (Flp 2:6-11) linaonesha “BABA ana haja na MWANA” na hivi anamtuma ulimwenguni kwa kazi maalumu. Mwana haoni kuwa sawa na Mungu ni “dili” sana, anajinyenyekeza na kutwaa hali dhaifu ya ubinadamu, anaishi kama sisi (isipokuwa dhambi) akiitii haja ya Baba hata mauti ya Msalaba. Historia ya mateso tuliyosomewa (Lk 22:14-23:56) inathibitisha Mwana anavyoitimiza Haja ya Baba.  Ni ajabu kuteseka hivi kwa ajili ya watu wengine... kwa myahudi ni kashfa kusikia mfalme anateswa hivi wengi walikata tamaa na kumuona Yesu wa kawaida, janjajanja tu na sio Mwana wa Mungu...  Iweje Mfalme ateswe? Kwa tendo hilo wayahudi wengi hawakuimarishwa na mateso ya Yesu isipokuwa wachache waliojaliwa.

Dominika ya Matawi: Fumbo la Pasaka: Mateso, kifo na ufufuko.
Dominika ya Matawi: Fumbo la Pasaka: Mateso, kifo na ufufuko.   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

“Bwana ana haja naye”... ndio, kila mmoja kwa namna yake, tunaitikiaje haja hiyo ya Mungu? Ni kwa kuwa kama Yeye tukiiga tabia zake na kutenda anavyotamani tutende, kumsindikiza na matawi yetu tukivumisha “hossana Mwana wa Daudi” iliyo shangwe ya sherehe, mlio wa baraka, utenzi wa sifa na shukrani... kwa matawi haya tunakumbushwa ukuu wa Mungu katika Kristo, yanatutafakarisha sadaka ya Kristo msalabani, yanatuhamasisha kumsifu na kumshukuru Mungu kwa zawadi ya ukombozi tukitazamia kwa hamu kufikia kiti cha enzi cha Mwanakondoo na kumshangilia na matawi ya mitende (Ufu 7:9) Katika ujumbe wa Kwaresima kwa 2025, tunahamasishwa kutambua kwamba wokovu wa kweli haupatikani kwa njia za kisiasa au za kimwili pekee, bali kupitia mateso na kifo cha Yesu. Huu ni muda wa kujiandaa kumfuata Yesu katika njia ya mateso, na kutafakari jinsi tunavyoshirikiana katika mateso yake kwa kutubu na kuishi kwa wema. Kwaresima inatufundisha kuhusu umuhimu wa kuchukua msalaba wetu na kumfuata Yesu kwa imani. Hii ni njia ya kushiriki katika furaha ya ufufuo wake. Tuambatane na Kristo hatua kwa hatua kuanzia kwenye lango la Yerusalemu hadi hekaluni kusafisha hekalu (miili yetu) lililogeuzwa pango la wanyang’anyi (Lk 19:45-46) halafu tunapanda naye chumba cha juu kupokea zawadi ya Ekaristi tak, Daraja ya Upadre na amri mpya ya mapendo, tutashuka naye Getsemane na kukesha naye (Mk 14:37), anapokamatwa tusimkimbie twende naye barazani (Praetorium) tukifuatilia mwenendo wa kesi, tupandishe naye Kalvari, tufe pamoja naye na tuzikwe ndani ya kaburi lile jipya, halafu waoo, kwa utukufu mkuu tufufuke pamoja naye.

Dominika ya Matawi: Fumbo la Pasaka: Mateso, kifo na ufufuko.
Dominika ya Matawi: Fumbo la Pasaka: Mateso, kifo na ufufuko.   (Vatican Media)

“Bwana ana haja naye”... heshima ya punda ilitokana na Kristo aliyekuwa juu yake, tunapata heshima sababu ya Yesu tuliyembeba, tukimtua tu yote ni bure... Baba ni punda, familia yake inamuheshimisha nasi tunampungia matawi ya mitende, asipoibeba atadharaulika... Mama ni punda msaidizi anayefanana na Punda baba (Mwz 2:18) na Bwana ana haja naye, hossana anayoimbiwa inatokana na Kristo aliyembeba yaani mumewe na wana na binti zake, akiwatua hao na kuishi tu mradi siku zinaenda hatapata heshima ya mke mwema aliye kielelezo cha Mama Kanisa Mtakatifu... Vijana nao ni punda “Bwana ana haja nao” hapo walipo, muda huu.. wasimshushe, waandae maisha yao wakipigania ndoto zao njema, wasishabikie yasiyo na maana, matumaini ya Kanisa na jamii yamo ndani mwao... “Bwana ana haja na watoto wetu”, watafaulu kutimiza haja hiyo wakilelewa vema kwa mifano mizuri ya wakubwa wao, tuwafundishe ujasiri, tusiwajaze hofu zisizo na maana, tuwaambie ukweli wa dunia hii, nao kwa wakati wao wataifikisha ‘haja ya Bwana’ kwa watu wote. Pasaka ya Kristo na yetu i mlangoni... Je, sisi kama punda wa Kristo tunayo afya japo kidogo? tujihadhari asipande juu ya migongo michafu yenye kupe bali tujitahidi kuwa punda wenye afya njema, wazuri, wasafi, wapole, wanyenyekevu, wasamehevu naye Mungu atatubariki... Hili linadai toba na msamaha, kutimiza wajibu, mahusiano mema, fadhila za upole, unyofu na unyenyekevu... Dominika ya Matawi inatufundisha kuwa wokovu wa kweli unapatikana kupitia njia ya mateso, kifo na ufufuo wa Kristo. Jubilei ya Matumaini inatufundisha kuwa, ingawa njia ya wokovu ni ngumu, Kristo ametufungulia njia ya matumaini na furaha ya uzima wa milele. Katika kipindi cha Kwaresima, tunaitwa kujiandaa kumfuata  KristoYesu kwa toba na wongofu wa ndani, ili kumtumikia kwa unyenyekevu, huku tukitafakari kuhusu mateso yake kwa ajili yetu.  Mkristo, “Bwana ana haja nawe” leo na siku zote, Amina.

Liturujia Matawi 2025
12 Aprili 2025, 16:09