Tafakari Dominika ya Matawi: Utii Na Unyenyekevu Wa Kristo Yesu
Na Padre Bonaventura Maro, C.PP.S., -Kolleg St. Josef, Salzburg, Austria.
Utangulizi: Wapendwa Taifa la Mungu, Dominika ya Matawi, tarehe 13 Aprili 2025 ni mwanzo wa maadhimisho ya Juma Kuu, Mama Kanisa anapoadhimisha Mafumbo ya Wokovu wa binadamu yanayofumbatwa katika mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu; ufufuko uletao wokovu na maisha ya uzima wa milele. Hiki ni kiini cha maadhimisho ya Mwaka wa Liturujia wa Kanisa. Waamini wanaliishi Fumbo hili kila wakati wanapoadhimisha Fumbo la Ekaristi Takatifu, chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa. Ibada ya Misa Takatifu inapyaisha Fumbo la Pasaka yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu. Hii ni Njia ya Msalaba kuelekea Mlimani Kalvari. Dominika ya Matawi, Mama Kanisa anakumbuka siku ile Kristo Yesu, alipoingia mjini Yerusalemu kwa shangwe kama Mfalme na Masiha na kushangiliwa kama Mwana wa Daudi anayeleta wokovu. Hii ndiyo maana ya wimbo wa Hosana. Ni Mfalme wa utukufu anayeingia Yerusalemu akiwa amepanda Mwana punda na kushangiliwa na Watoto wa Wayahudi kama kielelezo cha amani na unyenyekevu wake. Kristo Yesu ndiye Mbarikiwa ajaye kwa jina la Bwana. Kwa kuadhimisha Dominika ya Matawi, Kanisa linatuingiza katika maadhimisho ya Juma Kuu, tukikaribia sasa katika adhimisho la Fumbo la Pasaka, yaani mateso, kifo na ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo. Liturujia nzima ya Dominika ya Matawi inatutafakarisha sisi sote juu ya, “Unyenyekevu na utii wa Kristo Yesu katika kutimiza mapenzi ya baba” Kristo licha ya kuwa tangu Mwanzo alikuwa yu na namna ya Mungu (Flp 2:6-11), alijinyenyekeza, akawa mtii hata mauti ya msalaba kwa ajili ya kuuletea ulimwengu ukombozi wa milele. Dominika ya Matawi hufahamika pia kama Dominika ya Mateso yaani “Passion Sunday”, tukitambua kuwa ni baada ya tukio hilo ndipo tunaingia rasmi katika Juma kuu, tukitafakari juu ya safari ya mwisho ya Bwana wetu Yesu Kristo kuelekea katika mateso yake. Neno Passion latokana na Neno la Kiebrania “Pasha” yaani “Pasaka”, ambapo Wayahudi walikumbuka kuondoka kwao kutoka utumwani Misri (Passover) na kuanza safari ya ukombozi kueleka Nchi ya Ahadi.
Kwetu sisi Dominika hii ina maana gani? Ni kwa njia ya Mateso, kifo na ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo ndipo nasi sote tunaondolewa kutoka katika utumwa wa dhambi na tunashiriki katika maisha mapya ya uzima wa milele mbinguni, ndiyo Pasaka yetu sisi taifa jipya la Mungu. Kwa hivyo, sisi hatuadhimishi Dominika hii kama njia ya kuiga ama kurudia mambo ya kihistoria kama tutakavayosikia katika somo la Injili isomwayo kabla ya maandamano (Yn 12:12-16), bali ni kule kumwungama Kristo aliyekufa na kufufuka kwa ajili yetu sisi, kunakofanywa na umati huu wa watu katika Dominika hii. Mama Kanisa hutuonesha katika masomo ya Misa ya Dominika hii kwamba, njia ya Kristo ndiyo njia yetu sisi pia. Kanisa huweka pia mbele ya macho yetu mateso makali aliyoyapata Yesu, lakini hutueleza pia mapato yake, ndio utukufu wa ufufuko. Sisi tumekubali njia hii na katika maandamano tulimwahidi Kristo kumfuata. Katika juma kuu tunaalikwa kutimiza ahadi hii ya kumfuata Kristo kwa kushiriki kwa moyo maadhimisho ya kipasaka ambamo tunazamishwa katika tafakari ya kina juu ya mateso, kifo na kufufuka kwake Bwana wetu Yesu Kristo. Katika Dominika ya Matawi, tumwombe Yesu atupe nguvu si tu ya kumshangilia kama Masiha na Mfalme wetu, bali kwa Imani thabiti, unyenyekevu na utii kumkiri, kumpokea na kutembea naye katika njia yake ya Msalaba. Yeye mwenyewe aliwafundisha wafuasi wake na anatufundisha sisi sote kwamba, “Mtu yeyote akitaka kuwa mfuasi wangu, ni lazima ajikane nafsi yake, auchukue msalaba wake kila siku, anifuate” Lk 9:23-25. Tuombe Neema ya kuwa watii katika kutimiza mapenzi ya Mungu kwa ajili ya wokovu wetu na wokovu wa wengine.
Somo la 1: Ni kitabu cha Nabii Isaya 50:4-7. Somo la kwanza tulilolisikia, ni moja kati ya Nyimbo nne za Mtumishi wa Bwana katika kitabu hiki cha Nabii Isaya. Na sehemu hii ni wimbo wa tatu wa Mtumishi wa Bwana (Isa 50:4-10). Nabii Isaya arudia tena kutueleza, kwanza, juu ya wito wa Mtumishi wa Bwana, kuwa ni kutoka kwa Mungu mwenyewe. Pili, ni Mungu ndiye aliyemwimarisha kwa ajili ya utume wake, kwa Hekima ya Kimungu na uwezo wa kunena. Tatu, Uaminifu wa Mtumishi wa Bwana katika kutimiza utume wa Mwenyezi Mungu. Nne, Uvumilivu, uaminifu na utii Mtumishi wa Bwana. Mtumishi huyu si mwingine bali ni Bwana wetu Yesu Kristo, Masiya na mkombozi wa ulimwengu ambaye tunaingia katika Tafakari juu ya utimilifu wa wito na utume wake kwa maadhimisho ya Fumbo la Pasaka. Ndugu zangu katika somo hili la kwanza tuna mambo manne ya kujifunza: Kwanza: Wito wa Mtumishi wa Bwana, umeotoka kwa Mungu Mwenyewe, ndiyo wito wetu pia (The Vocation of the Servant of the Lord). Mtumishi wa Bwana anasema, “Bwana Mungu amenipa ulimi wa hao wafundishwao, nipate kujua jinsi ya kumtegemeza yeye aliyechoka” (Isa 50:4). Nabii Isaya anaturudisha tena kutafakari juu ya wito wa mtumishi mwaminifu wa Mungu. Ni Mungu ndiye aliyemwita kwa ajili ya kuifanya kazi yake, ni wito wa kinabii. Ndugu wapendwa, Mtumishi huyu Mwaminifu wa Bwana ndiye Bwana wetu Yesu Kristo ambaye alikubali wito wa Baba wa kuja kututangazia sisi sote Habari Njema ya Injili. Wito wa mtumishi huyu wa Bwana utukumbushe juu ya wito wetu sisi sote, kwamba tunatumwa kwenda kutangaza habari Njema kwa wengine kwa njia ya maneno, matendo na kwa maisha yetu yote. Kila mmoja wetu ajiulize katika wito ambao Mwenyezi Mungu ameniita au amekuita, nimekuwa mjumbe wa habari Njema? Nimekua mjumbe wa furaha, upendo, amani, wema, sadaka, upatanisho, huruma, uaminifu nk?
Tumwombe Yesu ambaye alipokea wito wa Mungu na kwa uaminifu mkubwa akawa mjumbe wa Habari Njema, nasi sote tuwe tayari kupokea wito wa Mungu na kuwa wajumbe wa Habari Njema kwa wengine. wagonjwa, maskini, wajane, waliodhulumiwa, waliokata tamaa, waliodharauliwa na watu, wanaoonekana hawana thamani katika jamii zetu, waliopoteza matumaini nk. Hii ni kazi ya kinabii, kikuhani na kifalme ambayo kila mmoja wetu anaishirikishwa kwa njia ya ubatizo wetu. Pili: Mtumishi wa Bwan ameimarishwa na Mungu Mwenyewe, nasi tumeimarishwa katika miito yetu (equipped by the Lord). “Bwana Mungu huniamsha huniamsha asubuhi baada ya asubuhi huniamsha sikio langu lipate kusikia kama watu wafundishwao” Nabii Isaya anatuambia kuwa Mtumishi huyu Mwaminifu wa Bwana ameimarishwa na Mungu ili aweze kuitenda kazi yake. Mtumishi huyu kwa kuimarishwa huko, alikwa mwaminifu wakati wote. Ndugu wapendwa, kila mmoja wetu kwa njia ya ubatizo amepewa wito na Mungu. Lakini kwa njia ya Sakramenti ya Kipaimara tumepokea Roho Mtakatifu, tumeimarishwa ili tuweze kwa uaminifu na uvumilivu kuishi vyema wito wetu kama Wafuasi wa Kristo kila mmoja kadiri ya hali yake. Hiyvo ni Roho Mtakatifu anayetupa nguvu za kumtangaza na kumshuhudia Yesu katika maisha yetu ya kila siku. Anatupa nguvu za kuvumilia katika changamoto mbalimbali tunazokutana nazo katika maisha yetu ya wito, ndoa takafu, Daraja Takatifu na katika utawa. Kila mmoja anapitia changamoto kwa namna yake. Katika yote, Roho Mtakatifu anatupa nguvu ili daima mapenzi ya Mungu yatimizwe katika maisha maisha yetu ya ushuhuda kwa wengine. Tumruhusu Roho Mtakaifu atende kazi ndani mwetu daima, atufundishe namna ya kutenda na kuwaza katika kumtumikia kwetu Mungu.
Tatu: Uaminifu na utii wa Mtumishi wa Mungu, ndio uaminifu wetu pia katika kumtumikia Mungu na wenzetu (Faithfulness of the Servant of God). Bwana Mungu amenizibua sikio langu wala sikua mkaidi, wala sikurudi nyuma (Isa 50:5). Nabii Isaya anatuonesha utii na uaminifu wa Mtumishi Mwaminifu wa Mungu. Ndiye Bwana wetu Yesu Kristo ambaye alikua Mwanamifu na mtii hata mauti ya msalaba (Fil 2:6-11). Ndugu wapendwa, Mtumishi mwaminifu wa Mungu anaonesha kutopinga wala kuwa mkaidi kwa Mapenzi ya Mungu. Pili anaonesha pia uaminifu kwa Mungu Baba katika kutimiza wito wake. Mimi na wewe tunapoingia kwa namna ya pekee katika juma hili kuu, tumwombe Mungu atusaidie ili nasi tuwe waaminifu na watii katika kutimiza mapenzi ya Mungu. Yesu alikubali kuacha enzi na utukufu Mbinguni akatii na kuja kukaa kati yetu sisi wadhambi, nasi tuwe tayari kuingia katika uhalisia wa maisha ya watu wengine. Tunaishi katika ulimwengu ambapo uaminifu unapotea siku baada ya siku. Kumekua na maelekeo ya ubinafsi, kila mmoja anajali kwanza nafsi yake. Tupo katika ulimwengu ambapo tumekosa ile hali ya kujali maumivu na mateso ambayo kwa namna moja au nyingine tunaweza kuwasababishia wengine, katika familia zetu, katika biashara zetu, katika jumuiya zetu za kitawa, katika maeneo yetu ya kazi nk. Kumekua na maelekeo ya kutafuta faida binafsi, hata kwa kukwepa kutimiza nyajibu zetu mbalimbali zanazotudai uwajibikaji wetu. Pasaka hii itukumbushe na iturudishe kwenye mstari pale ambapo tulishindwa kutimiza kwa uaminifu nyajibu zetu mbalimbali. Tunaishi katika ulimwengu ambapo tushindana ili kupata nguvu na mamlaka, tamaa ya mali na utajiri wa haraka hata kwa kuwaumiza na kuwaonea wanyonge na maskini. Tuombe neema ya kuwa waaminifu kila mmoja kwa mambo madogo nasi tutawekwa juu ya mengi.
Nne: Uvumilivu wa Mtumishi wa Bwana, nasi tuvumilie nyakati za changamoto katika miito yetu (perseverence of the Lord’s Servant). Mtumishi wa Mungu anasema, “Sikuficha uso wangu usipate fedheha na kutemewa mate. Maana Bwana Mungu atanisaidia, kwa sababu hiyo sikutahayari, kwa sababu hiyo nimekaza uso wangu kama gumegume nami na jua ya kuwa sitaona haya” Isa 50:7. Mtumishi mwaminifu wa Bwana alimtumainia Bwana hata nyakati za mateso. Bwana wetu Yesu Kristo hakukata tamaa, alimtumaini Mungu hata kuikabidhi roho yake mikononi mwa Baba. Ndugu wapendwa, tunapata daima nguvu, tunapotambua kuwa tunatembea na Yesu ambaye kwa unyenyekevu mkubwa alikubali mateso yote na kifo ili sisi tuupate ukombozi wa milele kutoka katika utumwa wa dhambi na mauti. Yesu amekaza uso wake kama gumegume, hili lilikua ni jiwe gumu ambalo halikuweza kupasuka kwa urahisi, ishara ya ustahimilivu na udumifu katika mateso. Kuna nyakati, tunapita katika changamoto mbalimbali katika maisha yetu ya kila siku. Katika yote tunapaswa kutambua kuwa njia ya Yesu ndiyo njia yangu mimi na wewe. Tunapaswa kukaza uso kama gume gume, yaani kuwa wavumilivu na wadumifu katika imani yetu hata tunapopita katika nyakati ngumu na za changamoto nyingi. Kamwe usimwache Yesu, mshirikishe Yesu msalaba wako, beba naye msalaba wako, unapoanguka, simama tena mpaka uufikie uzima wa milele. Yesu nipe ujasiri wa kuwa imara katika imani yangu, katika kukufuata katika njia yako. Huenda katika upadre wangu kuna nyakati napoteza matumaini, napaswa kumwangalia Yesu pale msalabani, huenda katika ndoa yako umepoteza matumaini, mtazame Yesu msalabani, huenda katika utawa umepoteza matumaini, mtazame Yesu pale Msalabani, huenda katika katika wito wako huoni njia tena mbele. Yesu amefungua mikono kunipokea mimi na wewe, amefungua moyo wake ili sisi sote tupate kimbilio na ulinzi thabiti, ameinamisha kichwa kuniangalia mimi na wewe ili nasi tumwangalie uso wake wenye huruma. Tusite tamaa katika changamoto zetu, jipe moyo, inuka anakuita.
Somo la Injili: Ni Injili kama ilivyoandikwa na Luka 22:14; 23:56. Somo la Injili Takatifu ni simulizi ndefu ya Mateso ya Bwana wetu Yesu Kristo. Katika simulizi hili tunaona jinsi utabiri wa Yesu juu ya kuhukumiwa na wakuu wa makuhani na waandishi, kuteswa na kufa msalabani. Alikwishawaambia mara kadhaa mitume wake kuhusu utimilifu wa utume na kazi ya Baba aliyokuja kuifanya ya kuuleta ulimwengu ukombozi wa milele. Mwinjili Luka anatualika kutafakari kila mmoja maisha yake katika mwanga wa wahusika mbalimbali katika simulizi hili la mateso ya Bwana wetu Yesu Kristo. Katika somo hili la Injili Takatifu, tutawatafakari wahusika wafuatao katika Mateso ya Bwana wetu Yesu Kristo. Kwanza: Bwana wetu Yesu Kristo, Masiha Mtii na Mnyenyekevu. Bwana wetu Yesu Kristo aliingia Yerusalemu akiwa amepanda mwanapunda (Luka 19:28-40), na watu walimshangilia, Hosana Mwana wa Daudi. Mwanapunda ni ishara ya unyenyekevu, akitimiza utabiri wa Nabii Zakaria 9:9, “Furahi Ee Binti Sayuni, piga kelele Ee Binti Yerusalemu; Tazama Mfalme wako anakuja kwako...ni Mnyenyekevu, amepanda mwanapunda” Kwa utii na unyenyekevu alikubali mateso na kifo na aliwasamehe wote waliomshitaki. Unyenyekevu: Bwana wetu Yesu Kristo anatufundisha unyenyekevu katika kutumikia. “Anayetaka kuwa mkubwa kwenu na awe mtumishi wenu na mtu yeyote anayetaka kuwa wa kwanza kwenu na awe mtumwa wa wote” (Mt 20:26-28). Katika karamu ya Mwisho alijitoa yeye mwenyewe kama chakula, ndio Ekaristi Takatifu. Lakini kubwa zaidi akawaosha mitume wake miguu yao. Yesu anatualika tuwe wanyenyekevu katika kutumikiana sisi kwa sisi, kila mmoja amwone mwenzake kuwa ni bora kuliko nafsi yake mwenyewe. Katika familia zetu, katika jumuiya zetu, katika nyadhifa mbalimbali tulizopewa kwa niaba ya watu, kila mmoja amwone mwenzake kuwa ni bora kuliko nafsi yake mwenyewe. Msahemevu: Yesu anatufundisha kuwasamehe wengine, waliotuumiza, waliotukwana, walitudharau, waliotunenea mabaya nk. Tupande na kustawisha ndani mwetu roho ya kuwa tayari kusamehe na kuwachilia. Yesu alisema, Baba uwasamehe kwa maana hawajui watendalo. Tuomwombe Yesu atupe roho ya kuwasamehe wengine na kutokuwabeba ndani ya mioyo yetu. Mtiifu: Yesu anatufundisha kuwa watii katika kutimiza mapenzi ya Mungu. Licha kuwa alikua ni Mungu, Yesu alikua mtii kwa Baba yake na alikubali kushuka na kuja kukaa kati yetu sisi ili aturudishie sisi hadhi ya kuwa tena watoto wa Mungu.
Pili: Mitume wa Yesu. Hawa walikua ni watu wa karibu kabisa na Bwana wetu Yesu Kristo. Aliwachagua, akawafundisha, akatembea nao katika safari zote, akatenda miujiza mbalimbali mbele yao na mambo mengine mengi katika utume wake wote. Mwisho anashiriki nao katika karamu ya mwisho. Licha ya hayo yote, hawakuelewa bado juu ya utume wa Bwana wetu Yesu Kristo na ndio sababu alipowaambia Habari za kuteseka na kufa hakumwelewa kabisa. Yuda Iskarioti anamsaliti Yesu, na Petro anamkana Yesu hadharani. Mitume wengine pia wengi walikimbia wakati Yesu alipoingia katika mateso yake. Ndugu mpendwa, Mitume hawa wa Yesu ndio mimi na wewe. Sisi tu wafuasi wake wa karibu kabisa, kwa njia ya Ubatizo na miito mingine mbalimbali. Ninatimiza wajibu wangu kiaminifu kama mfuasi mwaminifu wa Yesu? Au ninapokea wito ila yajapo mateso na magumu ninamkimbia Yesu? Je nimeacha familia yangu wakati changamoto zilipokuja? Nimekata tamaa katika wito wangu nilipokutana na magumu? Tukifanya hivyo, tunamkana na kumsaliti Bwana wetu aliyetupenda na kutuchagua, Katika hali yoyote tusimwache Bwana. Mtume Yohane alitembea na Bwana mpaka chini ya Msalaba pamoja na Mama yetu Bikira Maria. Tujue ya kuwa hakuna utukufu bila mateso na kufa. Yesu atupe nguvu ya kuwa wafuasi wastahimilivu. Kutembea naye katika nyakati zote, katika shida tupo naye, katika raha pia tupo naye, katika huzuni tupo, katika furaha hali kadhalika. Yesu, tupe nguvu ya kukufuata kwa moyo, tusikuache hata mara moja.
Tatu: Makutano na Pilato. Makutano ambao walimpokea Yesu Yerusalemu, wakamshangilia kwa shangwe, Hosana Mwana wa Daudi! Ni makutano hao hao walimpeleka Yesu kwa Pilato na kumshitaki. Wamemshtaki Yesu asiye na hatia yoyote ilihali walimshangilia na kumwita Mfalme. Pilato, licha ya kwamba hakuona kosa lolote kwa Yesu, alikosa maamuzi na kuamua kuamuru Yesu auwawe. Alishindwa kutenda haki kwa kuogopa macho na maneno ya watu. Mara kadhaa katika jamii zetu tunaweza kushangilia hujuma, unyanyasaji, maumivu, dhuluma, na mateso wanayosababishiwa wengine bila sababu. Huenda tumekuwa watu wa kupoke mazuri kutoka kwa wengine lakini sisi tukarudisha ubaya. Yesu aliwatendea wema mkubwa watu, ila hapa wote wamemshitaki bila kosa na kutaka ahukumiwe kifo. Pia tumeshinda kutenda haki kwa kuogopa watu, tumeshindwa kusimamia ukweli kwa kuogopa maneno ya watu. Tumwombe Mungu msamaha, mara zote ambazo kwa maneno na kwa matendo yetu tumewasababishia wengine maumivu na mateso. Tumewasabishia wengine vidonda kwa kuwasingizia uwongo na kuwahukumu bila sababu. Yesu, tupe nguvu ya kuwasamehe wote waliotukosea na kuwaomba msamaha wote tuliowaumiza, kwa mawazo, matendo na maneno yetu.
Nne: Akina Mama waliomsindikiza Yesu katika njia yake ya Msalaba. Mwinjili Luka anatuonesha nafasi ya akina mama ambao hawakuogopa macho ya watu. Walitembea na Yesu tangu Mwanzo mpaka alipokufa pale msalabani wakiongozwa na Bikira Maria Mama wa Yesu. Akina Mama waliomsindikiza Yesu katika njia yake ya Mateso wanakufundisha juu ya uthabiti na ustahimilivu wetu katika kumfuata Yesu. Hawa tofauti na makutano, walikuwa waaminifu katika kumfuata Bwana wao. Walikua naye katika nyakati za furaha lakini pia katika nyakati za mateso. Wanatufundisha pia nasi sote tunapaswa kuwa tayari kuingika katika uhalisia wa maisha ya wengine wanaoteseka kwa namna mbali mbali. Tushiriki kuwafuta uso kama veronica, wapo watu wengi ambao nyuso zao zinavuja damu kwa sababu mbalimbali katika maisha. Tushiriki pamoja na wengine katika kubeba mizigo yao mizito katika maisha, ndiyo misalaba yao.
Tano: Wakuu wa Makuhani na waandishi. Hawa mara kadhaa waliingia katika mgogoro na Bwana wetu Yesu Kristo kwa kuwa mafundisho ya Yesu yalipingana na baadhi ya tamaduni zao. Hawakua tayari kupokea mafundisho ya Yesu na mara kadhaa walimtafutia Yesu sababu ya kumwua. Ndugu wapendwa, mara kadhaa tumekuwa na maelekeo ya wivu, na chuki hasa kwa watu ambao pengine wametuzidi karama, vipaji au pengine Mwenyezi Mungu amewanua kuliko sisi. Tumekua wagumu katika kupokea mambo mema na mazuri kutoka kwa wenzetu. Tumwombe Mungu atusaidie daima tuwe tayari katika kukubali mambo mema na mazuri kutoka kwa wenzetu. Tusitafute sababu ya kuwaangusha wengine kwa sababau tu Mungu amewabariki na kuwainua bali tumwombe Mungu ili naye atuinue na sisi kwa wakati wake.
Sita: Wahalifu wawili waliosulubiwa pamoja na Yesu. Yesua alisulubiwa katikati ya wahalifu wawili, mmoja kulia na mwingine kushoto. Mhalifu mmojawapo alimdhihaki Yesu kwamba, ikiwa wewe ni mwana wa Mungu basi jiokoe nafsi yako na sisi. Lakini yule wa pili akamkemea na kisha akasema, Ee Yesu unikumbuke utakapoingia katika ufalme wako. Yesu akamwambia, amin amin nakuambia, leo hivi utakua nami peponi. Kila mmoja wetu ana nafasi ya kuupata uzima wa milele. Yesu anampokea kila mmoja anayekimbilia huruma yake, licha ya dhambi na udhaifu wetu. Yesu hataki hata mmoja wetu apotee. Tunaalikwa tunapoingia katika juma kuu, kurudia nia yetu ya dhati ya kuwa waaminifu kwa Kristo, ni muda wa kuchagua, au kukaa kulia kwa Yesu au kukaa kushoto kwake. Wiki kuu ni wiki ya kuziokoa roho zetu, kutokana uhalisia kwamba hakuna anayejua siku wala saa ambapo Yesu atatuita kutoka uzima huu. Muda ni sasa, saa ya wokovu ni leo.
Somo la pili: Ni kutok kwa Waraka wa Mtume Paulo kwa Wafilipi 2:6-11. Katika somo la pili, Mtume Paulo anatueleza juu ya unyenyekevu wa Bwana wetu Yesu Kristo, kwamba, licha ya kwamba alikua yu na namna ya Mungu, naye hakuona kule kuwa sawa na Mungu ni kitu cha kushikamana nacho, bali alijifanya kuwa hana utukufu akatwaa namna ya mtumwa akawa sawa na wanadamu. Kumbe nasi sote tunaalikwa kuiga unyenyekevu wa Kristo ambao kwao Mungua alimwinua, akamkirimia jina lipitalo kila jina. Kumbe nasi hatuna budi kujishusha na kujinyenyekeza katika kutimiza mapenzi ya Mungu ili baada ya maisha haya ya hapa duniani, tuinuliwe na kuvikwa taji ya utukufu pamoja na Yesu mbinguni. Hitimisho: Katika Dominika hii ya Matawi, tumwombe Yesu atupe nguvu si tu ya kumshangilia kama Masiya na Mfalme wetu, bali kwa Imani thabiti, unyenyekevu na utii kumkiri, kumpokea na kutembea naye katika njia yake ya Msalaba. Yeye mwenyewe aliwafundisha wafuasi wake na anatufundisha sisi sote kwamba, “Mtu yeyote akitaka kuwa mfuasi wangu, ni lazima ajikane nafsi yake, auchukue msalaba wake kila siku, anifuate” Lk 9:23-25. Tuombe Neema ya kuwa watii katika kutimiza mapenzi ya Mungu kwa ajili ya wokovu wetu na wokovu wa wengine.