Tafakari Dominika V Kwaresima Mwaka C: Haki, Huruma na Rehema
Na Padre Joseph Herman Luwela, - Vatican.
UTANGULIZI: Karibu mpenzi msikilizaji na msomaji wa tafakari ya Neno la Mungu kutoka hapa radio vatican ikiwa leo ni dominika ya tano ya Kwaresima mwaka C. Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa Kitume, “Misericordia et misera” “Huruma na haki” anasema, mwanamke mdhambi alikutana uso kwa uso. Mwanamke alikuwa mzinzi na, kadiri ya Torati, alihukumiwa afe kwa kupigwa mawe. Na Yesu, ambaye kwa mahubiri yake na kwa kujitoa kabisa sadaka, hadi msalabani, alirejesha sheria ya Musa kwenye lengo lake halisi la awali. Kiini chake si sheria au haki ya kisheria, bali kiini chake ni upendo wa Mungu, ambaye anajua kusoma moyoni mwa kila mtu, na kugundua hamu iliyofichama ndani kabisa, ambayo lazima itangulie juu ya yote. Katika simulizi hili la Injili, lakini, hazikutani dhambi na hukumu kinadharia, bali hukutana mwanamke mdhambi na Bwana Mwokozi. Yesu alitazama mwanamke huyo machoni na kusoma moyoni mwake: na humo alikuta hamu ya kueleweka, kusamehewa na kuokolewa. Dhambi yenye hitaji la kuhurumiwa ilivikwa huruma ya upendo. Yesu hakutoa hukumu yoyote, ila ile iliyotokana na huruma na rehema kwa hali ya yule mwanamke mkosefu. Yesu aliwajibu wale waliotaka kumshtaki na kumhukumu auawe, kwanza kwa kubaki kimya kwa muda mrefu, akitaka kuruhusu sauti ya Mungu izuke kwenye dhamiri zao, ya mwanamke na ya wale waliomshtaki. Nao waliacha mawe walioshika mkononi yaanguke chini, na mmoja mmoja wakatoka, wakaenda zao (taz. Yn 8:9). Na baada ya kubaki kimya hivi, Yesu alisema: “Mwanamke, wako wapi? Hakuna aliyekuhukumu kuwa na hatia? ... Wala mimi sikuhukumu. Enenda zako; wala usitende dhambi tena” (a. 10-11). Kwa kufanya hivyo, Yesu alimsaidia kutazama mbele kwa tumaini na kuwa tayari kuanza upya maisha yake; Kuanzia hapo, akipenda, ataweza “kuenenda katika upendo” (taz. Efe 5:2).
Mara unapovikwa huruma, hata kama inaendelea kuwepo ile hali ya udhaifu unaotokana na dhambi, hiyo hufunikwa na kushindwa na upendo unaowezesha kutazama mbele zaidi na kuishi tofauti. Yesu anatoa msamaha kwa mwanamke aliyeukwa amefumaniwa kwenye uzinzi. Wakati viongozi wa dini walikuwa wakitaka kumtupia jiwe, Yesu aliwaambia, “Yeyote asiye na dhambi na apige jiwe la kwanza,” na mwanamke alikwenda akiwa amesamehewa. Hii ni ishara ya huruma ya Mungu, inayothibitisha kwamba, kwa toba na imani, tunapata msamaha wa dhambi. Yesu anafunua dhamiri za watu wanatambua jinsi kila mmoja alivyodhaifu mbele ya Mungu na hivyo kila mmoja aanapaswa kukimbilia huruma na uponyaji kutoka kwa Yesu Mungu na mtu kweli, anakwenda kinyuma na sheria za Musa kwa kumnusuru na kumsamehe aliyefunaniwa katika uzinzi. Bahati mbaya hii ilitokea wakati wa Sherehe ya Vibanda (Tabernacle/Sukkot) mwezi Septemba/Tishrey. Sherehe ililenga kumshukuru Mungu kwa mavuno ya zabibu na kukumbuka babu zao walivyoishi vibandani miaka 40 jangwani kuelekea nchi ya ahadi... Ili kumbukumbu iwe hai walijenga vibanda vya makuti nje ya nyumba na kuishi humo siku nane. Ni sherehe ya hija (nyingine Pasaka na Pentekoste) watu walifurika Yerusalemu kwa mashangilio. Usiku waliwasha moto na kucheza ngoma. Katika moja ya matukio ya kukosa nidhamu watu wawili walikutwa katika uasherati, mwanamke akashikwa. Adhabu ya kosa hilo ni kifo (Law 20:10, Kumb 22:22). Badala ya kuhukumu wenyewe waliona ni fursa ya kumtega, kumnasa na kumshtaki Kristo, wakamtaka atoe hukumu.
UFAFANUZI: Ilikuwa mapema asubuhi, Yesu ndio amefika kutoka Gethsemani au Bethania alikokesha usiku mzima, amekalia kigoda kwenye kona moja ya Hekalu akifundisha, akaona viongozi wakimburuza mama mwenye uso wenye aibu, kilio na kufadhaika. Mwanaume aliyefanya naye kosa hilo hakuletwa, mara nyingi dhuluma na unyanyasaji huelekezwa watu dhaifu, wenye nguvu hulindwa. Ni muhimu kuwa na mifumo ya haki kwa wote. Adui za Kristo waliamini hachomoki... angesema sheria ya Musa ifuatwe angepingana na Warumi, na kujipinga mwenyewe juu ya msimamo wake wa msamaha... angeshauri asamehewe angelikuwa ameidharau sheria ya Musa. Bwana hakujibu, aliinama akiandika sakafuni kwa kidole, wakadhani amebanwa hana jibu, wakazidi kusisitiza (Yn 8:5), akajiinua polepole, akawatazama mmoja baada ya mwingine na kuwaambia kwa tambo “Asiye na dhambi miongoni mwenu na awe wa kwanza kumtupia jiwe (Yn 8:7)”, akainama tena, ishara ya kujishusha ‘level’ ya mdhambi akiwaacha huko juu wanaojihesabia haki wapambane na hali zao... neno hilo moja tu lilizidi kisu, lilipeleka ndani ya dhamiri zao mapigo makuu, mioyo iliwauma wakaona aibu, kila mmoja alizisoma dhambi zake kwenye maandishi ya Yesu sakafuni, wakakunja nyuso na kutoka kwa hatua za haraka, wazee hata wa mwisho wao... watoto nao walitoka, viongozi wa dini pia, maana yake jamii nzima walikuwa watenda dhambi… akabaki Yesu na yule mama, akamuuliza, ‘wako wapi wale washtaki wako? hakuna aliyekuhukumu kuwa na hatia?’ akajibu ‘hakuna Bwana!’
Katika muktadha wa Jubilei ya Matumaini, tafakari hii inatufundisha kuhusu huruma isiyo na mipaka ya Mungu. Jubilei ya Matumaini inasisitiza kuwa, hata tunapokuwa na dhambi nzito, Mungu atufanya tuwe huru kutoka kwa hatia zetu kwa kutubu. Kama vile Yesu alivyomsamehe mwanamke aliyeathiriwa na dhambi, vivyo hivyo Mungu anapokea kwa furaha wale wanaojikuta wamerudi kwake kwa toba na imani. Huu ni kipindi cha kutafakari kuhusu upendo wa Mungu unaovuka mipaka ya dhambi. Kwa wale wakuu mama yule hakuwa na thamani, hawakujali anaishi au anakufa, hawakuonja kama wanamuaibisha na kumdhalilisha, kiburi kiliwasukuma, hawakutaka kumstahi wala kumsitiri, walitaka kuonekana waaminifu wa sheria, wakitetea maslahi na vyeo vyao kwa hasara ya wengine. Lakini katika macho ya Yesu muhimu kwa dakika ile alikuwa yule mama, amrudishe kwa Baba na kumsaidia aanze maisha mapya ya neema ya utakaso, aufahamu upendo, huruma na ukarimu wa Mungu na kuongoka... Kwa Kristo yule mama alikuwa hazina isiyoelezeka, haijalishi ilivyofunikwa na udongo, jukumu lake lilikuwa kuichimba, kuisafisha na kuirudishia thamani yake... Mama alibaki miguuni pa Yesu akificha uso wake kwa aibu na hofu lakini hakukimbia… kati ya wote Mnazareti huyu alikuwa tofauti, mikononi mwake alionja amani na salama. Akitafakari Injili hii Mt. Augustino anasema, “mwanadamu katika dhambi zake amekutana na huruma ya Mungu uso kwa uso.”
Kristo hakuanza litania ya mawaidha/ushauri nasaha kama tufanyavyo sisi mtu akitukosea, alimtazama tu na kwa upole akamwambia, “wala mimi sikuhukumu! enenda zako, wala usitende dhambi tena.” Moyo wangu unatamani kuambiwa neno hili zuri, ni neno la faraja sana, linageuza mioyo na akili, linasafisha uovu, linatoa nafasi ya kujirekebisha, kwa hakika halikufutika kamwe moyoni na akilini mwa mama yule, lilidumu kuwa tanuru ya moto uwakao na kuteketeza kila lisilofaa katika upya wa maisha.Katika ujumbe wa Kwaresima 2025, tunahamasishwa kuishi kwa toba na huruma. Kama alivyomsamehe Yesu mwanamke, tunaitwa kuonyesha huruma kwa wengine na kujitahidi kuishi maisha ya kiroho yanayojikita katika msamaha. Kwaresima ni muda wa kutafakari juu ya udhaifu wetu, lakini pia ni muda wa kufurahi katika huruma ya Mungu ambayo inatufanya tuweze kupokea msamaha na kuanza upya. Kwa maneno haya ‘Enenda zako, wala usitende dhambi tena’ Mosi ni kama Yesu anasema ‘Ninajua umefanya mabaya lakini maisha bado yapo, jiokoe nafsi yako’... labda ndiyo sababu waovu wanaishi sana, Mungu anawapa nafasi wajiokoe nafsi zao... Pili, lilikuwa onyo, hakumruhusu mama yule aendelee katika dhambi ila kwa neno hilo ni kama alimwambia “. leo umesalimika, kesho sitakuwepo hutakuwa na wa kukusaidia, yatakupata mabaya zaidi, badilika, ishi kivingine, jaribu kuyapatia maana na thamani maisha yako, utakuwa heri.” Tatu, Yesu anasisitiza tuchukie dhambi tumpende mdhambi na tumsaidie kuacha. Tuwape moyo waliokata tamaa sababu ya historia yao mbaya wakifikiri hawawezi kusamehewa.
Tunaweza kuwachukia waliotaka kumpiga mawe mama yule, “Sisi je, hatufanyi hayo hayo?” mifuko yetu imebeba mawe, tunayarusha kwa kupekuwa habari mbaya na makosa ya wengine… kwa chuki ya namna yoyote kuhusu jirani, ndugu zako na yeyote awaye… kwa kukwamisha maendeleo ya wengine… kwa wivu wa mafanikio ya wengine… kwa kutoona mazuri ya wengine, kukosoa tu… kwa kutibua viapo vya ndoa… kutojali, kutoguswa na chochote, uonezi, ukorofi, ubinafsi… Hii ni Kwaresima, tujitathmini, Pasaka i karibu isije tukuta tumefumbata mawe ya kuwapigia wenzetu, tutazikosa neema za Fumbo la ufufuko. Tuchunguze dhamiri zetu na tuone wenzetu wanavyotuvumilia na kutustahi… Safari ni ndefu, Mtakatifu Paulo amesema mashindano ni magumu, tuliyofaulu yatupe motisha, tuliyoshindwa yatufunze “… ila natenda neno moja tu, nikiyasahau yaliyo ya nyuma, nikiyachuchumilia yaliyo mbele: nakaza mwendo niifikilie mede ya thawabu ya mwito mkuu wa Mungu katika Kristo Yesu… (Somo II, Flp 3:8-14) … usilegee wala kupunguza mwendo, ishi maisha yako ya Kikristo katika ukamilifu wake, tangaza na uishi upendo wa Mungu wakati wote.. Bwana wa majeshi yu pamoja nasi, anafanya njia pasipo na njia na kututendea mambo mapya (somo I, Isa 43:16-21) … katika yote thawabu iwe ni Kristo! Dominika ya Tano ya Kwaresima inatufundisha kuhusu huruma isiyo na mipaka ya Mungu na wito wa kuishi kwa toba. Jubilei ya Matumaini inatufundisha kuwa tunapata msamaha wa dhambi na huruma ya Mungu kwa toba ya kweli. Katika kipindi cha Kwaresima, tunaitwa kuwa na moyo wa huruma, huku tukisherehekea matumaini ya wokovu kupitia toba na imani kwa Kristo Yesu.