Tafakari Dominika V Kwaresima Mwaka C: Sheria, Haki, Upendo na Huruma
Na Padre Bonaventura Maro, C.PP.S., Kolleg St. Josef, Salzburg, Austria.
Utangulizi: Wapendwa Taifa la Mungu, leo ni Dominika ya 5 ya Kipindi cha Kwaresima, mwaka C wa Kanisa. Liturjia ya Neno la Mungu katika Dominika hii ya tano ya Kwaresma inatutafakarisha kuwa, “Mwenyezi Mungu anatuhurumia sisi wadhambi, anatuahidia maisha mapya.” Mwenyezi Mungu, Baba yetu mwenye Huruma, anachukia dhambi lakini hatuchukii sisi wadhambi, bali anatupa nafasi kila mara ya kufanya mabadiliko ya kweli, kukataa dhambi na kukumbatia huruma yake isiyo na mipaka. Tunapotambua kuwa sisi sote tu wadhambi na tumetindikiwa utukufu wa Mungu, hatutakua warahisi katika kuwahukumu wenzetu kuwa ni wadhambi, bali tutakuwa tayari kwa msaada neema ya Mungu, kutambua dhambi na udhaifu wetu. Tutaweza kufanya hija, kila mtu binafsi, ya kwenda ndani kabisa ya mioyo yetu, kuchunguza mahusiano kati yetu sisi na Mungu, na kati yetu sisi kwa sisi na kupokea mwaliko wa mabadiliko ya ndani. Katika Dominika ya tano ya Kipindi cha Kwaresima, tumshukuru Mungu, Baba yetu Mwenye Huruma, ambaye licha ya kukosa kwetu uaminifu kwake kwa sababu ya dhambi na udhaifu wetu, bado anaendelea kutupeanda, kutuhurumia na kutusamehe. Anatualika nasi sote kuwa na upendo na huruma, kuwa tayari kuwasamehe wale wote waliotukiosea kama vile sisi pia tulivyopokea huruma na msamaha kutoka kwa Mungu kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo. Somo la 1: Ni kitabu cha Nabii Isaya 43:16-21. Somo la kwanza tulilolisikia, ni kutoka kitabu cha Nabii Isaya latueleza jinsi Mungu kwa huruma yake alivyoanzisha safari mpya ya matumaini, safari ya wokovu kwa taifa lake kutoka utumwani Babeli kurudi tena katika nchi yao. Taifa la Israeli (Kabila la Yuda) kwa sababu ya kukosa uaminifu kwa Agano na amri za Mwenyezi Mungu, walipelekwa utumwani Babeli ambapo walikaa kwa muda wa miaka 70. Kwa kinywa cha Nabii Isaya, Mwenyezi Mungu anawapa watu wake ujumbe wa faraja na matumaini tena kwamba, kama vile alivyowatoa baba zao utumwani Misri, Mwenyezi Mungu atawatoa katika utumwa na kuwaongoza kwa mkono wake wenye nguvu kurudi katika nchi yao. Mwenyezi Mungu anawahakikishia watu wake kuwa amewasamehe dhambi na uovu wao. Ahadi hii ilitimia mwaka 539 BC ambapo taifa lake teule walirudi tena katika nchi yao. Mwenyezi Mungu miaka 700 baada ya utabiri wa Nabii Isaya ameitimiza kwetu sote taifa lake jipya ahadi ya ukombozi wa milele kwa njia ya Bwana wetu Yesu.
Ndugu zangu katika somo hili la kwanza tuna mambo matatu ya kujifunza. Kwanza: Mwenyezi Mungu anawakumbuka watu wake, anafanya kitu kipya kwa ajili yao (The Lord remembers his chosen People and does a new thing). Taifa la Israeli walikua utumwani kwa Babeli kwa muda wa miaka 70. Waliteseka kwa muda kipindi kirefu, muda wa kutosha. Katika hali hiyo ya mateso, hofu, mashaka, na mkato wa tamaa, Mwenyezi Mungu ananena nao kwa kinywa cha Nabii Isaya kuwakumbusha kuwa wapo utumwani kwa sababu ya dhambi na ukosefu wao wa uaminifu kwa Mungu. Licha ya hayo, bado Mungu anawapenda, anawaahidia ukombozi kutoka utumwani, anaahidi kufanya kitu kipya. Ndugu mpendwa, sisi sote kwa sababu ya dhambi tulikuwa watumwa na wafu. Licha ya dhambi zetu, bado Mungu hakutusahau, alianzisha mpango wake wa ukombozi tena na ameutimiza wakati utimilifu wa wakati ulipowadia (Gal 4:4-5). Kwa njia ya Mateso, kifo na ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo, Mwenyezi Mungu ametuhurumia, ametukumbuka na akatukomboa, ametufanya tena kuwa upya, alifanya kitu kipya, ndio zawadi ya ukombozi wetu. Kama vile Mungu mwenye nguvu na uweza alivyofanya kitu kwa ajili ya taifa lake teule, ndivyo Mungu anavyosema na mioyo yetu sisi tulio taifa lake jipya kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo. Mara kadhaa katika safari yetu ya maisha tunapopoteza matumaini kwa sababu mbalimbali. Katika familia zetu, katika masomo, katika kazi, katika miito mitakatifu, kuna nyakati tunakata tamaa kabisa. Tunaona kama hakuna matumaini tena na hatuoni maana ya maisha. Yesu anasema na mioyo yetu, kwa sauti ya upole, “Tazama nitafanya njia katika bahari, na mahali pa kupita katika maji yenye nguvu…tazama nitatenda neno jipya, sasa litachipuka.”
Ninakuombea ndugu mpendwa, Mwenyezi Mungu akukumbuke katika nia zako mbalimbali ambazo umeweka mbele zake kila mara upatapo nafasi ya kusema naye. Akukumbuke katika changamoto mbalimbali ambazo unapitia katika maisha ya ufuasi. Akumbuke mahangaiko yako ya kila siku katika maisha, akumbuke jitihada zako na majitoleo yako kwa ajili ya familia yako, na kwa ajili ya wengine, akatende Neno jipya nalo lichipue ndani mwako. Neno lake liamshe matumaini, Imani na mapendo yako kwa Mungu na kwa Jirani zako. Mwenyezi Mungu atupe pia ustahimilivu kufahamu kuwa hakuna hali inayodumu katika maisha yetu. Mwenyezi Mungu akakufungulie njia, akafungue milango ya neema na baraka zake juu yako, Imani yako iwe imara zaidi kwake, matuamini yako yawe hakika, na mapendo yako yawe ya kweli kwa Mungu ambaye alitupenda yeye kwanza. Pili: Ili Mungu atende kazi ndani mwetu hatuna budi kubadili mitazamo yetu kuhusu maisha yetu ya kale (look at the past and remember God’s wondrous acts). Mwenyezi Mungu ananena na watu kwa kinywa cha Nabii Isaya kwamba wasikumbuke tu maisha ya kale, wasikumbuke tu mambo ya kwanza na kuyatafakari mambo ya zamani, bali watazame nyuma na kumwona Mungu aliyetenda makuu katika historia ya ukombozi wao. Ndugu wapendwa, kipindi cha Kwaresma ni kipindi cha kumtafakari Mungu ambaye ametenda makuu katika historia ya ukombozi wetu. Tunatafakari namna Mungu wetu kwa upendo wake mkubwa alivyosafiri na watu wake katika historia ya ukombozi hadi kutimia kwa ahadi hiyo kwa ujio wa Bwana wetu Yesu Kristo. Tunapotazama na kutafakari hayo tunamshukuru Mungu ambaye ametupa ushindi dhidi ya kifo na mauti kwa njia ya mwanaye Yesu Kristo. Nasi sote kila mmoja kwa nafasi yake anapokaa na kutazama nyuma katika historia ya maisha yetu, namna Mungu alivyotutoa huko tulikokua, akatuinua na kutuleta hata hapa tulipo na bado anaendelea kutuinua, tunauona mkono wake wenye nguvu na kushuhudia matendo yake makuu. Tunapokaa chini na kuwaza kwa kina tunakosa majibu na tunaishia kusema, “Ni Mungu tu” Hata tuwe tumepitia magumu mengi kiasi gani, hayo yote hayakuwa makubwa kuliko nguvu na uweza wa Mungu wetu. Hata kama hatukupata vingi lakini ametupa uzima wa roho ambao ndio utajiri wote wa mbinguni. Mwenyezi Mungu umetutendea makuu, tulikua tukifurahi.
Tatu: Tunapoanza safari yetu mpya ya maisha, Mwenyezi Mungu anatupa nguvu rohoni (The Lord nourishes us in our new Exodus). Mwenyezi Mungu anawakumbusha taifa lake jinsi alivyowalisha na kuwanywesha katika safari ya babu zao kutoka misri kwenda nchi ya ahadi. Anaahidi kuwalisha na kuwanywesha tena watu wake katika safari yao mpya kutoka utumwani Babeli kurudi katika nchi yao. Kwaresima yatukumbusha kuwa sisi sote tumeanza safari mpya ya maisha, kutoka maisha ya dhambi na kuendea maisha mapya ya neema, maisha matakatifu. Safari hii ni safari ya mabadiliko makubwa ya kiroho. Tunasafiri kuelekea nchi yetu ya ahadi mbinguni na hivyo tunahitaji nguvu na afya rohoni. Mwenyezi Mungu kwa njia ya fumbo la pasaka ametupatia sisi chakula na kinywaji cha Mbinguni, Ekaristi Takatifu, Mwili na Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo ili itupatie nguvu na afya rohoni katika safari yetu mpya ambayo kila mmoja wetu anaianza katika ubatizo. Ni Yesu anayetusaidia pia kila mmoja kutembea katika njia yake ya Msalaba pamoja na Yesu.
Somo la Injili: Ni Injili ya Yohane 8:1-11. Somo la Injili Takatifu kutoka katika Injili ya Yn 8:1-11, ni simulizi juu ya Mwanamke aliyefumaniwa katika uzinzi, aliyeletwa na Mafasayo na Waandishi kwa Yesu. Katika tamaduni za Wayahudi, uzinzi ilikua ni kosa kubwa ambalo adhabu yake ilikua ni wote kupigwa mawe hadi kufa (rej. Law 20:10; Kum 22:22). Lengo la mafarisayo na waandishi kumleta mwanamke huyu kwa Yesu ni kumtafutia Yesu sababu ili wamkamate na kumuua. Yesu anatoa hapa fundisho kubwa kwa Mafarisayo, waandishi na kwetu sisi sote kwamba, Mwenyezi Mungu anachukia dhambi, ila anawapenda na kuwahurumia wanawe wote ambao hakuna hata mmoja anayeweza kusema hana dhambi. Anatukaribisha kwake, anatusamehe dhambi zetu na kutupa nafasi ya kuanza tena maisha mapya, kuweka nia ya dhati ya kuacha maisha ya zamani na kuanza maisha mapya ndani ya Kristo mfufuka. Nasi hatupaswi kuwahukumu wengine bali kusamehe na kuhurumia kama sisi tulivyosamehewa na kuhurumiwa na Mungu. Katika somo hili la Injili dominika ya leo tuna mafundisho manne ya kujifunza. Kwanza: Sala na Tafakari binafsi zinatusaidia kufahamu Mungu anasema nini nasi. Yesu alienda mpaka mlima wa Mizeituni. Hii ilikua ni sehemu ambapo Yesu alikwenda kusali (Lk 22:39) na huko tunaambiwa alikaa hata asubuhi, Yesu mara nyingi alitenga muda na kwenda kusali na kuzungumza na Mungu Baba yake. Kabla ya kufanya jambo lolote kubwa Yesu alipata muda wa kuzungumza na Mungu. Aliunganika na Mungu Baba yake na hivyo alikua tayari kuyafanya mapenzi ya Baba yake. Ndugu wapendwa, katika kipindi cha kwaresma tuaalikwa kusali. Tunaposali tunajenga urafiki na Mungu, tunakua karibu kila siku na Mungu, tukimsikiliza anasema nini na nasi katika maisha yetu kama wafuasi wake. Tunaposali, tunapata nguvu na uwezo wa kufanya maamuzi sahihi katika maisha yetu, maamuzi ya hekima na busara kuhusu maisha yetu na katika maisha ya wengine. Tunaposali tunamruhusu Mungu afanye kazi ndani mwetu, anatusaida kila mara kutambua udhaifu wake, tunapata nguvu ya kukataa vilema vyetu malimbali vya dhambi. Anatusaidia pia kuwekania ya dhati ya kuanza maisha mapya, safari ambayo kila mmoja wetu aliinza katika ubatizo wake. Tusali, kama Yesu alivyotufundisha kusali tukitambua mapendo yasiyo ya mipaka aliyo nayo Mungu kwetu sisi.
Pili: Yesu anatufundisha juu ya sheria ya haki upendo na huruma (Legalism verses Justice, Mercy and Grace). Katika sehemu hii ya Injili Takatifu, Yesu anatoa mtazamo mpya juu ya sheria. Mafarisayo walitafsiri sheria bila upendo na huruma. Sheria ilikua kandamizi isiyokua na haki. Licha ya kwamba sheria iliwataka wote wawili waliokamatwa katika uzinzi kupigwa mawe mpaka kufa (rej. Law 20:10; Kum 22:22), hapa tunaona analetwa tu mwanamke kwa Yesu na mafarisayo na waandishi wanamshitaki ili Yesu atoe hukumu ya kupigwa mawe mpaka kufa. Yesu anasimama kama hakimu mwenye haki, anayesimamia ukweli lakini kwa jicho la upendo na huruma. Ndugu Wapendwa, Yesu anatafsiri sheria kwa jicho la upendo, huruma na haki tofauti na mafarisayo na waandishi ambao walitaka mwanamke mzinifu apigwe kwa mawe mpaka kufa. Anatufundisha kuwa amekuja katikati yetu ili kutufunulia uso wa Baba mwenye huruma, akitutaka nasi sote kuwa na huruma kama Baba yetu wa mbinguni anavyotuhurumia sisi. Sisi sote kwa kosa la wazazi wetu wa kwanza Adamu na Eva itupasa kufa lakini kwa huruma, Mwenyezi Mungu akadhihirisha kwetu haki yake kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo. Kumbe, kila mmoja wetu anaalikwa kuwa tayari kukumbatia sheria mpya ya Yesu, sheria ya upendo. Tukitambua kuwa sisi sote tu wadhambi basi hatutakua warahisi katika kuwahukumu wengine pale ambapo wanatukosea nasi pia tutakua tayari kujinyenyekesha mbele za Mungu na kukumbatia daima huruma yake kubwa isiyo na mipaka. Tusijihukumu na kuona kuwa hatuna nafasi ya kupata huruma ya Mungu pengine kwa kufikiri dhambi na udhaifu wetu ni mkubwa sana. Neema na huruma ya Mungu kwetu sisi ni ya milele, upendo wake hauna mipaka na hukumu yake ni ya haki na ya kweli.
Tatu: Yesu anatualika sote kutubu na kuanza maisha mapya (Repentance and newness of life). Yesu anamwambia yule mwanamke aliyekamatwa katika uzinzi mara baada ya watu wote kuondoka na hakuna hata mmoja aliyejaribu kumtupia jiwe, “Wala mimi sikuhukumu. Enenda zako, Imani yako imekuponya” Ni maneno ya Faraja, maneno yenye kuleta matumaini mapya kwa mwanamke huyu mdhambi ambaye alihukumiwa kupigwa kwa mawe mpaka kufa kwa sababu ya dhambi yake. Ndugu wapendwa, Mungu anatupa nafasi ya pili kila mara katika maisha. Katika Dominika iliyopita tulisikia simulizi ya Mwana mpotevu, tukaona jinsi Mungu kwa upendo wake mkubwa anavyofanya jitihada (unconditional initiatives) katika kututafuta sisi wakosefu tunaopotea kila mara kwa sababu ya dhambi. Maneno haya Yesu anayomwambia mwanamke mzinzi ndiyo maneno tunayoambiwa katika sakamenti ya kitubio kwamba, “Mwenyezi Mungu amekuondolea dhambi zako zote, nenda na amani.” Tunamshukuru Yesu ambaye hachoki kutupokea. Amefungua mikono yake pale msalabani akituambia, “Njooni wanangu” Amefungua moyo wake ili sote tupate huruma yake isiyo na mipaka, huruma ambayo kwayo tunavikwa utu mpya, na kuanza maisha mapya. Mwenyezi Mungu atusaidie nasi sote tuwe tayari kuwapokea wengine kwa kuhurumia na kusamehe kama sisi tulivyohurumiwa na kusamehewa naye.
Nne: Tathmini binafsi inatusaidia katika kufanya mabadiliko ya ndani (a call to self-examination). Mafarisayo na waandishi walipomleta yule mwanamke mzinzi kwa Yesu walikua na lengo la kumtega Yesu ili wapate sababu ya kumshitaki na kumuua. Yesu anawaambia, “Yeyote asiye na dhambi miongoni mwenu na awe wa kwanza wa kumtupia jiwe” akainama chini akaandika kwa kidole chake katika nchi. Tafsiri ya kitendo hiki cha Yesu kuandika chini haipo wazi sana katika maandiko matakatifu ila baadhi ya waataalamu wanatuambia kuwa, pengine aliwapa nafasi kila mmoja kujichunguza dhambi nafsini mwake. Ndugu wapendwa, Yesu anatukumbusha kila mara kwamba tunapaswa kila mmoja kufanya hija na kuingia ndani kabisa ya moyo wake. Katika kipindi hiki cha Kwaresma tunaalikwa kurarua mioyo, yaani kufanya mabadiliko ya ndani na ya kweli na ya kudumu ndani ya mioyo yetu. Hatuwezi kufanya mabadiliko ya ndani kama hatupati nafasi kila mmoja kusema na nafsi yake, kujifanyia CT scanning au x-ray na kuona hivi mahusiano yangu na Mungu wangu yapoje? Mahusiano yangu na Jirani zangu yapoje? Vipi kuhusu mahusiano yangu na wanafamilia wenzangu, mume wangu, mke wangu, Watoto wangu, padre mwenzangu, mtawa mwenzangu nk? Tathmini binafsi itatupelekea kufanya mabadiliko ya kweli na ya kudumu katika maisha yetu.
Somo la pili: Ni kutoka katika Waraka wa Mtume Paulo kwa Wafilipi 3:8-14. Katika Somo la Pili, Mtume Paulo anatuambia kuwa, “Nayahesabu mambo yote kuwa si kitu kwa ajili ya uzuri usio na kiasi wa kumjua Kristo Yesu Bwana wangu” Paulo alikuwa myahudi aliyeshika kiaminifu dini ya kiyahudi na kwa maisha yake alilitesa na kulidhulumu kanisa. Lakini alipokutana na Kristo, Paulo anaanza maisha mapya kabisa. Mtume Paulo, alipopokea Imani, akaanza maisha mapya na juhudi katika kumtangaza Kristo. Sisi sote tumepokea Imani na kubatizwa. Ni ishara ya Mwanzo mpya wa maisha. Ili tuufikie ukamilifu wa neema hiyo kubwa tuliyopewa na Mungu kwa njia ya Kristo Bwana wetu hatuna budi kuzidi kila siku na kwa uaminifu mkubwa kuunganikana Kristo Bwana wetu. Hitimisho: Katika Dominika ya leo, tumshukuru Mungu, Baba yetu Mwenye Huruma, ambaye licha ya kukosa kwetu uaminifu kwake kwa sababu ya dhambi na udhaifu wetu, bado anaendelea kutupeanda, kutuhurumia na kutusamehe. Anatualika nasi sote kuwa na upendo na huruma, kuwa tayari kuwasamehe wale wote waliotukiosea kama vile sisi pia tulivyopokea huruma na msamaha kutoka kwa Mungu kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo.