Tafakari Dominika V ya Kwaresima Mwaka C wa Kanisa: Upendo, Huruma na Msamaha
Na Padre Pascha Ighondo, - Vatican.
Tafakari ya Neno la Mungu, Dominika ya tano ya Kipindi cha Kwaresima, mwaka C wa Kiliturujia katika Kanisa, siku ya 33 ya kujitakatifuza. Kadiri ya utamaduni na mapokeo ya Kanisa, kuanzia Dominika hii Misalaba inafunikwa, mpaka Ijumaa Kuu wakati wa kuadhimisha mateso ya Kristo na sanamu zinafunikwa mpaka wakati wa maaadhimisho ya vijilia vya Pasaka. Zimebaki siku saba tuingie Juma kuu linalofunguliwa na Dominika ya matawi.Tukiwa tuko ukingoni mwa Kipindi hiki cha Kwaresima, ni vyema kujitafakari na kujiuliza: Je, ile dhambi ninayoipenda kuliko zote nimeiacha, tendo gani la huruma nimetenda tangu kwaresima ianze, ni nini nilichojinyima kwa ajili ya wahitaji tangu Kwaresima ianze? Baba Mtakatifu Francisko anakazia kwa namna ya pekee Amri ya Upendo inayowawezesha waamini kujivika moyo wa rehema, utu wema, unyenyekevu, upole na uvumilivu kwa kujikita zaidi na zaidi katika fadhila ya msamaha na huruma. Vinginevyo, Jumuiya ya Kimataifa itajikuta ikikumbatia utamaduni wa kifo kwa mauaji ya vikongwe, wagonjwa na walemavu, bila hata ya kuguswa na mahitaji wala mahangaiko ya jirani zao. Huu ni wakati muafaka wa kuachana na sera za chuki, uhasama na hali ya kutaka kulipizana kisasi, tayari kukumbatia mchakato wa upatanisho na amani. Wema na huruma ni fadhila za watu makini wanaowaheshimu na kuwathamini wengine kama kielelezo cha Unabii unaomwilisha katika huduma. Masomo ya dominika hii yanasisitiza juu ya upendo na huruma ya Mungu kwa wadhambi. Ni katika muktadha huu wimbo wa mwanzo unaofungua maadhimisho ya dominika hii unasema hivi; “Ee Bwana, unihukumu, unitetee kwa taifa lisilo haki, uniokoe na mtu wa hila asiye haki. Kwa kuwa wewe Mungu ndiye uliye nguvu zangu” (Zab. 43:1-2). Naye mama Kanisa katika sala ya mwanzo anasali hivi; “Ee Bwana Mungu wetu, tunakuomba utusaidie tuwe na mapendo kama ya Mwanao, aliyeipenda dunia hata akajitoa auawe”.
Somo la kwanza ni la Kitabu cha Nabii Isaya (Isa 43:16-21). Katika somo hili Mungu kwa upendo na huruma yake anaahidi kuwakomboa waisaraeli kutoka utumwani Babeli kama alivyowakomboa kutoka utumwani Misri. Mungu alilichagua Taifa la Israeli kwa maandalizi ya kutuletea Mkombozi kwa kufanya nao Agano – makubaliano rasmi yaliyofanywa mlimani Sinai na kuwapa amri zake. Nabii Hosea anaueleza uhusiano uliokuwepo kati ya Mungu na Waisraeli kwa mfano wa uhusiano wa mume na mke – Bwana na Bibi Arusi. Waisraeli, kama bibi arusi wa Mungu, walikosa uaminifu kwa kumwasi Mungu. Matokeo ya uasi wao ni uhamisho wa Babeli. Baada ya kutumikishwa kwa mateso mengi, walitambua makosa yao wakayakiri, wakamlilia Mungu na kuomba msamaha naye akawasamehe na kuwaahidi ukombozi mpya na kuwarudisha tena katika nchi yao. Mungu anaahidi kuwafanyia makuu haya kwa mkono wake wenye nguvu na uwezo kama alivyowakomboa kutoka utumwani Misri. Ni katika muktadha huu Mzaburi katika wimbo wa katikati anaelezea makuu ambayo Mungu aliwatendea watu wake akisema; “Bwana alipowarejeza mateka wa Sayui, tulikuwa kama waotao ndoto. Ndipo kinywa chetu kilipojaa kicheko, na ulimi wetu kelele za furaha. Ndipo waliposema katika mataifa, Bwana amewatendea mambo makuu. Bwana alitutendea mambo makuu, tulikuwa tukifurahi. Ee Bwana, uwarejeze watu wetu waliofungwa, kama vijito vya kusini. Wapandao kwa machozi, watavuna kwa kelele za furaha. Ingawa mtu anakwenda zake akilia, azichukuapo mbegu za kupanda. Hakika atarudi kwa kelele za furaha, aichukuapo miganda yake” (Zab. 126). Nasi tukitambua makosa na dhambi zetu tukatubu, tukamlilia Mungu na kuomba msamaha, hakika atatusamehe na kutufany tufurahi tena.
Somo la pili ni la Waraka wa Mtume Paulo kwa Wafilipi (Wafil. 3:8-14). Katika somo hili mtume Paulo anatufundisha kuwa, tukiwa na imani juu ya nguvu ya mateso, kifo na ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo, tutayaona mambo ya dunia hii si kitu, ni ya kupita tu. Hivyo tutafunua mioyo yetu kwa makuu ambayo Mwenyezi Mungu anatutendea kwa njia ya Kristo na kuwa tayari kuacha dhambi na kukazana kutenda mema na kuukaza mwendo ili tulipate tuzo la uzima wa milele mbinguni. Injili ni ilivyoandikwa na Yohane (Yn 8:1-11). Sehemu hii ya Injili inahusu simulizi la mwanamke aliyefumaniwa katika dhambi ya uzinzi akisubiri hukumu na adhabu ya kupigwa mawe mpaka kufa kama sheria ya Musa ilivyosema; “Na mtu aziniye na mke wa mtu mwingine, naam, yeye aziniye na mke wa jirani yake, mtu mume aziniye, na mwanamke aziniye, hakika watauawa”(Wal 20:10; Kumb 22:22). Dhambi hii ya uzinzi katika Agano la Kale ilichukuliwa kuwa ni dhambi mbaya sana hata kufananishwa na dhambi ya kuabudu miungu mingine, dhambi ya Israeli kukosa uaminifu kwa Mungu wa kweli. Mungu alimwambia hivi Nabii Hosea; “Nenda ukampende tena mwanamke anayependwa na mume mwingine na ambaye ni mzinzi. Mpende kama Mimi ninavyompenda Israeli, ingawa yeye ameigeukia miungu mingine” (Ho.3:1). Hivyo tukipotenda dhambi tunakosa uaminifu kwa Mungu, tunafananishwa na mwanamke mzinzi.
Somo hili limesheheni mafundisho mengi sana. Kwanza kabisa linatuonesha chuki ya Mafarisayo kwa wadhambi, kwa Yesu na kwa mafundisho yake. Hivyo asubuhi na mapema wanamleta mwanamke aliyefumaniwa mbele yake, hekaluni wakati ameenda kusali na kuwalisha watu Neno la Mungu, ili wamjaribu kwa hila, wapate neno la kumshataki apate kuuawa. Iko hivi, kipindi hiki wayahudi walikuwa chini ya utawala wa kirumi na hawakuruhusiwa kutoa adhabu yoyote ya kifo. Hivyo Yesu angesema watekeleze sheria ya Musa, wampige huyu mwanamke kwa mawe mpaka kufa, yeye mwenyewe angekuwa na hatia ya kuuwawa kadiri ya sheria ya Serikali ya Kirumi. Lakini pia angepingana na mafundisho yake juu ya huruma, upendo na kutowahukumu wengine. Na angesema wasimuue, angepingana na sheria ya Musa. Na yeyote aliyepingana na sheria ya Musa alistahili adhabu ya kifo. Yesu kwa kufichua nia yao ovu anawaambia kuwa yule asiye na dhambi awe wa kwanza kumtupia jiwe (Yn 8:7). Simulizi linasema kuwa kimya kimya, waliondoka mmoja mmoja, wakitanguliwa na wazee hata wa mwisho wao. Yesu anamwambia huyu mwanamke “Wala mimi sikuhukumu. Nenda zako; usitende dhambi tena” (Yn 8:11). Hii haina maana kuwa Yesu hachukii dhambi, bali anawahurumia wakosefu ili wapate nafasi ya kutubu na kuacha dhambi.
Fundisho la pili ni hili, mbele za Mungu hakuna binadamu asiye na dhambi ndiyo maana wote waliondoka na hakuna aliyedhubutu kuwa wa kwanza kumrushia jiwe mwanamke mdhambi. Mungu haadhibu mara, bali anampa kila mtu nafasi ya kubadili mwenendo wake na kurudi katika njia ya kweli na haki. Mwanadamu mdhambi anaendelea kuishi kwa huruma na upendo wa Mungu na sio kwa mastahili yake. Mungu anaendelea kutupa nafasi ya kuishi hata kama tu wadhambi ili tutubu, tubadilike na kuomba msamaha naye daima anamsamehe kila anayekiri na kutubu makosa yake. Tunaalikwa kufanya toba, tusamehewe na tusirudie kutenda dhambi tena kwa neema za Mungu. Tuweke nia thabiti ya kuanza maisha mapya, maisha yanayompendeza Mungu. Lakini zaidi sana tusiwahukumu wengine kwa dhambi zao bali tuwasiaidie kuachana na mazoea ya kutenda dhambi. Fundisho la tatu ni hili, binadamu hana mamlaka ya kumhukumu mwingine kwa adhabu ya kifo maana uhai wa mwanadamu ni mali ya Mungu. Uhai ni zawadi na tunu pekee ambayo Mungu ametupatia sisi wanadamu, hivyo ni jukumu letu kuupokea, kuutunza na kuulinda. Thamani ya maisha yetu mbele za Mungu ni kubwa mno kwa kuwa tumeumbwa kwa sura na mfano wake. Kristo anadhihirisha dhamani ya maisha ya mwanadamu mbele mafarisayo na waandishi kwa kuwafanya watambue dhambi zao badala ya kutoa hukumu ya kifo kwa mdhambi tena kwa kumpiga mawe kuwa ni ni ukatili na uovu dhidi ya uhai.
Tutambue kuwa thamani ya uhai wa mwanadamu haifananishwi na chochote na iko mikononi mwa Mungu. Tuwaoneshe huruma waliokata tamaa na kuamua kuishi katika dhambi. Tuwatie moyo kuwa Mungu ni mwenye huruma, yupo tayari kuwasamehe wakimwendea kwa moyo wa toba na majuto. Ni katika tumaini hili mama Kanisa katika sala ya kuombea dhabihu anasali hivi; “Ee Mungu Mwenyezi, utusikilize sisi watumishi wako uliotujalia kujua dini ya kikristu. Ututakase kwa nguvu ya sadaka hii”. Basi tuyachuchumalia mambo ya mbinguni, tuyasahau ya nyuma na tuyahesabu kuwa si kitu. Tukaze mwendo katika kuishi maisha ya kitakatifu, huku tukiitumainia huruma na neema za Mungu ili tubaki kuwa waaminifu katika kuziishi amri zake kwa ajili ya sifa na utukufu wake nasi tutakatifuzwe tuweze kuisherehekea sikukuu ya Pasaka kwa furaha na amani tukiwa tumeungana Kristo Mfufuka kama anavyosali mama Kanisa katika sala baada ya Komunio akisema; “Ee Mungu Mwenyezi, tunakuomba tuwe tumeungana naye daima yeye ambaye tunashiriki Mwili na Damu yake.” Na hili ndilo tumaini letu.