Katekesi Kuhusu Fadhila Na Mizizi ya Dhambi: Kiburi Ni Kaburi La Utu wa Binadamu
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S., Vatican.
Mizizi ya dhambi, vilema vikuu vya dhambi au vichwa vya dhambi ni orodha ya maovu ambayo tangu zamani za Mababa wa Kanisa katika kanuni maadili ya Ukristo yanahesabiwa kumuelekeza binadamu kutenda dhambi nyingine, hata kubwa zaidi. Mizizi ya dhambi iko saba nayo ni: Majivuno, uzembe, kijicho, hasira, uroho, utovu wa kiasi na uzinzi, si dhambi kuu kuliko zote; lakini ndivyo vilema tunavyovielekea kwanza na ndivyo vinavyomsogeza mwanadamu mbali zaidi na Mwenyezi Mungu na hivyo kumtumbukiza katika makosa makubwa zaidi kama vile: uzushi, uasi wa dini, kukata tamaa na hatimaye, kumchukia Mungu. Mtu hafikii uovu mkubwa mara moja, bali polepole na hatua kwa hatua. “Hatimaye, ndugu zangu, mambo yo yote yaliyo ya kweli, yo yote yaliyo ya staha, yo yote yaliyo ya haki, yo yote yaliyo safi, yo yote yenye kupendeza, yo yote yenye sifa njema; ukiwapo wema wo wote, ikiwapo sifa nzuri yo yote, yatafakarini hayo.” Flp 4:8. Mababa wa Kanisa wanasema kwamba, fadhila ni tabia ya kawaida na imara ya kutenda mema. Yamruhusu mtu si kutenda mema tu bali kutoa kilicho chema kabisa cha nafsi yake. Mtu wa fadhila huelekea mema kwa hisi zake zote pamoja na nguvu za kiroho. Hutafuta mema na kuyachagua kwa matendo halisi. Kuna fadhila za kibinadamu ambayo ni hali thabiti, maelekeo imara, ukamilifu wa kawaida wa akili na utashi zinazotawala matendo ya binadamu, zinazoratibu harara na kuongoza mwenendo kufuata akili na imani. Zinawezesha raha, kujitawala na furaha katika kuishi maisha mema kimaadili. Fadhila adili hupatikana kwa juhudi za kibinadamu kuungana na upendo wa Mungu. Shabaha ya mtu mwenye fadhila ni kuwa kama Mungu. Kuna fadhila kuu ambazo hutenda kazi kama bawaba nazo ni: Busara, haki, nguvu, na kiasi. Rej. KKK 1803-1803. Kuna fadhila tatu za Kimungu: imani, matumaini na mapendo.
Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano tarehe 27 Desemba 2023 alianza mzunguko mpya wa Katekesi kuhusu fadhila na mizizi ya dhambi mambo msingi katika kuulinda moyo. Baba Mtakatifu amekwisha kuchambua mizizi hii ya dhambi hatua kwa hatua na kwamba, tiba ya uvivu ni uvumilivu wa kiimani. Amezungumzia pia kuhusu wivu, utepetevu, uchoyo, na majivuno. Baba Mtakatifu katika katekesi yake, Jumatano tarehe 6 Machi 2024 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican iliyosomwa kwa niaba yake na Monsinyo Pierluigi Giroli, kutoka Sekretarieti kuu ya Vatican, amesema, katika mizizi yote ya dhambi kiburi ni malkia mkuu anayemfanya mtu kuwa na shingo ngumu. Mtakatifu Petro Mtume alijigamba kusimama kidete kumlinda na kumtetea Kristo Yesu na kinyume chake ni Bikira Maria katika utenzi wake wa “Magnificat” anasema “Amefanya nguvu kwa mkono wake; Amewatawanya walio na kiburi katika mawazo ya mioyo yao;” Lk 1:51. “Lakini hutujalia sisi neema iliyozidi; kwa hiyo husema, Mungu huwapinga wajikwezao, bali huwapa neema wanyenyekevu.” Yak 4:6. Mababa wa Kanisa wanasema, malezi ya dhamiri ni kazi ya maisha yote. Kuanzia miaka ya mwanzoni humuamsha mtoto kujua na kujizoesha sheria ya ndani inayotambuliwa na dhamiri adilifu. Malezi ya busara hufundisha fadhila; huzuia na kuponya hofu, ubinafsi na kiburi, chuki itokanayo na hisi za kujiridhisha zinazotokana na udhaifu na makosa ya kibinadamu. Malezi ya dhamiri huthibitisha uhuru na huzaa amani ya moyo. Rej. KKK 1784. Chuki ya Mungu hutokana na kiburi, KKK 2094 na huo ni mwanzo wa husuda. KKK 2540.
Udhaifu na kushindwa katika sala; ukavu katika maisha ya sala, uchungu katika maisha ya kiroho ni jeraha la kiburi na aibu kwa mwanadamu mdhambi. Ili kushinda udhaifu huu kuna haja ya kujizatiti katika unyenyekevu, matumaini na udumifu. Baba Mtakatifu Francisko anasema, kiburi ni tabia ya mtu kutaka kujimwambafai kupita kiasi; ni hali ya kujikweza, kujidai na ubatili. Neno hili pia linaonekana katika mfululizo huo wa maovu ambayo Kristo Yesu anaorodhesha kueleza kwamba uovu daima hutoka katika moyo wa mwanadamu. Rej. Mk 7: 22. Mwenye kiburi ni mtu anayejiona kuwa ni zaidi ya vile alivyo; mtu anayetetemeka kutambuliwa kuwa mkuu kuliko wengine, daima anataka sifa zake zitambuliwe na kuwadharau wengine, akiwaona kuwa duni na wala si mali kitu! Tabia ya kujikweza inaendana sanjari na kiburi, ingawa tabia ya kujikweza ni ugonjwa unaosimikwa katika ubinafsi na kwamba, kati ya mizizi yote ya dhambi kiburi ni malkia mkuu anayemfanya mtu kuwa na shingo ngumu. Mwenye kiburi mara nyingi anajitenga na Mwenyezi Mungu na kwamba, inahitajika nguvu ya ziada ya kuweza kupambana na hatimaye, kushinda kiburi, changamoto na mwaliko kwa Wakristo. Kiburi ni mzizi wa dhambi unaomfanya mtu kujisikia kuwa kama Mungu kama Maandiko Matakatifu yanavyosimulia: “Kwa maana Mungu anajua ya kwamba siku mtakayokula matunda ya mti huo, mtafumbuliwa macho, nanyi mtakuwa kama Mungu, mkijua mema na mabaya.” Mwa 3:5. Kiburi ni mzizi wa dhambi ambao unagusa na kuharibu mshikamano na mafungamano ya watu; uharibu hisia za udugu wa kibinadamu, ambao kimsingi ungepaswa kuwa ni kiungo kinachowaunganisha watu! Kiburi kina mfanya mtu kuwa na shingo ngumu na mwenye kuwadharau wengine kuwa si mali kitu! Katika Injili, Kristo Yesu amefundisha machache sana kuhusu kanuni maadili na utu wema, lakini amekazia “Kamwe usihukumu.” Hawa ni watu ambao hawakubali kushauriwa au kukosolewa na ikiwa kama anakoselewa, basi atajibu mapigo kwa ukali na hata wakati mwingine kuvunja mahusiano!
Baba Mtakatifu Francisko anasema, ni vigumu kuweza kumsaidia mgonjwa mwenye kiburi, kinachohitajika ni uvumilivu tu, kwani iko siku kiburi chake kitaporomoka tu. Hivi ndivyo ilivyojitokeza kwa Mtakatifu Petro Mtume, alijigamba kusimama kidete kumlinda na kumtetea Kristo Yesu akisema, “Wajapochukizwa wote kwa ajili yako, mimi sitachukizwa kamwe.” Mt 26:33. Lakini baadaye akajitambua kwamba, hakuwa tofauti sana na Mitume wengine mbele ya kifo ambacho kilikuwa “kinamkodelea macho.” Baada ya tukio hili, Petro Mtume hakuthubutu tena kumkana Kristo Yesu, bali akalia kwa uchungu, Kristo Yesu baadaye, akamganga na kumtibu na hatimaye, akamkabidhi uzito wa kuliongoza Kanisa na hatimaye, akawa ni Mwanafunzi mwaminifu wa Kristo Yesu aliyemweka juu ya vitu vyake vyote. Rej. Lk 12:44. Wokovu unawajia watu kwa njia ya unyenyekevu na katika utenzi wa “Magnificat”, Bikira Maria anamwimbia Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa kuwa Mwenye nguvu amemtendea makuu, amefanya nguvu kwa mkono wake, amewatawanya walio na kiburi katika mawazo ya mioyo yao. Haiwezekani kumlaghai Mwenyezi Mungu, kwa sababu anataka kuwapatia watu wote wokovu. Ndiyo maana Yakobo Mtume baada ya kushuhudia Jumuiya yake iliyokuwa imejeruhiwa kutokana na malumbano ya ndani kutokana na kiburi aliandika hivi: “Lakini hutujalia sisi neema iliyozidi; kwa hiyo husema, Mungu huwapinga wajikwezao, bali huwapa neema wanyenyekevu.” Yak 4:6. Baba Mtakatifu Francisko amehitimisha Katekesi yake kwa kutoa mwaliko kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuhakikisha kwamba, wanatumia kikamilifu Kipindi hiki cha Kwaresima kupambana na ugonjwa wa kiburi kwa sababu ni kaburi la utu, heshima na haki msingi za binadamu!