Tafuta

Baba Mtakatifu ametembelea Banda la Maonesho kutoka Vatican yanayonogeshwa na kauli mbiu “Kwa macho Yangu.” Baba Mtakatifu ametembelea Banda la Maonesho kutoka Vatican yanayonogeshwa na kauli mbiu “Kwa macho Yangu.”   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Hija ya Kichungaji ya Papa Francisko Venezia: Hotuba Kwa Wasanii: Udugu na Usawa

Baba Mtakatifu ametembelea Banda la Maonesho kutoka Vatican yanayonogeshwa na kauli mbiu “Kwa macho Yangu.” Maonesho haya yanafanyika kwa ushirikiano kati ya Baraza la Kipapa la Utamaduni na Elimu pamoja Idara ya Utawala wa Magereza sanjari na Wizara ya Sheria ya Italia. Papa amewapongeza kwa mchango wao katika jamii na kwamba, ujumbe wake mahususi kwa wasanii wote popote pale walipo ni kwamba, Ulimwengu mambo leo una haja ya wasanii!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Uzuri na utakatifu wa kazi ya uumbaji unafanya rejea kwa Mungu Muumbaji wa vyote vinavyoonekana na visivyoonekana. Huu ni mwaliko kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kuwa ni wasanii na wajenzi wa uzuri wa kazi ya uumbaji inayopata chimbuko lake kutoka katika imani, ili hatimaye, waweze kumpenda na kumtukuza Mwenyezi Mungu asili ya uzuri na utakatifu wote. Kila mwamini anapaswa kutekeleza dhamana na utume huu kadiri ya maisha, wito na nafasi yake ndani ya Kanisa na jamii katika ujumla wake. Lengo ni kuwasaidia waamini kuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya matumaini, furaha, amani, udugu, wema na uzuri kwa watu wanaowazunguka. Hija ya kichungaji ya Baba Mtakatifu Francisko mjini Venezia, Dominika tarehe 28 Aprili 2024 imenogeshwa na kauli mbiu “Kukaa kwa umoja katika upendo wa Kristo.” Baba Mtakatifu ametembelea Banda la Maonesho kutoka Vatican yanayonogeshwa na kauli mbiu “Kwa macho Yangu.” Maonesho haya yanafanyika kwa ushirikiano kati ya Baraza la Kipapa la Utamaduni na Elimu pamoja na Idara ya Utawala wa Magereza sanjari na Wizara ya Sheria ya Italia. Baba Mtakatifu amewapongeza kwa dhamana na mchango wao katika jamii na kwamba, ujumbe wake mahususi kwa wasanii wote popote pale walipo ni kwamba, Ulimwengu mambo leo una haja ya wasanii na kwamba, hapo alipo anajisikia kama yuko nyumbani ndani ya Kanisa la “Maddalena.” Sanaa mara nyingi inakita mizizi yake kama “mji wa kimbilio, hali inayokinzana na vurugu, mifumo mbalimbali ya ubaguzi, ili kutoa utambulisho wa binadamu; tayari kujitambua, kujumuisha, kulinda, kuwaambata na kuwakumbatia wote.

Papa Francisko amekutana na kuzungumza na wasanii tarehe 28 Aprili 2024
Papa Francisko amekutana na kuzungumza na wasanii tarehe 28 Aprili 2024

Mtumishi wa Mungu Mussa katika Agano la Kale aliweka nyongeza ya mtandao wa miji mitatu ya makimbilio ya ng’ambo ya Mto Yordani. Rej. Kumb 4:41. Hii ni miji iliyowekwa ili kuzuia umwagaji wa damu ya watu wasiokuwa na hatia; kuratibu na kudhibiti ulipizaji wa kisasi, ili kuhakikisha kwamba, tunu msingi, utu na heshima vinalindwa na kudumishwa kwa kukumbatia na kuambata maridhiano. Hii ni changamoto kwa wasanii kuunda mtandao wa miji ya kimbilio, ili kushirikiana na wadau mbalimbali katika kuukomboa ulimwengu na mifumo ya ubaguzi, chuki dhidi ya wageni “Xenofobia”, ukosefu wa usawa wa kiikolojia pamoja na chuki dhidi ya maskini “Aporofobia”; matukio ambayo yanataka kuwatenga wengine, kwa mafao yake binafsi kwa kujikita katika uchoyo na ubinafsi. Huu ni mwaliko kwa wasanii kufikiria na kuanza kujikita katika miji ya kufikirika, ili kujenga na kudumisha udugu wa kibinadamu mahali popote pale walipo! Banda la Maonesho kutoka Vatican yanayonogeshwa na kauli mbiu “Kwa macho Yangu” mwaliko kwa wasanii na watu wenye mapenzi mema kujiangalia wao wenyewe, kwa kutambua kwamba, Kristo Yesu mwalimu wa kudumu, yuko pembeni mwao akiwaangalia na kuwatia shime na kwamba, sanaa inawaandaa watu kuwa na mwelekeo huu katika maisha yao. Sanaa inawaelimisha watu kuwajali na kuwasaidia wengine; ni mwono unaowaelimisha kuangalia kwa kutakafari, tayari kutofautisha kazi za sanaa zinazoandaliwa kupelekwa sokoni, kwa kujielekeza zaidi katika falsafa ya ubunifu; kwa kukazia na kulinda utakatifu wa watu wa Mungu pamoja na kuelimisha kutenda kazi. Maonesho haya yamefanyikia katika Gereza na Wanawake la Giudecca lililoko mjini Venezia, tukio ambalo linakutanisha chemchemi ya furaha na mateso, ili kuweza kukaa kwa pamoja.

Wasanii wawe ni wajenzi wa utu, heshima na haki msingi za binadamu
Wasanii wawe ni wajenzi wa utu, heshima na haki msingi za binadamu

Huu ni mwaliko wa kujenga na kudumisha utamaduni wa kusikiliza kwa makini kwa sababu kuna kitu cha kujifunza hapa. Baba Mtakatifu amewakumbuka wasanii marufu kama vile Frida Khalo, Corita Kent, Louise Bourgeois na wengine wengi. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kutoka katika sakafu ya moyo wake, ili kwamba sanaa iwasaidie waamini na watu wote wenye mapenzi mema kufungua macho yao, ili iwasaidie kuthamini kikamilifu mchango wa wanawake, kama wadau imara katika safari ya maisha ya mwanadamu. Mtakatifu Yohane Mbatizaji anatoa ushuhuda kwa Kristo Yesu. “Na hao walipokwenda zao, Yesu alianza kuwaambia makutano habari za Yohana, Mlitoka kwenda nyikani kutazama nini? Unyasi ukitikiswa na upepo? Mt 11:7. Baba Mtakatifu anawaalika wasanii kulihifadhi swali hili katika sakafu ya nyoyo zao, kwani hili ni swali linalowasukuma kuyaendea mapambazuko yajayo!   Kwa upande wake, Kardinali José Tolentino de Mendonça Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Utamaduni na Elimu ambaye pia ni Kamishna wa Banda la Sanaa kutoka Vatican amekazia mchago wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican katika kuboresha mahusiano kati ya Kanisa na wasanii na kwamba, hija ya kichungaji ya Baba Mtakatifu mjini Venezia ni changamoto ya kujikita katika uhuru, ili kila mtu kwa macho yake, aweze kujionea mwenyewe, kwa kufanya kazi kwa umoja na ushirikiano. Amewashukuru wasanii wote walioshiriki katika onesho hili.

Wasanii
28 April 2024, 15:05