Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko alipokutana na vijana mjini Venezia amewataka wawe ni mashuhuda wa tunu msingi na furaha ya Injili inayomwonesha Mungu akiwa kijana, na anayewapenda vijana. Baba Mtakatifu Francisko alipokutana na vijana mjini Venezia amewataka wawe ni mashuhuda wa tunu msingi na furaha ya Injili inayomwonesha Mungu akiwa kijana, na anayewapenda vijana.  (Vatican Media)

Hija ya Kichungaji ya Papa Francisko Venezia: Hotuba Kwa Vijana: Kusimama na Kuondoka

Baba Mtakatifu Francisko amewataka wawe ni mashuhuda wa tunu msingi na furaha ya Injili inayomwonesha Mungu akiwa kijana, na anayewapenda vijana, ili wagundue ndani mwao uzuri, tayari kufurahia maisha katika jina la Bwana, changamoto ni kusimama na kuondoka kama ilivyokuwa kwa Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa, tayari kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili sanjari na kumsaidia binamu yake Elizabeti aliyekuwa mhitaji kwa wakati ule.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Hija ya kichungaji ya Baba Mtakatifu Francisko mjini Venezia, Dominika tarehe 28 Aprili imenogeshwa na kauli mbiu “Kukaa kwa umoja katika upendo wa Kristo.” Viongozi wa Kanisa wajenge sanaa na utamaduni wa kusikiliza vijana kwa makini na kuzungumza nao kwa ujasiri unaofumbatwa katika ukweli na uwazi. Lengo ni kusaidia mchakato wa toba na wongofu wa kimisionari unaojikita katika maisha na utume wa Kanisa, kwa kusoma alama za nyakati, tayari kujibu kilio na matamanio halali ya vijana wa kizazi kipya sanjari na kutangaza na kushuhudia Injili ya matumaini kwa vijana wanaoonekana kuvunjika na kupondeka moyo! Mama Kanisa katika mbinu mkakati wake wa shughuli za kichungaji anataka kuwajengea vijana matumaini ya leo na kesho iliyo bora zaidi inayosimikwa katika: haki, amani; ustawi, maendeleo, utu na heshima ya binadamu. Vijana wafundwe kuthamini na kuenzi Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo. Wasindikizwe kwa imani, matumaini na mapendo, ili waweze kung’amua wito katika maisha yao na hatimaye, kufanya maamuzi magumu na endelevu!

Vijana ni jeuri, amana na utajiri wa Kanisa na Jamii katika ujumla wake
Vijana ni jeuri, amana na utajiri wa Kanisa na Jamii katika ujumla wake

Vijana ni amana na utajiri wa maisha na utume wa Kanisa na jamii katika ujumla wake. Changamoto za maisha ya kifamilia, kiuchumi, kijamii na kitamaduni; mambo yanayoibuka kwa kasi katika ulimwengu wa sayansi na maendeleo makubwa ya teknolojia yanapaswa kushughulikiwa kikamilifu kwa kuwajengea vijana uwezo wa kupambana na hali zao, bila kutafuta njia za mkato katika maisha! Madhara ya vita, njaa, magonjwa, rushwa na ufisadi ni kati ya mambo yanayochangia hali ngumu ya maisha ya vijana, kiasi cha kuwakatisha tamaa. Kuna haja ya kuimarisha utandawazi wa mshikamano utakaotoa fursa ya ajira, elimu, ustawi na maendeleo endelevu ya vijana kwa kuondokana na utamaduni usiojali wala kuthamini utu, maisha na haki msingi za binadamu. Vijana wajikite katika mchakato wa majadiliano ya kidini na kiekumene, ili kuondokana na misimamo mikali ya kidini na kiimani, mambo yanayohatarisha umoja, upendo, mshikamano na mafungamano ya kijamii.

Papa Francisko akikutana na vijana wa kizazi kipa kutoka Venezia
Papa Francisko akikutana na vijana wa kizazi kipa kutoka Venezia

Baba Mtakatifu Francisko alipokutana na vijana mjini Venezia amewataka wawe ni mashuhuda wa tunu msingi na furaha ya Injili inayomwonesha Mungu akiwa kijana, na anayewapenda vijana, ili wagundue ndani mwao uzuri, tayari wote kufurahia maisha katika jina la Bwana, changamoto na mwaliko wa kusimama na kuondoka kama ilivyokuwa kwa Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa, tayari kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili sanjari na kumsaidia binamu yake Elizabeti aliyekuwa mhitaji kwa wakati ule. Rej. Lk 1:39. Vijana wanaalikwa kusimama kwani wameumbwa kwa ajili ya maisha ya mbinguni, wasimame kutoka katika uchungu, tayari kuyainua macho yao mbinguni, tayari kupambana na changamoto za maisha kwa kutambua kwamba, ujana ni zawadi adhimu isiyokuwa na mbadala, na kwamba wanayo dhamana na wajibu wa kumshukuru Mungu kwa zawadi ya maisha na kwamba, Sala ya Baba Yetu ni ufunguo wa furaha ya siku, kwani kijana ni Mwana wa Mungu aliye juu mbinguni hata katika vikwazo na changamoto za maisha, vijana wajitahidi kusimama! Vijana wanapoteleza na kuanguka, Mwenyezi Mungu yuko tayari kuwashika mkono na kuwainua kama alivyofanya kwa Mtakatifu Petro Mtume, Maria Madgalena, Zakayo Mtoza ushuru pamoja na wengine wote, kwani Mwenyezi Mungu anatambua fika udhaifu na unyonge wa binadamu, tayari kuwashika mkono na kuwainua, jambo la msingi ni vijana kujitahidi kuwa waaminifu na wenye imani. Baba Mtakatifu anawahimiza vijana wa kizazi kipya kushirikishana mang’amuzi ya uwepo na upendo wa Mwenyezi Mungu katika maisha yao, kama wasifanye mambo kipweke pweke wala kibinafsi.

Papa Francisko akiwa mjini Venezia
Papa Francisko akiwa mjini Venezia

Vijana wahakikishe kwamba, wanakuwa ni marubani wa maisha yao na kamwe wasitawaliwe na luninga wala simu za viganjani, bali wajenge utamaduni wa kukutana na watu. Baba Mtakatifu anawaalika vijana kusimama ili kupokea zawadi na hatimaye, wao wenyewe wageuke na kuwa ni zawadi ya maisha kwa jirani zao wenye shida na mahangaiko mbalimbali na kamwe wasiruhusu washindwe na kutawaliwa na majonzi moyoni, tayari kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya jirani zao. Kama binadamu walioumbwa kwa sura na mafano wa Mungu kamwe wasithubutu kupoteza ule uzuri wa kazi ya uumbaji, tayari kutoka kwenye mitandao ya kijamii, tayari kuwa ni waundaji wa mambo mapya. Sala ya Baba Yetu ni sala inayobubujika kutoka katika sakafu ya nyoyo zao, inayoweza kumwilishwa katika upendo, kwa kumwiga Mungu katika uzuri na ukaribu wake; kwa kujisadaka bila ya kujibakiza, tayari kuleta mageuzi na kwamba, wajisadake bila woga. Baba Mtakatifu anawataka vijana wa kizazi kipya kusimama na kumfungulia Mungu nyoyo zao za maisha, tayari kutembea kifua mbele, huku wakiwa wameshikamana na wengine, daima wakiwa wamefumbatwa katika tunu msingi za Kiinjili katika njia ya maisha. Rej. Lk 17: 19.

Papa Vijana
28 April 2024, 15:40