Tafuta

Baba Mtakatifu amepata fursa ya kutembelea Gereza na Wanawake la Giudecca lililoko mjini Venezia kama fursa ya kukutana pamoja, kusali, kuonesha ukaribu wa Mungu katika maisha yao Baba Mtakatifu amepata fursa ya kutembelea Gereza na Wanawake la Giudecca lililoko mjini Venezia kama fursa ya kukutana pamoja, kusali, kuonesha ukaribu wa Mungu katika maisha yao  (Vatican Media)

Hija ya Kichungaji ya Papa Francisko Venezia: Hotuba Kwa Wafungwa Gerezani

Baba Mtakatifu amepata fursa ya kutembelea Gereza na Wanawake la Giudecca lililoko mjini Venezia kama fursa ya kukutana pamoja, kusali, kuonesha ukaribu wa Mungu pamoja na kushirikisha hisia za ujenzi wa udugu wa kibinadamu na kwamba, ametoka Gerezani humo akiwa amepyaishwa na kuwa ni mtu mwingine kabisa. Magereza ni mahali pagumu sana pa kuishi: kuna mafuriko ya wafungwa, uhaba wa rasimali fedha na watu; uvunjifu wa haki, utu na heshima; vurugu

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, magereza yanapaswa kuboreshwa zaidi, ili kulinda na kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu. Inasikitisha kusikia na kuona kwamba, magereza yanageuka kuwa ni mahali pa vurugu, uvunjifu wa sheria, kanuni na taratibu, maadili na utu wema; mahali ambapo utu na heshima ya binadamu vinasiginwa kwa kiasi kikubwa! Wafungwa wanapaswa kujengewa imani na matumaini ya kuwa na leo na kesho iliyo bora zaidi wanapohitimisha adhabu zao magerezani na mahabusu. Baba Mtakatifu anawataka watu kuondokana na tabia ya kujinyakulia madaraka mikononi mwao kwa kuwahukumu wengine kwani hawana vigezo sahihi. Ni kweli kabisa kwamba, mfungwa gerezani amevunja sheria na hivyo kushindwa kuishi kwa ustaharabu. Gerezani, mfungwa anatumikia adhabu yake, lakini ikumbukwe kwamba, hata katika mazingira yote haya, bado anapendwa na kuthaminiwa na Mwenyezi Mungu. Hakuna mtu anayeweza kuingia katika dhamiri yake na kuona ni kwa jinsi gani mfungwa huyu anavyoteseka pamoja na kusikitika kutokana na makosa aliyotenda!

Maisha gerezani kuna changamoto pevu.
Maisha gerezani kuna changamoto pevu.

Wakristo wawasaidie watu kutambua dhambi na makosa yao, tayari kuchunguza dhamiri na kuanza safari ya toba na wongofu wa ndani. Ukosefu wa uhuru kamili ni kati ya adhabu kubwa ambazo mwanadamu anaweza kupata hapa duniani. Hali hii inaweza kufikia hatua mbaya kabisa, ikiwa kama mazingira ya magereza ni hatarishi kwa usalama, utu na heshima yao kama binadamu. Changamoto kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema katika mazingira kama haya ni kusimama kidete kutafuta mbinu za kuweza kuwarejeshea tena wafungwa hadhi na utu wao kama binadamu. Hiki kiwe ni kipindi cha toba na wongofu wa ndani, tayari kuanza maisha mapya!

Magereza yasaidie kukuza na kudumisha karama na mapaji ya wafungwa
Magereza yasaidie kukuza na kudumisha karama na mapaji ya wafungwa

Hija ya kichungaji ya Baba Mtakatifu Francisko mjini Venezia, Dominika tarehe 28 Aprili imenogeshwa na kauli mbiu “Kukaa kwa umoja katika upendo wa Kristo.” Baba Mtakatifu amepata fursa ya kutembelea Gereza na Wanawake la Giudecca lililoko mjini Venezia kama fursa ya kukutana pamoja, kusali, kuonesha ukaribu wa Mungu pamoja na kushirikisha hisia za ujenzi wa udugu wa kibinadamu na kwamba, ametoka Gerezani humo akiwa amepyaishwa na kuwa ni mtu mwingine kabisa. Baba Mtakatifu anasema kuna watu wameingiza magerezani kwa mateso na machungu, lakini ikumbukwe kwamba kila mwanadamu anabeba ndani mwake: madonda na makovu; ni zawadi yenye thamani kubwa machoni mwa Mungu, tayari kujisadaka na kuwashirikisha wengine.

Papa anasema gereza ni mahali pagumu sana pa kuishi
Papa anasema gereza ni mahali pagumu sana pa kuishi

Baba Mtakatifu anasema, gereza ni mahali pagumu sana pa kuishi, magereza mengi yamefurika, kuna uhaba wa miundo mbinu na rasilimali watu na fedha; ni mahali ambapo kumekuwepo na uvunjifu wa haki, amani na utulivu na hivyo kuwa ni chanzo cha mateso na mahangaiko makubwa kwa wafungwa na wale walioko magerezani na mahabusu. Lakini magereza panaweza kugeuka na kuwa ni mahali pa kupyaisha maisha kiutu na kimwili; kwa kukazia utu, heshima na haki msingi za binadamu; mahali pa kukuza karama na mapaji ambayo pengine kutokana na hali na mazingira ya wafungwa yalifichwa na sasa yanaweza kuibuliwa na kuanza kutumika kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Ametembelea gereza kuwaonesha ukaribu wa Mungu katika maisha yao
Ametembelea gereza kuwaonesha ukaribu wa Mungu katika maisha yao

Huu unaweza kuwa ni mwanzo wa ujenzi wa maisha kwa kuangalia, kupima na kuthamini kwa ujasiri maisha ya mtu binafsi, kwa kuzingatia mambo msingi katika maisha, tayari kutembea katika mwanga, tayari kuanza mchakato wa ujenzi wa maisha yake. Magereza na mahabusu yatoe fursa kwa wafungwa na mahabusu kukua: kiroho na kimwili; kitamaduni na kitaaluma, kwa kuupatia utu nafasi mpya. Itakumbukwa kwamba, maisha ya mwanadamu yamesheheni makosa na mapungufu ya kibinadamu yanayopaswa kusamehewa; madonda ya kugangwa na kuponywa na kwamba, watu wote wanaweza kugangwa na kuponywa; kwa wale waliponywa kubeba ndani mwao uponyaji; waliosamehewa kuwa ni vyombo na mashuhuda wa msamaha na wale waliozaliwa upya, wanabeba ndani mwao maisha mapya, huku wakiwa na matumaini ya leo na kesho iliyo bora zaidi kwa kutambua kwamba, wakati uliokubalika ndio sasa; tazama, siku ya wokovu ndiyo sasa. Rej. 2Kor 6:2. Kila siku iwe ni mwanzo wa maisha mapya na kwamba, Bikira Maria awe ni Mama wa huruma kwa wote, changamoto na mwaliko wa kutokata wala kujikatia tamaa, bali kusonga mbele kwa ari na ujasiri.

Magereza
28 April 2024, 15:23