Tafuta

Maendeleo makubwa ya teknolojia ya akili mnemba “Artificial Intelligence": Fursa na vitisho vya teknolojia ya akili mnemba Maendeleo makubwa ya teknolojia ya akili mnemba “Artificial Intelligence": Fursa na vitisho vya teknolojia ya akili mnemba  (AFP or licensors)

Ujumbe wa Papa Francisko Kwenye Mkutano wa Teknolojia ya Akili Mnemba, Paris 2025

Ni katika muktadha wa maendeleo makubwa ya teknolojia ya akili mnemba “Artificial Intelligence, viongozi kutoka katika takribani nchi mia moja kwa kushirikiana na wadau wengine wa maendeleo kuanzia tarehe 10 hadi tarehe 11 Februari 2025 wanakutana Jijini Paris, nchini Ufaransa, kwenye mkutano wa kilele unaojadili kuhusu fursa na vitisho vya maendeleo ya teknolojia ya akili mnemba. Utu, heshima, haki msingi za binadamu pamoja na kanuni maadili vipewe kipaumbele

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, kuna umuhimu wa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa utu, heshima na kanuni maadili ili kujibu changamoto za kijamii zinazoendelea kuibuliwa na maendeleo ya teknolojia ya akili mnemba kiasi cha kuathiri utu wa binadamu. Teknolojia huzaliwa kwa kusudi na, katika athari zake kwa jamii ya wanadamu, daima huwakilisha aina ya utaratibu katika mahusiano ya kijamii na mpangilio wa mamlaka, hivyo kuwawezesha watu fulani kufanya vitendo maalum huku wakiwazuia wengine kufanya tofauti.  Kwa njia iliyo wazi zaidi au kidogo, mwelekeo huu wa nguvu wa teknolojia daima unajumuisha mtazamo wa ulimwengu wa wale walioivumbua tekenolojia hii na kuiendeleza. Teknolojia ya akili mnemba isaidie kujenga leo na kesho iliyo njema na bora zaidi, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Kumbe, msukumo wa kimaadili ni muhimu sana katika maendeleo ya teknolojia ya akili mnemba. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba watu wote wenye mapenzi mema wataendelea kushirikiana kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi; kwa kusimama kidete kuwalinda na kuwatetea wanyonge na kwamba, maendeleo ni kwa ajili ya wengi. Teknolojia ya akili mnemba inaendelea kushika kasi ya ajabu katika maendeleo ya binadamu. Viongozi wa dini mbalimbali duniani wanahimizwa kushikamana kama ndugu, ili kutoa msukumo wa pekee katika ujenzi wa haki, amani na udugu wa kibinadamu. Viongozi wa kidini wanasema, ni dhamana na wajibu wa viongozi wa kidini kuhakikisha kwamba, wanashikamana kwa dhati ili kukabiliana na changamoto za maendeleo makubwa ya teknolojia ya akili mnemba; kwa kuzingatia kanuni maadili na utu wema na kwamba, kuna haja ya kuwa na uongozi utakaosimamia kanuni maadili ya teknolojia ya akili mnemba.

Mkutano wa kilele wa maendeleo ya teknolojia ya akili mnemba
Mkutano wa kilele wa maendeleo ya teknolojia ya akili mnemba   (AFP or licensors)

Teknolojia ya akili mnemba inatumia hali ya binadamu, changamoto kwa binadamu wenyewe ni kuwa wazi kwa Mwenyezi Mungu pamoja na binadamu wenzao na kwamba, teknolojia hii inawaelekeza binadamu kwa maendeleo ya siku zijazo. Dhamiri ndicho kiini cha siri zaidi cha binadamu na hekalu la Mungu, ambamo sauti yake inasikika na utimilifu wa sheria hii ni upendo kwa Mungu na jirani. Baba Mtakatifu anataka kuona kwamba: Utu, heshima, haki msingi, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi yanaheshimiwa katika kipindi hiki cha maendeleo makubwa ya teknolojia ya akili mnemba. Ni hatari sana ikiwa kama teknolojia ya akili mnemba itatumika katika vita, kumbe, haki na amani vinapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza. Ni katika muktadha wa maendeleo makubwa ya teknolojia ya akili mnemba “Artificial Intelligence” viongozi kutoka katika takribani nchi mia moja kwa kushirikiana na wadau wengine wa maendeleo kuanzia tarehe 10 hadi tarehe 11 Februari 2025 wanakutana Jijini Paris, nchini Ufaransa, kwenye mkutano wa kilele unaojadili kuhusu fursa na vitisho vya maendeleo ya teknolojia ya akili mnemba.

Maendeleo makubwa ya teknolojia ya akili mnemba: fursa na vitisho vyake
Maendeleo makubwa ya teknolojia ya akili mnemba: fursa na vitisho vyake   (AFP or licensors)

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe aliomwandikia Rais Emmnuel Macron wa Ufaransa anakazia umuhimu wa udhibiti wa mwanadamu katika maendeleo makubwa ya teknolojia ya akili mnemba kwa sababu teknolojia hii kwa sasa inaonekana kama tishio la utu, heshima na haki msingi za binadamu. Baba Mtakatifu anawapongeza washiriki kwa kutoa kipaunbele cha pekee, katika kulinda na kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu mintarafu kweli za kiutu, kijamii, kiuchumi na kitamaduni. Huu ni mkutano unaowashirikisha wadau wakuu wa maendeleo ya teknolojia ya akili mnemba, kutoka sehemu mbalimbali za dunia. Wanasayansi waongozwe na “moyo” ambao kimsingi ni sakafu ya hisia na kwamba, hisia hizi kamwe haziwezi kumdanganya mtu! Moyo wa mwanadamu ni muhimu. Hili ni suala la kuwa wazi katika kuangalia namna mbalimbali ambazo hazizuii ubunifu na maendeleo ya mwanadamu bali kuzielekeza nguvu hizo kwenye njia mpya. Rej. Laudato si, 191.

Utu, heshima, haki msingi za binadamu ni mambo muhimu katika teknolojia
Utu, heshima, haki msingi za binadamu ni mambo muhimu katika teknolojia   (AFP or licensors)

Baba Mtakatifu Francisko anazungumzia kuhusu changamoto za maendeleo ya sheria za Kimataifa zinazopaswa kukazia pamoja na mambo mengine ni pamoja na: Umoja, mwongozo utakaoratibu maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia ya kidigitali; kwa kuheshimu na kulinda haki msingi za binadamu, ili kudumisha misingi ya haki na amani sanjari na kusikiliza na kuzingatia maoni ya watu mbalibali mintarafu teknolojia ya akili mnemba. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, Mkutano wa Paris kuhusu fursa na vitisho vya maendeleo ya teknolojia ya akili mnemba utaunda Jukwaa la Kimataifa kitakachokuwa ni chombo cha maendeleo katika mapambano dhidi ya umaskini pamoja na kulinda na kudumisha tamaduni na lugha mahalia, hali itakayowawezesha walimwengu kuunda takwimu zinazoweza kutumika katika teknolojia ya akili ya akili mnemba, ili kuakisi ukweli wa tofauti na utajiri unaobubujika kutoka katika familia kubwa ya binadamu. Baba Mtakatifu anasema, hivi karibuni Vatican imechapisha Angalisho kuhusu Uhusiano kati ya Akili Mnemba pamoja na Akili ya Binadamu, mambo yanayojadiliwa kwenye mkutano huu. Kumbe, kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kujikita katika kuangalia athari za teknolojia ya akili mnemba katika mahusiano ya kijamii, mawasiliano na elimu, huku binadamu akipewa kipaumbele cha kwanza, katika ustawi na maendeleo yake kiroho na kiutu, ili aweze kuwajibika zaidi na kuendelea kuwa wazi kwa wahitaji na maskini. Mabadiliko ya kweli hayana budi kuzingatia utu, heshima na haki msingi za binadamu.

Akili Mnemba Paris 2025
11 Februari 2025, 14:36