Tafuta

Baraza la Maaskofu Katoliki Brazil, CNBB, tarehe 5 Machi 2025 limezindua Kampeni ya 61 ya Kwaresima ya Udugu wa Kibinadamu Baraza la Maaskofu Katoliki Brazil, CNBB, tarehe 5 Machi 2025 limezindua Kampeni ya 61 ya Kwaresima ya Udugu wa Kibinadamu  

Kampeni ya 61 ya Kwaresima ya Udugu wa Kibinadamu Kwa Mwaka 2025: Mazingira!

Baraza la Maaskofu Katoliki Brazil, CNBB, tarehe 5 Machi 2025 limezindua Kampeni ya 61 ya Kwaresima ya Udugu wa Kibinadamu kwa kuongozwa na mada “Udhaifu na Umuhimu wa Ikolojia” na hivyo kunogeshwa na kauli mbiu: “Mungu akaona kila kitu alichokifanya, na tazama, ni chema sana.” Mwa 1:31. Baba Mtakatifu Francisko anawataka watu wa Mungu nchini Brazil kusimama kidete kulinda, kutunza na kudumisha mazingira bora nyumba ya wote; utume wa wote.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Jumatano ya Majivu ni mwanzo wa Kipindi cha Kwaresima, Siku 40 za toba na wongofu wa ndani unaosimikwa katika: Sala, Neno la Mungu, Maisha ya Kisakramenti, Kufunga na Matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Baba Mtakatifu Francisko kwa ufupi kabisa anasema kwamba, Kwaresima ni safari inayofumbata maisha ya mtu mzima kiroho na kimwili. Ni mchakato wa kutoka katika utumwa kuelekea katika uhuru wa kweli, unaomwelekeza mwamini kwa Baba yake wa mbinguni asili ya huruma na chemchemi ya mapendo. Ni safari ya kumrudia tena Kristo Yesu ili kumshukuru kwa zawadi ya mateso, kifo na ufufuko uletao wokovu, uzima na maisha ya milele. Hii pia ni safari ya kumrudia Roho Mtakatifu, ili kujipatanisha na Mwenyezi Mungu pamoja na jirani, tayari kuonja ile furaha ya kupendwa na Mungu. Kwaresima ni safari ya kiroho inayowaandaa waamini kuadhimisha Fumbo la Pasaka na hatimaye kulitolea ushuhuda wa maisha adili na matakatifu. Kwaresima ya Mwaka huu, inachukua uzito wa pekee, kwani ni sehemu ya Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo yanayonogeshwa na kauli mbiu: “Peregrinantes in spem” yaani: “Mahujaji wa matumaini.” Huu ni muda muafaka wa kupyaisha imani, matumaini na mapendo thabiti, kwa kuishi kama ndugu wamoja, sanjari na kusikiliza pamoja na kujibu kilio cha Dunia Mama na Kilio cha Maskini. Ni muda wa toba na wongofu wa ndani na wa kiikolojia, tayari kusimama kidete kulinda na kutunza mazingira bora nyumba ya wote.

Watu wa Mungu lindeni kuhifadhi na kutuza mazingira nyumba ya wote
Watu wa Mungu lindeni kuhifadhi na kutuza mazingira nyumba ya wote

Ni katika muktadha huu, Baraza la Maaskofu Katoliki Brazil, CNBB, tarehe 5 Machi 2025 limezindua Kampeni ya 61 ya Kwaresima ya Udugu wa Kibinadamu kwa kuongozwa na mada “Udhaifu na Umuhimu wa Ikolojia” na hivyo kunogeshwa na kauli mbiu: “Mungu akaona kila kitu alichokifanya, na tazama, ni chema sana.” Mwa 1:31.Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa Baraza la Maaskofu Katoliki Brazil, CNBB, anaitaka Jumuiya ya Kimataifa kusimama kidete kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote, kwani hii ni sehemu ya kazi ya Uumbaji ambayo Mwenyezi Mungu amemkabidhi mwanadamu na kwamba, anayo dhamana ya kuhakikisha kwamba, anakirithisha kizazi kijacho mazingira bora na salama. Baba Mtakatifu anawapongeza na kuwashukuru Maaskofu Katoliki wa Brazil kwa kuendesha Kampeni ya Kwaresima ya Udugu wa Kibinadamu, mwaliko kwa watu wa Mungu kufanya tafakari ya kina, kuhusu utunzaji bora wa mazingira, kadiri ya Maandiko Matakatifu. Huu ni mwaliko kwa watu wa Mungu nchini Brazil, kufanya toba na wongofu wa ndani unaozamishwa na hivyo kukita mizizi yake katika Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko kuhusu utunzaji bora wa mazingira: “Laudato si” yaani “Sifa kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote” uliochapishwa tarehe 24 Mei 2015 na kukamilishwa na Waraka wa Kitume wa “Laudate deum” yaani “Asifiwe Mungu Kwa Ajili ya Viumbe Vyake Vyote.”

Utubzahu bora wa mazingira nyumba ya wote ni wajibu wa wote
Utubzahu bora wa mazingira nyumba ya wote ni wajibu wa wote

Waraka huu unakita ujumbe wake juu ya athari za mabadiliko ya tabianchi duniani, upinzani na hali ya kuchanganyikiwa, shughuli za kibinadamu, Uharibifu na hatari zake; kukua kwa dhana ya kiteknolojia, tathmini mpya ya matumizi bora ya madaraka; Udhaifu wa sera za kimataifa na umuhimu wa kusanidi upya mfumo wa pande nyingi. Mikutano ya Kimataifa juu ya Mabadiliko ya Tabia nchi, ufanisi na kuanguka kwake; Matarajio ya Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi wa COP 28 huko Dubai, 2023. Motisha za maisha ya kiroho: katika mwanga wa imani sanjari na kutembea kwa pamoja katika ushirika na uwajibikaji. Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wa Kitume wa “Laudate deum” yaani “Asifiwe Mungu Kwa Ajili ya Viumbe Vyake Vyote” juu ya athari za mabadiliko ya tabianchi anasema na kwamba, watu wengi wanaathrika sana mintarafu afya ya binadamu, kazi, upatikanaji wa rasilimali, makazi pamoja na uhamiaji wa nguvu. Haya ni matatizo ya kijamii yanayogusa na kutikisa utu, heshima, haki msingi na maisha ya binadamu. Kumbe, huu ni mwaliko kwa watu wote wa Mungu kufanya toba na wongofu wa ndani, ili kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote.

Utu, heshima na haki msingi za binadamu zilindwe
Utu, heshima na haki msingi za binadamu zilindwe

Baba Mtakatifu anakaza kusema, Kampeni ya Kwaresima kwa mwaka 2025 ni mchango wa Kanisa Katoliki nchini Brazil katika maadhimisho ya Mkutano wa 30 wa nchi Wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi COP30 utakaofanyika huko Belèm do Parà, nchini Brazil kuanzia tarehe 10-21 Novemba 2025. Huu ni mwaliko kwa Jumuiya ya Kimataifa kushinda changamoto ya uharibifu wa mazingira nyumba ya wote, tayari kusimama kidete kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, Kipindi hiki cha Kwaresima kitazaa matunda mengi ya matumaini, kama sehemu ya maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo. Watu wa Mungu nchini Brazil, wajenge utamaduni wa kushikamana na kusaidiana; kwa kujikita katika toba na wongofu wa Kiinjili, tayari kusimama kidete kudumisha ikolojia. Mwishoni mwa ujumbe wake, Baba Mtakatifu anawaweka watu wote wa Mungu nchini Brazil nchini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria wa Aparecida, lakini zaidi kwa wote wanaojisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya ulinzi na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote.

Kampeni ya Kwaresima 2025
06 Machi 2025, 15:57