Tafuta

Baraza la Makardinali kwa moyo wa shukrani, upendo na mshikamano linapenda kutoa shurani zake za dhati kwa wakuu wa Serikali, Makanisa, Jumuiya za Wakristo, waliohudhuria au kutuma wawakilishi wao kwenye mazishi ya Papa Francisko Baraza la Makardinali kwa moyo wa shukrani, upendo na mshikamano linapenda kutoa shurani zake za dhati kwa wakuu wa Serikali, Makanisa, Jumuiya za Wakristo, waliohudhuria au kutuma wawakilishi wao kwenye mazishi ya Papa Francisko   (ANSA)

Baraza la Makardinali Latuma Salam za Shukrani Kwa Watu wa Mungu

Kwa hakika, mazishi ya Papa Papa Francisko yameonesha moyo wa upendo na mshikamano wa udugu wa kibinadamu na kwamba, uwepo wao limekuwa ni jambo la faraja sana kwa Mama Kanisa katika kipindi hiki cha majonzi makubwa. Hii ilikuwa ni heshima kubwa kwa Hayati Baba Mtakatifu Francisko aliyejipambanua na hatimaye akasimama kidete kuwa ni chombo na shuhuda wa imani, amani na ujenzi wa udugu wa kibinadamu na watu wote wa Mataifa. Shukrani Sana!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kardinali Kevin Joseph Farrell, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Walei, Familia ambaye pia “Camerlengo” mkuu wa Kanisa Katoliki. Huyu ni kiongozi mkuu wa shughuli za Kanisa wakati kunapotokea kwamba, Kiti cha Khalifa wa Mtakatifu Petro kiko wazi kwa sababu mbalimbali. Jumatatu ya Pasaka, tarehe 21 Aprili 2025 alitangaza kwa masikitiko na majonzi makubwa kifo cha Baba Mtakatifu Francisko, aliyekuwa na umri wa miaka 88 kilichotokea Jumatatu tarehe 21 Aprili 2025 majira ya Saa 1:35 Asubuhi kwa Saa za Ulaya sawa na Saa 2:35 Asubuhi kwa Saa za Afrika Mashariki na Kati. Katika tamko lake, alisema, Baba Mtakatifu Francisko ni kiongozi aliyejisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Katika maisha na utume wake amewafundisha watu wa Mungu umuhimu wa kutangaza na kumwilisha tunu msingi za maisha ya Kiinjili kwa uaminifu, ujasiri na upendo kwa wote, upendeleo wa pekee ikiwa ni kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa vipaumbele vya jamii. Mama Kanisa anamshukuru sana Hayati Baba Mtakatifu Francisko kwa ushuhuda na mfano wa maisha yake kama mfuasi wa Kristo Yesu, Kanisa linapenda kuiweka roho ya Hayati Baba Mtakatifu Francisko kwenye huruma na upendo unaobubujika kutoka katika Fumbo la Utatu Mtakatifu.

Shukrani kwa watu wa Mungu kwa uwepo na ushiriki wao kwa mazishi
Shukrani kwa watu wa Mungu kwa uwepo na ushiriki wao kwa mazishi   (ANSA)

Ni katika muktadha huu, Kardinali Giovanni Battista Re, Dekano wa Baraza la Makardinali, Jumamosi tarehe 26 Aprili 2025 amewaongoza watu wa Mungu katika maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kumwombea Hayati Baba Mtakatifu Francisko pumziko la amani, furaha na maisha ya uzima wa milele, nyumbabni kwa Baba wa milele, ambako furaha yake haina mwisho. Kardinali Giovanni Battista Re, katika mahubiri yake kwa ufupi kabisa alitoa muhtasari wa maisha na utume wa Hayati Baba Mtakatifu Francisko, kama shuhuda wa huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu; kwa kusimama kidete kulinda na kutetea utu, heshima na haki msingi za binadamu na hasa maskini na wale wote waliokuwa wanasukumizwa pembezoni mwa jamii. Alisimama kidete kuragibisha umuhimu wa utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote kwani uharibifu wa mazingira ni chanzo cha umaskini mkubwa. Baba Mtakatifu Francisko alikazia ujenzi wa udugu na urafiki wa kijamii ili kulinda na kudumisha misingi ya haki, amani na utunzaji bora wa mazingira. Kimsingi vita ni kielelezo cha kushindwa kwa binadamu wote, kumbe, kuna haja ya kujenga na kudumisha mchakato wa ujenzi wa madaraja ya kuwakutanisha watu wote kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Ujumbe wa Tanzania kwenye mazishi ya Papa Francisko
Ujumbe wa Tanzania kwenye mazishi ya Papa Francisko

Baraza la Makardinali kwa moyo wa shukrani, upendo na mshikamano linapenda kutoa shukrani zake za dhati kwa wakuu wa Serikali, Makanisa, Jumuiya za Wakristo, waliohudhuria au kutuma wawakilishi wao kwenye mazishi ya Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi tarehe 26 Aprili 2025. Baraza la Makardinali linawashukuru pia wawakilishi wa dini mbalimbali duniani, waliohudhuria mazishi haya. Kwa hakika, mazishi haya yameonesha moyo wa upendo na mshikamano wa udugu wa kibinadamu na kwamba, uwepo wao limekuwa ni jambo la faraja sana kwa Mama Kanisa katika kipindi hiki cha majonzi makubwa. Hii ilikuwa ni heshima kubwa kwa Hayati Baba Mtakatifu Francisko aliyejipambanua na hatimaye akasimama kidete kuwa ni chombo na shuhuda wa imani, amani na ujenzi wa udugu wa kibinadamu na watu wote wa Mataifa. Baraza la Makardinali kwa namna ya pekee, linaipongeza Serikali ya Italia na viongozi wake; wadau wa sekta ya mawasiliano ya jamii kwa kazi kubwa waliyoifanya kwa ajili ya kuwahabarisha watu wa Mungu kile kilichokuwa kinaendelea hapa mjini Vatican. Makardinali wanawashukuru na kuwapongeza wafanyakazi wa Vatican kwa moyo wa ukarimu, sadaka na majitoleo yao, yaliyofanikisha mambo yote yakatendeka katika hali ya usalama na amani. Baraza la Makardinali, hatimaye, linawapongeza vijana wenye umri chini ya miaka ishirini, waliohudhuria Jubilei yao sanjari na kushiriki mazishi ya Baba Mtakatifu Francisko. Vijana hawa wameonesha na kushuhudia Uso wa Kanisa hai la Kristo Yesu Mfufuka pamoja na watu wote wa Mungu katika ujumla wao, wanapoendelea kutembea katika matumaini kwa siku zijazo.

Watu wa Mungu walifurika kwenye mazishi ya Papa Francisko
Watu wa Mungu walifurika kwenye mazishi ya Papa Francisko   (ANSA)

Baraza la Makardinali, katika mkutano wake wa tano, Jumatatu tarehe 28 Aprili 2025 limeamua kwamba, mchakato wa uchaguzi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro uanze rasmi Jumatano tarehe 7 Mei 2025. Kuna jumla ya Makardinali 135 wenye haki ya kupiga na kupigiwa kura, lakini wanaoshiriki ni 133. Kuna Makardinali kutoka katika nchi 15 ambao wanashiriki kwa mara ya kwanza katika uchaguzi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro. Muda wa kumaliza uchaguzi huu, bado unaendelea kubaki kitendawili. Kadiri ya Katiba ya Kitume ya “Universi Dominici Gregis” iliyotungwa na Mtakatifu Yohane Paulo II kunako tarehe 22 Februari 1996, Idadi ya Makardinali wanaopaswa kupiga au kupigiwa kura ni 120, lakini, idadi hii imekuwa ikizidi mara zote. Ni katika muktadha huu, Kardinali Giovanni Angelo Becciu, kwa kutanguliza ustawi, maendeleo na mafao ya Kanisa na hivyo kusaidia katika ujenzi wa ushirika, amani na utulivu wa mkutano wa uchaguzi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro, ameamua kwa ridhaa yake mwenyewe kutokushiriki na kwamba, ana matumaini juu ya vyombo vya sheria na haki, hatimaye vitaweza kumwondolea hatia iliyoko mbele yake na hivyo kuwa mtu huru zaidi.

Baraza la Makardinali linawashukuru watu wa Mungu kwa uwepo na ushiriki
Baraza la Makardinali linawashukuru watu wa Mungu kwa uwepo na ushiriki   (ANSA)

Waamini wanaalikwa kufunga na kusali, ili kuwasindikiza Makardinali katika tukio hili lenye umuhimu wa pekee katika maisha na utume wa Kanisa. Kardinali Giovanni Battista Re, Dekano wa Baraza la Makardinali, Jumatano tarehe 7 Mei 2025 ataongoza Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya Uchaguzi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro: “Pro eligendo Romano Pontifice.” Ibada hii ya Misa Takatifu itaanza majira ya Saa 4:00 Asubuhi kwa Saa za Ulaya, sawa na Saa 5:00 kwa Saa za Afrika Mashariki na Kati. Jumatano jioni, majira ya Saa 10: 30 za Jioni kwa Saa za Ulaya sawa na Saa 11:30 kwa Saa za Afrika Mashariki na Kati, Makardinali wataanza kuingia kwenye Kikanisa cha Sistina, tayari kuanza mkutano wa Uchaguzi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro “Conclave”, kwa kujifungia huko ndani kwa ufunguo.  

Baraza la Makardinali

 

30 Aprili 2025, 15:31