Dhamana na Utume wa Makardinali Katika Maisha na Utume wa Kanisa
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Ukulu wa Mtakatifu Petro ni kielelezo cha mamlaka aliyopewa na Kristo Yesu ili kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu katika kifungo cha upendo. Mtume Petro alikirimiwa neema ya pekee iliyomwezesha kumkiri Kristo Yesu kuwa ni Mwana wa Mungu na hivyo kupewa funguo, kama Askofu wa kwanza wa Roma na baada yake wako waandamizi wake, waliopewa dhamana ya kutangaza na kushuhudia: huruma, upendo na msamaha unaobubujika kutoka kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. “Kiti cha ukulu wa Mtakatifu Petro” ni mahali ambapo Askofu mkuu wa Jimbo la Roma anakaa na kuongoza na kwamba, Kanisa kuu ni ishara ya mamlaka ya Askofu na mafundisho yake ya Kiinjili ambayo kama Askofu, mrithi wa Mitume anaitwa, kulinda na kuyasambaza mafundisho hayo kwa Jumuiya za Kikristo.
Mababa wa Kanisa wanasema, Kanisa kuu la kwanza kabisa ni katika “Chumba cha juu ambako Kristo Yesu walikuwa wamekusanyika kwa Karamu ya Mwisho na kupokea pamoja na Bikira Maria zawadi ya Roho Mtakatifu. Rej. Mt 26: 17-25; Mk 14: 12-21; na Yn 13:21-30. Baadaye, Mtume Petro alihamia Antiokia, mji uliohubiriwa na Barnaba na Paulo na ambapo wanafunzi wa Kristo Yesu waliitwa "Wakristo" kwa mara ya kwanza (Mdo. 11:6). Mwenyezi Mungu katika huruma na upendo wake wa daima alitaka kuwakusanya watoto wake waliotawanyika sehemu mbalimbali za dunia ili wawe wamoja. Akamtuma Mwanaye wa Pekee Kristo Yesu, ili awe: Mwalimu, Mfalme na Kuhani wa watu wote. Akamtuma pia Roho Mtakatifu, Bwana na Mleta uzima, asili ya muungano na umoja wa Kanisa katika: fundisho la Mitume, Ushirika, Ekaristi Takatifu na Sala. Katika ushirika wa Kikanisa yapo pia Makanisa maalum (Ecclesiae particulares) yashikayo mapokeo yao wenyewe, bila kuathiri mamlaka kuu ya Kiti cha Petro Mtume kinachosimamia ushirika wote wa mapendo, hulinda tofauti za haki zilizopo na kuendelea kudumisha ushirika wa Kanisa la Kristo. Hivyo, watu wote wanaitwa kwenye ushirika huu wa Kikatoliki wa Taifa la Mungu, ambao huashiria na kuhamasisha amani timilifu, ili wote wanaoitwa kwa neema ya Mungu wapate wokovu. Rej. LG 13.
Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanasema, katika Kanisa hili la Kristo Yesu, Kuhani Mkuu wa Roma, aliye mwandamizi wa Mtakatifu Petro, ambaye Kristo Yesu alimkabidhi kondoo na wanakondoo wake ili awachunge, kwa agizo la kimungu amepokea mamlaka ya juu kabisa, kamili na yanayojitegemea na ya jumla kwa ajili ya huduma ya roho za watu “Curam animalum.” Hivyo basi, kwa kuwa amewekwa kuwa mchungaji wa waamini wote, ili kukuza manufaa ya wote na ya Kanisa zima na pia ya Makanisa mahalia, anashika mamlaka ya juu ya kawaida juu ya Makanisa yote. Kwa upande mwingine na Maaskofu wamewekwa na Roho Mtakatifu kuwa waandamizi wa Mitume kama wachungaji wa watu, na pamoja na Baba Mtakatifu na chini ya Mamlaka yake, wanao utume wa kudumisha kazi ya Kristo Mchungaji wa milele, kwa sababu Kristo Yesu aliwapa Mitume na waandamizi wao agizo na mamlaka ya kuwafundisha mataifa yote, ya kuwatakatifuza watu katika ukweli na kuwachunga. Rej. Christus Dominum, n. 2-3.
Hayati Baba Mtakatifu Francisko aliwahi kusema lengo la kuwa na Makardinali wawakilishi kutoka sehemu mbalimbali za dunia ni kuweza kushuhudia Ukatoliki wa Kanisa; kuendeleza umoja wa Kanisa na Khalifa wa Mtakatifu Petro pamoja na Makanisa mahalia. Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican wanasema, kusudi uaskofu uwe na umoja usiogawanyika, Kristo Yesu alimweka Mtakatifu Petro, juu ya Mitume wengine, na katika yeye akatia chanzo na msingi unaodumu na unaoonekana wa umoja wa imani na ushirika. Kimsingi Makardinali ni washauri wakuu wa Khalifa wa Mtakatifu Petro katika maisha na utume wake. Makardinali hawa ni sehemu ya viongozi wa Kanisa la Roma na wanashiriki katika huduma ya kitume. Makardinali wanapaswa kuwa ni vyombo na mashuhuda wa Kristo Yesu na Injili yake sehemu mbalimbali za dunia. Wanatekeleza dhamana na wajibu wao kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Makardinali wanakiri kanuni ya imani na kula kiapo cha utii kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro. Wanavikwa kofia nyekundu ya kikardinali alama na kielelezo cha heshima ya ukardinali. Lakini, ikumbukwe kwamba, alama nyekundu maana yake ni kwamba, wao wako tayari kujisadaka bila ya kujibakiza kiasi hata cha kumwaga damu yao kwa ajili ya imani na usalama wa watu wa Mungu; wako tayari kujitosa kimasomaso kwa ajili ya uhuru na uenezaji wa Kanisa Katoliki. Makardinali wanavikwa pete rasmi, alama ya upendo wao kwa Mtakatifu Petro, ili waweze kuimarisha na kudumisha upendo wao kwa Kanisa la Kristo.
Mwishoni, Makardinali wamepangiwa Makanisa ya huduma ndani ya Jimbo kuu la Roma, kwani wao ni sehemu ya familia ya Mungu Jimbo kuu la Roma. Hatimaye, kila Kardinali anapewa Waraka unaomwonesha kuteuliwa na hatimaye kusimkwa kama Kardinali na hivyo kuwa ni kati ya washauri wakuu wa Khalifa wa Mtakatifu Petro katika maisha na utume wa Kanisa la Kiulimwengu. Pale ambapo Kiti kitakatifu kiko wazi, “Sede Vacante” Baraza la Makardinali linakusanyika kusali na hatimaye, kumchagua Papa mwingine, ili kuendeleza kazi ya kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu. Ni katika muktadha huu wa dhamana na utume wa Baraza la Makardinali katika Kanisa, Dominika ya Huruma ya Mungu, tarehe 27 Aprili 2025, Jioni, Baraza la Makardinali limeungana na watu wa Mungu kusali Masifu ya Pili ya Jioni kwa ajili ya kumkumbuka na kumwombea Hayati Baba Mtakatifu Francisko, Masifu ambayo yameongozwa na Kardinali Rolandas Makrikas, Kamishna Maalum wa Kipapa wa Kanisa kuu la Bikira Maria Mkuu, ambaye pia ni Mwandamizi wake. Hii ilikuwa ni fursa kwa Baraza la Makardinali kuungana na watu wa Mungu waliokuwa wamefurika kwenye Kanisa kuu la Bikira Maria mkuu kwa ajili ya Masifu ya Pili ya Dominika ya Huruma ya Mungu pamoja na kutoa heshima zao kwenye kaburi la Hayati Baba Mtakatifu Francisko. Makardinali na watu wa Mungu katika ujumla wao, walipata nafasi ya kusali kwenye kaburi la Hayati Baba Mtakatifu Francisko, kwenye Kikanisa cha Bikira Maria Afya ya Warumi, “Salus Populi Romani”, mahali ambapo, Hayati Baba Mtakatifu Francisko amefika hapo kusali zaidi ya mara 126, kwa hakika alikuwa na Ibada kubwa kwa Bikira Maria. Kanisa limesali na kumwombea Baba Mtakatifu Francisko ili Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo, aweze kumpokea mbele ya Uso wake katika mwanga wa milele na usingizi wa amani, huku akiwa na tumaini la ufufuo wa wafu, maisha na uzima wa milele!