Tafuta

Kardinali Pietro Parolin, aliyekuwa Katibu mkuu wa Vatican, Dominika tarehe 27 Aprili 2025 ameongoza Ibada ya Misa Takatifu, Siku ya pili ya Novendia, maalum kwa wafanyakazi pamoja na raia wanaoishi mjini Vatican. Kardinali Pietro Parolin, aliyekuwa Katibu mkuu wa Vatican, Dominika tarehe 27 Aprili 2025 ameongoza Ibada ya Misa Takatifu, Siku ya pili ya Novendia, maalum kwa wafanyakazi pamoja na raia wanaoishi mjini Vatican.   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Dominika ya Huruma ya Mungu: Kiini cha Maisha na Utume wa Papa Francisko

Kardinali Parolin katika mahubiri yake amegusia kuhusu: Majonzi makubwa katika kipindi hiki cha maombolezo ya Papa Francisko, lakini jambo la msingi ni furaha ya Pasaka; changamoto mamboleo katika maisha ya vijana, lakini wanapaswa kujikita katika upendo ambao hustahimili yote. Upendo wenye huruma ni kiini cha mafundisho ya Baba Mtakatifu Francisko, chemchemi ya imani, matumaini na mapendo. Kanisa ni chombo na shuhuda wa huruma ya Mungu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Pasaka ya Bwana ni fursa nyingine kwa waamini kuweza kuonja upendo na huruma ya Mungu kwa njia ya msamaha wa dhambi. Yesu Mfufuka analipatia Kanisa dhamana ya kuwatangazia watu huruma na msamaha wa Mungu, unaowakirimia waamini amani, utulivu wa ndani na furaha inayobubujika kwa kukutana na Kristo Mfufuka. Huruma ya Mungu katika mwanga wa Pasaka ni kielelezo cha ufahamu ambao unaweza kuchukua mitindo mbalimbali katika maisha ya mwanadamu yaani: kwa kutumia milango ya fahamu, kwa kufundishwa, lakini kubwa zaidi ni kwa njia ya mang’amuzi ya huruma ya Mungu inayofungua akili na nyoyo za watu ili kuweza kufahamu kwa kina na mapana zaidi fumbo la maisha ya Mungu na maisha ya mtu binafsi. Huruma ya Mungu inawawezesha waamini na watu wote wenye mapenzi mema kutambua kwamba: vita, chuki, uhasama na ubaya wa moyo ni mambo ambayo hayana msingi kabisa na kwamba, waathirika wakubwa ni wale watu wanaofungwa katika hali kama hizi, kwani ni mambo yanayowapokonya utu wao.

Siku ya Pili ya Maombolezo ya Kifo cha Papa Francisko
Siku ya Pili ya Maombolezo ya Kifo cha Papa Francisko   (ANSA)

Huruma ya Mungu inafungua malango ya moyo ili kuonesha upendo na ukarimu kwa watu wanaoishi katika upweke na kusukumizwa pembezoni mwa jamii, ili kweli waweze kujisikia ndugu na watoto wapendwa wa Baba wa milele. Huruma ya Mungu inawawezesha watu kutambua na kuguswa na mahitaji msingi ya jirani zao hasa wale wanaohitaji kuonjeshwa faraja na upendo. Huruma ya Mungu anaendelea kusema Hayati Baba Mtakatifu Francisko inawasha moto wa upendo mioyoni mwa watu, kwa kuguswa na mahitaji yao pamoja na kuwashirikisha. Kimsingi, huruma ya Mungu inawawezesha waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuwa ni vyombo na mashuhuda wa haki, amani na upatanisho. Ikumbukwe kwamba, huruma ya Mungu ni kiini cha imani, maisha na utume wa Kanisa; ushuhuda makini wa Ufufuko wa Kristo Yesu. Bikira Maria, Mama wa huruma ya Mungu awasaidie waamini: kuamini na kuishi kwa furaha yote haya.

Kristo Yesu ni chemchemi ya matumaini kwa vijana
Kristo Yesu ni chemchemi ya matumaini kwa vijana   (Vatican Media)

Dominika ya Pili ya Pasaka kadiri ya Mapokeo ya Kanisa na mwendelezo wake kama Dominika ya huruma ya Mungu, ambamo Kanisa linatumwa na Kristo Yesu kuwa ni chombo cha huruma na upatanisho kwa kuwaondolea watu dhambi zao! Dominika ya Pili ya Pasaka inajulikana pia kama “In Albis” yaani “Dominika nyeupe”, siku ambayo Wakristo waliobatizwa kwenye mkesha wa Pasaka walikuwa wanavua mavazi yao meupe, yaliyokuwa yana maanisha utu mpya wa watoto wa Mungu waliozaliwa kwa Maji na Roho Mtakatifu kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo. Mavazi haya meupe wakati huo yalivaliwa kwa muda wa juma zima, kumbe, Jumapili Nyeupe ilikuwa ni mwanzo wa maisha mapya ndani ya Kristo Mfufuka na Kanisa lake! Mtakatifu Yohane Paulo II kunako mwaka 2000 wakati wa maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2000 ya Ukristo aliamua kuipatia Dominika hii umuhimu wa pekee na kuwa ni Dominika ya huruma ya Mungu, hii ni changamoto na mwaliko kwa waamini kuendelea kujichotea nguvu na neema zinazobubujika kutoka katika huruma ya Mungu. Injili ya Siku inaonesha jinsi ambavyo Yesu alivyowapatia Mitume wake dhamana ya kuwaondolea watu dhambi zao kwa kuwapatia Roho Mtakatifu.

Kristo Yesu ni ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu
Kristo Yesu ni ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu   (Vatican Media)

“Sacrum novendiale, Novendia” ni kipindi cha siku tisa za maombolezo kinachofuatia kifo cha Baba Mtakatifu na kuanza mara baada ya mazishi ya Khalifa wa Mtakatifu Petro na tarehe yake hupangwa na Baraza la Makardinali na maadhimisho haya yanafanyika kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Ni katika muktadha huu, Kardinali Pietro Parolin, aliyekuwa Katibu mkuu wa Vatican, Dominika tarehe 27 Aprili 2025 ameongoza Ibada ya Misa Takatifu, Siku ya pili ya Novendia, maalum kwa wafanyakazi pamoja na raia wanaoishi mjini Vatican. Kardinali Parolin katika mahubiri yake amegusia kuhusu: Majonzi makubwa katika kipindi hiki cha maombolezo ya Baba Mtakatifu Francisko, lakini jambo la msingi ni furaha ya Pasaka; changamoto mamboleo katika maisha ya vijana, lakini wanapaswa kujikita katika upendo ambao hustahimili yote. Upendo wenye huruma ni kiini cha mafundisho ya Baba Mtakatifu Francisko, chemchemi ya imani, matumaini na mapendo na kwamba, Kanisa ni chombo na shuhuda wa huruma ya Mungu.

Bikira Maria Mama wa Huruma ya Mungu
Bikira Maria Mama wa Huruma ya Mungu   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Kardinali Parolin amesema, siku ile ya kwanza ya Juma, wanafunzi walikuwa wamejifungia ndani kwa hofu ya Wayahudi, mioyo yao, ikiwa imesheheni majonzi makubwa kwa sababu Kristo Yesu waliyemfuata alikuwa ameteswa na kufa Msalabani, kiasi kwamba, wakajisikia kuwa ni watoto yatima, watu wasiokuwa na mwelekeo, watu ambao walikuwa katika hofu na mashaka makubwa; na mwisho walikuwa ni watu wasiokuwa na ulinzi. Hii ndiyo hali ambayo Kanisa kwa sasa katika kipindi hiki cha maombolezo ya Baba Mtakatifu Francisko linaonja, kiasi cha kujisikia kama ilivyokuwa kwa Mitume wa Kristo Yesu, waliokuwa wamegubikwa na majonzi makubwa. Katika hali ya majonzi na masikitiko makubwa, Kristo Yesu Mfufuka akawatokea na hivyo kuwa ni chanzo cha furaha kuu.

Kristo Mfufuka ni chemchemi ya huruma ya Mungu
Kristo Mfufuka ni chemchemi ya huruma ya Mungu   (ANSA)

“Furaha ya Injili huijaza mioyo na maisha ya wote wanaokutana na Kristo Yesu. Wale wanaokubali zawadi yake ya ukombozi wanawekwa huru kuondokana na dhambi, uchungu, utupu wa ndani na upweke. Pamoja na Yesu, daima furaha inazaliwa upya na huo unakuwa ni mwanzo wa uinjilishaji mpya unaosimikwa kwa Kristo Mfufuka.” Evangelii gaudium, 1. Furaha ya Pasaka ni kitulizo katika majonzi na hasa miongoni mwa vijana wa kizazi kipya ambao katika maadhimisho ya Jubilei ya Vijana Wenye Umri chini ya Miaka 20 kutoka sehemu mbalimbali za dunia walitamani kuonana uso kwa uso, walitamani kusikia uwepo angavu wa Kanisa na ule wa Baba Mtakatifu aliyetamani kukutana na kuwasalimia, huku akipita kati kati yao. Vijana wanapaswa kusimama kidete ili kuweza kukabiliana na changamoto mamboleo na hasa changamoto ya teknolojia ya Akili Unde, AI., lakini vijana watambue kwamba, Kristo Yesu ni funuo wa matumaini ya kweli na kamwe hatawaacha hata katika nyakati ngumu za maisha, anapenda kukutana na kuzungumza nao, ili awatie shime ya kuendelea kuishi, kwa kushirikishana mang’amuzi ya maisha, mawazo, karama, ndoto na hivyo kutambua uso wa jirani zao wanaopaswa kupendwa. Kristo Yesu atawasaidia vijana hawa ili waendelee kuwa wakarimu, waaminifu na watu wanaowajibika barabara katika maisha yao; atawasaidia kutambua kile kilicho chema na kizuri katika maisha na kwamba, upendo hustahimili yote 1Kor 13: 7.

Jubilei ya Vijana Chini ya Miaka 20
Jubilei ya Vijana Chini ya Miaka 20   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Kardinali Parolin amesema, Mama Kanisa anaadhimisha Dominika ya Huruma ya Mungu, muhtasari wa mafundisho makuu ya Baba Mtakatifu Francisko, aliyetaka kuwaona Wakristo wakijizatiti katika mchakato wa uinjilishaji mpya unaojikita katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko! Huruma ya Mungu si dhana ya kufikirika inayoelea kwenye ombwe anasema Hayati Baba Mtakatifu Francisko, bali ni sifa kuu ya Mungu na mafundisho ya Kanisa. Yesu alikuja ulimwenguni ili kumkomboa mwanadamu kutoka katika dhambi na mauti kwa kumjalia maisha ya uzima wa milele. Ni mganga wa kweli anayewatafuta wagonjwa na wala si wenye haki ambao hawahitaji kutubu na kumwongokea Mungu. Ikumbukwe kwamba, Mungu anataka binadamu wote waokoke. Yesu anataka kuwaendea wote ili kuwaonjesha huruma na upendo wa Mungu Baba. Hawa ni wadhambi na wote waliotengwa na Jamii, ili aweze kuwaganga na kuwaponya, tayari kuwarudishia hadhi yao kama watoto wateule wa Mungu. Upendo wa Mungu unaowakumbatia wadhambi wakati mwingine unaonekana kuwa ni kashfa mbele ya macho ya binadamu. Yesu anataka kuwaponya na kuwaokoa wale wanaoteseka kiroho na kimwili; tayari kuwaonjesha huruma ya Mungu. Mafundisho ya huruma ya Mungu ni amana na utajiri mkubwa kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko, unapaswa kulindwa, kuhifadhiwa na kuendelezwa. Huruma ya Mungu ni kiini cha imani, kinachowawezesha waamini kujenga na kudumisha mahusiano na mafungamano yao na Mwenyezi Mungu pamoja na jirani zao na hivyo kutambua kwamba, kwa hakika wanapendwa na kuthaminiwa na Mungu. Maisha ya mwanadamu yanakita mizizi yake katika huruma ya Mungu, inayosamehe na kuwaondoa waamini katika dimbwi la uchoyo na ubinafsi; inayowaondoa katika hali ya chuki, uhasama na vita.

Mafuriko ya watu yameshiriki katika Ibada ya Misa Takatifu
Mafuriko ya watu yameshiriki katika Ibada ya Misa Takatifu   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Kardinali Parolin amesema, huruma ya Mungu ni chemchemi ya: upendo, msamaha na maondoleo ya dhambi. Baba Mtakatifu Francisko ni chombo na shuhuda wa Kanisa angavu linaloinama kwa huruma na mapendo kuwatibu na kuwaganga waamini kwa njia ya mafuta ya faraja na divai ya matumaini. Na kwamba, amani ya kweli ni matunda ya haki, huruma na msamaha. Katika maadhimisho ya Dominika ya Huruma ya Mungu wafanyakazi na wenyeji wa mji wa Vatican wameadhimisha Siku ya pili ya Novendia kwa ajili ya kumkumbuka na kumwombea Baba Mtakatifu Francisko. Kardinali Parolin, amewashukuru na kuwapongeza wafanyakazi wote wa Vatican kwa huduma makini wanayoitoa kila siku kwa ajili ya Khalifa wa Mtakatifu Petro. Kardinali Parolin, amemweka Hayati Baba Mtakatifu Francisko chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, kwenye Kanisa kuu la Bikira Maria Mkuu, ambako kwa sasa anapumzika, ili aendelee kulisimamia Kanisa na kulienzi katika hija ya binadamu kuelekea katika ujenzi wa amani na udugu wa kibinadamu.

Huruma ya Mungu 2025

 

 

27 Aprili 2025, 15:49