Hayati Papa Francisko: Fumbo la Kifo Katika Mwanga wa Pasaka
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Kardinali Kevin Joseph Farrell, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha ambaye pia ni “Camerlengo” mkuu wa Kanisa Katoliki ndiye kiongozi mkuu wa shughuli za Kanisa wakati kunapotokea kwamba, kiti cha Khalifa wa Mtakatifu Petro kiko wazi kwa sababu mbalimbali, Jumatatu ya Pasaka, tarehe 21 Aprili 2025 ametangaza kwa masikitiko na majonzi makubwa kifo cha Baba Mtakatifu Francisko, aliyekuwa na umri wa miaka 88 kilichotokea Jumatatu tarehe 21 Aprili 2025 majira ya Saa 1:35 Asubuhi kwa Saa za Ulaya sawa na Saa 2:35 za Asubuhi kwa Saa za Afrika Mashariki na Kati. Katika tamko lake, amesema, Baba Mtakatifu Francisko ni kiongozi aliyejisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Katika maisha na utume wake amewafundisha watu wa Mungu umuhimu wa kutangaza na kumwilisha tunu msingi za maisha ya Kiinjili kwa uaminifu, ujasiri na upendo kwa wote, upendeleo wa pekee ikiwa ni kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa vipaumbele vya jamii. Mama Kanisa anamshukuru sana Baba Mtakatifu Francisko kwa ushuhuda na mfano wa maisha yake kama mfuasi wa Kristo Yesu, Kanisa linapenda kuiweka roho ya Hayati Baba Mtakatifu Francisko kwenye huruma na upendo unaobubujika kutoka katika Fumbo la Utatu Mtakatifu.
Kardinali Fridolin Ambongo Besungu, Rais wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika na Madagascar (SECAM) katika salam zake za rambirambi anasema, Kanisa Barani Afrika linamshukuru Hayati Baba Mtakatifu Francisko: kwa maisha, utume na ushuhuda wake kama: Baba wa huruma ya Mungu, amani na maskini; aliyesimama kidete kutangaza na kushuhudia utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote na katika mchakato wa ujenzi wa udugu wa kibinadamu. Ni shuhuda wa matumaini kwa watu waliopondeka na kuvunjika moyo. Ni kiongozi aliyesimama kidete kulinda na kutetea: utu, heshima na haki msingi za binadamu, akataka kuona watu wanajenga madaraja ya kuwakutanisha watu; kwa kujikita katika majadiliano katika ukweli na uwazi, ili kushughulikia changamoto za Jumuiya ya Kimataifa katika ulimwengu mamboleo. Alipenda kuwaona watu wa Mungu wakijikita katika ujenzi wa Kanisa la Kisinodi na Kimisionari, kwa kujenga na kudumisha utamaduni wa kusikilizana na kuheshimiana kama ndugu wamoja.
Kardinali Kevin Joseph Farrell, Jumatano tarehe 23 Aprili 2025 ameongoza waamini kutoa heshima zao za mwisho kwa Hayati Baba Mtakatifu Francisko, zoezi linaloendelea kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican hadi Ijumaa tarehe 25 Aprili 2025 majira ya Saa 1: 00 za Usiku kwa saa za Ulaya sawa na Saa 2:00 kwa Saa za Afrika Mashariki na Kati. Kardinali Kevin Joseph Farrell, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha ambaye pia ni “Camerlengo” mkuu wa Kanisa Katoliki, ataongoza jopo la viongozi wakuu kutoka Sekretarieti kuu ya Vatican kufunga sanduku la Hayati Papa Francisko. Jumamosi tarehe 26 Aprili 2025, Kardinali Giovanni Battista Re, Dekano wa Baraza la Makardinali ataongoza Ibada ya Mazishi ya Baba Mtakatifu Francisko na hatimaye, kuzikwa kwenye Kanisa kuu la Bikira Maria Mkuu. Hayati Baba Mtakatifu Francisko anasema siku zote amekabidhi maisha na huduma yake ya Kipadre na Kiaskofu chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria Mama wa Bwana wetu Kristo Yesu, Bikira Maria Mtakatifu. Anaomba kwamba, maisha yake ya kibinadamu yabaki yakipumzika, katika Kanisa kuu la Bikira Maria Mkuu, huku akingojea Siku ya ufufuo wa wafu. Kardinali Kevin Joseph Farrell, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha ambaye pia ni “Camerlengo” mkuu wa Kanisa Katoliki, ataongoza jopo la viongozi wakuu kutoka Sekretarieti kuu ya Vatican, kusindikiza Jeneza la Baba Mtakatifu Francisko hadi kwenye Kanisa kuu la Bikira Maria Mkuu na hatimaye kushuhudia maziko yake!
Hayati Baba Mtakatifu Francisko alitamani kuona safari yake ya mwisho ya hapa duniani ikiishia mahali patakatifu pa Bikira Maria, mahali ambapo alienda kwa ajili ya sala mwanzoni na mwishoni mwa kila hija ya kitume, ili kukabidhi nia yake kwa Bikira Maria pamoja na kumshukuru kwa unyenyekevu, ulinzi na tunza yake ya kimama. Hayati Baba Mtakatifu Francisko anaomba kaburi lake liwekwe kwenye Kikanisa cha Bikira Maria Afya ya Warumi “Salus Populi Romani.” Hayati Baba Mtakatifu Francisko alitaka kaburi lake lichimbwe ardhini, rahisi bila mapambo maalum bali libaki likiwa na maandishi ya pekee “Franciscus.” Gharama ya maandalizi na hatimaye maziko yake, zitagharimiwa na mfadhili ambaye amempanga, safari ya kuhamishiwa kutoka kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro, tayari alitoa maagizo kwa Kardinali Rolandas Makrikas, Kamishna Maalum wa Kipapa wa Kanisa kuu la Bikira Maria Mkuu.
Hayati Baba Mtakatifu Francisko anasema, Kristo Yesu ameliangazia Fumbo la mateso na Kifo cha binadamu, kwa njia ya ushuhuda wa maisha na matendo yake, hasa pale, watu wanapoondokewa na wapendwa wao! Hata Kristo Yesu, mbele ya kaburi la rafiki yake Lazaro alitoa machozi, ushuhuda kwamba, Yesu yuko karibu sana na waja wake kama ndugu! Kwa uchungu mkubwa alimwombea Lazaro kwa Baba yake wa mbinguni, chemchemi ya uhai na hatimaye, akamwamuru Lazaro aliyekufa kutoka nje ya kaburi! Huu ndio mwelekeo wa matumaini ya Kikristo katika kukabiliana na Fumbo la Kifo! Kristo Yesu “anasimama dede” kupambana na kifo ambacho kimejitokeza katika kazi ya uumbaji kinyume kabisa cha upendo wa Mungu na Kristo Yesu, Mkombozi wa ulimwengu ambaye ameganga na kuponya Fumbo la Kifo katika maisha ya mwanadamu. Mababa wa Kanisa wanasema, maana ya Kikristo ya kifo imefunuliwa katika mwanga wa Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo ambaye ndani yake mna tumaini la Wakristo.
Mkristo anayekufa katika Kristo Yesu huuacha mwili ili kwenda kukaa pamoja na Mwenyezi Mungu, milele yote! Kwa Mkristo, siku ya kifo huanzisha, mwishoni mwa maisha yake ya Kisakramenti, utimilifu wa kuzaliwa kwake upya kulikoanzishwa na Sakramenti ya Ubatizo, kufanana kamili na sura ya Mwana, kulikotolewa kwa Mpako wa Roho Mtakatifu na ushirika katika karamu ya Ufalme, uliotangulizwa katika Ekaristi, hata kama ana lazima bado kutakaswa zaidi ili kuvikwa vazi la arusi! Waamini wanahamasishwa kulitafakari Fumbo la kifo, kama sehemu ya matumaini ya Kikristo kwani, Kristo Yesu mwenyewe anasema, ndiye ufufuo na uzima na kwamba, yeyote anayemwamini ajapokufa atakuwa anaishi na kwamba, heri yao wale wote wanaokufa katika Kristo Yesu. Matumaini ya Kikristo yawasaidie waamini kukabiliana na Fumbo la kifo kwa imani na matumaini na kwamba, hata ustaarabu wa watu wa kale umepitia katika fumbo hili na kwa hakika, ibada ya kifo ni sehemu ya vinasaba vya maisha ya binadamu.
Mzaburi anasema, “Basi, utujulishe kuzihesababu siku zetu, tujipatie moyo wa hekima.” Haya ni maneno yanayowatia waamini matumaini badala ya kujisikia kuwa wanyonge wanapoyaona maisha yao yana yoyoma na kutoweka mara kama ndoto ya mchana. Kifo kinayaanika maisha ya binadamu na kumwondolea kiburi na kuwahimiza watu kujenga na kudumisha upendo, kutafuta na kuambata mambo msingi katika maisha, ili sadaka na majitoleo yao yaweze kuwapatia amani na utulivu wa ndani wanapokabiliana na Fumbo la Kifo! Kristo Yesu anapenda kuimarisha matumaini ya waja wake kwamba, Yeye ndiye ufufuo na uzima! Jambo la msingi ni wao kumwamini. Mbele ya Fumbo la Kifo binadamu ni mnyonge na ni “mdogo sana kama kidonge cha piliton”. Lakini, neema katika hali na mazingira kama haya, inaweza tena kuamsha imani na Yesu mwenyewe kuwashika mkono watu wake na kuwaambia “Talitha kum” tafsiri yake “Msichana, nakuambia, inuka.” Haya ni maneno ambayo Yesu anapenda kumwambia kila mtu, simama na fufuka tena! Baba Mtakatifu Francisko anasema, haya ndiyo matumaini ya Kikristo mbele ya Fumbo la Kifo. Kwa mwamini hili ni lango ambalo liko wazi; lakini kwa mwenye mashaka, ni giza linalomwandama na kumtumbukiza mtu katika majonzi na msiba mkuu. Kwa kila mwamini, hii itakuwa ni neema siku ile mwanga huu utakapoangaza.
Hayati Baba Mtakatifu anasema, kifo ni sehemu ya matukio ya maisha ya mwanadamu, ni urithi na kumbukumbu. Tangu pale mwanadamu anapozaliwa, anaanza safari ya kuelekea katika Fumbo la kifo, changamoto na mwaliko kwa waamini kumwomba Mwenyezi Mungu ili aweze kuwajalia kufa kifo chema badala ya kujifungia katika muda na ubinafsi wao! Mama Kanisa anawataka watoto wake kujiandaa vyema ili kukabiliana na Fumbo la kifo katika maisha yao. Kifo ni urithi unaofumbatwa katika ushuhuda ambao unapaswa kutolewa kwa wale wanaobaki. Baba Mtakatifu anawataka Wakristo kujiuliza swali la msingi, Je, wewe leo ukifa utaacha ushuhuda gani nyuma yako? Swali hili liwasaidie waamini kujiandaa kufa vyema. Lakini, kabla ya kuitupa mkono duniani Je, kuna jambo gani ambalo ningependa kulifanya leo hii? Fumbo la kifo liwasaidie waamini kufikiri na kutenda kila siku wakitambua kwamba, daima wako safarini kuelekea kufani! Maswali haya ni muhimu kwa waamini wote, ili kuweza kujiandaa vyema, ili hatimaye, kukabiliana vyema na Fumbo la kifo! “Requiescat in pace, noster papa Franciscus.”