Tafuta

Papa Francisko: Majadiliano ya kiekumene ni sehemu ya vinasaba vya maisha na utume wa Kanisa. Papa Francisko: Majadiliano ya kiekumene ni sehemu ya vinasaba vya maisha na utume wa Kanisa.  (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Hayati Papa Francisko: Majadiliano ya Kiekumene Katika Maisha na Utume wa Kanisa

Hayati Baba Mtakatifu Francisko anakazia uekumene wa: damu, maisha ya kiroho, sala na huduma. Anasema uekumene wa damu na ule wa utakatifu wa maisha ni mambo msingi yanayoshuhudiwa na Wakristo sehemu mbalimbali za dunia katika umoja, udugu na upendo kama kikolezo cha ujenzi wa Ufalme wa Mungu. Huu ni Ufalme wa ukweli na uzima, ufalme wa haki na amani, ufalme wa mapendo na ni ufalme ambao Mwenyezi Mungu anatawala na ujenzi wa Kanisa lake.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanasema, utengano kati ya Wakristo hupingana wazi na mapenzi ya Kristo Yesu na ni kikwazo kwa ulimwengu na hudhuru tendo takatifu la kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Mtakatifu Yohane Paulo II alitaka kuona kwamba, Kanisa Katoliki linaendeleza majadiliano ya kiekumene na Wakristo wa Makanisa na Madhehebu mbalimbali, ili siku moja wote wawe wamoja chini ya Kristo Yesu, Mchungaji mkuu. Kwa upande wake, Hayati Baba Mtakatifu Francisko anakazia uekumene wa: damu, maisha ya kiroho, sala na huduma. Anasema uekumene wa damu na ule wa utakatifu wa maisha ni mambo msingi yanayoshuhudiwa na Wakristo sehemu mbalimbali za dunia katika umoja, udugu na upendo kama kikolezo cha ujenzi wa Ufalme wa Mungu. Huu ni Ufalme wa ukweli na uzima, ufalme wa haki na amani, ufalme wa mapendo na ni ufalme ambao Mwenyezi Mungu anatawala katika mioyo ya watu wake sanjari na ujenzi wa Fumbo la Mwili wa Kristo yaani Kanisa. Hayati Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, uekumene wa damu unajikita katika: Vita, dhuluma na nyanyaso dhidi ya Wakristo. Lakini, ikumbukwe kwamba, damu ya mashuhuda hawa wa imani ni chachu ya Ukristo. Uekumene wa maisha ya kiroho na utakatifu wa maisha unafumbatwa katika toba na wongofu wa ndani; kwa kujikana na kujivika fadhila ya unyenyekevu; moyo wa ukarimu na udugu; upole, uvumilivu na kutumikia bila ya kujibakiza. Wakristo wanakumbushwa kwamba, kadiri wanavyojitahidi kuishi maisha matakatifu mintarafu tunu msingi za Kiinjili, ni kwa kadiri ileile watahamasisha na kutekeleza umoja wa Wakristo na udugu wa kibinadamu kati yao. Uekumene wa huduma unatekelezwa kwa njia ya sera na mikakati ya shughuli za kichungaji sanjari na maisha ya kitume.

Majadiliano ya kiekumene: Umoja na tofauti msingi.
Majadiliano ya kiekumene: Umoja na tofauti msingi.   (Vatican Media)

Hayati Baba Mtakatifu Francisko anawaalika Wakristo kuitafakari Sura ya Kristo Mteseka, ili kupyaisha matumaini ya watu wa Mungu, tayari kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa watu wa Mataifa kama ilivyokuwa kwa Mitume wa Yesu. Hawa ni Mitume ambao walisadaka maisha yao, kiasi cha kuanzisha uekumene wa damu unaoendelea kurutubisha majadiliano ya kiekumene. Hata leo hii bado kuna Wakristo wanaoendelea kuteseka katika Ijumaa ya Madhulumu, wakionesha kimya kikuu cha Jumamosi kuu na hatimaye, kuzaliwa upya Dominika ya Ufufuko wa Bwana! Hawa ndio wafia dini na waungama imani, mfano bora wa kuigwa kwa vijana wa kizazi kipya. Mashuhuda na wafiadini hawa ni amana na utajiri wa pamoja. Mashuhuda hawa wa imani wamezamishwa katika mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu na hatimaye, kuungana naye tena baada ya ufufuko, ili na wao waenende katika upya wa uzima. Hayati Baba Mtakatifu anayataka Makanisa kutembea kwa pamoja kwa nguvu ya kumbukumbu inayokita mizizi yake katika historia ya uinjilishaji kwenye karne ya kwanza. Ni katika mazingira haya, wakristo wakawa na ujasiri wa kutangaza na kushuhudia roho ya kinabii, wakajibidiisha katika mchakato wa utamadunisho. Hiki ni kipindi ambacho Kanisa lilibahatika kuwa na mashuhuda wa imani na waungama dini; utakatifu wa maisha, ukawa ni chachu inayomwilishwa katika medani mbalimbali, kiasi cha kuutolea ushuhuda na kuvumilia nyanyaso na madhulumu! Hata leo hii, Wakristo wanahamasishwa kumwimbia Mungu utenzi wa sifa na shukrani, ili kwa njia ya neema, waweze tena kugundua ndani mwao kumbukumbu ya umoja na ushirika, ili kuyaangazia mapito yao.

Uekumene unasimikwa katika toba na wongofu wa ndani
Uekumene unasimikwa katika toba na wongofu wa ndani   (Vatican Media)

Wakristo wanaitwa na kuhamasishwa kutembea kwa pamoja huku wakisikiliza Neno la Mungu kama ilivyokuwa kwa wafuasi wa Emau. Hii ni changamoto kwa Wakristo kwa pamoja kumsikiliza Kristo Yesu, hasa nyakati hizi ambazo zinashuhudia mabadiliko makubwa ya kijamii na kitamaduni; maendeleo makubwa ya sayansi, teknolojia, ustawi, maendeleo na ukuaji wa kiuchumi. Utandawazi umedhohofisha kanuni maadili na utu wema; unaendelea kung’oa tunu msingi za maisha ya watu; umesababisha uchafuzi mkubwa wa mazingira nyumba ya wote na zaidi yao, umewafunga watu katika uchoyo, chuki na ubinafsi. Umefika wakati wa kumwomba Mwenyezi Mungu ili aweze kuwanusuru watu kutoka katika utamaduni wa chuki na uhasama, ubaguzi, sanjari na kumong’onyoka kwa tunu msingi za maisha ya ndoa na familia. Huu ni utandawazi unaowakatisha vijana tamaa ya maisha bora zaidi. Wote hawa wanahitaji kukutana na Kristo Mfufuka, chemchemi ya matumaini mapya kwa kusikiliza, kulitangaza na kulishuhudia Neno lake. Baba Mtakatifu anapenda kuwahamasisha wakristo kutembea pamoja katika uekumene wa sala na kuumega mkate kwa pamoja, changamoto inayohitaji waamini kuheshimiana, kuthaminiana na kushirikiana katika Injili ya huduma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii; kwa kuwapokea na kuwaonjesha mshikamano, tayari kujikita katika ujenzi wa udugu wa kibinadamu. Wakristo wanapaswa kutembea kwa pamoja, kuelekea kwenye Pentekoste mpya, kama ilivyokuwa kwenye ile Pentekoste ya kwanza, wakiwa wameungana na Bikira Maria, Mama wa Kanisa, wakashukiwa na Roho Mtakatifu na kutambua utajiri wa lugha, kiasi cha kumshuhudia Kristo Mfufuka. Roho Mtakatifu ndiye anayeliwezesha Kanisa kujenga umoja katika utofauti, kwa kukazia mambo msingi yanayowaunganisha. Roho Mtakatifu ni chombo cha ujenzi wa udugu wa kibinadamu na anayewapatia neema ya kuweza kutembea kwa pamoja katika upya wa maisha! Roho Mtakatifu anawawezesha kuwa na ujasiri wa kushirikishana na kushikamana katika maisha na utume wa Kanisa. Roho Mtakatifu ni nguvu ya mashuhuda na waungama imani.

Uekumene unaosimikwa katika uhalisia wa maisha ya watu wa Mungu
Uekumene unaosimikwa katika uhalisia wa maisha ya watu wa Mungu   (Vatican Media)

Ni katika muktadha wa kifo cha Baba Mtakatifu Francisko, Patriaki Bartolomeo wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox la Costantinopoli, anasema, kwa hakika alikuwa ni kiongozi aliyesimama kidete kutangaza na kushuhudia umuhimu wa mwendelezo wa mchakato wa majadiliano ya kiekumene. Patriaki Bartolomeo wa kwanza anampongeza Baba Mtakatifu Francisko kwa kuendelea kuimarisha majadiliano ya kitaalimungu na ujenzi wa Kanisa la Kisinodi, ili kurahisisha ukaribu wa Makanisa haya mawili, unaofumbatwa katika dhana ya Sinodi, kwa kutambua kwamba, Kanisa, kimsingi tayari ni Sinodi, kwa sababu limeanzishwa na Kristo Yesu na linaongozwa na Roho Mtakatifu na kwamba, mchakato wa ujenzi wa Kanisa la Kisinodi ni muhimu sana. Hizi ni juhudi pia zinazoendelea kutekelezwa katika majadiliano ya taalimungu ya kiekumene mintarafu ukulu wa Mtakatifu Petro na Dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa. Ile sentensi “Atokaye kwa Baba na Mwana: “Filoque” na Mafundisho kuhusu kutokukosea kwa Papa anapofundisha akiwa ameungana na Maaskofu wengine, “Infallibility” yamefikia mahali pazuri, kwani huu ni mchakato ambao umesimikwa katika unyenyekevu, upendo na uponyaji na ukweli, ili Wakristo wote kwa pamoja waweze kuufikia umoja wa imani na kumfahamu sana Mwana wa Mungu, hata kuwa mtu mkamilifu, kiasi cha kufikia kwenye cheo cha kimo cha utimilifu wa Kristo Yesu. Rej. Efe 4: 13.

Majadiliano ya kiekumene ni sehemu ya vianasa vya maisha na utume wa Kanisa
Majadiliano ya kiekumene ni sehemu ya vianasa vya maisha na utume wa Kanisa   (Vatican Media)

Kwa hakika mchakato wa ujenzi wa Kanisa la Kisinodi umekuwa ni chombo cha majadiliano ya kiekumene, amani na upatanissho na kwamba, Kanisa la Kiorthodox la Costantinopoli linaungana na Hayati Baba Mtakatifu kuombea amani sehemu mbalimbali za dunia, ili vita ikome, na hatimaye, Mwenyezi Mungu aweze kuiongoza “miguu yetu kwenye njia ya amani.” Lk 1: 49. Madhara ya vita ni makubwa kamwe hayawezi kubebwa na mtu mmoja. Mji wa Roma umepambwa kwa damu ya mashuhuda wa imani: Mtakatifu Petro na Paulo, Mitume, huu ni mwaliko wa Kanisa kujikita katika kutafuta, kujenga na hatimaye kudumisha amani. Makanisa na Madhehebu mbalimbali ya Kikristo yanajiandaa kuadhimisha Jubilei ya Miaka 1, 700 tangu Mtaguso wa Kwanza Nicea ulipoadhimishwa kunako mwaka 325 na kilele cha maadhimisho haya ni mwaka 2025, tukio la pekee na muhimu sana. Mwaka 2025 wakristo wote wameadhimisha Pasaka ya Bwana siku moja. Patriaki Bartolomeo wa kwanza wa Kanisa la Kiorthodox la Costantinopoli, anasema, walikwisha kupanga na Baba Mtakatifu Francisko kuliadhimisha tukio hili kubwa kwa pamoja, tukio ambalo litaendelezwa na Mrithi wake. Viongozi wa Makanisa mbalimbali katika ujumla wao, wameonesha masikitiko yao kutokana na kifo cha Baba Mtakatifu Francisko.  

Majadiliano ya kiekumene
24 Aprili 2025, 14:43