Tafuta

Papa Francisko: Maskini ni amana na utajiri wa Kanisa Papa Francisko: Maskini ni amana na utajiri wa Kanisa  (ANSA)

Hayati Papa Francisko: Maskini ni Amana na Utajiri wa Kanisa

Kanisa linatoa huduma ya upendo na mshikamano wa udugu wa kibinadamu kwa maskini, kwa kujali na kuthamini utu, heshima na haki zao msingi. Ni katika muktadha huu, maskini wa hali na mali; maskini wa maadili na utu wema, ndio watakaoupokea mwili wa Hayati Baba Mtakatifu Francisko wakiwa na mawaridi meupe mikononi mwao, kabla ya kuingizwa kwenye Kanisa kuu la Bikira Maria Mkuu kabla ya mazishi yake, Jumamosi tarehe 26 Aprili 2025. Injili ya Maskini!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Jumamosi tarehe 26 Aprili 2025, Kardinali Giovanni Battista Re, Dekano wa Baraza la Makardinali anaongoza Ibada ya Mazishi ya Baba Mtakatifu Francisko na hatimaye, kuzikwa kwenye Kanisa kuu la Bikira Maria Mkuu. Hayati Baba Mtakatifu Francisko anasema siku zote amekabidhi maisha na huduma yake ya Kipadre na Kiaskofu chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria Mama wa Bwana wetu Kristo Yesu, Bikira Maria Mtakatifu. Anaomba kwamba, maisha yake ya kibinadamu yabaki yakipumzika, katika Kanisa kuu la Bikira Maria Mkuu, huku akingojea Siku ya ufufuo wa wafu. Kardinali Kevin Joseph Farrell, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha ambaye pia ni “Camerlengo” mkuu wa Kanisa Katoliki, ataongoza jopo la viongozi wakuu kutoka Sekretarieti kuu ya Vatican, kusindikiza Jeneza la Baba Mtakatifu Francisko hadi kwenye Kanisa kuu la Bikira Maria Mkuu na hatimaye kushuhudia maziko yake! Kanisa linawategemea sana maskini katika maisha na utume wake, kwani maskini ni amana na utajiri wa Kanisa katika mchakato wa Uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Kimsingi, maskini ndio walengwa wakuu wa Injili. Dhana ya umaskini inajikita katika umaskini wa hali na mali; maadili na utu wema; kwani wote hawa, Kristo Yesu amejisadaka kwa ajili ya kuwatangazia Habari Njema ya Wokovu. Wakristo wanapaswa kuwajali, kuwathamini na kuwapenda maskini na watu wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii kama afanyavyo mama mzazi kwa watoto wake. Kanisa linatoa huduma ya upendo na mshikamano wa udugu wa kibinadamu kwa maskini, kwa kujali na kuthamini utu, heshima na haki zao msingi, kwani hata wao wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Ni katika muktadha huu, maskini wa hali na mali; maskini wa maadili na utu wema, ndio watakaoupokea mwili wa Hayati Baba Mtakatifu Francisko wakiwa na mawaridi meupe mikononi mwao, kabla ya kuingizwa kwenye Kanisa kuu la Bikira Maria Mkuu kabla ya mazishi yake, Jumamosi tarehe 26 Aprili 2025.

Hayati Baba Mtakatifu chombo na mjumbe wa matumaini
Hayati Baba Mtakatifu chombo na mjumbe wa matumaini   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Hili ni kaburi ambalo limechongwa kutokana na mawe yaliyoletwa kutoka Liguria, Kaskazini mwa Italia, asili ya Baba Mtakatifu. Hayati Baba Mtakatifu Francisko alitaka kaburi lake lichimbwe ardhini, rahisi bila mapambo maalum bali libaki likiwa na maandishi ya pekee “Franciscus.” Gharama ya maandalizi na hatimaye maziko yake, zitagharimiwa na mfadhili ambaye amempanga, safari ya kuhamishiwa kutoka kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro, tayari alitoa maagizo kwa Kardinali Rolandas Makrikas, Kamishna Maalum wa Kipapa wa Kanisa kuu la Bikira Maria Mkuu. Hayati Baba Mtakatifu anawaombea thawabu stahiki kwa Mwenyezi Mungu wale wote waliompenda na watakaoendelea kumwombea. Anasema, alitolea mateso aliyokumbana nayo katika sehemu ya mwisho wa maisha yake kwa Bwana kwa ajili ya amani na ujenzi wa udugu wa kibinadamu kati ya watu! Hayati Baba Mtakatifu Francisko kwa namna ya pekee, anawaalika Wakristo pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kujifunza kutoka kwenye shule ya maskini kwani kati ya maskini na watu wasiokuwa na makazi maalum, humu humu kuna watakatifu na watu ambao wanaweza kuwafundisha wengine tunu msingi za maisha ya kijamii, kiutu na kiroho. Maskini si mzigo bali ni shule makini kwa watu wa Mungu. Kumbe, kuna umuhimu wa kusimama kidete kulinda na kutetea ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Maskini ni kielelezo cha Kristo Yesu kati ya watu wake. Katika shule ya upendo, watu wanatafuta faraja, mahusiano na mafungamano; utu na heshima ya binadamu na kwa njia hii, waamini wanaweza kujifunza kutoka kwa maskini kwa kuwakaribisha, kuwasikiliza, kuwakirimia na kuwahudumia kwa: Unyenyekevu, upendo na nidhamu ya hali ya juu.

Maskini ni amana na utajiri wa Kanisa
Maskini ni amana na utajiri wa Kanisa   (Vatican Media)

Kanisa linajengwa na waamini wanaosimama kidete kulinda, kutetea na kushuhudia tunu msingi za maisha ya Kikristo, kama kielelezo makini cha imani tendaji na sehemu muhimu sana ya kuyatakatifuza malimwengu kwa chachu ya Injili. Adui mkubwa wa Kanisa ni pale uchu wa mali na madaraka vinapoingia kwa kupitia mlango wa nyuma. Maskini ni hazina, amana na utajiri wa Kanisa, hawa ndio walengwa wakuu wa Habari Njema ya Wokovu. Matendo ya huruma ndicho kigezo kikuu ambacho Kristo Yesu atakitumia Siku ya Hukumu ya Mwisho. Waamini wawe makini dhidi ya uchu wa mali na madaraka, mambo ambayo yanaweza kuhatarisha hata maisha yao ya kiroho na kujikuta wametumbukia katika kiburi, ubinafsi, uchoyo na hatimaye kumezwa na malimwengu. Lakini, ikumbukwe kwamba, haya ni mapambano endelevu katika maisha ya kiroho! Hakuna kulala hadi kieleweke! Bwana Étienne Villemain ni mwamini mlei na baba wa familia ambaye tangu mwaka 2005 amekuwa akiishi na maskini na watu wasiokuwa na makazi maalum nyumbani mwake. Ni mwanzilishi wa Chama cha Lazare kinachowahudumia maskini na watu wasiokuwa na makazi katika nyumba zake 18 wanamoishi watu zaidi ya elfu tatu. Mwamini mlei huyu pia ndiye muasisi wa wazo la Maadhimisho ya Siku ya Maskini Duniani iliyotangazwa na Baba Mtakatifu Francisko kama matunda ya Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya Huruma ya Mungu. Wawakilishi wa Chama cha Lazare, hivi karibuni walikutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko mjini Vatican. Katika mazungumzo yao, Baba Mtakatifu alikazia kwa namna ya pekee: utu, heshima na haki msingi za binadamu; toba, wongofu wa ndani na msamaha; maskini kama amana na utajiri wa maisha na utume wa Kanisa. Hayati Baba Mtakatifu Francisko anasema, utu, heshima na haki msingi za binadamu zinapaswa kulindwa na kuendelezwa na wote. Haya ni mambo ambayo hayajalishi hata kidogo kuhusu: tabaka la mtu, hali ya afya yake na nafasi katika jamii. Utu wa mtu ni sharti muhimu la kuweza kuishi vyema ndani ya jamii.

Maskini ni walengwa wakuu wa Habari Njema ya Wokovu
Maskini ni walengwa wakuu wa Habari Njema ya Wokovu   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Hayati Baba Mtakatifu anasema, toba, wongofu wa ndani na msamaha ni mambo muhimu sana katika maisha ya waamini. Watu wajifunze kutoa na kupokea msamaha na kwamba, hii ni hija ya maisha inayopaswa kutekelezwa kila kukicha kwa njia ya unyenyekevu, hadi kuhakikisha kwamba, moyo uliokuwa umevunjika na kupondeka umetibiwa na kupona kabisa! Huu ni mwaliko kwa waamini kuachana na kiburi cha kutaka kulipiza kisasi na mwelekeo huu ni kinyume kabisa cha Injili. Maisha ya Mkristo yanapaswa kuwa ni kielelezo cha ushuhuda wa imani inayomwilishwa katika matendo. Kanisa kamwe haliwezi kupanuka na kuongezeka kwa njia ya wongofu wa shuruti! Ushuhuda wenye mvuto na mashiko ni mbolea tosha kabisa ya ustawi na maendeleo ya Kanisa.Hayati Baba Mtakatifu Francisko anakiri kwa kusema kwamba, kwa bahati mbaya sana kuna watu ambao wameelemewa na uchu wa fedha na mali, kiasi cha kumezwa na malimwengu, hali inayowafanya kumweka Mwenyezi Mungu kando ya maisha na vipaumbele vyao. Lakini pia, kuna watu wenye utajiri wa fedha na mali, wanaotumia neema na baraka hizi kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya jirani zao. Kwa maneno machache ni watu wanaotumia utajiri huku wakiongozwa na tunu msingi za Kiinjili. Utajiri wa wakleri na watawa unaweza kuonekana kuwa ni kashfa kwa watu wa Mungu. Waamini wanahamasishwa na Mama Kanisa kumfuasa Kristo Yesu ambaye ni mseja, fukara na mtii. Ufukara ni nguzo ya maisha bora kwani hii ni chemchemi ya wema, ukarimu, sadaka na majitoleo kwa Mungu na jirani. Baba Mtakatifu anasema, inawezekana kabisa kufungua nyumba ya maskini mjini Vatican, lakini kinachokosekana ni ujasiri wa Khalifa wa Mtakatifu Petro ili kutekeleza wazo na dhamana hii.

Utu, heshima na haki msingi za binadamu zilindwe
Utu, heshima na haki msingi za binadamu zilindwe   (Vatican Media)

Baba Mtakatifu anawaalika waamini kutafakari kwa kina na mapana jinsi ambavyo wanajitahidi kuwa wakarimu na watu wenye upendo kwa jirani zao kutokana na karama na utajiri ambao Mwenyezi Mungu amemkirimia kila mmoja wao! Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko: “Misericordia et misera” “Huruma na haki” ni mwaliko wa kumwilisha huruma ya Mungu katika medani mbalimbali za maisha ya kijamii kwa njia ya umoja na mshikamano wa upendo. Kanisa linapenda kujizatiti zaidi katika mapambano dhidi ya umaskini ndiyo maana kila mwaka Jumapili ya XXXIII ya Mwaka wa Kanisa inaadhimishwa Siku ya Maskini Duniani ili kutoa nafasi kwa Kanisa kutafakari kuhusu maskini ambao kimsingi ni amana, hazina na utajiri wa maisha na utume wa Kanisa. Lengo kuu ni kujenga misingi ya haki jamii kwani hakuna haki na amani ya kweli, ikiwa kama bado kuna makundi makubwa ya maskini wanaoteseka kwa baa la njaa, magonjwa, umaskini, ujinga, utupu na upweke hasi katika maisha. Huruma ni kielelezo makini cha imani na ushuhuda wa Kikristo. Huu ni mwaliko wa kutafakari dhana ya umaskini duniani kwa kutumia miwani ya matendo ya huruma: kiroho na kimwili, ili kujenga utamaduni wa huruma ya Mungu katika maisha ya watu, kwa kuwathamini, kuwajali na kuwasaidia kadiri ya uwezo na fursa zilizopo.

Papa Francisko ni Baba wa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni
Papa Francisko ni Baba wa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni   (Vatican Media)

Hayati Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, Kanisa linawajibika kimaadili kuwasaidia na kuwahudumia maskini, ndiyo maana baada ya kufunga rasmi maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, ameanzisha Maadhimiso ya Siku ya Maskini Duniani, ili Jumuiya za Kikristo sehemu mbalimbali za dunia, ziweze kuwa alama wazi ya upendo wa Kristo Yesu kwa maskini na wahitaji zaidi. Siku hii ni muhimu sana ili kuonesha upendeleo wa Yesu kwa maskini, mwaliko kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kuwasikiliza, kuwahudumia na hatimaye, kuwaonesha maskini upendo na mshikamano, kwa kutambua kwamba, hata wao wameumbwa na wanapendwa na Baba wa mbinguni.  Siku ya Maskini Duniani iwe ni nafasi ya kuwaonjesha huruma na upendo maskini na wahitaji; ni siku ya kuwakaribisha na kuwakirimia wageni, hali inayowasaidia waamini kumwilisha imani yao katika matendo. Watu wawe tayari kupokea msaada na kujitahidi kuishi kwa kuzingatia mambo msingi ya maisha, daima wakiwa tayari kujiachilia kwa huruma ya Mungu. Iwe ni Siku ya kumwilisha Sala ya Baba Yetu Uliye Mbinguni, ambayo kimsingi ni sala ya maskini, tayari kusikiliza na kujibu kilio cha maskini wanaohitaji mambo msingi katika maisha. Sala ya Baba Yetu inawawajibisha waamini kupokea na kugawana hata kile kidogo kilichopo, tayari kuvunjilia mbali ubinafsi, kwa kutoa nafasi ya kushirikisha furaha ya ukarimu. Siku ya Maskini Duniani iwe ni fursa makini ya uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili; nafasi ya kutambua kwamba, maskini wanawasaidia waamini wenzao kutambua ukweli na tunu msingi za Kiinjili.

Papa Francisko Injili ya Maskini
25 Aprili 2025, 15:01