Ijumaa 25 Aprili usiku saa 2 kamili jeneza la Papa Francisko litafungwa
Vatican News.
Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na Mshereheshaji wa maadhimisho ya Kipapa, Askofu Mkuu Diego Ravelli amebainisha kuwa: tarehe 25 Aprili 2025 saa mbili kamili usiku masaa ya Ulaya na saa 3 kamili saa za Afrika Mashariki na Kati katika Basilika ya Mtakatifu Petro mjini Vatican, mwadhama Kardinali Kevin Joseph Farrell, Camerlengo wa Kanisa Takatifu la Roma atakaongoza ibada ya kufunga jeneza la Baba Mtakatifu Francisko kwa mujibu wa maelekezo ya (Ordo Exsequiarum Romani Pontificis (nn. 66-81), yaani Kanuni za Mazishi ya Papa wa Roma).”
Watakaoshiriki maadhimisho hayo: Mwadhama Kardinali Kevin Joseph Farrell, Camerlengo wa Kanisa Takatifu la Roma, Mwadhama Kardinali Giovanni Battista Re Decano wa Baraza la Makardinali, Mwadhama Kardinali Dominique Mamberti, Kardinali wa kishemasi, Mwadhama Kardinali Mauro Gambetti, Askofu Mkuu wa Basilika ya Kipapa ya Mtakatifu Petro, Mwadhama Kardinali Pietro Parolin, Katibu wa Vatican, Mwadhama Kardinali Baldassare Reina, Makamu mkuu wa Baba Mtakatifu Jimbo la Roma, Mwadhama Kardinali Konrad Krajewski, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Upendo, Askofu Mkuu Edgar Peña Parra, Katibu Msaidizi wa Vatican.
Askofu Mkuu Ilson de Jesus Montanari, Makamu Camerlengo wa Kanisa Takatifu la Roma, Monsinyo Leonardo Sapienza, Mkuu wa Nyumba ya Kipapa, Wanasheria wa Vatican, Waungamishaji wa kawaida wa Vatican, Katibu wa Baba Mtakatifu, Watu wengine waliowekwa na Mshehereshaji wa maadhimisho ya Kipapa. Wote hawa wanatakiwa kukutana saa 1.30 usiku katika Altare ya Maungamo. wakiwa tayari na mavazi ya kiklero.