Ijumaa Kuu2025 : Tafakari ya Teknolojia ya Akili Unde ya Msalaba
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Mama Kanisa katika adhimisho la Ijumaa kuu anafanya kumbu kumbu ya mateso na kifo cha Yesu Kristo Mkombozi wa dunia. Siku ya kufunga kama kielelezo cha nje kinachoonesha ushiriki wa waamini katika mateso ya Yesu Kristo. Hakuna adhimisho la Fumbo la Ekaristi Takatifu kwani Kristo ambaye ndiye chemchemi ya Sakramenti zote za Kanisa anateseka na hatimaye, kufa Msalabani. Ijumaa kuu jioni, Kanisa limeadhimisha Mateso na Kifo cha Kristo Yesu, anayejionesha kuwa ndiye Mtumishi mwaminifu wa Mungu aliyetabiriwa na Manabii katika Agano la Kale. Ni Mwana Kondoo wa Mungu anaye yamimina maisha yake kwa ajili ya ukombozi wa wengi. Msalaba ni alama kuu inayochukua kipaumbele cha pekee katika Maadhimisho ya Ijumaa Kuu. Ni kielelezo cha Mti wa Ushindi wa Kristo dhidi ya dhambi na mauti, ndiyo maana, waamini wamepata fursa ya kuweza kuabudu Msalaba wa Kristo. Fumbo la Msalaba wa Kristo Yesu yaani: Mateso, kifo na ufufuko wake ni kilele cha ufunuo wa: huruma, upendo, ukuu, utukufu na utakatifu wake, changamoto kwa Wakristo ni kushikamana pamoja na Kristo katika mapambano, ili siku moja waweze kushinda pamoja naye! Huu ndio ujumbe wa matumaini unaofumbatwa kwa namna ya pekee katika Fumbo la Msalaba, mwaliko kwa waamini kumtafakari Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu kuwa ni kiini cha imani ya Kikristo. Fumbo la Msalaba ni alama ya upendo wa Mungu kwa binadamu; kielelezo cha sadaka ya hali ya juu kabisa ya Kristo Yesu dhidi ya ukosefu wa haki msingi za binadamu; ubinafsi, dhuluma na nyanyaso. Msalaba ni alama ya ushindi dhidi ya dhambi na mauti.
Msalaba ni kielelezo cha mateso, dhuluma na nyanyaso dhidi ya Wakristo wanaouwawa kikatili kwa kuchomwa moto wangali hai; na wakati mwingine nyanyaso na dhuluma hizi zinatendwa katika hali ya ukimya mkubwa. Kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican Ibada ya Ijumaa kuu ambayo kimsingi imegawanyika katika sehemu kuu tatu yaani: Liturujia ya Neno la Mungu inayohusisha mahubiri ambayo yametolewa na Padre Roberto Pasolini, OFM Cap., Mhubiri wa Nyumba ya Kipapa pamoja na Sala za Waamini kwa ajili ya Kanisa na Ulimwengu katika ujumla wake. Sehemu ya Pili ni Liturujia ya Ibada ya Kuabudu Msalaba na Sehemu ya tatu ni Ibada ya Komunio Takatifu. Padre Roberto Pasolini, OFM Cap., katika mahubiri yake, amejikita zaidi katika Fumbo la Msalaba kama kielelezo cha hali ya juu kabisa cha upendo na huruma ya Mungu kwa binadamu; Kristo Yesu alijitoa kwa watesi wake katika uhuru kamili; Katika mateso makali, akaona kiu na hatimaye, kukata roho, kielelezo cha imani ya juu kabisa iliyomwezesha Kristo Yesu kujiaminisha kwa Baba yake wa mbinguni. Ijumaa kuu, Mama Kanisa anatafakari juu ya teknolojia ya Akili Unde ya Msalaba: “Artificial Intelligence of the Cross” inayofumbatwa katika upendo kwa ajili ya wokovu wa ulimwengu, Mwenyezi Mungu akamuenzi juu ya Msalaba, kiasi cha kujiaminisha kwa Baba yake wa mbinguni.
Akiwa Bustanini Getsemani katika uchungu na mateso makali, akajitambulisha kwa watesi wake, baada ya busu la usaliti kutoka kwa Yuda Iskarioti, kielelezo kwamba, alijiandaa kikamilifu ili kuweza kukabiliana na “Saa yake ya mateso na kifo” chimbuko la maisha na uzima wa milele. Akiwa juu Msalabani, akaona kiu Yn 19:28-29. Akiwa katika utupu wa kibinadamu, akaonesha kwamba, kwa hakika alitakiwa kupendwa, kupokelewa na kusikilizwa kama binadamu, mwaliko kwa waamini wanapokabiliana na mateso, uchungu na fadhaa wasikae kimya, kielelezo cha unyenyekevu wa hali ya juu na hamu ya kuendelea kuishi. Kristo Yesu alikata roho kwa kusema, “Yametimia.” Yn 19:30, kielelezo kwamba, upendo wa dhati ni chemchemi ya wokovu wa ulimwengu na kwamba, maneno ya Kristo Yesu Msalabani ni ushuhuda wa sadaka ya Kristo Yesu bila ya kujibakiza hata kidogo.“Kristo Yesu ni tumaini letu” ni sehemu ya Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo yanayonogeshwa na kauli mbiu “Peregrinantes in spem” yaani “Mahujaji wa matumaini.” Padre Roberto Pasolini, OFM Cap., anawataka waamini kuwa imara katika imani yao kwa Kristo Yesu hata wakati ambapo Fumbo la Msalaba linawakodolea macho. Ebr 4:14. Mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kwa wafu ni chemchemi ya upatanisho, chanzo cha upendo na huruma ya Mungu kwa waja wake. Katika maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo, waamini wanataka kutangaza na kushuhudia utukufu na ukuu wa Msalaba wa kristo kama kielelezo cha Injili ya matumaini na msaada wakati wa udhaifu wa kibinadamu. Msalaba wa Kristo ni kielelezo cha upendo wa hali ya juu kabisa kwa binadamu wote, mwaliko kwa waamini kupendana kiasi hata cha kuwapenda na kuwaombea adui zao. Na kwa jinsi hii, waamini watakuwa kweli ni mashuhuda na vyombo vya ukweli unaookoa walimwengu na kwamba, Mwenyezi Mungu ni Baba yao na kwamba, wote ni ndugu wamoja katika Kristo Yesu.