Katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro ibada na kufunga jeneza la Papa Francisko imefanyika
Na Angella Rwezaula - Vatican.
Kama ilivyokuwa imetangazwa hapo awali, ibada ya kufunga jeneza la Baba Mtakatifu wa Roma imefanyika Ijumaa Aprili 25 leo usiku saa 2:00 kamili masaa ya Ulaya ikiwa ni saa 3.00 kamili saa za Afrika Mashariki na kati mbele ya Madhabahu ya Kukiri kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican.
Katika ibada iliyoongozwa na Camerlengo, wa Kanisa Takatifu la Roma, Msimamizi wa Maadhimisho ya Liturujia, Kardinali Kevin Joseph Farrell, Askofu Mkuu Diego Ravelli alisoma hati ambayo iliwekwa kwenye jeneza mwishoni mwa maadhimisho hayo.
Mbali na yale yaliyokuwa yameoneshwa katika taarifa kutoka Ofisi ya Maadhimisho ya Liturujia za kipapa, pia baadhi ya wanafamilia wa marehemu Papa walishiriki ibada hiyo.
Maadhimisho hayo yaliyofanyika kwa mujibu wa maagizo ya(Ordo Exsequiarum Romani Pontificis), Kanuni ya mazishi ya Papa wa Roma yalihitimishwa saa 3.00 usiku.
Na wakati wote wa usiku, wajumbe wa chama cha Mtakatifu Petro watahakikisha uwepo wao kwa sala na mkesha kwa ajili ya mwili wa Papa, hadi maandalizi ya Misa Takatifu itakayofanyika kesho asubuhi tarehe 26 Aprili 2025 katika Uwanja wa Mtakatifu Petro mjini Vatican.