Kuhamishwa kwa mwili wa Papa Francisko hadi Kanisa Kuu
Na Angella Rwezaula - Vatican.
Imefanyika ibada fupi iliyofanyika katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumatano asubuhi, tarehe 23 Aprili 2025 kwa ushirikishi wa Baraza la Makardinali walioanza kukusanyika mjini Roma kufuatia kifo cha Baba Mtakatifu Francisko kilichotokea tarehe 21 Aprili 2025. Kardinali Kevin Farrell, Camerlengo wa Kanisa Takatifu la Roma, alianza ibada ya kiliturujia katika Kanisa Mtakatifu Marta kwa sala fupi kwa ajili ya roho ya Baba Mtakatifu Francisko.
Katika sala ya ufunguzi, Kardinali Farrell alimshukuru mwenyezi Mungu kwa huduma ya miaka 12 ya hayati Papa Francisko. "Tunapoondoka sasa katika nyumba hii, tumshukuru Bwana kwa zawadi zisizohesabika alizowapa Wakristo kupitia mtumishi wake, Papa Francisko. Tumwombe Yeye, kwa rehema na fadhili zake, amjalie marehemu Papa makao ya milele katika ufalme wa mbinguni, na kuwafariji kwa tumaini la kimbingu familia ya papa, Kanisa la Roma, na waamini ulimwenguni kote," alisema.
Mwili wa Papa umehamishiwa katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro
Baadaye baraza la Makardinaili walianza maandamano ya kuleta jeneza kupitia Uwanja wa Mtakatifu Marta wa Vatican, chini ya Tao la Kengele, na kuingia katika Uwanja wa Mtakatifu Petro, kama ilivyokuwa tayari imeratibiwa.
Zaidi ya watu 20,000 walikuwa wamekusanyika katika uwanja huo kutoa heshima zao kwa marehemu Papa, huku wakisikika kwa makofi duni, lakini ya kudumu wakati jeneza lake likibebwa kwenye ngazi na kuingia kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro.
Jeneza lenye mwili wa Papa liliwekwa mbele ya madhabahu ya juu na kwaya na wale waliokuwepo waliimba Litania ya Watakatifu kwa Kilatini kwa ajili ya kupumzika kwa roho yake.
Kisha Kardinali Farrell aliongoza Liturujia fupi ya Neno, ambayo ilijumuisha usomaji kutoka Injili ya Yohane (17:24-26) ya sala ya Yesu ya ukuhani akitangaza upendo wa Mungu kwake na kwa wanafunzi wake.