Maombolezo ya Kifo cha Papa Francisko: Jimbo Kuu la Roma
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
“Sacrum novendiale, Novendia” ni kipindi cha siku tisa za maombolezo kinachofuatia kifo cha Baba Mtakatifu na kuanza mara baada ya mazishi ya Khalifa wa Mtakatifu Petro na tarehe yake hupangwa na Baraza la Makardinali na maadhimisho haya yanafanyika kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Ni katika muktadha huu, Kardinali Pietro Parolin, aliyekuwa Katibu mkuu wa Vatican, Dominika tarehe 27 Aprili 2025 ameongoza Ibada ya Misa Takatifu, Siku ya pili ya Novendia, maalum kwa wafanyakazi pamoja na raia wanaoishi mjini Vatican. Kardinali Parolin katika mahubiri yake amegusia kuhusu: Majonzi makubwa katika kipindi hiki cha maombolezo ya Baba Mtakatifu Francisko, lakini jambo la msingi ni furaha ya Pasaka; changamoto mamboleo katika maisha ya vijana, lakini wanapaswa kujikita katika upendo ambao hustahimili yote. Upendo wenye huruma ni kiini cha mafundisho ya Baba Mtakatifu Francisko, chemchemi ya imani, matumaini na mapendo na kwamba, Kanisa ni chombo na shuhuda wa huruma ya Mungu.
Kardinali Baldassare Reina, maarufu kama “Baldo”, Makamu Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Roma, Jumatatu jioni tarehe 28 Aprili 2025 akiwa ameungana na waamini wa Jimbo kuu la Roma, ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu, Siku ya Tatu ya Novendia. Katika mahubiri yake amegusia majonzi makubwa kwa watu wa Mungu Jimbo kuu la Roma ambao wanaomboleza kwa kuondokewa na Mchungaji wao mkuu, sasa wamekuwa kama kondoo wasiokuwa na mchungaji, huyu ni mchungaji aliyewapenda sana kondoo wake, lakini wakumbuke kwamba, Kristo Yesu ndiye mchungaji wa kweli, aliyeleta mageuzi katika historia ya ukombozi wa mwanadamu, anatambua uzito wa mchakato wa uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji msingi ya binadamu. Kipindi hiki cha majonzi ni muda muafaka wa kupyaisha imani, matumaini na mapendo kwa Kristo Yesu na Kanisa lake, kwani maisha yana nguvu zaidi ya kifo.
Kwa mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu, anawatangazia waja wake: mbingu, dunia na Yerusalemu mpya; changamoto na mwaliko wa kuamka na kuanza kutekeleza kwa vitendo yale mageuzi yaliyofanywa na Baba Mtakatifu Francisko enzi ya uhai wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro na kuendelea kuliombea Kanisa ili liweze kupata Mchungaji mkuu: mwenye uwezo wa kuwaondolea watu woga na wasi wasi katika maisha tayari kuambata na kukumbatia tunu msingi za Kiinjili; Kiongozi mwenye ufunuo wa Uso wa Mungu mwingi wa huruma na mapendo; kiongozi, atakayetoa dira na mwelekeo wa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia, tayari kuwapaka mafuta ya faraja wale waliovunjika na kupondeka moyo kwa kuwanyweshwa divai ya matumaini yanayobubujika kutoka kwa Kristo Yesu na Kanisa lake.
Ni muda wa kusali na kuliombea Kanisa, ili liendelee kukita mizizi yake katika tunu msingi za Kiinjili, kwa kuwa na wachungaji wema na watakatifu, wenye uwezo wa kuyamimina maisha yao kwa ajili ya kondoo wao. Kwa mateso, kifo na ufufuko wake, Kristo Yesu amewatangaza na kushuhudia huruma na upendo wa Mungu usiokuwa na kifani. Kifo cha Kristo Yesu ni chemchemi ya msamaha na huruma ya Mungu; wokovu wa wengi. Mama Kanisa anaadhimisha Pasaka ya Baba Mtakatifu Francisko, aliyejisadaka bila ya kujibakiza katika mchakato wa kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu. Hata katika dakika yake ya mwisho hapa duniani, akatangaza na kushuhudia huruma ya Mungu kwa waja wake. Bikira Maria Afya ya Warumi, “Salus Popoli Romani” amsimamie, amlinde na hatimaye, aweze kuipokea roho yake mbinguni. Itakumbukwa kwamba, tarehe 29 Aprili 2025 ni Siku ya Nne ya Maombolezo na wahusika wakuu ni wahudumu wakuu kutoka katika Makanisa makuu ya Kipapa, Jimbo kuu la Roma.